KUFIKIA MATARAJIO YAKO.
KUFIKIA MATARAJIO YAKO.
Tupo
katika mchakato wa kuyaendea mafanikio yako na matarajio yako. Tukiangalia
safari ya wana wa Israel inatupa maswali mengi ya kujiuliza kwa maana Biblia
inasema safari yao ni kivuli cha safari yetu katika wokovu, ukitaka kujua
safari yako ikoje na inaishiaje angalia safari ya wana wa Israel, itakupa
mwangaza wa safari unayoiendea.
Ninapo itazama safari ya wana wa
Israel nina maswali, je! Ni wangapi watakao faulu kufika mwisho wa safari yao?
Wana wa Israel walikuwa wanaenda katika nchi ya dhahabu, maziwa na asali,
hawakuwa na safari ya kwenda mbinguni bali ni safari ya kuendea matarajio na
mbaraka wao. Kama kuna wakati wa kujiuliza maswali ni kupitia safari ya wana wa
Israel ambayo kwetu sisi ndio kioo na ramani yetu ya kuelekea uzima wa milele.
Kabla haujaanza safari yako ya
kuelekea katika Baraka zako ziko changamoto nyingi utakutana nazo kama vile
wana wa Israel walivyokutana nazo walivyokuwa njiani, hayo yaliyowasibu na wewe
ukubali au usikubali utakutana nayo kabla haujakutana na mbaraka wako, sasa
swali langu ni kuwa ni wangapi watakao faulu. Je ni wangapi wataondoka katika
tabia za dhambi au tabia za zamani? Biblia inasema hamjafanya vita na dhambi
hata mkamwaga damu, kumbe kuna vita kati yako na dhambi na sio na shetani, huu
ndio mpambano wako mkubwa na wala sio shetani au majini. Mpambano wa mtu
aliyeokoka ni kati yake na dhambi huo ndio mpambano wake mkubwa ambao unabebwa
na tabia za kale, tabia za mababu na tabia za watu wote na sio kwenye hayo
mengine unayoyaona. Hii siyo vita ya leo bali ni vita ambayo ilianzishwa na
Mungu mwenyewe baada ya anguko la Adamu na Hawa. Mwanzo 4:7 “ Kama ukitenda vyema, hutapata kibali?
Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe,
walakini yapasa uishinde.” Hapa hakuna ibilisi wala mchawi, safari
ya maisha ya mtu anayetamani kuwa na maisha yaliyo bora ana mpambano kati yake
na dhambi. Dhambi inakukaribia kwa sababu ya tabia zako, sio kwa sababu ya
ibilisi, wachawi wala matambiko, la! Bali ni kwa sababu ya tabia, hapo ndipo
palipokuwa na mpambano wa wewe ni nani, mpambano wa kesho yako ndio uko hapo.
Adui mkubwa wa wokovu wako ni
dhambi, na huyo adui ana rafiki yake mpendwa ambaye wewe ndio umemuumba, ni
nani huyo? Ni tabia. Mwanzo 4:7 “ Kama
ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea
mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Mungu
anakutamani ili moyo wako umkaribishe, lakini dhambi haihitaji uikaribishe bali
tabia yako tu, kuna tabia ukiwa nayo dhambi inakukaribia na kufurahi na wewe.
Biblia inasema yapaswa uishinde. Kama kuna mtihani ambao mwanadamu amepewa ni
kubadilisha tabia, mabadiliko hayo ya tabia kwa mwanadamu hayajalishi ni
maskini au tajiri, upo kanisani, barabarani, umeoa au umeolewa, au hujaoa au
kuolewa ni mtoto au kijana, tabia haina umri wala imani. Unaweza ukawa una
imani lakini tabia yako inakusababisha uwe uliyeshindwa. Unaweza ukawa hauna
imani lakini tabia yako ikawa inamvutia Mungu na kusababusha akushindie. Kaini
sio kwamba alikuwa hana imani, la! alikuwa nayo na ndiyo maana alikwenda
kumtolea Mungu dhabihu; Mfalme Sauli alikuwa na Imani lakini kwa nini aliishia
hapo alipo ishia? Shida sio imani bali ni tabia yake. Tabia yako inaweza
kukupelekea kushinda au kushindwa. Jiulize nafsini mwako tabia gani unayo wewe,
je! Inamvutia Mungu au mapepo na majini?.
