Historia ya Kanisa
Historia
ya Kanisa
Historia ya Kanisa ni fani
inayochunguza historia ya
Ukristo na
ya miundo yake mbalimbali tangu Kanisa
lilipoanzishwa na Yesu Kristo katika karne ya 1
hadi leo.
Kwa kawaida historia hiyo hugawanywa
katika hatua nne:
1.
kipindi cha Mitume wa Yesu na
Mababu wa Kanisa (karne I-karne IX)
2.
Karne za kati (karne IX-karne XV)
3.
kipindi cha marekebisho (karne XVI-karne XVIII)
4.
kipindi cha sasa (karne XIX-karne XXI)
Yaliyomo
- 1 Pande
mbili za Kanisa
- 2
Mwanzilishi wa Kanisa
- 3 Mwanzo wa
Kanisa
- 4 Maendeleo
wakati wa Mitume
- 5 Uenezi
katika karne za kwanza
- 6 Dhuluma
za muda mrefu katika Dola lote la Roma (64-313)
- 7 Uhuru wa
dini katika dola na matokeo yake
- 8 Atanasi
na mababu wengine wa Mashariki
- 9 Umonaki -
maisha ya pekee
- 10
Wamisionari Wamisri katika mabara matatu
- 11
Augustino na mababu wengine wa Magharibi
- 12
Mafarakano ya mataifa mazima na umoja wa Kanisa
- 13 Uenezi
wa Uislamu ulivyorudisha nyuma Ukristo na umisionari wake
- 14 Kanisa
lilivyoendelea hasa Ulaya
- 15
Kuingiliana kwa dini na siasa
- 16
Marekebisho ya karne IX-XII
- 17 Utajiri
wa Kanisa
- 18 Uhaba wa
elimu
- 19 Vita vya
msalaba
- 20
Ugandamizaji wa wazushi
- 21
Fransisko na tapo la mafukara
- 22 Farakano
la Magharibi
- 23 Yohane
Hus na Umoja wa Ndugu
- 24 Mwisho
wa Karne za Kati
- 25
Urekebisho wa Kikatoliki na Matengenezo ya Kiprotestanti
- 26 Vita
kati ya madhehebu ya Kikristo
- 27
Umisionari kupamba tena
- 28
Upietisti
- 29
Umisionari wa Kiprotestanti
- 30 Kanisa
Katoliki na la Kiorthodoksi katika karne ya 18
- 31 Ukristo
katika karne ya 19
- 32 Karne ya
20
- 33 Tanbihi
- 34 Marejeo
- 35 Viungo
vya nje
Pande
mbili za Kanisa
Kwa mtazamo wa imani,
historia hiyo yote inaonyesha upande mmoja udhaifu na ukosefu wa Wakristo hata katika ngazi za juu, lakini pia uwezo wa neema ya Mungu wa kuleta watakatifu wapya katika mazingira yoyote.
Ni kwamba kwa Wakristo,
Kanisa ni kitu kizuri na muhimu sana. Ni bibiarusi wa Yesu, ni mwili wa
Kristo, ni chombo cha Mungu cha kuunganisha waumini
wake kwa Roho Mtakatifu. Limepewa na Mungu wito wa kuwaletea watu Neno lake. Hivyo linatangaza Habari Njema, ambayo ni faraja kwa watu wanaotaka
kukata tamaa. Linaombea watu. Linasaidia wenye dhiki. Linatetea haki za binadamu. Ndiyo sababu ya kusema: Nasadiki Kanisa takatifu.
Lakini Kanisa lina
upande mwingine. Kati ya habari za siku zetu tunaweza kusikia juu ya magomvi
ndani ya madhehebu fulani. Viongozi wanaweza kushindana. Vikundi
vinaweza kujitokeza na kujitenga na Kanisa. Mambo ya hela yanaweza kupata uzito
kuliko mambo ya kiroho. Masharti ya ajabuajabu yasiyo na msingi katika imani na mafundisho ya
mitume, yanaweza kuzushwa ghafla na kutangazwa kuwa ya lazima mbele za Mungu.
Tukiingia katika
historia ya Kanisa kwa undani tunapata habari nyingi za kusikitisha. Ni kwamba
Wakristo ni binadamu. Waliopokea wokovu katika Kristo wako njiani kwenda mbinguni. Lakini bado ni wanadamu wenye dhambi na wenye kasoro. Kasoro hizo za kibinadamu zinaonekana katika historia ya
Kanisa pia.
Mwanzilishi wa Kanisa
Komunyo ya Mitume, kadiri ya Luca
Signorelli, 1512.
Mwanzo wa Kanisa ni kule
Yerusalemu, mji mkuu wa nchi inayoitwa kwa majina mbalimbali katika
historia yake ndefu, kama Kanaani, Israeli, Palestina au Uyahudi.
Mnamo mwaka 30 BK Yesu wa Nazareti alikufa msalabani. Aliuawa na serikali ya kikoloni ya Kiroma. Liwali (gavana) Mroma, kwa jina Pontio Pilato, alitoa dhidi yake hukumu ya mauti kwa sababu ya maombi ya
viongozi wa Kiyahudi.
Yesu alishtakiwa mbele
yake kuwa anataka kujipatia cheo cha Mfalme wa Wayahudi yaani kupindua utawala wa Kiroma. Viongozi Wayahudi wenyewe waliona kosa lake ni kwamba amejitangaza
kwa uongo kuwa Masiya au Mwana wa Mungu. Lakini hilo halikuwa kosa machoni pa Waroma (ambao
walikuwa Wapagani), hivyo wakatumia mashtaka yaliyoeleweka mbele za
Pontio Pilato.
Biblia ya Kikristo inatuambia jinsi
wafuasi wa Yesu walivyoanza kukata tamaa lakini baadaye wakakutana na Yesu aliyefufuka. Akaonana nao na kuwafundisha katika kipindi cha
siku arobaini baada ya Pasaka na hatimaye akapaa mbinguni.
Mwanzo wa Kanisa
Pentekoste ya Mitume
ilivyochorwa mnamo mwaka 586 katika Biblia ya Rabbula nchini Iraki.
Siku ya hamsini baada ya Pasaka mji wa Yerusalemu ulijaa
wageni kutoka sehemu nyingi za dunia. Walikuwa Wayahudi na
watu waliovutiwa na dini yao: walikuwa wamefika kushiriki sikukuu za Kiyahudi.
Siku hiyo wanafunzi wa
Yesu walimpokea Roho Mtakatifu. Matokeo yake ni kwamba walitoka nje ya mkutano wao wakaanza kumshuhudia Bwana wao mbele ya watu wote.
Wengi wakasikia na wengi wakaamini wakabatizwa.
Kati ya wasikilizaji wa
mahubiri ya wafuasi wa Yesu walikuwepo watu kutoka Asia, Ulaya na Afrika Kaskazini, na baadhi yao wakabatizwa. Ndio mwanzo wa ushirika
wa Kikristo.
Siku ile inaitwa "Pentekoste": neno hilo la Kigiriki, maana yake ni "hamsini", yaani siku 50
baada ya Pasaka. Pentekoste ni sikukuu ya kuzaliwa kwa Kanisa.
Wote waliobatizwa siku
ya Pentekoste "waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kindugu,
kumega mkate na kusali".(Mdo 2:42).
"Waumini wote
waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana
pamoja".(Mdo 2:44)
"Jumuiya yote ya
waumini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja
aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana
vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana
waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kukabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila
mmoja kadiri ya mahitaji yake". (Mdo 4:32-35).
Ushirika wa Wakristo leo
unaonekana tofauti katika mambo mbalimbali. Tusishangae: Yesu alitumia mfano wa
mbegu ndogo inayotarajiwa kuwa mti mkubwa baadaye. Watu
120 wa kwanza wamekuwa leo 2,500,000,000! Picha aliyotuachia Luka si sheria ambayo ni lazima tuifuate, bali ni mfano bora tu kwetu,
ambao tuzingatie kwamba kila mahali mazingira ni tofauti.
Tangu miaka 2000
Wakristo wamepata kusikia tena na tena habari hizo wakapata mawazo mazuri jinsi
gani ya kujenga jumuiya ya kindugu na ya kusaidiana katika mazingira yao hapa
duniani.
Mpaka leo tabia kadhaa zilizotajwa
katika Biblia zinakubalika kuwa alama za Kanisa:
- a. kujifunza toka kwa
mitume wa Yesu
- b. kuishi pamoja
kindugu na kuwasaidia wanyonge
- c. kumega mkate, yaani
kushiriki sakramenti
- d. kusali
Hali ya kushirikiana
mali zote haikuendelea kama utaratibu wa kawaida wa Wakristo wote. Lakini
kutokana na mfano huo zimejitokeza jumuiya mbalimbali katika maisha ya Kanisa.
Maendeleo wakati wa Mitume
Wakati wa maisha ya
Mitume, dhuluma zilizotabiriwa na Yesu zilianza kutoka kwa Wayahudi
wasiomuamini na kutoka kwa watu wengine. Wa kwanza kuuawa alikuwa Stefano, na kati ya Mitume Yakobo Mkubwa.
Kabla ya kufa, wengi kwa
kuuawa, mitume waliweka waandamizi wao, ambao kati yao
walitajwa maaskofu mapadri na mashemasi. Mapema ulipatikana muundo mmoja wa uongozi kila jimbo, yaani askofu mmoja akisaidiwa na mapadri na mashemasi,
badala ya mitindo mbalimbali iliyojitokeza awali. Ni hasa Ignas wa Antiokia ambaye katika barua zake anathibitisha
muundo huohuo kila mahali alipopitia kutoka Siria hadi Italia mwanzoni mwa karne ya 2.
Kusulubiwa kwa Mtakatifu Petro, mchoro wa Filippino
Lippi, 1481-1482 hivi, Firenze, Italia.
Katika barua hizo Ignas
anaonyesha heshima ya pekee kwa Kanisa la Roma akiandika kuwa "linasimamia
upendo". Hiyo ilichangiwa na kwamba mjini Roma ndiko Mitume Petro na Paulo
walipomfia Yesu katika dhuluma ya Kaisari Nero (64-68).
Kati ya mambo muhimu
zaidi yaliyojitokeza wakati wa Mitume ni maandishi mbalimbali ambayo baadhi
yake yalianza kukusanywa na katika karne zilizofuata yalikuja kuunda Agano Jipya kama sehemu ya pili ya Biblia.
Maandishi ya kwanza ni barua zilizoandikwa na Mtume Paulo na wengineo tangu mwaka 50 hivi. Tangu mwaka 65 hivi zilianza
kupatikana Injili, ambazo ni vitabu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu. Luka mwinjili aliiongezea ile ya kwake kitabu cha pili (Matendo ya Mitume) kuhusu uenezi wa Kanisa kutoka Yerusalemu hadi
Roma. Hatimaye kuna kitabu cha Ufunuo ambacho peke yake ni kwa kinabii, kikitumia mtindo
wa kiapokaliptiko.
Uandishi (na halafu uteuzi) wa vitabu hivyo 27 kati ya vingine vyote ni sehemu muhimu
ya maendeleo ya Kanisa chini ya Roho Mtakatifu.
Baada ya hapo vitabu
viliendelea kuandikwa kwa kutetea, kutangaza na kufafanua imani sahihi: hivyo havikukusanywa katika Agano Jipya, lakini
ndivyo mwanzo wa teolojia kama fani maalumu. Tofauti za ufafanuzi huo, kama zile kati ya shule ya
Aleksandria na shule ya Antiokia, ndizo chanzo cha mabishano yaliyochangia mafarakano
makubwa yaliyotokea hasa katika karne ya 5, ingawa kuanzia mwaka 325 mitaguso
mikuu ilikusanya maaskofu wengi kutoka sehemu mbalimbali ili kumaliza migogoro.
Tofauti za lugha na utamaduni, pamoja na utaifa, zilichangia sana mafarakano.
Uenezi katika karne za
kwanza
Dola la Roma lilipofikia
kilele cha uenezi wake mwaka 117.
Ukristo katika karne za
kwanza ulienea haraka katika mabara matatu: Asia Magharibi, Afrika Kaskazini na Ulaya ya Kusini na Magharibi, mbali ya maeneo ya
mbali zaidi kama Nubia, Ethiopia, Persia hadi India.
Siri mojawapo ya uenezi huo ni kuwepo kwa Dola la Roma. Serikali yake ilitawala nchi nyingi kuanzia kando ya Sahara upande wa kusini mpaka Uholanzi na Uingereza wa leo upande wa kaskazini, halafu kutoka milima ya Mesopotamia (leo Iraq) upande wa mashariki mpaka Ureno wa leo upande wa magharibi.
Watu wa Roma walifaulu kujenga dola hilo kubwa katika muda wa karne nyingi. Kwa jumla
walitawala kwa hekima, hivyo wakafaulu kuendelea muda mrefu. Mwanzoni uraia ulikuwa kwa wakazi huru
wa mji wa Roma tu, lakini polepole hata wakazi wa maeneo mengine chini ya Roma
wakapewa haki za
uraia.
Uwepo wa dola hilo
ulisaidia sana uenezaji wa Ukristo. Ingawa watawala wake walijaribu muda mrefu
kupinga imani mpya, kuwepo kwa utaratibu mmoja katika eneo kubwa hivyo
kulisaidia kazi ya mitume na wahubiri wa Injili. Sababu ni
kwamba:
- a. katika eneo kubwa
hakuna mipaka inayoweza kuzuia usafiri na mawasiliano.
Ukisafiri leo kutoka Moroko kuelekea Misri
unavuka mipaka minne, unahitaji paspoti na vibali vingi kila safari.
- b. kulikuwa na
usafiri. Merikebu
zilizunguka pote katika Mediteranea zikibeba mizigo na watu. Waroma pia
walikuwa hodari kujenga barabara
kwenye nchi kavu.
Walihitaji barabara hizo kwa matumizi ya kijeshi lakini zilisaidia pia
mawasiliano mengine ya kiuchumi na usafiri.
- c. Walitumia popote hela
moja, wakawasiliana katika lugha zilezile za Kigiriki
na Kilatini.
Mashariki Kigiriki kilikuwa lugha ya elimu ya juu na ya biashara. Magharibi walitumia
zaidi lugha ya Kilatini. Mpaka leo lugha hizo ni muhimu kama lugha za
elimu. Kwa mfano maneno mengi ya sayansi (fizikia,
kemia, biolojia,
jiografia
n.k.) yanayotumiwa katika lugha mbalimbali, asili ni ileile ya Kigiriki.
Utawala wa Kiroma
ulileta kipindi kirefu cha amani na cha maendeleo ya kiuchumi. Lakini maendeleo hayo
yalijengwa juu ya utaratibu mkali wa unyonyaji wa nchi na mikoa ndani
ya dola. Kila sehemu wakazi walipaswa kulipa kodi. Kama kabila fulani lilijaribu kupinga utawala wa Roma wanajeshi wake
wakafika haraka na kuzima ghasia.
Kwa mfano Wayahudi
walipojaribu kujipatia uhuru tena mnamo mwaka 70 B.K. mji wa Yerusalemu
uliharibiwa kabisa na wakazi wote wakauzwa utumwani. Watoto wa watumwa wakawa watumwa vilevile. Njia nyingine ya
kugeuzwa mtumwa ilikuwa kutolipa madeni. Mdaiwa aliweza
kushtakiwa na aliposhindwa kulipa aliuzwa mwenyewe kama malipo ya madeni yake.
Idadi ya watumwa ilikuwa kubwa: katika mikoa kadhaa ya Dola la
Roma watumwa walikuwa asilimia 20 za wakazi wote. Wengi wao walikuwa na maisha
mabaya, lakini wengine waliweza kupata maendeleo na hata kupewa uhuru na
mabwana wao.
Wale watumwa walifurahia
sana kusikia mafundisho mapya ya kwamba kila mtu ni mtoto wa Mungu na anapendwa
naye. Wakashangaa sana kusikia ya kwamba Yesu Kristo alikufa msalabani kwa
ajili ya dhambi za watu wote, na Mungu hajali sifa au cheo cha mtu.
Wakiingia katika ushirika wa Kikristo waliweza kushangaa wanavyoruhusiwa
kukutana na watu huru na hata matajiri. Ibada za kipagani zilitenga matabaka ya kijamii. Haikuwa kawaida kwa tajiri kusali pamoja na watumishi wake.
Watumwa walisikia katika
ibada za Wakristo nyaraka za Mtume
Paulo zinazokazia usawa kati ya Wakristo wote,
akisititiza ya kwamba Wakristo wote watazamane kama ndugu na viungo vya mwili mmoja. "Maana
katika Roho mmoja tulibatizwa sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, ikiwa tu
watumwa au ikiwa tu huru"(1Kor 12:13)
Ndiyo sababu ujumbe wa
Kristo ulienea hasa kati ya maskini na watumwa. Lakini hata watu wa matabaka ya juu
walivutwa na neno la Injili na mfano mzuri wa maisha ya Wakristo, uhodari wao katika mateso
mbalimbali na utaratibu wao wa kusaidiana.
Dhuluma za muda mrefu
katika Dola lote la Roma (64-313)
Dola la Roma lilikuwa na eneo kubwa sana katika nchi
zinazozunguka Mediteranea katika mabara matatu. Mataifa mengi waliishi chini ya
utawala wake. Utawala huo ulianza kabla ya
Yesu kuzaliwa ukaendelea mpaka karne ya 5 baada ya Kristo upande wa magharibi wa bahari ya Kati na hadi karne ya 15 upande wa mashariki.
Kwa jumla serikali ya Roma iliwaachia watu uhuru waendelee na desturi au mila zao ila tu ilikuwa lazima walipe kodi na kukubali utawala
mkuu.
Watu wengi sana walikuwa
na imani ya miungu mingi. Waliabudu mahekaluni mbele ya sanamu za miungu ile. Walikuwa na imani ya kwamba miungu
ilifanana kiasi na wanadamu ila ni mikubwa na yenye nguvu zaidi na inaishi milele. Vinginevyo waliamini miungu kuwa na tabia nyingi zinazofanana na
tabia za kibinadamu.