Mungu alimpenda sana Musa, Musa
alikuwa ni mtu mwenye imani na pia alikuwa anaumba imani kwa wengine, lakini
aliambiwa na Mungu achukue wana wa Israel kwenda Kaanani lakini yeye mwenyewe
hakuingia. Kwa nini Musa hakuingia Kaanani? Kutokana na tabia yake. Je! wewe
unatabia ya aina gani? Musa alifanya dhambi gani mpaka akanyimwa kuingia
Kaanani? Musa alikuwa na hasira na kwa sababu ya hiyo ikampelekea kutokufanya
kama alivyoelekezwa na Mungu, alifanya hivyo mara moja tu na ikamgharimu. Ni
mara ngapi wewe haukufanya kama ulivyoelekezwa na Mungu ukafanya unavyojua wewe
kwa sababu ya hasira, kiburi au kujua?. Mungu akusaidie. Maombi ni akiba na
yanasimama badala ya neno mbele za Mungu, yaweke maombi yako yawe kama akiba,
watu wengi wanaweka pesa kama akiba lakini wewe weka maombi yako kwa Mungu kama
akiba, kuna siku utakuwa hauwezi hata kuomba lakini yale maombi yako uliyoomba
miaka miwili au mitatu iliyopita yatamkumbusha Bwana. Tabia ni tendo, iwe ni
kwa kuwaza au kutenda. Musa pamoja na machungu yote aliyopitia kwa sababu ya
wana wa Israel lakini hakuonja yale maziwa wala asali, kwa sababu gani? Kwa
sababu ya tabia yake.
Mwanzo 21:9 “Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri,
ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka.” Hapa nini kilitokea?
Tabia iliinuka, tabia ilileta vurugu nyumbani kwa Ibrahimu. Tabia sio kwa mtoto
tu, unaweza ukawa ni mtoto au mtu mzima lakini tabia itakuonyesha jinsi ulivyo.
Mwanzo 21:10-12 “Kwa hiyo
akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi
hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa
Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe
baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila
akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.”
Usimdharau mkeo kwa sababu hajazaa, wala usimdharau kwa sababu yoyote ile,
unakuta mtu ameoa mke baada ya muda anaanza kumuona huyo mke ana sura mbaya na
hamtaki tena, usimuache mke wako kwa sababu yoyote ile; kwa sababu wakati
unamuoa walikuwepo wadada wengine wazuri zaidi ya mkeo lakini wewe ukamchagua
huyo. Usije ukawaona wadada wengine ni wazuri kuliko mkeo ukaona kuwa mkeo
hafai hapana. Kuna wengi wameshindwa kufanikiwa kwa sababu ya tabia zao, Je!
wewe mwanaume upo tayari kumsikiliza mke wako? Au wewe mwana mke uko tayari
kumsikiliza mume wako? Wengi wenu Mungu hawabariki kwa sababu tu ya
kutokuelewana kwenu, Mungu akiona mnagombana kila mara na hamsikilizani kamwe
hatawabariki kwa sababu anaona mtauana. Ukiona ndoa inachanua jua kuwa kuna
kusikilizana ndio maana Mungu anawabariki.
Mwanzo 21:14-16 “Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa
mkate na kiriba cha maji, akampa Ha jiri akimtwika begani pake, na kijana,
akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba. Yale maji
yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda akakaa
akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone
kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.”
Wengi mmefukuzwa mbali na Baraka zenu kwa sababu ya tabia zenu.
Tabia yako inaweza kukuzuia usizione
baraka zako zilipo. Kumbu kumbu 28:3 “Utabarikiwa
mjini, utabarikiwa na mashambani.” Hapo ulipo baraka zako zipo
lakini je! Tabia yako inakuruhusu uzione hizo baraka? Je! tabia yako inamruhusu
Mungu akubariki?.