Kwa upande mwingine
waliamini ya kwamba hata mtu anaweza kupanda ngazi na kuwa kama mungu akiwa na
sifa za kutosha zinazokubalika mbele za miungu yote na hasa mungu mkuu. Ndiyo
asili ya kumtangaza mtawala mkuu au Kaisari wa Roma kuwa na sifa za kimungu.
Dhuluma ya kwanza
yalitokea mwaka 64 BK, ya mwisho mwaka 309 BK. Katika kipindi
hicho kirefu, vilirudia tena na tena vipindi vya mateso vikifuatana na vipindi
vya amani. Lakini miaka yote Ukristo ulikuwa dini isiyo halali. Kila
mara mateso yaliweza kuanza upya.
Mwishoni mwa karne ya 1 B.K. Kaisari Domitiano alianza kudai ibada za kimungu kwake mwenyewe.
Popote katika eneo kubwa la Dola la Roma watu waliitwa kusimamisha sanamu zake
na kumwabudu. Kwa wakazi wengi jambo halikuwa geni sana maana yake kwao jina
moja liliongezeka katika orodha ya miungu iliyoabudiwa.
Lakini kwa Wakristo tendo hili lilikuwa gumu mno. Imani ya Kikristo hukataa
kuwepo kwa miungu mingi, vilevile hukataza kuiabudu.
Basi, Wakristo walikataa
kuabudu sanamu za Kaisari. Tendo hili lilionekana kama kusaliti serikali. Wakuu
wa mikoa na majimbo walianza kuwaadhibu wale wanaokataa ibada hiyo.
Lakini katika mwendo wa
miaka ibada za sanamu za Kaisari zikaongezeka. Matatizo yakakua, vita vikaongezeka, uchumi na biashara vikashuka chini. Thamani ya
fedha ikapungua. Watu wengi
wakaanza kukata tamaa na kutafuta msaada katika dini mbalimbali. Hivyo
mafundisho ya kidini yalizidi. Hapo wazo lilikua la kuwa anayekana kuwepo kwa
miungu ni hatari kwa umma. Ni mwasi
atakayesababisha hasira ya miungu juu ya watu wote: ni lazima aadhibiwe.
Katika hali hiyo
Wakristo walijenga utaratibu mzuri wa kufundishana
na kusaidiana katika matatizo. Halafu wakakaza sana mafundisho ili waumini
wasimame imara katika matatizo na dhuluma. Wakaendelea kuombea serikali na watu
wote. Wakajitahidi kuonyesha kwa maisha na matendo yao ya kwamba Ukristo ni imani
yenye amani na upendo isiyoharibu umma. Wakakutana katika nyumba za watu binafsi, au kule Roma pia kwenye
"katakombi" yaani makaburini chini ya ardhi kwani polisi haikuruhusiwa kuingia makaburini.
Pia wasomi walijitokeza
kuandika vitabu ili kutetea Ukristo dhidi ya masingizio na chuki ya wengi;
walifafanua imani ilivyo na kuonyesha kwamba maisha ya wafuasi wa Yesu hayaendi
kinyume cha sheria za dola, hivyo dhuluma dhidi yao hazikubaliki.
Uhuru wa dini katika dola
na matokeo yake
Mozaiki ya Konstantino pamoja na bombwe la majengo ya Konstantinopoli.
Mateso ya Wakristo
yaliendelea mpaka mwaka 311. Lakini idadi yao iliendelea
kuongezeka kote katika Dola la Roma. Mwaka 312 B.K. mtu kwa jina Konstantino alitafuta Ukaisari (cheo cha mtawala mkuu)
akishindana na mgombea mwingine. Inasemekana
siku moja aliota ndoto, akaona alama ya msalaba akasikia sauti iliyosema: "Kwa
alama hii utashinda". Hapo aliwaruhusu wanajeshi wake waliokuwa Wakristo
kusali akamshinda mgombea mwingine katika vita. Mwaka 313 B.K. Kaisari
Konstantino akatangaza sheria iliyoruhusu Wakristo kuabudu kwa uhuru. Ukristo ukawa dini inayokubaliwa katika
Dola la Roma.
Kipindi kipya kikaanza
katika historia ya Ukristo. Kwa wengi hali hiyo ilikuwa ajabu la Mungu mwenyewe
aliyemaliza matatizo yao, jinsi Biblia ilivyosema katika kitabu cha Ufunuo. Wakristo wakazidi kujenga na kupamba makanisa kila
mahali. Vilevile ibada zilizidi kupangwa kwa utaratibu mzuri wa matini na
vitendo. Maaskofu waliweza kukutana bila matatizo. Mikutano ya maaskofu
(mitaguso ya ngazi mbalimbali) iliamua juu ya masuala na matatizo
yaliyojitokeza.
Mwaka 325 mkutano wa kwanza wa
Kanisa zima ukafanyika kule Nisea (Asia Ndogo). Wakristo wa nchi mbalimbali walikuwa
wanatofautiana katika maelezo yao juu ya tabia ya Kimungu na ya kibinadamu za
Kristo. Yaani kiasi gani Yesu ni mwanadamu na kiasi gani yeye ni Mungu. Kama alikuwa mwanadamu,
je aliumbwa kama wanadamu wote? Lakini kama anaitwa Mungu ndiye Muumba mwenyewe. Kama yeye ni Mungu - aliwezaje kuumia msalabani?
Au ni Mungu aliyejificha tu katika umbo la mwili, kumbe hakuteswa kweli,
ilikuwa kama igizo tu.
Maaskofu
waliokutana kule Nikea wakapatana juu ya mafundisho ya "Kanuni ya Imani ya
Nisea" yanayosema
"Twamwamini Bwana mmoja, Yesu Kristo, mwana pekee wa Mungu, mwana wa azali
wa Baba, yu Mungu kutoka kwa Mungu, yu nuru kutoka kwa nuru, yu
Mungu kweli kutoka kwa Mungu kweli, Mwana wa azali, asiyeumbwa; aliyeshuka
kutoka mbinguni kwa ajili yetu wanadamu na kwa wokovu wetu; akatwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu katika Bikira Maria, akawa mwanadamu; akasulibiwa kwa ajili yetu zamani
za Pontio Pilato; aliteswa, akazikwa, siku ya tatu akafufuka kama
yanenavyo maandiko matakatifu; akapaa mbinguni, ameketi mkono wa kuume wa Baba;
kutoka huko atakuja tena kwa utukufu kuwahukumu walio hai na wafu; na ufalme wake hauna
mwisho." Maneno hayo hutumika mpaka leo katika ibada za kikristo (pamoja
na "kanuni ya Imani ya
Mitume").
Baada ya Konstantino
Kanisa lilikua sana. Watu wengi walijiunga na Ukristo. Zamani ilikuwa hatari
kuwa Mkristo, kumbe sasa imekuwa faida, hata watu wenye imani
haba waliosita zamani wakajiunga na Kanisa. Baada ya Konstantino makaisari
wenyewe walikuwa Wakristo.
Mwaka 380 mambo yaligeuka kinyume
cha hali ya awali: serikali ya Kaisari Theodosi I ilitangaza Ukristo wa Kikatoliki kuwa dini rasmi ya dola. Kanisa lilipewa hela na serikali. Kaisari
mpya aliwekwa wakfu katika ibada kanisani. Kabla yake Armenia ilikuwa nchi ya
kwanza kupokea Ukristo kama dini ya taifa (301). Ushindi huo ulifanya wengi
watamani vyeo ndani ya Kanisa, kwa kuwa viliendana sasa na heshima na mali:
hivyo ubora ulipungua.
Mwishoni serikali
ilianza kufunga na kubomoa mahekalu ya Wapagani. Asiyekuwa Mkristo alianza kupata matatizo.
Ilitokea mara kadhaa ya kwamba walimu wapagani walipigwa na kuuawa na umati wa Wakristo.
Katika miji mbalimbali
watu walianza kuwatesa hata kuwaua Wayahudi wakiwashutumu kwamba ndio waliomwua
Yesu. Sisi tunaweza kushangaa jinsi hali hiyo ilivyoweza kutokea. Yesu mwenyewe
alikuwa Myahudi na mpaka msalabani alifuata taratibu za taifa la Israeli. Mtume Paulo alifundisha ya kwamba Wayahudi hawawezi kupoteza
ahadi na agano la Mungu kwao hata wakimkataa Yesu Kristo.
Bila shaka Yesu hakutaka
watu walazimishwe kujiunga na Kanisa lake. Lakini katika mawazo na uzoefu wa
Waroma dini na serikali zilikuwa kitu kimoja. Ikiwa sasa Kaisari, wakubwa wa
serikali na watu wengi walikuwa Wakristo walihisi ni kawaida kwa wote kufuata
dini hiyo. Kumbe Kanisa lilianza kutumiwa na wanasiasa kwa malengo yao ya kidunia.
Atanasi na mababu wengine
wa Mashariki
Ni huko Aleksandria
ulikotokea uzushi mkuu wa historia yote ya Kanisa: padri Ario alikanusha umungu wa
Yesu. Mafundisho yake yalienea kote mashariki na kuungwa mkono na watawala kwa
nguvu za dola. Lakini ni Kanisa la Misri lililompinga kwa uimara wa pekee, bila
kujali dhuluma.
Picha takatifu ya Atanasi wa
Aleksandria, Askofu mkuu (Patriarki) wa Aleksandria na mtetezi mkuu wa umungu wa Yesu Kristo.
Kati ya wote,
alijitokeza Atanasi wa
Aleksandria anayeitwa Mkuu (Aleksandria, Misri, 295 hivi - Aleksandria, 2 Mei 373), Patriarki wa Kanisa Katoliki la madhehebu ya Misri kati ya mitaguso mikuu miwili ya kwanza: Nisea I (325) na Konstantinopoli
I (383).
Maisha yote ya Atanasi
yalihusika na juhudi kubwa za Kanisa kwa ajili ya kufafanua na kutetea imani sahihi juu ya Yesu na juu ya Utatu hata akaitwa mapema
“nguzo ya Kanisa” (Gregori wa
Nazianzo).
Pamoja na kupatwa na vurugu nyingi maishani (hasa
kufukuzwa mara tano kutoka mji wake), Atanasi aliandika sana: hotuba na barua, lakini pia vitabu juu ya imani, historia, ufafanuzi wa Biblia, pamoja na maisha ya Kiroho. Kitabu chake maarufu kimojawapo kinahusu umwilisho wa Neno; humo aliandika kuwa Neno wa
Mungu “alifanyika mtu ili
sisi tuweze kufanywa Mungu”.
Lakini kitabu ambacho
kilienea na kuathiri zaidi maisha ya Kanisa labda ni "Maisha ya
Antoni" ambacho kilieneza
umonaki haraka mashariki na vilevile magharibi.
Mbali ya Atanasi, katika
karne ya 4 na ya 5 Kanisa la
Mashariki lilizaa mababu wengine
bora: Basili Mkuu (Kaisarea wa Kapadokia, leo Kayseri, nchini Uturuki, takriban 329 – Kaisarea wa
Kapadokia, 1 Januari 379, Gregori wa
Nazianzo (Arianzo, leo Güzelyurt nchini Uturuki, 329 - Arianzo, 25 Januari 390) na Yohane Krisostomo (Antiokia wa Siria, leo Antakya, nchini Uturuki, 347 hivi - Comana
Pontica, Uturuki, 14 Septemba 407). Wote walikuwa maaskofu na wote walipitia kwanza umonaki.
Ndio waliofafanua kwa dhati zaidi mafumbo ya Ukristo, kuanzia lile la Utatu
mtakatifu, na ndio waliobaki kielelezo kwa liturujia na uchungaji bora.
Umonaki - maisha ya pekee
Watawa ni Wakristo
walioamua kuishi kwa njia ya pekee. Leo hii mashirika ya watawa ni maelfu. Kwa
kawaida kila shirika lina mkazo wake wa pekee, kama vile maisha ya kimya katika sala au huduma
za upendo: hospitali, nyumba za mayatima, ufundishaji, uinjilishaji, misheni, au n.k. Hivyo mtawa anaweza kuwa na maisha
ya kutotoka katika nyumba ya shirika lake au anaweza kuishi kati ya Wakristo na
wasio Wakristo akiwatolea huduma zake.
Mara nyingi tumezoea
kuwaona katika Kanisa Katoliki. Lakini wako vilevile kati ya Waanglikana na Walutheri, ingawa si wengi. Ulaya wako hata masista Wamoravian na Wabaptisti.
Mtawa amepokea katika maisha yake ushauri wa mtume Paulo (ambaye
hakuoa): «Nawaambia wale wasiooa bado, Ni heri wakae kama nilivyo» 1Kor 7:8. Yesu mwenyewe
aliwahi kueleza ya kwamba watakuwepo wale watakaochagua maisha ya pekee bila familia na uzazi kwa ajili ya Ufalme wa Mungu (Mt 19:12: "Wako matowashi waliojifanya kuwa matowashi kwa ajili ya ufalme wa
mbinguni»).
Kwa jumla watawa ni
kundi muhimu linalosaidia sana kazi ya kiroho katika Ukristo. Wako huru kuliko
wengine kujitolea katika huduma za Kanisa, kwani hawalazimiki kufikiria maendeleo ya watoto wao. Watawa wanaweza kuishi peke yao lakini mara nyingi
wanajiunga na shirika au jumuiya na kuweka nadhiri za useja mtakatifu, ufukara na utiifu.
Asili ya jumuiya hizo
iko Misri. Katika karne ya 3 mateso yalizidi chini ya serikali ya Waroma
Wapagani. Wakristo wengine walijificha jangwani wakiogopa kulazimishwa kutoa sadaka kwa sanamu. Wengine waliona jinsi familia yao ilivyouawa katika
dhuluma za kidini. Wengine karibu walikata tamaa wakiona Wakristo wengine
walivyokana imani kwa kuogopa mateso. Kumbe wengine hawakuona raha tena katika maisha ya
kawaida, wakajitenga na dunia wakaenda porini kuishi kule maisha ya kufunga na kusali.
Watawa hao waliitwa kwa
jina la Kigiriki "wamonaki" (monos= moja; monakos= anayekaa peke yake).
Walikaa jangwani katika maeneo yaliyokuwa mbali na miji na vitovu vya utawala
wa Kiroma. Lakini waliheshimiwa sana na wananchi wa kawaida. Walitumia muda
mwingi wakisali na kusoma Biblia. Watu wakazoea kuwaendea kuomba ushauri wao
katika mambo ya kiroho au maisha kwa ujumla, kuombewa katika magonjwa n.k. Wengine walizoea kupokea zawadi za wanavijiji wakaelekea maisha ya kuombaomba.
Antoni abati anaitwa
baba wa umonaki kwa jinsi alivyovuta wengi kwenye mtindo huo mpya wa maisha ya kiroho katika Ukristo.
Wamonaki wa kwanza
walikaa kila mmoja peke yake bila kushirikiana. Antoni wa Misri alikuwa mmojawao, naye akaona umuhimu wa kuweka
utaratibu fulani kati ya wamonaki wenzake.
Mwanafunzi wake Pakomi aliendeleza mkazo wake akawaunganisha wamonaki mahali pamoja
akawapa utaratibu wa kazi na sala. Katika utaratibu huo kila mmonaki (pia
masista katika mashirika yao) hutoa ahadi au nadhiri tatu: 1.
Useja mtakatifu: atachagua maisha bila ndoa; badala yake kujiunga
na shirika la wenzake kama familia ya kiroho. 2. Ufukara: ataacha mali yake ya binafsi na
hatatafuta tena utajiri wa kidunia. 3. Utii: atamtii mkuu wa shirika hilo
aliyechaguliwa kati yao (huitwa "Abba/Abati") na kutii
taratibu za ushirika wake.
Utaratibu huo wa umonaki
ulienea haraka: watawa wakaanza kukaa na kufanya kazi pamoja ili kujipatia
mahitaji yao wenyewe. Baadaye vituo vya wamonaki vilikuwa vitovu vya elimu
ambapo sehemu ya wamonaki walisoma, kuandika (au kunakili) vitabu, kuanzisha shule n.k.
Tangu karne IV umonaki ulijitokeza magharibi pia: huko Italia, Ufaransa na Hispania kulikuwa na monasteri za kike na za kiume
zilizosimamiwa na maaskofu watakatifu. Kati yao wa kwanza kupitia umonaki ni Martino wa Tours (316-397).
Hasa maandishi ya Yohane Kasiano (360-435) yalieneza hekima ya wamonaki wengi wa mashariki alioongea
nao.
Augustino wa Hippo (354-430), babu wa Kanisa muhimu kuliko wote, baada ya kuongoka na kutembelea
baadhi ya monasteri, alirudi Afrika Kaskazini aanzishe maisha ya pamoja. Kwanza
aliishi na walei wenzake, halafu akiwa askofu aliishi na mapadri wake,
akawashirikisha utajiri wake wa akili na roho ili wafanye vizuri utume. Katika kanuni yake,
iliyotumika kwa wanawake pia, umoja uliwekwa kuwa lengo lenyewe la utawa, si
jambo lake mojawapo tu. Hata yeye aliathiri sana maisha ya kitawa ya magharibi
kote.
Benedikto wa
Nursia (480-547) ndiye aliyeunda
umonaki wa magharibi kwa namna ya kudumu hasa kwa njia ya kanuni aliyoitunga
polepole, kutokana na mang’amuzi yake, Kanuni ya Mwalimu asiyejulikana na mafundisho ya Bazili na mababu
wengine wa jangwani.
Kanuni yake iliunganisha
vizuri maelekeo mawili ya umonaki wa zamani: kumtafuta Mungu kwa juhudi
upwekeni na kuishi kwa umoja. Sifa yake nyingine ni mchanganuo mzuri wa sala na kazi mbalimbali ambazo ziliokoa elimu ya zamani na
kufufua uchumi wa Ulaya Magharibi baada ya makabila ya Kijerumani
kuvuruga kote. Yeye alidumisha ubaba wa Kiroho katika jumuia nzima: ndiyo maana
abati ana nafasi ya pekee na ya kudumu kwa wamonaki, ambao aliwafafanua kuwa
watu “wanaoishi katika monasteri na kutii kanuni moja na abati mmoja”. Kwake
monasteri ni shule ya utumishi wa
Bwana, ambapo abati ndiye
mwalimu, na kanuni ndiyo kitabu. Kinyume cha watawa wazururaji wa zamani hizo
za misusuko, Benedikto alidai udumifu katika monasteri.
Kutokana na kila
monasteri kujitegemea, Wabenedikto wakapata sura tofautitofauti bila ya kuachana na
kanuni. Ushirikiano kati ya monasteri mbalimbali unategemea asili yake na
mitindo yake.
Kati ya aina nyingine za
umonaki wa magharibi inakumbukwa hasa ile ya Wakristo wa
Kiselti (Ulaya visiwani). Hao hawakuwa
na majimbo bali walimtegemea askofu-abati wa monasteri ya jirani
na kufuata desturi za kimonaki, hasa maisha magumu ya malipizi na maungamo ya
mara kwa mara. Kutoka huko wamonaki wengi walihamia Ulaya bara kama wasafiri wa
Kristo na wamisionari wakieneza desturi hizo. Kati yao anasifiwa hasa Kolumbani (540-615).
Hatimaye wakaja kukubali
kanuni ya Benedikto pamoja na desturi za Kanisa la Roma.
Wamonaki wengine pia
walichangia sana uenezaji wa Ukristo Ulaya, k.mf. Augustino wa
Canterbury (+605), aliyetumwa Uingereza na Papa Gregori I (540-604), mmonaki wa kwanza kufikia Upapa, halafu Bonifas (672-754), mtume wa Ujerumani na mfiadini.
Frumensyo, mmisionari wa
ufalme wa Aksum (Ethiopia ya leo).
Wamisionari Wamisri katika
mabara matatu
Panteno wa Chuo cha
Aleksandria alikwenda India kuhubiri Injili. Wamisionari wa Kanisa la Misri
walianzisha Kanisa katika Sudan na Ethiopia za leo.
Hata sehemu mbalimbali
za Ulaya zinakumbuka wamisionari kutoka Afrika waliohubiri huko Injili wakati wa Dola
la Roma. Askari Wamisri katika jeshi la Roma walikaa miaka mingi Uswisi na kwingineko. Kati yao kulikuwa na Wakristo waliohubiri
huko Injili kwa mara ya kwanza.
Kule Ireland Wamisri waliunda monasteri mnamo mwaka 500 na kufundisha Injili.
Waireland wanafunzi wa Waafrika hao ndio wainjilisti wa Ujerumani na Uholanzi baadaye.
Augustino na mababu wengine
wa Magharibi
Augustino wa Hippo
akibatizwa na askofu Ambrosi, mwaka 387.
Augustino (Thagaste, leo Souk Ahras nchini Algeria, 13 Novemba 354 – Hippo, leo Annaba, Algeria, 28 Agosti, 430) alikuwa mtawa, mwanateolojia, padri na hatimaye askofu mkuu wa Hippo.
Ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki katika Afrika Kaskazini mwanzoni mwa karne ya 5.
Katika historia yote Augustino ni kati ya watu wenye akili kubwa zaidi, iliyopenya
masuala yoyote, pamoja na ubunifu wa ajabu na moyo mpana. Aliunda upya
teolojia ya mapokeo akiitia chapa yake mwenyewe.
Kati ya mababu wa Kanisa, ndiye aliyetuachia maandishi mengi zaidi, kuanzia
yale maarufu sana yanayoitwa "Maungamo", kwa kuwa humo
miaka 397-400 aliungama sifa za Mungu na ukosefu wake mwenyewe kwa
kusimulia alivyoishi hadi miaka ya kwanza baada ya kuongoka.
Kila wakati ulifurahia
zaidi kitu fulani katika Augustino. Siku hizi anapendwa hasa kwa unyofu wake katika
kujichunguza na kutoa siri zake, akikiri makosa yake na kuyageuza yawe sifa kwa Mungu.
Uzingatifu wake wa fumbo
la nafsi yake ambamo fumbo la Mungu limefichama, ni mzuri ajabu
kiasi cha kubaki hata leo kilele cha kujitafiti kiroho. Aliandika: “Usiende
nje, rudi ndani mwako; ukweli unakaa katika utu wa ndani; na ukiona umbile lako ni geugeu, panda juu yako. Lakini kumbuka, unapopanda
juu yako, unapanda juu ya roho inayofikiri. Basi, ufikie pale mwanga wa akili
unapowaka”. Tena: “Naona ni lazima wanadamu warudishiwe tumaini la kupata
ukweli”.
Posidi, mtu wa kwanza
kuandika habari za maisha ya Augustino (kwa Kilatini, “Vita Augustini”),
alisema “waamini wanamkuta daima hai” katika vitabu vyake. Kweli havionyeshi
imepita miaka 1600 tangu viandikwe: humo anaonekana kama rafiki yetu wa wakati
huu anayesema nasi kwa imani isiyozeeka.
Augustino mwenyewe
aliviorodhesha 1,030, ambavyo si vyote.
Kazi yake kubwa haikuwa
kuandika maelezo juu ya vitabu na maneno ya Biblia yenyewe alivyofanya Origene, bali kuingiza Biblia katika mazingira ya kiroho, ya
kijamii na ya kisiasa ya wakati wake. Hapo, akitegemea mamlaka ya imani
inayodhihirishwa na Biblia, maandiko ya Kimungu yasiyoweza kukosea yakisomwa
katika mapokeo ya Kanisa lililoorodhesha vitabu vinavyoiunda, aliuliza maswali
na kutoa majibu yaliyo muhimu mpaka leo.
Akilinganisha imani na
akili, Augustino alichunguza hasa fumbo la Mungu (Ukweli mkuu na Upendo wa milele, unaohitajiwa na roho ili kupata amani) na la binadamu (ambaye ni sura na mfano wa Mungu).
Huyo katika roho yake isiyokufa, bado ana uwezo wa kuinuka hadi kwa Mungu,
ingawa uwezo huo umeharibiwa na dhambi na unahitaji kabisa kurekebishwa na neema.
Teolojia yake kuhusu Utatu inaendeleza ile ya
mapokeo na kuathiri Kanisa lote la Magharibi. Augustino anaweka wazi kuwa Nafsi tatu ni sawa lakini
hazichanganyikani; tena anajaribu kuufafanua Utatu kwa kutumia saikolojia (mfano wa kumbukumbu, akili na utashi). Kitabu muhimu zaidi
kuhusu Utatu (kwa Kilatini kinaitwa “De Trinitate”) alikiandika miaka 399-420. Kilichukua muda mrefu
kwa kuwa alisimamisha uandishi wake miaka minane “kwa sababu ni kigumu mno na
nadhani wachache tu wanaweza kukielewa; basi kuna haraka zaidi ya kuwa na vitabu
vingine tunavyotumaini vitafaidisha wengi”.
Hivyo alielekeza nguvu
zake kutunga vitabu vya katekesi kwa wasio na elimu (hasa “De Catechizandis
Rudibus”). Akijibu hoja za Wadonati, ambao walitaka Kanisa la
Kiafrika na kuchukia mambo ya
Kilatini, alikubali kurahisisha lugha hata kufanya makosa ya kisarufi kusudi wamuelewe zaidi akifafanua umoja wa
Kanisa ulivyo muhimu kwa
mahusiano na Mungu na kwa amani duniani.
Papa Gregori I,
aliyeitwa Mkuu kutokana na umuhimu wake katika historia ya Kanisa.
Hasa hotuba zake,
zilizoandikwa na wengine wakati alipokuwa anazitoa kwa watu akiongea nao
kirahisi, zimechangia kueneza ujumbe wake. Tunazo bado karibu 600, lakini zilikuwa zaidi ya
3,000.
Pia alifafanua upya
imani kuhusu umwilisho wa Mwana wa Mungu, akiwahi kutumia misamiati iliyokuja kupitishwa na Mtaguso wa
Kalsedonia (451): uwepo wa hali mbili
(ya Kimungu na ya kibinadamu) katika nafsi moja. Lengo la umwilisho lilikuwa wokovu wa watu, hivyo hakuna anayeweza kuokoka bila Kristo
aliyejitoa sadaka kwa Baba, “akitakasa, akifuta na kutangua makosa yote ya
binadamu, akiwakomboa kutoka mamlaka ya shetani”.
Mbali ya Augustino, Kanisa la
Magharibi katika karne ya 4 hadi
ya 6 lilizaa mababu wa Kanisa wengine walioathiri moja kwa moja imani, maadili,
liturujia na uchungaji: kwanza askofu Ambrosi (Trier, leo nchini Ujerumani, 340 hivi - Milano, Italia, 4 Aprili 397), ambaye ndiye aliyembatiza Augustino, halafu padri Jeromu (Strido, leo nchini Korasya 347 - Bethlehemu, Israeli, 420) na Papa Gregori I (Roma, Italia, 540 hivi – Roma, 12 Machi 604) .
Mafarakano ya mataifa
mazima na umoja wa Kanisa
Katika karne ya 4 dola kubwa la Roma lilianza kupata matatizo.
Makabila kutoka Ulaya kaskazini yalianza kuhamia kusini. Hali ya hewa kule ilibadilika: watu wakakosa chakula cha kutosha. Hiyo ilisababisha kipindi kirefu cha vita na vurugu. Waliohama wakawasukuma
majirani wao walioanza kuhamahama vilevile. Matembezi hayo yalifika kwenye
mipaka ya Dola la Roma. Waroma walishindwa kuwazuia kutokana na uzazi wao kupungua na
polepole mataifa yale yasiyostaarabika yakaingia katika eneo la dola na kutwaa
mikoa mbalimbali. Waroma wakatumia hela nyingi sana kwa ajili
ya jeshi lao lakini bila kufanikiwa.
Mwaka 395 Kaisari akagawa dola la
Roma katika sehemu mbili, yaani Magharibi (makao makuu Roma) na Mashariki
(makao makuu Bizanti). Mpaka wa katikati ulifuata tofauti ya utamaduni
kati ya maeneo yaliyotumia zaidi lugha ya Kigiriki na maeneo yaliyotumia zaidi
Kilatini. Ugawaji huo ulikuwa na kusudi la kurahisisha utawala na utetezi.
Lakini mwaka 410 makabila yasiyostaarabika yaliteka na kuharibu mji wa
Roma. Mwaka 476 Kaisari wa mwisho wa Magharibi aliuawa.
Ubatizo wa Chlodwig, mfalme wa Wafaranki,
uliingiza kabila hilo kubwa katika Kanisa Katoliki. Tukio lilivyochongwa katika
pembe ya ndovu (karne ya 9).
Makabila ya Kijerumaniki yalichukua utawala katika sehemu zote za Ulaya mpaka
Afrika Kaskazini. Dola la Roma la Magharibi likagawanywa katika nchi nyingi
ndogondogo. Kila sehemu makabila toka Kaskazini yalitawala kama tabaka dogo la
juu wakiwategemea wenyeji kuendelea kuzalisha mali na wenyewe kupokea kodi zao.
Lakini utaratibu, mawasiliano na usalama viliharibika kabisa. Uchumi na
utamaduni vilirudi nyuma. Umoja wa kisiasa uliharibika, badala yake yalitokea
maeneo mengi madogo ya kikabila. Ulaya Magharibi ilibaki na chombo kimoja tu
chenye umoja uliovuka mipaka: Kanisa Katoliki chini ya uongozi wa Askofu wa
Roma. Ndiye aliyetunza urithi wa jina kubwa la Roma akiheshimiwa pia kama mwandamizi wa Mtume Petro. Yeye kama mchungaji mkuu alilazimika kuwajibika ili
kuokoa jahazi. Ndivyo walivyofanya hasa Papa Leo I na Papa Gregori I. Wafaranki, kabila kubwa la Kigermanik waliwahi kujiunga na Kanisa Katoliki
wakawa msaada mkubwa kwa Mapapa. Isipokuwa, kwa kuwaachia watawale Italia ya Kati, walisababisha Papa aanze kuwa kama mfalme wa dunia
hii, jambo lililoathiri sana majukumu yake ya kiroho hadi mwaka 1870.
Kwa sababu elimu
ilishuka chini popote Ulaya Magharibi, ni ndani ya Kanisa tu kwamba mapadri na
wamonaki wakaendelea kusoma na kutunza elimu ya kale. Kwa juhudi za wamonaki Wabenedikto na wengineo, ustaarabu wa kale uliokolewa katika
vitabu vyake na uinjilishaji uliendelea katika Ulaya ya Kati. Ni kwamba watu kutoka Ulaya kaskazini hawakuwa
wasomi. Hivyo watawala wao walitegemea watu wa Kanisa wakitaka kuandika au
kusomewa barua au mikataba. Polepole watawala wapya pamoja na makabila
yao wakapokea Ukristo. Walifundishwa kwamba mfalme hupewa madaraka yake na Mungu, hivi anapaswa kufuata shauri la
Kanisa ambalo linatangaza mapenzi ya Mungu. Kutokana na hali hiyo ya
kiutamaduni na ya kiroho Kanisa lilikuwa na athari kubwa sana.
Utamaduni na utaratibu
wa kale viliendelea katika sehemu ya mashariki ya dola. Mtawala wa Bizanti
akaendelea kutumia cheo cha Kaisari wa Roma. Taratibu za siasa, serikali na
uchumi ziliendelea. Makaisari wengine wa Mashariki walijaribu kutawala tena
eneo lote la zamani hata upande wa magharibi lakini ilishindikana. Kanisa huko
liliendelea kuwa dini rasmi ya serikali. Kwa sababu serikali ilikuwa yenye
nguvu zaidi, Kanisa lilikuwa chini yake. Kaisari alikuwa mlezi mkuu wa kanisa.
Ndiye aliyemthibitisha Askofu Mkuu wa Bizanti na maaskofu wa dayosisi.
Kwa sababu ya matatizo
ya ndani ya dola la Roma la Mashariki (= Bizanti) mafarakano yalitokea katika
nchi za Misri na Siria zilizokuwa chini ya Kaisari wa Bizanti. Katika nchi
hizo, baada ya mtaguso wa
Kalsedonia (451), sehemu kubwa ya
Wakristo walijitenga na kuendelea kama Kanisa la kitaifa. Kanisa la Misri lilifuatwa na Kanisa la Nubia na la
Ethiopia. Kwa namna hiyo makanisa hayo ya kale ya Afrika yameendelea hadi leo
kwa namna ya pekee. Ilitokea vilevile kwa Kanisa la Siria, la Armenia n.k.
Hawakuwa tena waamini binafsi walioshika msimamo tofauti na ule rasmi, bali
Wakristo karibu wote wa nchi fulani chini ya maaskofu wao waliojitenga na umoja
wa Kanisa.
Kanisa la Mashariki kwa
Dola la Roma lilipofikia kilele cha uenezi wake.
Kabla ya hapo, kufuatana
na mtaguso wa Efeso (431), Wakristo wa nje ya Dola la Roma upande wa mashariki
(Mesopotamia, Uajemi n.k.) walikuwa wameshajitenga na kuendeleza maisha ya
Kikristo chini ya dhuluma za Dola la
Uajemi, huku wakieneza habari
njema mbali zaidi na zaidi, hadi China na Indonesia.
Kumbe Kanisa Katoliki
liliendelea tofautitofauti katika sehemu hizo za mashariki na magharibi za Dola
la Roma. Wakristo wa Magharibi (nchi za Ulaya magharibi pamoja na Afrika
kaskazini) wakafuata uongozi wa Papa yaani Askofu wa Roma. Kanisani walitumia
lugha ya Kilatini. Wakristo wa Mashariki wakafuata maaskofu wao waliokuwa chini
ya serikali ya Kaisari wa Bizanti. Kama lugha walitumia Kigiriki.
Pamoja na magomvi katika
uenezaji wa Ukristo kwenye maeneo ya Ulaya yaliyokuwa bado ya Kipagani (hasa
kati ya Waslavi), tofauti hizo zilisababisha desturi na mawazo yaliyozidi
kutofautiana. Ziliweka msingi wa kutokea kwa madhehebu mawili makubwa yanayoendelea mpaka leo yaani Kanisa
Katoliki la Kiroma (magharibi) na Kanisa la
Kiorthodoksi (mashariki).
Baada ya mafarakano ya
muda (hasa la miaka 863-867 kuhusu upatriarki wa Fosyo), mwaka 1054 wajumbe wa Askofu wa
Roma walimtembelea Askofu Mkuu wa Bizanti. Walianza kupingana vikali na
mwishoni wakalaaniana. Tangu mwaka ule farakano lilikuwa rasmi kati ya Ukristo
wa Magharibi na Waorthodoksi.
Ilichukua miaka mingi
kushinda laana hizo. Mwaka 1967 Papa Paulo VI wa Roma alimtembelea Askofu Athenagoras wa Bizanti
(leo: Istanbul) wakapatana tena na kusameheana makosa ya zamani.
Uelewano umeanza kujengwa pia kati ya makanisa yaliyofarakana zamani na Bizanti
kama vile Wakopti na Wasiria.
Uenezi wa Uislamu
ulivyorudisha nyuma Ukristo na umisionari wake
Uenezi wa Uislamu hadi
mwaka 661.
Mwaka 622 B.K. Mwarabu kwa jina Muhammad alikimbia mji wa Maka. Wakazi wa Maka
walikuwa wamemkasirikia Muhamad. Kwa miaka 12 aliwahi kuhubiri juu ya ufunuo aliodai ameupokea kutoka kwa malaika wa Mungu. Alipinga desturi na maadili ya watu wa mji wake. Akatangaza "Uislamu" yaani imani katika Mungu mmoja aliyetoa amri zake kwa wanadamu.
Kumbe viongozi wa Maka waliona anaharibu dini ya jadi ya kuabudu sanamu za miungu. Makabila ya Waarabu
walikuja kila mwaka kuabudu sanamu za Maka katika jengo la Kaaba. Wakati wa ziara hizo
biashara ya Maka ilistawi vizuri sana. Muhammad alionekana anaweza kuwazibia
viongozi hao riziki wakakasirika wakajaribu
kumwua lakini akakimbia.