Mwanzo 21:17 “Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa
Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope,
maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.” Ni maombi yangu
kwa Mungu kuwa akafungue macho yako ili uweze kuona zile baraka ambazo ziko
karibu na wewe, kuna baraka na muujiza wako upo hapo hapo ulipo lakini ili
uweze kuona lazima Mungu afungue macho yako, akisha fungua macho yako na ukaona
shida yako imeisha.
Kwa nini watu wanafanya biashara
alafu zinakufa? Ni kwa sababu sio kile ambacho Mungu amewapa, unakuta mtu ndani
ya moyo wake tangu mwanzo ana msukumo wa kufanya biashara fulani lakini akianza
kufanya hiyo biashara akiona haiendi vizuri ndipo anaanza kuwaza sijui niuze
nguo au mchele, yaani anauza kila kitu; kile ambacho umesikia kutoka ndani ya
moyo wako ukikifanya hicho umetoboza. Unaanza biashara si kwa sababu una hela,
la! Bali unaanza kwa sababu Mungu amekupa.
Biashara yoyote ambayo Mungu amekupa
hauanzi na kuwa na hela bali unaanza na wazo ndipo pesa zinakuja. Unapaswa
kujiuliza maswali yafuatayo:-
- Je! Tabia yangu inaniruhusu
mimi kuona?
- Je! Tabia yangu ina chelewesha
Mungu kunipa yale yaliyo ya kwangu?
KUMILIKI NA KUTAWALA.
Zaburi
16:5-6 “BWANA ndiye fungu la posho
langu, Na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu. Kamba zangu zimeniangukia
mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri.”
Yeyote
aliye weka kura yake katika uwepo wa Mungu basi ameweka kura yake mahali sahihi
na kamba zake zimeangukia mahali pema.
Laiti kama
maandiko yasemavyo watu wangeyachukulia kwa umakini mahangaiko yangekoma.
Mungu
hakusikii kwa sababu umefunga na kuomba sana la! Bali anakusikia kwa sababu
umeelewa Neno lake.
Ufunuo1:1
“Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na
Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi;
naye akatuma kwa mkono wa Malaika akamwonyesha mtumwa wake Yohana; “
Ufunuo ni
wa Yesu, mwenye Ufunuo huo ni Mungu na Yeye amempa Yesu ili awape watumwa wake.
Siku ukielewa umeshinda, hauhitaji kufunga na kulia sana ili upate, hakuna hata
mmoja anayestahili au asiyestahili kupokea bali tunapokea kwa sababu tumekubali
kupokea.
Sio kwamba
unapokea kwa sababu wewe ni bora sana au haupokei kwa sababu wewe si bora, la!
Ili upokee ya Mungu haitokani na dhambi zako au kwamba hauna dhambi bali
inatokana na Maamuzi yako umeamua nini leo na sio jana, inawezekana jana
umetenda dhambi nyingi lakini Je! leo umeamua nini?.
Ufunuo sio
mali yetu bali ni mali ya Mungu, anatuletea sisi tunaomwamini ili tupate kujua
yaliyo mbele yetu, sasa ukiamini kile ambacho Yeye amesema basi umepokea.
Ufunuo 1:3
“Heri asomaye na wao wayasikiao
maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u
karibu.”
Je! Wewe
umesoma au umesikiliza? Basi una heri wewe usomaye na wewe usikiaye.
Watu wengi
wanasikia na kuona lakini bado wanateseka, tatizo liko wapi? Lipo katika
Mapenzi ya Mungu.
1 Yohana
5: 14 “Na huu ndio ujasiri tulio
nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.”
Ukiomba
kitu sawa sawa na Mapenzi ya Mungu utapata unachoomba, tatizo lipo katika
Mapenzi, Je upo kwenye Mapenzi yake? Sio kuimba, kushangilia wala kuomba bali
ni Mapenzi yake.
Yohana
3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Mapenzi ya Mungu kwako
ni nini? Ni wewe usipotee, sasa swali linakuja, Je! Wewe unaishi maisha ya
upotevu? Kama hauishi maisha ya upotevu basi omba lolote na Yeye atakupa.
1 Yohana
5:16 “Na kama tukijua kwamba
ATUSIKIA, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.”