Akisafiri pamoja na
marafiki wachache akaelekea mji wa Jathrib (leo Madina). Pale alipokewa vizuri, na wenyeji wakamwamini. Habari
zake zikaenea haraka pande zote za Uarabuni. Makabila mbalimbali ya Waarabu
walimwunga mkono. Akawa kiongozi wao kidini, kijeshi na kisiasa. Mwaka 630 akawashinda watu wa
Maka kivita lakini alionyesha busara kwa kuwahurumia mradi wajiunge na Uislamu.
Alipokufa mwaka 632 B.K. karibu Waarabu
wote waliunganishwa chini ya bendera ya imani mpya ya Uislamu. Katika jina la Mungu (kwa Kiarabu: Allah) wafuasi wake wakashambulia maeneo jirani ya Waroma wa
Bizanti na ya Waajemi.
Dunia nzima ilishangaa
kusikia habari ya kwamba Waarabu kutoka jangwani walifaulu kuwashinda wanajeshi
hodari wa Kiroma na wa Kiajemi. Lakini katika miaka iliyotangulia dola hizo
mbili kubwa ziliwahi kupigana vita virefu na vikali. Wananchi wote na wanajeshi
wao walichoka. Uchumi ulidhoofika baada ya miaka 20 ya vita.
Tena wenyeji wa Misri na
Shamu (Siria) walisikitikia utawala wa Kaisari wa Bizanti. Walidai tangu muda
mrefu uhuru wa kitaifa lakini wakagandamizwa. Waarabu walikutana na maadui
waliokosa nguvu. Hivyo uenezaji wao ulikuwa wa haraka sana.
Ushindi wa Wafaranki juu
ya Waislamu huko Tours (732) ulizuia uenezi wa dini hiyo Ulaya Magharibi.
Mwaka 636 Waarabu wakawashinda
Waroma wa Bizanti kule Shamu wakateka Dameski na Yerusalemu. Mwaka uleule wakawashinda Waajemi
kule Mesopotamia (Iraq). Mwaka 639 wakaingia Misri na kuteka Aleksandria miaka mitatu baadaye. Mwaka 642 waliteka sehemu kubwa
ya Uajemi wenyewe. Miaka 670/696 waliteka mkoa wa "Afrika" ya Kiroma pamoja na
Karthago (Tunisia ya leo). Mwaka 711 wakavuka mlangobahari na kuingia Hispania (Ulaya Kusini). Walifika mpaka Ufaransa wakarudishwa na
wenyeji mwaka 732 lakini walitawala
sehemu za Hispania kwa karne saba zilizofuata.
Walishindwa kuteka
Bizanti yenyewe iliyoendelea kutawala Asia Ndogo lakini wakaenea Asia ya Kati. Mwaka 751 walipigana na jeshi la China. Na kule Mashariki
wakasimama ana kwa ana mbele ya wanajeshi wa Wahindi na Wachina. Miaka mia moja baada ya kifo cha Muhamad
sehemu kubwa ya dunia kati ya Moroko na Bonde la Indus ilikuwa chini ya bendera
ya Uislamu.
Utawala wa Kiislamu
ulifikia nchi hizo kwa njia ya vita. Mwanzoni walikuwa Waarabu kadhaa tu:
walichukua madaraka ya serikali kuu na kujenga makambi ya kijeshi katika kila
nchi. Vijana wa Kiarabu walifuata baba zao wakiitikia wito wa
dini uliokuja pamoja na nafasi ya kupata maisha nafuu. Walifundishwa kwamba
ikiwa watakufa vitani watapokewa na Mungu kama mashahidi wa imani na kuingia Paradiso moja kwa moja. Lakini wasipokufa vitani watakuwa
matajiri wakitawala nchi mpya na kupokea kodi za wenyeji wasio
Waislamu. Imani ya aina hii iliwapa nguvu kweli na iliendelea kuvuta Waarabu
wengi kutoka kwao kuhamia Afrika Kaskazini na Asia ya Kati.
Chini ya utawala wa
Waarabu Waislamu, wenyeji waliruhusiwa kuendelea na desturi zao lakini hawakuwa
na haki zote za uraia. Wasio Waislamu walitozwa kodi kubwa ya pekee. Mahakamani hawakuweza kushuhudia dhidi ya Mwislamu,
walilazimishwa kuvaa nguo za pekee tofauti na Waislamu, walikataliwa kupanda farasi, kujenga makanisa mapya, au kutumia kengele makanisani. Waislamu walipata kipaumbele katika mambo yote.
Hivyo polepole wenyeji walianza kutumia lugha ya Kiarabu pamoja na kujiunga na
Uislamu. Bila shaka wazazi wengine walitumaini kuwasaidia watoto wao wapate
maendeleo maishani wakifuata dini ya watawala.
Masharti ya kujiunga na
Uislamu yalikuwa rahisi sana. Hakuna mafundisho magumu, mwanzoni inatosha
kutamka "shahada" ya Kiislamu ambayo ni fupi sana: As-haddu
inna la ilaha ila allah, wa Muhamad rasul ullah. (Nakiri ya kwamba Mungu
ndiye mmoja tu, na Mohamad ni mtume wa Mungu). Lakini baadaye haikuwezekana
kurudi katika Ukristo maana sheria ya Kiislamu iliruhusu Mkristo kugeuka
Mwislamu lakini ilikataza kwa adhabu ya kifo Mwislamu asitoke katika imani hiyo na kufuata dini
nyingine.
Kwa kawaida Wakristo
hawakulazimishwa kuacha imani yao. Viongozi wa Waarabu washindi walifanya
mikataba na maaskofu wa Kikristo katika maeneo waliyoyateka. Wakristo
waliahidiwa ulinzi wa makanisa yao
wakiambiwa wanaweza kuendelea na mila na desturi walivyozoea.
Lakini vipindi vya
kulazimisha vilitokea tena na tena, hasa baada ya mataifa mapya kuwa Waislamu. Waarabu
wenyewe walionyesha ustahimilivu zaidi kwa wenye imani
nyingine (Wakristo, Wayahudi, Wafuasi wa dini ya Uajemi n.k.). Lakini Waturuki, Waajemi na Wamongolia baada ya kuwa Waislamu walikuwa wakali. Hasa vipindi
vya vita kati ya Wakristo kutoka Ulaya na Waarabu viliongeza uchungu kwa Wakristo waliokuwa
chini ya utawala wa Kiarabu. Katika vipindi hivyo Wakristo chini ya Waislamu
waliweza kuangaliwa kama wasaliti na kuteswa, makanisa yao kubomolewa au
kugeuzwa misikiti, n.k.
Pamoja na Wakristo wengi
kugeuka Waislamu, umisionari kwa mataifa mengine ya Afrika na Asia ulizuiwa na
dola la Kiislamu lililozunguka karibu pande zote nchi za Kikristo.
Athari nyingine ya
Uislamu katika historia ya Kanisa, hasa la Mashariki, ilikuwa dharau kwa sanamu
na picha takatifu zilizoenea tangu karne za kwanza BK. Ni kwamba, kisha kupigwa
vitani na Waislamu mara kadhaa, kwenye miaka ya 720 Kaisari Leo
III wa Bizanti alizikataza
hizo na kuagiza zilizokuwepo ziteketezwe. Lengo lake lilikuwa kupunguza uadui
wa Waislamu dhidi ya Wakristo na dola la Roma. Lakini waamini wengi wa dola lake walipinga uamuzi
huo, wakiungwa mkono na Papa Gregori III. Hatimaye Mtaguso wa pili wa
Nisea (787) ulitetea na kupitisha
uhalali wa picha hizo katika Ukristo.
Kanisa lilivyoendelea hasa
Ulaya
Tangu kuja kwa Uislamu
uenezaji wa Injili katika Afrika ulikwama na kurudi nyuma. Kusini kwa Sahara ilifika kupitia Nubia lakini baada ya Nubia
kuwa ndani ya eneo la Kiislamu athari hii haikuendelea. Kumbe uenezi wa Ukristo
katika kipindi kile ulipatikana Ulaya na Asia.
Kule Ulaya makabila mengi yaliendelea kupokea Ukristo. Wakati mwingine watu
walivutwa na mahubiri kuacha Upagani na kubatizwa. Mara nyingi waliona ya kwamba miungu
ya kikabila haina msaada tena katika mazingira iliyobadilika. Waliweza kuvutwa
na mfano bora wa wamonaki walioishi kati yao, au kushangazwa na elimu au
maendeleo yao. Wakati mwingine wafalme waliamua kuwa Wakristo kwa sababu za
kiroho au za kisiasa wakabatizwa pamoja na kabila au taifa zima. Katika mawazo
ya Wazungu wa kale dini haikuwa jambo la mtu binafsi bali jambo
la kijamii. Wakati mwingine washindi wa vita waliamua kuwabatiza maadui ili
kujenga uhusiano wa kiroho nao. Ndiyo sababu ya ubatizo wa mabavu ulioweza kutokea
katika nchi kadhaa.
Karolo Mkuu na Papa Adrian I. Karolo alitawazwa na Papa Leo III kuwa Kaisari wa magharibi (800). Ushirikiano kati ya
Mapapa na Makaisari wa Dola Takatifu la
Kiroma (leo Ujerumani na nchi za kandokando) ulikuwa na mafanikio kadhaa
na matatizo mengi zaidi na zaidi.
Mfano mmojawapo ni
ubatizo wa Wasaksoni, kabila kubwa katika eneo la Ujerumani kaskazini.
Baadhi ya mababu wao walivuka bahari na kuteka Uingereza pamoja na Waangli. Wakati ule Wajerumani wengi walikuwa Wakristo
lakini Wasaksoni waliendelea kutetea Upagani wao.
Mfalme wa eneo la
Ufaransa na Ujerumani Magharibi aliyeitwa Karolo Mkuu alipigana nao mara kwa mara. Mwishowe aliona
wakibaki Wapagani hatawashinda. Mwaka 800 B.K. aliwapa chaguo: upanga au ubatizo. Mwanzoni walikataa akawaua machifu 4000 wa Wasaksoni
katika siku moja. Waliobaki wakabatizwa wakawaamuru wenzao kubatizwa vilevile.
Hivyo eneo kubwa lilipokea Ukristo, lakini si kwa sababu ya imani, ila kwa
kulazimishwa.
Si ajabu ya kwamba kwa
muda mrefu Ukristo wa Ulaya katika nchi mbalimbali ulikuwa wa juujuu tu,
ukaonyesha dalili za mchanganyiko wa Injili na desturi za kale za Upagani.
Kumbe Ukristo ulikwenda njia ndefu sana tangu zamani za mashahidi wa
Aleksandria na Karthago waliokufa badala ya kukana Ukristo wao mpaka wale
Wakristo wapya wa Kisaksoni walioona heri wabatizwe kuliko kufa.
Maeneo mapya ya Ukristo
yalifuata desturi za kule walikotokea wahubiri wao. Ndivyo makabila ya Ulaya
kaskazini walivyojiunga na Kanisa Katoliki la
Kilatini. Kumbe makabila ya
Mashariki wakawa Waorthodoksi wakipokea ubatizo kutoka kwa wajumbe wa Askofu wa
Bizanti. Mpaka leo Ulaya mataifa ya Warusi, Waukraina, Waromania, Wabulgaria na Waserbia (pamoja na Wagiriki wenyewe) ni Waorthodoksi. (Afrika ni hasa nchi za
Misri, Ethiopia na Eritrea zinazofuata mapokeo ya Kiorthodoksi ya Kikopti). Mnamo mwaka 1000 karibu maeneo yote ya
Ulaya yalikuwa na Wakristo, ingawa mara nyingi kwa jina tu.
Kule Asia Ukristo wa
Kiorthodoksi uliendelea vizuri katika nchi nyingi. Tangu mwanzo mpaka leo lipo
Kanisa la India Kusini (jimbo la Kerala). Wamisionari wa Kanisa la Mesopotamia na Uajemi
walihubiri kote Asia ya Kati hadi Uchina na Indonesia. Lakini maendeleo hayo yalirudishwa nyuma na
mashindano kati ya Ukristo na Uislamu. Kiasili Uislamu ulikuwa na uvumilivu kwa
dini za Wakristo na Wayahudi. Katika maeneo ya Waarabu kama Misri au Siria
Kanisa liliendelea kupata ustahimilivu: liliweza kuendelea na ibada ya Kikristo
ingawa kwa matatizo.
Lakini huko Asia
makabila na mataifa mapya walipokea Uislamu, mara nyingi kwa njia ya vita.
Makabila hayo ya Waturuki na Wamongolia yalifuata imani ya Kiislamu kwa ukali kuliko Waarabu wenyewe.
Walilazimisha wote waliokuwa na imani tofauti (Wakristo, Wabuddha au wafuasi wa dini za jadi) wawe Waislamu. Mtawala Mwislamu wa Wamongolia, Tamerlano, aliua Wakristo lukuki na kubomoa makanisa elfu kadhaa alipofanya vita
vyake Asia ya Kati. Katika vita hivyo Ukristo wa Asia ya Kati uliharibika
kabisa. Maeneo makubwa yalichomwa moto, watu walilazimishwa
kwa upanga kuwa Waislamu au kuuawa. Mnamo mwaka 1400 Ukristo wa Asia ulibaki
katika Mashariki ya Kati tu (Asia ya Magharibi) pamoja na India Kusini. Kumbe
uzito wa Ulaya uliongezeka katika Kanisa kwani ni huko tu lilipoweza kuendelea
bila maadui wa nje.
Kuingiliana kwa dini na
siasa
Mwaka 1200 kwa jumla Ulaya ilikuwa
bara la Kikristo. Kanisa Katoliki (au: la Kiorthodoksi katika Mashariki)
lilikuwa dini rasmi. Popote Kanisa lilikuwa chini ya ulinzi wa serikali.
Watu wote walipaswa kuonekana Wakristo. Watu pekee wenye tofauti walikuwa
Wayahudi, lakini waliruhusiwa kuishi katika nchi kadhaa tu; katika nchi nyingine
walifukuzwa. Katika mila na desturi za Ulaya
zilizotangulia kuja kwa Ukristo umoja huo wa dini na kabila ulikuwa kawaida.
Hivyo kwa upande mmoja
Ukristo ulikuwa na nguvu sana Ulaya wakati ule. Lakini kwa ndani ulikuwa na udhaifu wa aina mbalimbali.
Wataalamu wengine wa historia ya Ulaya huita kipindi hicho "Karne za Kati" au hata "Nyakati za Giza". Maana
yake ni kipindi kati ya kuanguka kwa utamaduni na uchumi wa hali ya juu uliokuwapo wakati wa Dola la Roma na
kipindi cha kuanzia mwaka 1500 ambacho uchumi na elimu vilianza kusonga mbele tena.
Tutajaribu kuangalia pande zote mbili, yaani mafanikio na matatizo.
Katika nchi nyingi
tumezoea kwamba serikali haina
dini. Kila mwananchi ni huru kuchagua imani yake. Kumbe wazo hilo si la
kawaida popote duniani. Mpaka leo tunasikia habari za nchi zinazotoa kipaumbele
kwa dini au madhehebu fulani upande wa serikali. Taratibu hizo ni mabaki ya
zile zilizokuwa kawaida katika sehemu nyingi za dunia. Zamani katika nchi
nyingi ilikuwa kawaida kuangalia mambo ya dini na mambo ya dola pamoja.
Agano Jipya halina amri yoyote juu ya kuunda
"serikali za Kikristo". Kinyume chake Wakristo walifundishwa na mtume
Paulo kuiombea serikali ya Kipagani ya Kaisari wa Roma. Lakini baada ya viongozi wa mataifa kuwa Wakristo
waliona lazima kulitumia Kanisa kama chombo kinachoongeza umoja na nguvu ya
nchi.
Katika Ulaya ya Karne za
Kati Kanisa na serikali vilikwenda pamoja. Katika sehemu za Waorthodoksi Kanisa
lilikuwa chini ya wafalme waliokubaliwa kuwa walezi wake wakuu. Ulaya magharibi
kwenye Wakatoliki wengi Kanisa lilikuwa huru zaidi. Lakini hata huko mambo
yaliingiliana.
Utaratibu wa utawala
wakati ule ulikuwa wa kikabaila yaani machifu na watu wa familia za wakubwa walitawala maeneo chini ya serikali kuu
ya mfalme.
- a. Wafalme na hata
watawala wadogo walipewa madaraka
yao katika nchi kwa ibada maalumu kanisani.
- b. Watawala
waligandamiza wapinzani wa Kanisa kwani waliona wangeleta vurugu hata kisiasa.
- c. Watawala
walikabidhi madaraka mengi kwa maaskofu. Askofu aliweza kuunganisha
uongozi wa Kanisa na mamlaka ya kiserikali katika eneo lake. Viongozi wa
Kanisa waliaminika kuliko machifu wa kawaida. Machifu wakikabidhiwa
madaraka fulani kwa muda walijaribu mara nyingi kuyashika kama mali
yao. Wakatafuta kuongeza mali yao kuwa urithi wa familia. Faida
ya kutumia watu wa Kanisa ilikuwa kwamba mapadri na hasa maaskofu hawaoi,
hawana watoto, hawana hamu
ya kutafuta urithi kwa ajili ya watoto wao.
- d. Maaskofu (na
viongozi wengine wa Kanisa) walichaguliwa mara nyingi kutokana na sifa zao
za kisiasa kuliko uwezo wa kuongoza kiroho. Kwa sababu cheo cha askofu
kiliambatana na mapato makubwa, ni familia za machifu
zilizopeleka wanao katika nafasi hizo. Kwa njia hiyo matabaka
ya kijamii yalionekana vilevile ndani ya Kanisa: viongozi wake walitoka
katika familia za wakubwa, nafasi za chini walipewa watumishi kutoka
familia za matabaka ya chini.
Marekebisho ya karne IX-XII
Ni kawaida ya binadamu kuanzisha kazi kwa nguvu halafu kuchoka, kuanza
safari kwa kasi halafu kupunguza mwendo. Vilevile jumuia zina vipindi vya bidii
na vya ulegevu.
Kanisa lenyewe, ingawa
ni takatifu, linaathiriwa na ukosefu wa wanae. Ila Roho Mtakatifu haliachi bila ya msaada wa watu motomoto ili
kulirekebisha.