Nini maana ya Kusikia? Kusikia maana yake ni Kukubali.
Siku zote,
wakati wote na muda wote Mungu ni Pendo; Kwa sababu ya Usingizi ulionao au
Ujinga uliopo kichwani ndio maana unafikiri kuwa Mungu hataki kukujibu maombi
yako, unapaswa kuelewa kuwa Mungu ni Pendo na Yeye anapenda watu, ukisema kuwa
hataki kujibu maombi yako hiyo ni akili yako ila Yeye anakupenda.
1 Yohana
5: 14 “Na huu ndio ujasiri tulio
nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.”
Je!
unakubali kuwa Mungu anakusikia? Kabla haujaomba lazima kwanza uwe na uhakika
kuwa anakusikia.
- Kabla haujaomba tengeneza
mazingira ya Yeye kukusikia kwanza ili unapoomba apate kukusikia na
kukujibu.
- Unatengenezaje mazingira ya
kusikiwa na Mungu? Kwa wewe kujua Mapenzi yake juu yako, Mapenzi ya Mungu
kwako ni yapi? Ni wewe usipotee, tafakari Je tabia ulizonazo ni sahihi au
zinakupeleka upotevuni? Je upo kwenye dhambi? Ukiona upo hivyo tengeneza
toba yako ili ikuvute karibu na Yeye ili hata utakapoomba Yeye akusikie.
- Usijichoshe kuongea na Mungu
wakati mazingira yako yanafanana na ibilisi, utaishia kusema nimeomba sana
lakini Mungu hanijibu, atakujibuje wakati wewe ukitoka tu kuomba unaenda
kusengenya na ndani ya moyo wako kumejaa uchungu.
- Kabla haujaongea na Mungu
chochote hakikisha ndani ya moyo wako kuna neno ambalo umelisoma na neno
hilo ni kweli na akili yako na moyo wako unakubali kuwa hiyo ni kweli
yako.
- 1 Yohana 5:16 “Na kama tukijua kwamba ATUSIKIA,
tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.”
- Jambo la pili ambalo unapaswa
kuwa nalo ni wewe kukubali kuwa hapo ulipo Yeye atakusikia.
- Kabla haujakubaliana na kuona
ule ukaribu kuwa Mungu yupo karibu yako na anakusikia usiombe kitu
chochote.
Lazima
wewe uliyeokoka ulinde Heshima ya JINA la Mungu wako na la Bwana YESU ndipo
utakapoomba lolote na Yeye atakujibu, lakini unakuta mlokole ndio wa kwanza
kufanya vituko mpaka Bwana Yesu mwenyewe anashangaa, unasababisha Jina la Mungu
linatukanwa na wale wasioamini hii ni mbaya.
Kwako wewe
uliyeokoka onesha kwamba umeokoka kwa kulinda na kuheshimu Jina la Mungu na
kufanya yaliyo Mapenzi yake kwako.
Mapenzi ya
Mungu kwako ni yapi? Mapenzi ya Mungu kwako ni Wewe, sasa swali linakuja hivi,
Je! wewe unafanya Mapenzi yake? Yeye amefanya Mapenzi yake Kwako na kumtoa
Mwanaye wa pekee kwa ajili yako ili Wewe usipotee bali uwe na Uzima tele, Je!
Wewe unafanya Mapenzi yake?.
Nehemia
1:4 “Hata ikawa niliposikia maneno
hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga,
nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni;”
Hapa tunaona
kuwa Nehemia alikuwa akitafakari yaliyomsibu, alijuta na kusikitika katika kile
kilichotokea na kuapa kuwa hatarudia. Nehemia alifanya hivyo kwa siku kadha wa
kadha na siyo siku moja, baada ya hayo ndipo akajipeleka mwenyewe mahali ambapo
uwepo wa Mungu upo, baada ya Nehemia kuomba hayo ndipo akapokea kile alichokuwa
akiomba.
Daniel 7:1
“Katika mwaka wa kwanza wa
Belshaza, mfalme wa Babeli, Danielii aliona ndoto, na maono ya kichwa chake,
kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.”
Baada ya maombi ya Daniel ndipo jibu lake likaja.