Utawa unahusika kabisa
na utakatifu wa Kanisa: ukistawi mmoja, unastawi wa pili pia. Hasa katika karne IX hadi XII Kanisa la magharibi lilitambua wazi haja ya
urekebisho katika umonaki na katika maisha yake yote.
Kati ya matukio muhimu
yaliyoandaa ukombozi wa Kanisa kutoka mikono ya wanasiasa kuna uundaji wa monasteri
ya Cluny (leo nchini Ufaransa) mwaka 910 ikiwa chini ya Mtume
Petro (yaani chini ya Papa tu), si chini ya mtawala wa dunia hii. Monasteri
hiyo ilizaa nyingine nyingi kote Ulaya ambazo kwa kutoingiliwa waliweza
kuongozwa na watu wa kiroho waliochaguliwa na wamonaki wenyewe kwa malengo ya
imani.
Kati ya matawi mapya ya
Kibenedikto yaliyotokana na juhudi hizo, mbali ya lile la Cluny (ambalo lilikazia liturujia kuliko kazi za mikono), lile la Camaldoli (lililofufua ukaapweke) na lile la Citeaux (ambalo lilirudia maisha magumu katika ufukara na
kazi).
Wamonaki wa matawi hayo
wakaja kushika nafasi muhimu katika kurekebisha Kanisa, hasa Petro Damiani (1007-1072), Papa Gregori VII (1028-1085) na Bernardo wa
Clairvaux (1090-1153).
Wakati huohuo Bruno (1035-1101) alianzisha aina mpya ya ukaapweke iliyodumu kuwa na
juhudi hadi leo (Wakartusi).
Kaisari
Henri IV akiomba msamaha wa Papa Gregori VII huko Canossa (1077) katika mchoro wa Carlo
Emanuelle.
Kutoka monasteri za
namna hiyo walitokea viongozi wa Kanisa waliokomboa Upapa pia katika kuingiliwa
na wanasiasa. Muhimu zaidi kati yao ni Papa Gregori VII aliyeshindana na
Kaisari akitumia mamlaka ya kiroho. Mwenzake aliyesababisha Mapapa wachaguliwe
na makardinali tu ni Petro Damiani, Mbenedikto wa urekebisho mwingine, ule wa Camaldoli (Italia).
Wakati huohuo, ili
kuboresha maisha ya mapadri wanajimbo, toka zamani ulisisitizwa uundaji wa
jumuia kati yao, ambamo wasali na kufanya utume kwa pamoja.
Hasa kuanzia karne XI wengi walifanya hivyo kwenye makanisa makubwa kama
mtindo mpya wa kitawa unaosisitiza liturujia ya fahari pamoja na uchungaji.
Inavyoweza kueleweka,
hao walifuata kanuni ya Augustino na kuitwa Wakanoni. Maarufu zaidi katika yao
ni Norbert (1082-1134), mwanzilishi wa Wapremontree.
Utajiri wa Kanisa
Kanisa lilikuwa tajiri
sana. Makanisa yalijengwa na wakubwa waliotoa baadaye shamba fulani kuwa mradi wa kanisa lile. Ilikuwa
kawaida kwa kanisa kumiliki mashamba yenye nia mbalimbali: moja kugharimia matengenezo ya jengo, lingine kumtunza mchungaji au paroko, lingine kumlipa msaidizi wake n.k.
Kanisa kubwa lenye watumishi wengi lilikuwa na
mapato makubwa. Watu wa vijiji kadhaa walitakiwa kuchanga sehemu ya mavuno yao na kulifanyia kanisa kazi siku mbili kwa juma kama kodi kwa ajili ya gharama za jengo, mapadri kadhaa au askofu.
Mara nyingi zawadi hizo za mashamba au vijiji zilitolewa kama sadaka, kama alama ya toba au kama shukrani. Sadaka za makabaila
ziliongeza utajiri wa Kanisa.
Familia za makabaila
zilichagua nafasi za uaskofu kwa watoto wao. Mwana wa chifu aliyepokewa katika upadri alizuiliwa kuunda familia na kurithi cheo cha baba, lakini
alipanda ngazi ndani ya Kanisa, kupata cheo cha heshima katika jamii na kuwa na mapato
makubwa yaliyomwezesha kuishi maisha mazuri na tajiri kama familia yake.
Wakati wa njaa maskini waliweza kupata misaada kanisani, hasa katika nyumba
za watawa. Wamonaki waliweza kuwasaidia maskini hata kwa kuuza hazina ya kanisa hata mapambo ya dhahabu yaliyopatikana wakati wa utajiri. Lakini mara nyingi
maaskofu walijisikia kuwa wakubwa na wengi wao hawakujali matatizo ya wadogo.
Uhaba wa elimu
Karne za Kati kule Ulaya zilikuwa kipindi pasipo elimu kwa watu
wengi. Kwa jumla utamaduni wa juu wa Kiroma ulikuwa umeanguka chini. Karibu
watu wote hawakujua kusoma wala kuandika. Katika nchi nyingi ni watawa tu waliosoma.
Tatizo mojawapo lilikuwa uhaba wa vitabu. Mashine za kupiga chapa vitabu hazikujulikana. Maana yake kila kitabu
kiliandikwa kwa mkono. Nakala ya Biblia ilihitaji
kuandikwa na mtu kwa muda wa mwaka au zaidi. Hivyo vitabu
vilikuwa ghali sana. Mtu wa kawaida alishindwa kununua kitabu, hata kama
angeweza kusoma. Kumbe Wakristo wengi sana hawakuwahi kusoma Biblia.
Zaidi ya hayo Kanisa
Katoliki lilitumia popote Biblia katika lugha moja tu, yaani Kilatini, ambacho kilikuwa pia lugha ya ibada zote kwa ajili
ya nyimbo, masomo na sala. Kutumia lugha moja
popote kulisaidia sana kutunza umoja wa Kanisa.
Lakini watu wa kawaida
hawakuelewa Kilatini, hata mapadri wengi hawakukielewa vizuri. Kidogo ingekuwa
kama kusoma Biblia na kuhubiri katika makanisa ya Afrika kwa Kiingereza au Kifaransa tu.
Hali hii ilisababisha
elimu ya Kikristo kuwa chini kati ya waamini wa kawaida. Hivyo walijali sana
mambo ya pembeni kama vile masalia ya watakatifu. Watu wengi waliona muhimu sana kuhiji kwenye "mahali
patakatifu" wakiamini ya kwamba safari za aina hii zinaleta sifa mbele za
Mungu.
Ilikuwa vema kusafiri
ili kusali kwenye kaburi la mtakatifu, k.mf. shahidi aliyekufa kwa ajili ya
imani yake zamani, lakini mifano mbalimbali inaonyesha jinsi gani imani ya
asili ya ushirikina ilikuwa bado na nguvu baada ya Ukristo kuenea.
Vita vya msalaba
Mtawa Petro
mkaapweke akihubiri vita vya
msalaba mbele ya makabaila wa Ufaransa.
Wakristo waliohiji
Yerusalemu kutoka Ulaya walishambuliwa njiani mara kwa mara. Naye Kaisari wa Bizanti aliomba msaada wa Wakristo wa
magharibi dhidi ya mashambulio ya
Waturuki Waislamu.
Kuanzia mwaka 1095 Wakristo Wakatoliki wa
Ulaya walijaribu kuwaondoa Waislamu katika nchi za Mashariki ya Kati. Papa aliwaita mataifa ya Kikatoliki ya Ulaya
kuikomboa nchi takatifu. Tangu mwaka 1096 hadi mwaka 1270 kampeni za kijeshi zilianzishwa
Ulaya kuelekea Yerusalemu.
Kampeni hizo huitwa
"Vita vya msalaba" kwani wanajeshi walipokea kanisani alama ya msalaba wa kitambaa waliobandika juu ya nguo zao. Walifundishwa kuwa
vita hivyo ni vitakatifu: atakayekufa atafika mbinguni kwa hakika. Wataalamu wanahisi kama hapo athari za mafundisho ya Kiislamu
juu ya "jihadi" zimeingia katika Ukristo.
Mwaka 1099 jeshi la Ulaya lilifika
mbele ya kuta za Yerusalemu. Baada ya mapigano mafupi jeshi la msalaba
liliwashinda wateteaji Waislamu. Katika hasira ya mapigano waliua ovyo wakazi wengi sana, wazee na watoto, wakiwemo Waislamu,
Wakristo na Wayahudi. Mkabaila Mfaransa alipokea cheo cha "Mfalme wa Yerusalemu".
Lakini miaka 100 baadaye
Sultani Salah-ed-Din wa Misri aliwafukuza wanamsalaba tena kutoka
Yerusalemu. Miaka 40 baadaye alirudisha mji huo kwa hiari baada ya kupatana na
Mfalme Mjerumani.
Lakini muda wote huo
Wazungu walitawala sehemu ya Palestina na Siria tu. Waislamu waliwaona kama maadui. Hata
Wakristo wenyeji (Waorthodoksi) hawakuwakubali kuwa wakombozi kwani walijaribu
kuwaunganisha Wakristo wote chini ya Kanisa Katoliki.
Safari moja iliyoondoka
Ulaya mwaka 1204 ili kuikomboa Yerusalemu, kumbe ilifika mpaka Bizanti tu
ambako wanajeshi wa msalaba waliteka mji, kupora utajiri na kumfukuza Kaisari
wa Bizanti. Miaka 100 baadaye Kaisari alirudi na kuunda upya Ufalme wa Roma ya
Mashariki.
Mwaka 1291 jeshi la Kiislamu
liliwafukuza kabisa wanajeshi wa msalaba katika nchi takatifu wasirudi tena.
Lakini kabla ya kuondoka waliwahi kuvunja nguvu ya Bizanti kiasi cha kutosha.
Kumbe Ulaya Magharibi iliharibu ulinzi wa dola la mashariki dhidi ya Waturuki
waliofaulu baadaye kuingia Ulaya.
Badala ya kufukuzwa,
jeshi la Waturuki lilianza kuishambulia Ulaya
Kusini-Mashariki. Mwaka 1453 ulianguka mji wa Bizanti, na mwaka 1529 Waturuki walifika mpaka
Vienna, mji mkuu wa Mfalme wa Ujerumani. Hapo walirudishwa nyuma,
lakini nchi nyingi za Ulaya Kusini-Mashariki pamoja na Wakristo wao walikaa
chini ya Waturuki kwa karne tatu zijazo.
Katika karne XII, ambapo baadhi ya Wakristo walipiga vita vya msalaba
kuikomboa nchi takatifu, na baadhi walitekwa na Waislamu kuwa watumwa,
zilianzishwa aina mpya za watawa ambao washike maisha ya Kiroho pamoja na upanga ili kusindikiza, kukaribisha,
kulinda na kutibu waliohiji Yerusalemu, au wajitolee kukomboa watumwa hata kwa
kubadilishana nao.
Mt. Yohane wa Matha
Baadhi ya mashirika hayo
yanadumu mpaka leo, lakini yamebadili sana malengo na mbinu. Kati ya
waanzilishi wakumbukwe Yohane wa Matha (1154-1213) na Petro Nolasco (1180-1249).
Kwa ujumla majaribio ya
vita vya msalaba ya kuikomboa nchi takatifu yalishindikana. Vita hivyo
vilidhoofisha Wakristo wa Mashariki waliozoea kuishi chini ya Waarabu Waislamu.
Kipindi cha vita vya
kidini kilisababisha mateso mengi kwa Wakristo
Waorthodoksi chini ya Waislamu. Walilipa madeni yaliyoachwa nyuma na
ndugu zao kutoka Ulaya Magharibi.
Katika uhusiano mgumu
kati ya dini hizo mbili kule Ulaya na Mashariki ya Kati, Waislamu wanastahili
pia sifa. Ahadi nyingi walizozifanya zilivunjika, lakini mahali pengi Wakristo
walipewa nafasi za kuendelea kuishi kati ya Waislamu hata kama ilikuwa kwa ubaguzi na mateso.
Maisha haya yalikuwa
mara nyingi magumu, lakini mahali pengi waliweza kubaki. Waliruhusiwa kuendelea
na ibada zao (lakini waliweza kukataliwa kujenga makanisa au hata kutengeneza
makanisa ya kale isipokuwa kwa kulipa tena kodi za nyongeza).
Katika mambo ya ndoa au urithi wa mali
walikuwa chini ya makanisa yao. Viongozi wa makanisa yao waliwajibika mbele ya
serikali ya Kiislamu juu ya ushirikiano mwema. Kwa namna hiyo jumuiya za
makanisa kama vile la Kigiriki, la Kikopti, la Kisiria, la Kiarmenia n.k.
zilihifadhiwa mpaka leo katika nchi za Kiarabu, isipokuwa idadi ya waumini wao
iliendelea kupungua. Sababu kuu ni kwamba kama Mkristo amekuwa Mwislamu
hakuweza kurudi tena. Sheria ya Kiislamu inamruhusu Mkristo kugeukia Uislamu,
lakini mtu aliyekuwa Mwislamu anastahili adhabu ya kifo akigeukia Ukristo au
dini nyingine. Pamoja na hayo Wakristo walianza kuhamia nchi ambako watakuwa
raia huru bila kasoro.
Kumbe historia
inaonyesha kwamba giza lipo hata upande wa Wakristo. Wakati ule Wakristo wengi
walikosa vilevile ustahimilivu kwa watu wenye imani tofauti. Hakuna Mwislamu
aliyeweza kubaki katika nchi za Hispania na Ureno baada ya kuvunjwa wa
utawala wa Kiarabu.
Inatosha kulinganisha
hali ya Waislamu kule Hispania. Sehemu kubwa ya Hispania ilikuwa miaka mamia
chini ya utawala wa Waarabu Waislamu. Katika vita vingi mfululizo Wahispania
waliteka nchi yao tena. Mwaka 1492 mfalme wa mwisho
Mwislamu alishindwa. Waislamu wakaishi chini ya utawala wa Wahispania
Wakatoliki. Lakini miaka michache baadaye Waislamu wote walilazimishwa wapokee
ubatizo, wengine waliuawa au kufukuzwa.
Bila shaka hayo ni
matokeo ya hali ya vita kati ya Waislamu na Wakristo. Wahispania walionyesha
tabia zinazofanana na zile za Wamongolia Waislamu walioharibu makanisa yote ya Asia ya Kati.
Lakini ipo mifano
mingine: Wakristo wote walifyekwa Uarabuni kwenyewe kumbe Waislamu waliweza
kubaki chini ya Waaustria Wakristo waliotawala nchi za Ulaya Kusini-Mashariki.
Kweli kati ya dini hizo mbili hakuna anayeweza kujisifu tu juu ya historia ya
dini yake bila kukiri makosa na kasoro pia.
Ugandamizaji wa wazushi
Serikali ziliona ni
lazima kutetea umoja wa
Kanisa. Hivyo viongozi wa
Kanisa walishawishika kutumia nguvu ya serikali kuhakikisha uongozi wao
ufuatwe. Ikiwa walijitokeza Wakristo waliodai mabadiliko au kupinga uongozi wa
Kanisa, serikali iliingilia kati na kuwagandamiza kama "wazushi". Ilikuwa hasa
utajiri wa Kanisa na wa maaskofu wengi uliosababisha ugomvi.
Katika karne ya 13 Ufaransa alijitokeza mfanyabiashara Petro Waldo aliyesikia wito wa
Kristo katika maisha yake. Aliwapa maskini mali yake yote akaanza maisha ya
kuhubiri akijaribu kumwiga Bwana Yesu.
Papa Inosenti III ndiye aliyefikisha
Upapa hadi kilele cha mamlaka zote Ulaya.
Akafundisha ya kwamba
Mkristo wa kweli anapaswa kumfuata Yesu hata katika maisha ya umaskini.
Akauliza: mbona Kristo alikuwa maskini, lakini maaskofu wa leo ni matajiri?
Wafuasi wake kwanza waliruhusiwa, halafu wakaanza kukutana nje ya makanisa.
Kanisa liliwatangaza kuwa wazushi wakatafutwa na kukamatwa na serikali. Wengine
wakafungwa gerezani, wengine wakauawa.
Baadaye ilikuwa kawaida
kuweka "wazushi" mbele ya mahakama za pekee na hata kuwachoma moto. Papa Inosenti III akaunda idara ya pekee "Baraza
la Ulinzi wa Imani". Ofisi hiyo ilikuwa na kazi ya kuwatafuta
"wazushi" na kuwahoji juu ya imani zao. Wakionekana kuwa na makosa
wasitake kutubu walikabidhiwa mikononi mwa serikali iliyotoa adhabu ya kifo. Hata hivyo mawazo yao yaliendelea kuzunguka kati ya
watu wa kawaida. Wawaldo walihubiri kwa siri katika nchi nyingi.
Fransisko na tapo la
mafukara
Mchoro wa zamani wa Fransisko wa Asizi unaoaminiwa kufanana naye
kuliko yote.
Kama kawaida bidii kwa
urekebisho wa Kanisa zilifanikiwa kiasi tu: hasa walei hawakuridhika na wengine
walianza kukata tamaa juu ya hali ya Kanisa.
Pia hija na vita vya msalaba
vilifanya wengi wajionee nchi ya Yesu na hivyo kuvutiwa upya na maisha yake.
Ndiyo sababu walistawisha mifumo mbalimbali ya Kiinjili na kulenga maisha ya
Kanisa la mwanzoni.
Dhidi ya mwenendo wa
mapadri na wamonaki, walisisitiza ufukara na unyofu hata wengi walifikia
hatua ya kuliasi Kanisa. Ulikuwa wakati wa utajiri kuzidi hata kufanya watu
kadhaa waukinai.
Katika matatizo hayo
Mungu aliita watu wairudishe upya roho ya Injili. Hivyo katika karne XIII yalianzishwa mashirika mbalimbali (hasa Wafransisko na Wadominiko, lakini pia Waaugustino, Wakarmeli na Watumishi wa Maria) yaliyoitwa ya ombaomba
kwa jinsi yalivyokaza ufukara.
Fransisko wa Asizi alizaliwa katika
familia tajiri akawa kijana aliyependa sana muziki na sherehe. Vitani alifungwa mwaka mmoja akaanza kumtafuta
Mungu.