Daniel
9:20-21 “Basi hapo nilipokuwa
nikisema, na kuomba, na kuiungama dhambi yangu, na dhambi ya watu wangu
Israeli, na kuomba dua yangu mbele za BWANA, Mungu wangu, kwa ajili ya mlima
mtakatifu wa Mungu wangu;”.
Tunapaswa
kuchukulia mambo ya Mungu kwa uhalisia na si katika ndoto, tunapaswa kusogea
karibu na Yeye ili tuweze kuuona Wema wa Mungu kwa jinsi anavyotupenda.
Unapaswa
kupata Urithi wako, ndio utaupata; lakini ni lini? Ni sasa. Kuna wengine
wanakufa kabla ya kufikia Urithi wao kwa sababu gani? Kwa sababu hawachukulii
mambo ya Mungu kwa uhalisia.
Daniel
aliona katika ndoto na kisha akaona kwa uhalisia, Je! unataka kuona mambo ya
Mungu kwa uhalisia? Unapaswa kujiandaa, Daniel alijiandaaje? Daniel 1:6-8 “……. Lakini Danieli aliazimu moyoni mwake ya
kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi
akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi.”
Daniel aliamua kuondokana na mambo ya unajisi, alijiandaa mwenyewe kwa kuwa
Mtakatifu.
Kushika
mambo ya Mungu inahitaji Utakatifu, jiandae kwa kuwa Mtakatifu ili uweze
kuyashika mambo ya Mungu.
Unajiandaaje
ili uweze kupokea Vitu vya Mungu? Kwa Wewe KUSAMEHE wengine na kuwa na Moyo
safi.
Mathayo
5:7-8 “Heri wenye rehema; Maana hao
watapata rehema. Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu.”
Wale wanaoweza Kusamehe wengine na wao watasamehewa, Rehemu wengine ili na wewe
upate kurehemiwa na sio mwingine anapopata tatizo wewe unafurahi, uwe na Moyo
safi ambao hauna hila.
Kabla
haujamwambia Mungu lolote angalia kwanza nafsini mwako Je wewe umesamehe?.
Swala la
Kusamehe halimuhusu yule anayesamehewa bali linakuhusu Wewe unayesamehe,
ukisamehe unakuwa na uhuru mbele za Mungu lakini usiposamehe kamwe hauwezi kuwa
na uhuru mbele za Mungu.
Jifunze
kusamehe wengine.
Je kwani
ukisamehe unapungua nini? Haupungui kiungo chochote bali cha zaidi sana wewe
unakuwa huru na uzito unaondoka ndani yako.
Usikate
tamaa kwa sababu ya yale yaliyokuzunguka au kwa sababu ya uchovu unaokutana
nao, kumtumikia Mungu sio rahisi ni kweli kuna maumivu, machungu na dharau,
lakini usikate tamaa. Yakobo hakukata tamaa katika kile alichokuwa anakitaka
hakuangalia ni miaka mingapi alibadilishiwa mshahara wake lakini aliendelea
kumwamini Mungu. Haijalishi nini kinatokea katika Maisha yako usikate tamaa
endelea kumwamini Mungu.
Wewe ndio
unaweza kuibadilisha Kesho yako, adui anaweza kumtumia yeyote yule hata mkeo au
mumeo ili wewe umkosee Mungu, lakini wewe usifanye hivyo, kuna mtu unakuta anamwacha
mke wake au mume wake kwa sababu tu ana tabia mbaya, acha awe hivyo alivyo
lakini wewe mtazame Mungu yule aliyekupa huyo mke au mume, kama ataamua
kukuacha muache akuache lakini wewe usifanye hivyo.
Usimkosee
Mungu kwa sababu tu rafiki yako amemkosea, inasikitisha unakuta mtu mmoja
akikosea na mwingine anaiga, lakini wewe usifanye hivyo bali iangalie safari
yako na Mungu wako. Hamkuzaliwa tumbo moja kila mtu alikuja kwa wakati wake
huku duniani hivyo wewe mpendeze Mungu wako, mtu mmoja asikufanye ukamkosea
Mungu wako.
Maoni