Siku moja aliposali
akasikia sauti, "nenda ukatengeneze Kanisa langu linalotaka
kubomoka". Basi, akachukua pesa akaanza kutengeneza
kanisa dogo lililokuwa bovu sana. Baba yake akakasirika akiona
kijana anapoteza mali ya familia. Fransisko akakutana na baba mbele ya Askofu uwanjani akavua nguo zake na
kumrudishia baba pamoja na pesa zakeː "Kuanzia sasa nitasema tu, Baba yetu uliye mbinguni".
Fransisko akaishi maisha
kama mtawa akimwomba Mungu amwonyeshe njia. Siku moja kanisani alisikia somo la
Mathayo 10:7-20, akajua: Hiyo ndiyo njia yangu! Alielewa
maana yake "ukatengeneze Kanisa langu": kwamba si jengo lile dogo
alipoanzia, lakini Kanisa la Kristo lililobomolewa kwa sababu ya ujumbe wa Injili kusahauliwa.
Alianza maisha ya
ufukara akijaribu kuiga mfano wa Yesu. Akazunguka akivaa kanzu ya gunia na kuhubiri upendo wa Mungu. Vijana wengine wakamfuata wakaunda utaratibu wa
maisha ya pamoja.
Fransisko akaona ya
kwamba nyumba za wamonaki zilikuwa tajiri sana (mmonaki mwenyewe hakuwa na
mali, lakini jumuiya yake iliweza kuwa tajiri). Kwa wafuasi wake alikataza
jumuiya zisiwe na mali.
Fransisko alipendwa sana
kwani alionyesha imani na furaha katika Kristo na upendo kwa watu wote. Mwenyewe alisafiri
mpaka Afrika akahubiri mbele ya Sultani wa Misri. Ingawa wakati ule vita
vilikuwa vinaendelea kati ya jeshi la Kikatoliki la Ulaya na Waislamu, Sultani
alimpokea kwa heshima, akamsikiliza na kumruhusu kurudi kwake.
Fransisko aliamini ya
kwamba majaribio yote ya kuwashinda Waislamu kwa silaha ni ya bure. Kwa Mkristo
hakuna njia nyingine kuliko mfano wa Bwana Yesu, yaani upendo na unyenyekevu.
Mfumo wa Wafransisko
ulienea haraka sana. Ndugu hao walitembea popote wamevaa usiku na mchana kanzu ileile na kupewa chakula kutoka kwa Wakristo wa kawaida. Tofauti na wamonaki,
wakaishi kati ya watu wakihubiri na kufundisha. Walikuwa mfano wa kumtegemea
Mungu kabisa katika umaskini kwani hawakuwa na mali wala mapato kuliko sadaka
za hiari kutoka kwa Wakristo.
Katika maisha hayo
walifanana na vikundi kama Wawaldo lakini wakawafundisha
Wakristo kufuata uongozi wa Kanisa na maaskofu. Hivyo Wafransisko walikuwa
silaha muhimu ya Kanisa Katoliki dhidi ya waliopinga utajiri wake. Mahali pengi
Wakristo wa kawaida wakajiunga na jumuiya za kiroho zilizokuwa chini ya ulezi
wa Wafransisko.
Dominiko wa Guzmán, mwanzilishi wa Shirika la Ndugu Wahubiri.
Muda uleule Mhispania kwa jina Dominiko Guzman (1170-1221) aliunda shirika la watawa. Kusudi lake lilikuwa kuhubiri.
Akiwa padri aliguswa na uenezi wa uzushi akajitahidi kutatua tatizo hilo. Ili akubaliwe na watu
wote kama mhubiri halisi wa Injili alishika ufukara wa Yesu na mitume wake: kwenda wawiliwawili, kwa miguu, bila ya kuchukua
chochote kwa safari. Hivyo aliliandalia Kanisa kundi la watu wanaofanya kazi ya
kuhubiri, ambayo awali ilikuwa maalumu ya maaskofu. Kwa lengo hilo utawa wake
ulipunguza miundo ya kimonaki na urefu wa liturujia ili kuacha nafasi ya kusoma
na kusali zaidi mmojammoja: hivyo ndugu wahubiri watajipatia ukweli ambao wawashirikishe wengine kwa kuhubiri na kufundisha.
Ndio utume unaolingana zaidi na maisha ya sala na kusoma.
Wafransisko na Wadominiko walinyosha kiasi kasoro za kukosa mahubiri katika Misa ya kawaida. Walifanya
kazi muhimu sana ya kuwafundisha watu wadogo waliokuwa maskini na bila elimu
wala uwezo wa kusoma. Baadaye Wadominiko waliogopwa pia kwa kazi ya kutafuta na
kushtaki walioitwa "wazushi".
Watawa wa kike
hawakuweza kufuata mtindo uleule: waliishi kimonaki lakini kwa kuzingatia
ufukara na udugu wa Kifransisko na kwa kuombea utume wa hao ndugu wadogo. Klara wa Asizi (1193-1253), “mche mdogo” wa Fransisko, ndiye mwanamke wa kwanza
kutunga kanuni ya kitawa. Tapo hilo ni maarufu kwa marekebisho yaliyofuatana
hadi leo kuhusu ufukara.
Giovanni di
Paolo, "Mt. Katerina wa
Siena", 1475 hivi. Fogg Art Museum, Cambridge, Uingereza.
Tangu karne XII wanawake wengine pia walichangia sana ustawi wa
utawa, wa maisha ya Kiroho na wa Kanisa kwa jumla hata kwa maandishi yao. Kati
yao Katerina wa Siena (1347-1380), wa utawa wa tatu wa Mt. Dominiko, ametangazwa kuwa mwalimu wa Kanisa.
Kuanzia karne XIII zilijitokeza pia jumuia nyingine ambazo pengine
zinahusiana na mashirika ya kitawa (yaani za Utawa wa Tatu), lakini hazina nadhiri au si za hadhara. Kwa kuenea, zikaja kuwa na muundo
kama wa mashirika (1401), ingawa kwa kawaida ya kwao yalikuwa na jumuia za kiume
na za kike ndani yake.
Baada ya upinzani
mwingi, wanawake wakaja kukubaliwa wafanye utume na kuanzisha mashirika
yasiyobanwa na ugo. Kwa namna ya pekee Anjela Merici (1474-1540) alitaka wafuasi wake waishi na kutumikia kati ya watu;
baada ya karne nne shirika lake likakubaliwa kutambulika kuwa la kilimwengu.
Upande wa wanaume Filipo Neri (1515-1595) ndiye maarufu zaidi kati ya walioanzisha jumuia ambapo
watu wanaishi pamoja ili kujipatia malezi na kufanya utume fulani, lakini bila ya kuwekwa wakfu.
Farakano la Magharibi
Wengi wanaona karne ya 13 kuwa kilele cha matunda wa Kanisa Katoliki katika kulea upya Ulaya
magharibi kwa kuzaa hasa mashirika ya
ombaomba ya Fransisko wa Asizi
na Dominiko Guzman, mitindo mipya ya sanaa, pamoja na vyuo vikuu walipostawi walimu wa Kanisa kama Thoma wa Akwino na Bonaventura.
Lakini utaifa, uliotokea Ulaya magharibi kuanzia ufalme wa Ufaransa katika karne ya 14, ulivuruga umoja wa Kanisa na matatizo yalionekana
mpaka ngazi ya Upapa. Mara nyingi Papa mpya (Askofu wa Roma) alichaguliwa
kufuatana na ukoo au sifa za kisiasa tu. Cheo cha Papa kiliingizwa katika siasa kubwa kati ya wafalme
wa Ujerumani, Uingereza na Ufaransa.
Mwaka 1300 Papa Bonifas VIII alidai kuwa na madaraka juu ya wafalme wote. Mfalme
wa Ufaransa alikasirika akataka kulipiza kisasi.
Migongano hii
ilisababisha tatizo la Mapapa kwenda kukaa miaka 68 (1309-1377) huko Avinyon (leo nchini Ufaransa) badala ya kuongoza mjini Roma.
Aliyefaulu kumrudisha Papa katika jimbo lake hilo ni Katerina wa Siena, bikira mwenye karama ya unabii.
Lakini baada ya muda
mfupi makardinali waliofanya uchaguzi wa Papa mpya walisababisha farakano ndani ya Kanisa
lililoendelea kwa muda wa karibu miaka 40 (1378-1417). Katika hilo Farakano la
Kanisa la Magharibi, baadhi ya maaskofu na waamini wengine walimfuata Papa wa
Roma na baadhi Antipapa wa Avignon wakidhani ndiye Papa wa kweli.
Hali ilizidi kuwa mbaya:
mwaka 1409 walikuwepo watu watatu waliojiita "Papa" na
kukubaliwa na sehemu ya maaskofu. Maaskofu na Wakristo walichoka sana farakano
hilo. Mwaka 1417 Mtaguso mkuu wa
Konstanz (Ujerumani) ulifaulu
kuwaondoa wote watatu na kumchagua Papa mpya, Martin V.
Farakano la magharibi
liliisha kwa Mtaguso wa
Konstanz. Viongozi mbalimbali
wakajitahidi kufuta maovu ndani ya Kanisa lakini hawakufaulu sana. Walikuwepo
watu wakubwa wengi mno waliofaidika na hali halisi.
Nyumba za wamonaki
zilienea sana, pia kwa sababu ilikuwa kawaida kupeleka utawani watoto wasioweza
kurithi.
Cheo cha uaskofu
kilikuwa nafasi iliyotafutwa sana na familia za makabaila kwa ajili ya wanao
wasioweza kurithi cheo cha baba. Uaskofu ulipatikana mara nyingi kwa njia ya kuwahonga wenye haki ya kumchagua au kumthibitisha askofu.
Viongozi wa Kanisa katika eneo fulani walipokea hela kabla ya kumchagua askofu
mpya. Papa wa Roma alidai hela kabla ya kumthibitisha askofu yeyote
aliyechaguliwa. Mfalme alidai hela kabla ya kumkabidhi askofu madaraka ya
kiserikali katika eneo lake.
Lakini malipo hayo yote
yalifidiwa tena na watu wa kawaida, wakulima na wafanyabiashara wa eneo hilo waliopaswa kumlipa
askofu kodi zao kila mwaka.
Maaskofu wengine
walianguka kabisa wakitumia hela zao katika vita dhidi ya majirani wao, kwa
ujenzi wa maboma na makanisa uliopita uwezo wao, au kwa maisha ya ulevi na uasherati. Askofu alikataliwa
kuoa lakini wengi walikuwa na wapenzi wao na kuwajengea nyumba kubwa pamoja na
watoto wao.
Wakristo wengi
wakasikitika juu ya hali hii. Mapapa mbalimbali walijaribu kusimamisha maovu
hayo lakini bila mafanikio makubwa.
Yohane Hus na Umoja wa
Ndugu
Padri Yohane Hus alikuwa mwalimu wa teolojia kwenye Chuo Kikuu. Mwaka
1412 alihubiri kwa nguvu sana kule Praha (leo mji mkuu wa Ucheki), akafundisha ya kwamba mamlaka kuu Kanisani ni katika Biblia si katika maamuzi ya
maaskofu au Papa.
Maaskofu wakamtangaza
kuwa mzushi. Alishtakiwa mbele ya mfalme lakini wengi walimfuata. Akahifadhiwa
na kufichwa na kabaila katika boma lake.
Miaka 1414-1418 kulikuwa na Mtaguso mkuu wa Kanisa Katoliki kule Konstanz, Ujerumani. Hus akaitwa kujitetea mbele ya mkutano
huo, akaahidiwa ulinzi wa mfalme, yaani kwamba ataweza kurudi tena hata
akionekana kuwa mzushi. Lakini kinyume cha ahadi alikamatwa akahukumiwa kuwa
mwasi na mzushi, akachomwa moto akiwa hai.
Wafuasi wake katika
mikoa ya Bohemia na Moravia (leo Ucheki) wakasikitika mno. Wengine wakachukua
silaha wakataka kutenga nchi yao kutoka uongozi wa Kanisa.
Vita vya miaka mingi
vilianza kati ya Wahus na askari wa mfalme na maaskofu. Alama ya Wahus ilikuwa kikombe cha Ekaristi kwani Hus alifundisha ya kwamba Wakristo wote wanapaswa
kupokea kikombe kanisani (katika karne XII Kanisa Katoliki lilianza desturi ya kutoa kikombe
kwa mapadri tu).
Mwishoni Ukristo wa
Bohemia na Moravia uligawanyika. Wahus wakali waliojaribu kuunda utaratibu wa
kisiasa juu ya mahubiri ya Yesu na kuwalazimisha wote kuufuata kwa silaha
wakashindwa. Wengine wakafuata Wahus wasio wakali waliopatana na wakubwa wa
nchi. Wengine wakabaki ndani ya Kanisa Katoliki, wakaruhusiwa kuwa na ibada ya Misa
(chakula cha Bwana) wakipokea sakramenti katika maumbo ya mkate na divai.
Mwaka 1457 kikundi kidogo cha
wafuasi wa Hus waliochoka uuaji na vita vya kidini walianzisha jumuiya ya Kikristo
iliyoitwa "Umoja wa Ndugu", wakajaribu kuishi kama ndugu wakikaa pamoja, kufanya
kazi na kusali pamoja. Mwanzoni hawakupokea matajiri waliotaka kujiunga nao.
Mbinu hii ilifanana na
watawa aina ya Wafransisko lakini walikuwa jumuiya ya watu wenye ndoa na watoto.
Waliona muhimu wasiwe na taratibu za utawala katika Kanisa, lakini viongozi
wawe kama ndugu na watumishi wa wengine. Hawakutaka kumlazimisha yeyote katika
mambo ya imani kama ilivyokuwa katika maeneo ya Wakatoliki na ya Wahus wengine.
Mwanzoni walihudumiwa
kiroho na mapadri wa Kanisa Katoliki, lakini mwaka 1467 waliamua kuchagua
watumishi wao wenyewe, wakiwemo mpaka leo mashemasi, makasisi na maaskofu. Umoja huo ulienea Bohemia na
Moravia ukawa chanzo cha madhehebu ambayo yalistawi upya kuanzia mwaka 1722 na yanaitwa ya "Wamoravia" (leo wengi wao wanaishi nchini Tanzania).
Mwisho wa Karne za Kati
Karne za 15 na 16 zilikuwa muhimu katika historia ya Ukristo.
Huko Asia ya Kati jeshi
la Wamongolia Waislamu chini ya kiongozi Timur liliteka na kuharibu
nchi nyingi. Makanisa yalichomwa moto popote Asia ya Kati na Uajemi mpaka
Palestina. (Wakaharibu vilevile nyumba za dini nyingine kama Wabuddha au Wahindu).
Mwaka 1453 mji mkubwa wa
Bizanti ukatekwa na jeshi la Waturuki Waislamu. Ulikuwa mwisho wa Dola la Roma
lilivyoendelea katika eneo la mashariki. Tangu muda ule Wakristo wote wa
Mashariki ya Kati wameishi chini ya Waislamu.
Waturuki wakaendelea
kuingia Ulaya ya Kusini-Mashariki. Kwa muda wakatawala eneo la nchi za Ugiriki, Bulgaria, Romania, Masedonia, Serbia, Albania, Montenegro na Hungaria za leo. Ukristo wa Kiorthodoksi ulibaki huru katika
nchi za Urusi na Ethiopia tu.
Lakini Hispania wafalme
Wakatoliki walifaulu kuwafukuza Waarabu kutoka rasi ile. Tangu mwaka 711 hadi 1491 sehemu za Hispania na
Ureno zilikuwa chini ya Waarabu Waislamu. Baadhi ya wenyeji walisilimu.
Kumbe 1491 mji wa mwisho
uliotawaliwa na Waarabu ulitekwa, na mfalme wake akakimbilia Moroko. Wakristo wa nchi hizo walichukua nafasi ya kulipiza
kisasi kwa mateso yote ya nyuma. Waislamu waliobaki walilazimishwa kubatizwa,
wengine waliuawa.
Ingawa uhusiano kati ya
mataifa ya Waislamu na ya Wakristo ulikuwa mgumu yaliendelea kufanya biashara. Kwa jumla Waarabu walikuwa na ujuzi zaidi katika mambo ya
elimu na ufundi. Vilevile walifaulu sana katika biashara. Ni Waarabu
walionunua bidhaa kule India na kuzipeleka mpaka Italia.
Wazungu walisikitikia
sana bei kubwa ya bidhaa hizo na hasa faida kubwa ya wafanyabiashara Waislamu
lakini wakazinunua kwani wenyewe walishindwa kuzitengeneza.
Katika kipindi kilekile
mawazo mapya yalienea duniani. Anguko la Bizanti mwaka 1453 lilisababisha wasomi wengi wa mashariki
kukimbilia Ulaya Magharibi wakileta vitabu vyao. Wataalamu walianza kusoma tena
vitabu vya Wagiriki na Waroma wa kale. Elimu ilisonga mbele. Hasa mijini shule ziliundwa.
Mjerumani kwa jina Gutenberg alitengeneza mashine ya kwanza ya kupiga chapa
vitabu. Hivyo vitabu vilianza kupatikana kwa urahisi. Habari zikazunguka haraka
kati ya nchi na nchi, hali isiyojulikana karne nyingi tangu anguko la Dola la
Roma.
Yakaanza kusambaa tena
mafundisho ya kale kuwa dunia si tambarare lakini mviringo kama chungwa. Alijitokeza nahodha Mwitalia kwa jina Kristoforo Kolombo aliyetaka kujaribisha
mafundisho hayo. Ikiwa dunia kweli ina umbo la chungwa inawezekana kuelekea magharibi kutoka Hispania na kufika mashariki katika Bara Hindi. Kwa njia hiyo inawezekana kufanya biashara moja kwa
moja na nchi tajiri za mashariki bila kuwapa faida wafanyabiashara Waarabu.
Mfalme wa Hispania akampa Kolombo fedha za kuandaa meli tatu.
Mwaka 1492 Kolombo akaondoka
Hispania akakuta bara jipya magharibi lililoitwa baadaye Amerika. (Mwenyewe alifikiri amefika Bara Hindi, hivyo
akawaita wenyeji "Wahindi" na visiwa alipofika mwanzoni mpaka leo huitwa "West
Indies" = India Magharibi).
Wahispania walipora
utajiri wa mataifa ya Amerika yaliyokosa silaha za kushindana nao. Utajiri huo
mpya ulisaidia maendeleo ya Ulaya kupiku yale ya mataifa ya Waislamu na ya
Asia.
Urekebisho wa Kikatoliki na
Matengenezo ya Kiprotestanti
Martin Luther mwenye
umri wa miaka 46.
Umoja halisi wa Kanisa
unaweza kupatikana tu katika ukweli wa Injili ya Yesu Kristo. Ni habari mbaya kwamba katika karne ya 16 kuupigania ukweli huo kulivunja umoja wa Ukristo wa
magharibi. Haiwezekani kushangilia
mafarakano ya wafuasi wa Yesu.
Yale ya karne hiyo
yalitokana na kuelewa tofauti kweli za imani ya Kikristo na yalikuwa na ukali kwa sababu pande zote
zilisadiki kwamba kushikilia kwa usahihi ufunuo wa Mungu ni suala la wokovu wa milele. Kwa mfano, Martin Luther aliandika, «Sikubali mafundisho yangu yahukumiwe na
yeyote, hata kama ni malaika. Asiyekubali mafundisho yangu hawezi kufikia
wokovu».[1]
Pamoja na hayo, mambo
mengi yalichangia farakano, si teolojia tu, bali siasa, uchumi, jamii na
utamaduni. Wakati huo mara nyingi hoja za imani na malengo ya
kisiasa vilichanganyikana: wanasiasa wengi walitumia hoja hizo ili kufikia malengo ya
kiutawala, na vilevile wanateolojia walitumia siasa kutetea mafundisho yao ili kuvuta
watu. Ndiyo sababu Luther alichorwa kama shujaa wa taifa la Ujerumani.
Mara nyingi pande zote
zilipotosha maana ya wapinzani na kuwachora vibaya wakivunja amri ya nane
inayokataza uongo dhidi ya jirani. Hata waliojitahidi kusema ukweli tu juu
ya wengine kwa kawaida hawakujitahidi vya kutosha kuelewa msimamo wao na kuona
kwamba pengine si mbaya zaidi. Kila mmoja alitaka ushindi akachangia ugomvi uliorithishwa kwa vizazi vilivyofuata.
Hivyo, kilichosababisha
zaidi farakano si masuala ya imani yaliyojadiliwa na Waprotestanti, bali lawama zao dhidi ya hali mbaya ya Kanisa la
wakati huo iliyokuwa inakera wengi na kuwaelekeza kuunga mkono urekebisho.
Hapo kale neno hilo (kwa
Kilatini reformatio) lilihusu badiliko la hali mbaya iliyopo ili kurudia
hali nzuri zaidi ya awali. Katika Karne za Kati lilitumika mara nyingi kwa
marekebisho ya umonaki.
Katika karne ya 15 haja
ya urekebisho ilionekana wazi si tu kwa mashirika ya kitawa bali kwa Kanisa
lote. Hasa Mtaguso wa Konstanz (1414-1418) ulidai kabisa ufanyike «katika kichwa na katika viungo». Lakini kwa jumla mitaguso yote ya Karne za Kati na mikutano mingi ya Bunge la Dola la Ujerumani ililenga urekebisho wa Kanisa.
Kwa kweli Karne za Kati
zilikuwa na mchanganyiko wa mambo yaliyopingana: ibada za nje tu na za dhati
kabisa; teolojia iliyoelekeza kutenda kwa msingi wa nipe nikupe na
hakika ya kwamba binadamu anategemea kabisa neema ya Mungu; kutojali wajibu hata upande wa viongozi wa Kanisa na marekebisho safi ya
mashirika ya kitawa.
Karne XV ilikuwa kipindi
cha umotomoto wa pekee katika Kanisa, ambapo walei wengi zaidi na zaidi
walipata elimu nzuri, hivyo walitamani hotuba bora na mafundisho ya kuwasaidia kuishi Kikristo zaidi.
Luther aliitikia haja hizo zilizomgusa sana kama mtu wa wakati wake.
Mwenyewe alitumia kwa
nadra neno urekebisho, lakini likaja kuwa jina la kawaida la matukio yale mengi
ya miaka 1517 - 1555, yaani kuanzia uenezi wa hoja 95 za Martin Luther hadi amani ya Augsburg. Kati yake mabishano ya Kikanisa yaliyosababishwa na
teolojia ya Luther, yalichanganyikana mapema na siasa, uchumi na utamaduni,
kutokana na hali halisi ya wakati huo, mbali kuliko mwenyewe alivyofikiri.
Viongozi Wakatoliki,
yaani Papa na Mfalme mkuu wa Ujerumani, waliona kwa masikitiko kutokea kwa
mafarakano lakini mawazo yao yalitekwa na shughuli nyingi za siasa na vita hata
wakatumia nguvu zao kushindana kati yao.
Mwanzoni walimwona
Luther kuwa padri mdogo tu apaswaye kurudishwa kwenye njia iliyo halali. Papa Leo X hakuona umuhimu mkubwa katika habari zake: mwaka 1521 akamtenga Luther katika
Kanisa, halafu akapokea habari za Bunge la Ujerumani lililomhukumu Luther kuwa
mzushi na adui wa taifa.
Miaka 1522/1523 akafuata Papa Adriano VI: akiona uenezaji wa haraka wa mafundisho ya Luther
kila mahali akakiri Kanisa lilikuwa na makosa. Lakini uongozi wake ulidumu muda
mfupi mno.
Papa Klementi VII aliyefuata hakuwa na
mawazo ya kiroho, akashughulikia zaidi siasa akipigana vita na Mfalme juu ya
kutawala mikoa mbalimbali ya Italia.
Mwaka 1527 jeshi la Mfalme
liliteka Roma, Papa akakimbia. Walipatana mwaka 1529 lakini mwaka uleule
Waturuki Waislamu walifika mbele ya mji mkuu wa mfalme, Vienna. Kwa shida tu
jeshi la Wakristo liliwashinda.
Mfalme Karolo V wa Ujerumani alikuwa pia Mfalme wa Hispania. Mwaka
1521 jeshi la Wahispania liliteka Meksiko, baadaye Peru katika Amerika Kusini. Dhahabu na fedha za huko zilianza kuletwa Hispania. Mfalme
hakuwa na muda wala nguvu kushindana na sehemu kubwa ya makabaila wa Ujerumani
waliomuunga mkono Luther.
Kivulini mwa matokeo hayo
mafundisho ya Waprotestanti yalienea haraka pande nyingi za Ulaya. Kuanzia
mwaka 1530 ilikuwa wazi kwamba farakano limetokea, likitenga na Papa
sehemu kubwa ya Ulaya Kaskazini pamoja na matengenezo yenyewe kuvunjikavunjika
katika madhehebu mbalimbali.
Sasa sauti ya wale
waliodai urekebisho ndani ya Kanisa Katoliki ilisikika zaidi. Papa Paulo III akachukua hatua mbili: kwanza aliandaa mtaguso wa
maaskofu wote halafu aliimarisha Baraza la Ulinzi wa Imani. Ofisi hiyo ilikuwa
na kazi ya kufuatilia habari zote za upinzani dhidi ya Kanisa Katoliki na
kuomba serikali zilizokuwa mikononi mwa Wakatoliki kugandamiza wote waliotaka
kufuata mafundisho ya Luther na wenzake.
Baraza hilo lilikuwa na
nguvu sana: kwa jumla lilifaulu kufuta vikundi vyote vya Wainjili katika nchi
kama Italia, Ureno na Hispania. Lakini ugandamizaji huo uliongeza uchungu kati
ya madhehebu ukasababisha ugandamizaji wa Wakatoliki katika maeneo ya Walutheri
na ya Wareformati.
Chombo kingine kilikuwa
"Orodha ya vitabu vilivyopigwa marufuku" kwa kila Mkatoliki
asivisome, navyo havikuruhusiwa katika nchi katoliki. Orodha hiyo ilifutwa
rasmi na Papa Paulo VI mwaka 1965.
Ignas wa Loyola,
mwanzilishi wa Shirika la Yesu, alivyochorwa na Peter Paul Rubens.
Chombo kingine muhimu
zaidi cha urekebisho wa
Kikatoliki kilikuwa Shirika la Yesu, jumuia ya mapadri iliyoongozwa na "Jenerali" wake akitumia nidhamu ya kijeshi.
Mwanzilishi wake ni Ignas wa Loyola, Mhispania ambaye alikuwa mwanajeshi. Mwaka 1521 alijeruhiwa vibaya vitani. Alipokaa hospitalini muda mrefu akasikia wito wa Mungu uliobadilisha maisha yake.
Kisha kuacha jeshi, akamtolea Bikira Maria upanga wake akawa "Mwanajeshi wa Kiroho". Alifuata kwa
juhudi zote maisha ya kiroho na kutunga Mazoezi ya
Kiroho ili kuongoza watu
wamfuate Yesu Kristo.
Mwaka 1534, Ignas alikusanya vijana sita wakaweka nadhiri za ufukara, useja mtakatifu na utiifu, halafu ile ya kumtii daima Papa.
Kisha kusoma teolojia akapadrishwa. Akakusanya kikundi cha marafiki akiwaongoza kujenga
maisha ya kiroho kwa njia ya mazoezi ya pekee. Wote walifuata utaratibu uleule.
Kila mwaka walikutana kwa kipindi cha sala, kutafakari na kusoma kilichofuata
hatua au mbinu maalumu. Wengi walianza kumfuata na chama chake kikakubaliwa na
Papa mwaka 1540.
Shabaha kuu ilikuwa kutetea Kanisa chini ya Papa.
Kila mwanachama
alitakiwa kuwa na elimu ya juu. Hivyo Kanisa Katoliki liliimarika katika
teolojia, jambo lililowahi kukazwa zaidi na Waprotestanti.
Mapadri Wajesuiti
walifanya hasa kazi ya ualimu wakiunda shule na kufundisha vijana
elimu pamoja na upendo kwa Kanisa Katoliki.
Mkazo mwingine ulikuwa
kufufua utaratibu wa maungamo. Popote Ulaya Wajesuiti walikuwa
washauri hasa wa watawala Wakatoliki. Waliposikiliza ungamo la dhambi zao walipata nafasi nzuri ya kuwapa mawazo na kusababisha
hatua za serikali dhidi ya Waprotestanti.
Hivyo kwa athari ya Wajesuiti polepole
Uprotestanti ulirudi nyuma katika nchi za Ulaya ambako wakazi wengi walikuwa
wameanza kufuata mafundisho ya Martin Luther na Calvin lakini watawala walikuwa bado Wakatoliki.
Mbali nao, mashirika
mengine yalifanya kazi kubwa ya kuzuia uenezi wa Uprotestanti, kuanzia Wafransisko waliowahi kutambua hatari kabla ya viongozi wa
Kanisa. Baadaye ulikuwa hasa urekebisho wa Wakapuchini uliorudisha wengi katika Kanisa Katoliki kwa upole, usikivu na ushuhuda wa maisha
safi yenye kujitosa.
Miaka 1545-1563 maaskofu wa Kanisa
Katoliki walikutana Trento, Italia kaskazini, wakajadiliana juu ya mafundisho na hali ya Kanisa,
wakachukua hatua za kuondoa matatizo na kuimarisha imani. Maazimio yake makuu
yalibaki muhimu mpaka karne ya 20:
- a) Msingi wa imani ni
Biblia pamoja na mapokeo ya Kanisa.
- b) Sakramenti ziko
saba.
- c) Juu ya kuhesabiwa
haki (jinsi ya kupata wokovu) ni kwamba mwanadamu hahesabiwi haki kwa
sababu ya matendo yake mema bali kwa neema ya Mungu, lakini lazima
mwanadamu ashiriki katika kupokea na kutumia neema hiyo.
- d) Kanisa peke yake lina
mamlaka ya kueleza maana ya Biblia; Mkristo asijisomee bila mwongozo wa
Kanisa; toleo pekee la Biblia linalofaa ni lile linalotolewa na Kanisa
Katoliki katika lugha ya Kilatini (lililoitwa "Vulgata" - pamoja
na vitabu vya "Deuterokanoni" vilivyotengwa na Luther).
- e) Kufuta maovu katika
Kanisa: kampeni za kuuza vyeti vya rehema, malipo ya maaskofu kwa Papa ili
awathibitishie cheo, askofu kuwa na majimbo zaidi ya moja (walivyofanya
zamani kwa sababu ya mapato).
- f) Mapadri wawe na
elimu, wote wapitie masomo ya seminari, kila mmoja afuate utaratibu wa
kusoma Biblia kila siku, mahubiri yawepo katika kila Misa ya Jumapili.
- g) Itungwe Katekisimu
ya kwanza ya Kanisa Katoliki, pamoja na vitabu vipya vya liturujia.
Kwa jumla Mtaguso wa Trento ulishindwa kuwavuta Wainjili warudi, lakini
uliendeleza urekebisho wa Kanisa Katoliki. Katika nchi zilizobaki chini ya Roma
Kanisa lilipata nguvu tena kwa kuimarisha mafundisho ya kale pamoja na kuondoa
kasoro mbalimbali. Hata hivyo haikuwezekana kufuta farakano lililotokea tayari.
Vita kati ya madhehebu ya
Kikristo
Karolo V vitani
alivyochorwa na Tiziano (1548) ili kuadhimisha ushindi wake katika mapigano ya
Mühlberg.
Karolo V, Kaisari wa Dola Takatifu la
Kiroma, aliendesha Vita vya
Schmalkald (1546-1547) dhidi ya maeneo ya Walutheri yaliyokuwa ndani ya dola hilo kubwa la Ujerumani.
Lengo lake lilikuwa
kuwalazimisha watawala wadogo waliowaunga mkono Walutheri wafute matengenezo
yote.
Mwanzoni alishinda (20 Julai 1547); kwenye Bunge la
Augsburg (1547-1548) alidai Walutheri
wakubali kuwa chini ya maaskofu na Papa wa Kanisa Katoliki. Ingawa aliruhusu ndoa ya mapadri na kupokea ekaristi kwa maumbo yote mawili (mkate na divai), maitikio hayakuwa
mazuri hata kidogo: kukawa na vurugu kubwa.
Mwaka 1552, baada ya njama ya watawala hao dhidi
ya Karolo V, vilianza tena vita ambavyo vilimlazimisha kukimbia Austria. Hatimaye watawala Walutheri walipatana na mwanae, mfalme Ferdinand III. Hivyo jaribio la kufuta Ulutheri kijeshi lilishindikana kabisa.
Vita vilimalizika mwaka 1555 kwa amani ya Augsburg. Mapatano hayo yalilenga kuwezesha wananchi wenye imani tofauti waishi katika taifa lilelile. Watawala
walipewa haki ya kuwachagulia madhehebu ya dini raia wao. Wasiokubali
kufuata imani ya mtawala, walipewa tu haki ya kuhamia eneo lingine ambapo
mtawala wake alikuwa na imani yao.
Hivyo katika Dola la
Kijerumani yalikubalika rasmi maeneo yaliyoshikilia Ungamo la Augsburg na yale yaliyobaki
katika Kanisa Katoliki, lakini si wenye imani tofauti na hizo mbili, kama vile Wareformati na Waanabaptisti.
Amani ya Augsburg kwanza
ilifaulu kuleta mahusiano imara upande wa siasa, lakini baadaye
haikuweza kuzuia mlipuko wa vita vikali vya karne XVII: vita vya miaka 30 (1618-1648).
Madola ya Ujerumani yalipigana
kati yao, na nchi za nje zilishiriki zikiwemo Hispania, Ufaransa, Uswidi, Uholanzi na Denmark, lakini mapigano yake yalitokea hasa katika Ujerumani kwenye eneo la Dola Takatifu la
Kiroma.
Ni kwamba uhusiano kati
ya madhehebu ya Kikristo ulikuwa mbaya kwa muda mrefu. Karibu katika kila nchi
Wakristo walilazimishwa kufuata madhehebu rasmi, ama Ukatoliki ama Ulutheri.
Ikiwa mtawala fulani aliona vema kukubali mawazo ya Luther mapadri wote
walipewa chaguo la kufuata Ulutheri au kuhama nchi. Vilevile baada ya kifo
chake ikiwa mtawala aliyefuata alikuwa na msimamo tofauti, mapadri wakarudi na
wachungaji wa Kiinjili wakafukuzwa.
Raia hawakuulizwa wenyewe
wanasadiki nini, isipokuwa katika miji iliyojitawala na kuwa na utaratibu wa
kidemokrasia. Lakini hata mijini huko haikuwa kawaida kuruhusu madhehebu mawili
mahali pamoja.
Mafundisho ambayo kwetu
leo yanaonekana kuwa na tofauti ndogo yaliweza kumfikisha mtu gerezani au hata
kifoni.
Uhusiano mbaya ulikuwepo
vilevile kati ya wafuasi wa Luther na Wareformati. Katekisimu zao zilitumika
kama bendera. Walishutumiana kuwa wazushi wasioelewa vizuri kiini cha imani.
Kilichofuata ni kipindi
cha vita vya kidini kule Ulaya. Kilele kilikuwa Vita vya Miaka 30 ambavyo
vilianza kule Bohemia na Moravia kwa sababu watawala wadogo waliokuwa karibu na
Umoja wa Ndugu walijaribu kumpindua Mfalme Mkatoliki.
Vita hivyo vilianza kama
mapigano ya kidini kati ya madhehebu tofauti ya dola moja la Ujerumani, lakini
viliendelea kuwa vita vya Ulaya nzima ambako nchi ya Wakatoliki kama Ufaransa
ilishikamana na Uswidi ya Kiprotestanti dhidi ya Kaisari Mkatoliki.
Vita hivyo vilileta
uharibifu mkubwa mno katika Ujerumani. Kuna makadirio ya kwamba karibu theluthi moja ya wakazi wote walikufa kutokana na mauaji, njaa na magonjwa. Katika maeneo ya Ujerumani ya Kusini zaidi ya nusu ya watu walipotea.
Wanajeshi walikuwa askari wa kukodiwa ambao mara nyingi hawakulipwa bali walipewa uhuru wa kutwaa kwa mabavu
chochote walichotaka.
Uchovu ulileta
majadiliano juu ya amani. Mwaka 1648 wawakilishi wa wafalme walipatana katika amani ya Westfalia kuhusu kanuni za amani.
- Madhehebu matatu
yaliyokubaliwa Ulaya ni Wakatoliki, Walutheri na Wareformed;
mengine (kama Waanabaptisti na Umoja wa Ndugu) yaliangaliwa kuwa ya
kizushi popote.
- Kila mtawala aliamua
kwa dola lake ni yapi kati ya madhehebu matatu halali yatafuatwa lakini
raia walikuwa na haki ya kutoka katika nchi kama mtawala alikataa dini
yao. Sheria ilikuwa: "Cuius regio, eius religio" (mwenye nchi ni
mwenye kuamua dini)
- Katika maeneo kadhaa
Wakristo wa madhehebu tofauti walipewa ustahimilivu, lakini katika maeneo
mengine walipaswa kuhamia nchi ya madhehebu yao au kufuata madhehebu rasmi
ya nchi.
- Ikiwa mtawala
atabadili madhehebu baadaye wananchi wataruhusiwa kuendelea walivyozoea.
- Uholanzi
na Uswisi zilitoka katika Dola
Takatifu la Kiroma kama nchi huru
za pekee.
- Mfalme wa Uswidi
alitwaa maeneo makubwa katika Ujerumani ya Kaskazini
Kumbe mapatano hayo
yaliunda ramani ya kimadhehebu kule Ulaya yenye maeneo ya Wakatoliki,
Walutheri au Wareformati watupu. Jumuiya ndogo ziliendelea kugandamizwa
wakapata ustahimilivu mahali pachache. Hivyo wafuasi wa madhehebu madogo
walilazimika kuficha imani yao au kuhamahama katika Ulaya.
Wakati ule nafasi mpya
ilitokea: Mfalme wa Uingereza alikuwa na makoloni Marekani lakini alikosa watu.
Akatafuta walowezi kwa ajili ya makoloni yake akiwaahidia wote kwamba watapata
shamba pamoja na uhuru wa dini. Hivyo watu kutoka nchi nyingi za Ulaya walianza
kuhamia Marekani, hasa wale waliokosa uhuru huo. Mpaka leo nchi mbalimbali za
Ulaya zinafuata hasa madhehebu moja, na Marekani ina madhehebu makubwa ambayo
hayana wafuasi wengi Ulaya, k.mf. Wabatisti.
Umisionari kupamba tena
Fransisko Saveri
akimuongoa Paravas huko Goa, India, katika picha ya karne ya 19.
Wakati wa matengenezo na
mafarakano ulikuwa pia kipindi kilicholeta habari za nchi mpya kwa watu wa
Ulaya. Mataifa ya Wahispania na Wareno yalijenga aina mpya za meli zilizoweza kusafiri
kote duniani hata kuvuka bahari kubwa.
Wafanyabiashara na wanajeshi wao walizunguka pande zote za dunia
wakiambatana na mapadri wao. Hao walikutana na wenyeji wengi wa nchi mbalimbali
wasio Wakristo, au walikuwa Wakristo lakini si washiriki wa Kanisa Katoliki
(kama Waethiopia au Wahindi wa Kusini).
Wakaanza kuwaeleza
imani, wakahubiri mbele ya Mfalme wa China, mbele ya Negus Negesti wa Ethiopia na mbele ya watawala wa Amerika Kusini.
Tatizo la misheni hizo
lilikuwa kwamba liliambatana na uenezaji wa kijeshi wa Hispania na Ureno. Hasa Amerika wamisionari walijikuta kati ya mahitaji ya walowezi, waliotaka kuhudumiwa kiroho, na mahitaji ya wazalendo, waliogandamizwa vibaya na walowezi walewale.
Serikali ya kikoloni
ilikuwa vilevile serikali ya mfalme Mkatoliki. Haikuwa rahisi kwa wamisionari
kutofautisha kati ya pande hizo mbili. Mara nyingi Kanisa lilibariki tu utawala
wa kikoloni uliogandamiza wenyeji.
Lakini mara kwa mara
walijitokeza Wakristo wengine waliopinga unyama na kuleta taarifa za kweli kule Ulaya. Mmojawao alikuwa Askofu Bartolomeo Las
Casas aliyewashtaki walowezi
Wahispania kwa sababu waliua wenyeji wengi wakiwalazimisha kufanya kazi zao migodini na mashambani bila kujali afya zao. Akafaulu kuleta sheria zilizolinda Waamerika na kupunguza ukali dhidi ya watumwa,
lakini walowezi walijaribu kumwua.
Zaidi tena Wajesuiti
walijaribu kuwalinda Waindio wa Paraguay wakiwakusanya katika vijiji vya
ujamaa vilivyojitegemea kiuchumi na hata kisiasa. Lakini walishtakiwa na
walowezi majirani waliotaka kuwinda watumwa, ati wanadhoofisha utawala wa
kikoloni. Mwishoni Wajesuiti walifukuzwa na serikali, na vijiji vya Wakristo
wenyeji waliharibiwa na wawindaji wa watumwa.
Kule Asia mapadri wa Shirika la Yesu walifaulu kupanda mbegu ya Injili mpaka Japani na China. Walijitahidi kupatanisha Injili na utamaduni wa nchi hizo ambao ni tofauti na desturi za Ulaya.
Lakini uongozi wa Kanisa kule Roma uliwakataza wasitumie mbinu hizo. Hivyo
Wakristo wa Japan walionekana kufuata dini ya kigeni. Kwa sababu hiyo waligandamizwa,
ila wachache walishika imani yao kwa siri mpaka kutokea kwa uhuru wa dini katika karne ya 19.
Kati ya wote anakumbukwa
hasa Fransisko Saveri (Francisco de Jasso y Azpilicueta) (Javier, Navarra, leo nchini Hispania, 7 Aprili 1506 - kisiwa cha Shangchuan, China, 3 Desemba 1552), padri wa Shirika la Yesu, ambalo alichangia kulianzisha pamoja na Ignas wa Loyola.
Baadaye alitangaza Injili katika nchi nyingi za Ulaya, Afrika na Asia hata akawa kati ya wamisionari maarufu zaidi ya historia ya Kanisa.
Kati ya miaka 1500 na 1850 wamisionari Wakatoliki
walihubiri kwenye pwani ya Afrika, hata Afrika Mashariki. Walifuata uenezi wa Wareno waliojaribu kutawala
pwani hiyo kama vituo vya biashara kati ya Ulaya na Bara Hindi. Ustawi wa pekee ulipatikana katika ufalme wa Kongo (kusini kwa mto huo) ambapo Wakristo walifikia kuwa 50% za wakazi wote,
na kati yao alipatikana askofu Mwafrika wa kwanza kutoka Kusini kwa Sahara, Dom Enrique.
Kutoka kwa makao yao ya Sofala na Msumbiji walijaribu pia kutawala biashara ya dhahabu iliyochimbwa katika eneo la Mwene Mtapa (Zimbabwe).
Kati ya matunda bora ya
uinjilishaji huo wanakumbukwa "Mashahidi wa
Mombasa" waliomfia Yesu
mwaka 1631.
Mizizi ya Kanisa Afrika
ilikauka tena mnamo karne za 16-18 kwa sababu ya kuingiliana kwa hotuba ya
Injili na siasa ya ukoloni. Udhaifu wa kibinadamu uliongezea ugumu wa mazingira
na hali ya hewa kwa ajili ya wamisionari kutoka Ulaya.
Upietisti
Philipp
Jakob Spener (1635–1705) anaitwa pengine
"Baba wa Upietisti".
Upietisti (kwa Kiingereza Pietism, kutoka neno la Kilatini pietas, yaani heshima kwa Mungu, kwa wazazi, kwa ndugu na kwa nchi asili) ulikuwa tapo lenye athari kubwa kati ya
Walutheri, lakini pia kwa madhehebu mengine ya Uprotestanti, na hata kwa Wakatoliki huko Ulaya na Amerika Kaskazini[2] tangu mwishoni mwa karne ya 17.
Uliunganisha mikazo ya Kilutheri kuhusu mafundisho ya Biblia ya Kikristo na mikazo ya Kikalvini kuhusu maadili imara.
Asili yake ni Ujerumani ya leo na kazi ya Philipp Jakob
Spener, mwanateolojia Mlutheri aliyesisitiza mabadiliko ya Mkristo kwa aina ya kuzaliwa upya. Ingawa yeye hakudai
wafuasi wake wajitenge na Wakristo wenzao, mahimizo yake yalielekea huko.
Upietisti ulienea kwanza
Uswisi na nchi nyingine za lugha ya Kijerumani barani Ulaya, halafu Skandinavia na Baltiki (ulipoathiri zaidi tena utamaduni wa Kikristo kupitia watu kama Hans Nielsen
Hauge huko Norway, Carl Olof
Rosenius huko Sweden, Katarina
Asplund huko Finland na Barbara von
Krüdener katika nchi za
Baltiki), na hatimaye Ulaya nzima.
Kutoka huko ulipelekwa
Amerika Kaskazini, hasa kwa njia ya wahamiaji kutoka Ujerumani na Skandinavia,
ukaathiri Waprotestanti wenye asili tofauti ukachangia katika karne ya 18 mwanzo wa Ukristo wa
Kiinjilisti, ambao leo una waumini milioni mia tatu.
Tapo la Upietisti ndani
ya Ulutheri lilifikia kilele chake katikati ya karne ya 18, lilififia kati karne ya 19 na kutoweka Amerika mwishoni mwa karne ya 20.
Hata hivyo, baadhi ya
misimamo yake iliathiri Uprotestanti kwa jumla, ikimchochea kasisi Mwanglikana John Wesley kuanzisha tapo la Wamethodisti, na vilevile Alexander
Mack kuanzisha tapo la Schwarzenau
Brethren kati ya Waanabaptisti.
Huko Marekani, Upietisti ulitawala pia kati ya Quakers, Wakalvini, Wabaptisti, Waanglikana n.k.
Umisionari wa Kiprotestanti
Tumeshaona kwamba tangu
mwaka 1500 wamisionari Wakatoliki walienda sehemu mbalimbali za dunia. Katika karne ya 17 Waprotestanti walienea nje ya Ulaya, lakini bila
kumtangaza Kristo kwa wenyeji, kwa mfano katika makoloni ya Marekani mashariki
ya leo. Kumbe katika 18 walianza kuiga mifano ya wamisionari Wakatoliki.
Uenezaji wa Ukristo wa
Kiprotestanti ulianzishwa na Wakristo kutoka nchi za Ulaya zilizoendelea kama
Uingereza, Ufaransa na Ujerumani. Mapinduzi ya
viwandani yaliongeza sana uwezo
wa kiuchumi wa mataifa hayo.
Biashara ya
kimataifa ilianza kuunganisha
nchi za mbali sana. Vyombo vya usafiri kama vile meli, reli na baadaye hata ndege vilifikisha watu na bidhaa kila sehemu za dunia. Watu walianza kupata habari za nchi
zisizojulikana kwao mpaka wakati ule.
Wakristo wa nchi za
Ulaya walitumia mawasiliano hayo. Labda tunaweza kulinganisha hali hiyo na sera za mitume ambao
walitumia njia zilizofunguliwa na biashara ya Kiroma katika karne za kwanza.
Wengine waliona uwezo wao kama wito wa Mungu kwa Wakristo
wa Ulaya katika karne ile hasa.
Mahali pengi Ulaya
Wakristo hawakuridhika tena na hali ya Kanisa. Ukristo ulikwisha kuwa sehemu ya
utamaduni na jambo la kawaida. Bila kutafakari sana, mtoto alibatizwa,
akafundishwa na kupewa Kipaimara, akafunga ndoa kanisani, akawabatiza
watoto wake halafu akazikwa kwa ibada.
Kanisa lilikuwa kama idara ya serikali iliyosaidia
taifa kuweka utaratibu wa kidini kwa manufaa ya maadili ya umma. Serikali zilihimiza
watu washiriki na kuhudhuria ibada. Wasipofika kanisani waliweza kutozwa faini.
Lakini mazingira na hali
ya maisha vilibadilika. Watu walianza kuhamia mijini, jumuiya za vijiji
zilianza kulegea na kuvunjika.
Mahali pengi watumishi
wa makanisa hawakujua kujibu maswali mapya ila tu kukumbusha mazoea ya kale na mila nzuri za zamani.
Ndiyo asili ya matapo ya
uamsho yaliyotokea kwa nguvu
sana. Wasioridhika na hali hiyo walikutana nje ya makanisa. Katika maeneo ya
Kiprotestanti hali ilitegemea. Penye uongozi wenye busara walipewa nafasi zao shirikani. Watu waliguswa upya na neno la Mungu na Roho wake, walitafuta njia mpya za kuishi na kuonyesha imani
yao. Hivyo vilijitokeza vyama vya kusaidia wagonjwa, wajane, mayatima na maskini.
Penye uongozi mkali
uliokataa njia na mbinu mpya Wakristo walikutana na kusali katika nyumba za
watu. Wengine walianzisha jumuiya na madhehebu ya pekee. Lakini sehemu kubwa ya
Wakristo wa uamsho walielewa kazi yao ya kutengeneza upya makanisa yao badala
ya kuunda vikanisa vipya.
Katika maeneo ya
Wakatoliki matapo yaliyofanana na uamsho yalisababisha mara nyingi kutokea kwa
shirika jipya la watawa au la walei. Muundo wa Kanisa
Katoliki unasaidia kuwapa watu wenye wito au vipawa vya pekee nafasi zao katika
mashirika hayo.
Kanisa la Anglikana liliunda kamati ya kupeleka Injili katika nchi za
ng'ambo lakini ilishughulikia hasa Waingereza waliohamia makoloni. Polepole
wazalendo wachache walianza kuwaendea pia, jambo lililokuwa gumu kutokana na
hali ya ukoloni wenyewe.
Kanisa la kwanza la
Kiprotestanti lililotuma wamisionari hasa kwa watu wasiomjua Kristo lilikuwa ni
la Ndugu wa Herrnhut (Wamoravia).
Katika kijiji hicho kidogo cha Ujerumani waliishi wakimbizi kutoka
Moravia waliopewa ustahimilivu kuanzisha upya ushirika wa Umoja wa Ndugu
kufuatana na urithi wao kutoka Ucheki. Walikuwa watu wa kawaida kama wakulima
na mafundi.
Siku moja katika mwaka 1732 walikutana na mgeni,
kwa jina Antoni, mtumishi wa Mdenmark aliyemtembelea Mkuu wa Herrnhut, Ludwig von
Zinzendorf. Antoni alikuwa mtumwa mwenye asili ya Afrika aliyenunuliwa na bwana wake katika
Visiwa vya Karibi. Baadaye akapewa uhuru wake akasafiri pamoja na bwana wake
hadi Denmark.
Kwa Antoni Ndugu wa
Herrnhut wakasikia kwa mara ya kwanza habari za hali mbaya ya watumwa Waafrika
kule Karibi, na jinsi walivyozuiwa kusikia neno la Mungu pamoja na mateso yao
mengine. Usiku ule ndugu wawili wakasali pamoja na asubuhi yake wakamwendea Mkuu wa Herrnhut wakamwomba ruhusa
ya kusafiri hadi Karibi ili wawahubirie wale watumwa. Katika sala hiyo ya
maseremala wawili ilianza kazi ya misheni ya Umoja wa Ndugu (Wamoravia).
Baadaye Ndugu Wamoravia
waliendelea kuhubiri kule Greenland, Urusi, Nikaragua, Afrika Kusini na kati ya Waindio wa Amerika. Mawasiliano mapya
yakaleta habari hiyo katika kila pembe ya dunia zisizosikika zamani kwa watu
wengi.
Wamoravia walihubiri
mahali pengi Ulaya kati ya Wakristo wa madhehebu yote bila kuwashawishi
wajiunge nao lakini walieneza sana habari za misheni.
Wakiitikia mfano wa
Ndugu wa Herrnhut Wakristo kutoka vikundi mbalimbali vya uamsho walianza
kuelewa wajibu wao wa kueneza Injili kote duniani.
David Livingstone (1813-1873) kutoka Uskoti ni kati ya wamisionari bora wa Afrika.
Mnamo mwaka 1800 Wakristo Waingereza
waliunda vyama mbalimbali vya misheni, kama Wabatisti mwaka 1792, Chama cha Misheni cha
London mwaka 1795 na Chama cha Misheni cha Kanisa (la Kianglikana = Church
Missionary Society/CMS) mwaka 1799. Waprotestanti wa nchi nyingine za Ulaya
walifuata.
Mara nyingi wakati ule
si viongozi wa madhehebu ya Kiprotestanti (isipokuwa kwa kiasi Waanglikana)
walioendesha kazi ya misheni, kwa kuwa walijali maeneo yao tu wakikosa mtazamo
wa dunia nzima kama wenzao Wakatoliki.
Kumbe walikuwa walei na
wachungaji wa kawaida waliounda vyama vya misheni, kuiombea kazi hiyo, kutafuta
habari za nchi nyingine na kuchanga pesa wakiandaa vijana watakaokuwa tayari kuacha ndugu zao wakielekea nchi za
mbali zisizojulikana nao.
Kanisa Katoliki na la
Kiorthodoksi katika karne ya 18
Wakati Ukristo ulipozidi
kuenea na kuchangamka katika bara lote la Amerika, huko Ulaya Kanisa Katoliki
lilipitia kipindi cha udhaifu, hasa kutokana na mashambulizi ya falsafa ya
Mwangaza dhidi yake.
Falsafa hiyo ilienea
katika matabaka ya juu ya nchi nyingi na kufuatwa na serikali zake, ambazo
zilianza kulibana kwa njia nyingi, hasa kwa kuzuia mashirika ya kitawa.
Mambo yalizidi kuwa
magumu Mapinduzi ya
Ufaransa yalipopiga vita dini,
kuanzia Ukatoliki. Akili ilisimikwa kama mungu mpya. Kalenda mpya ilitengenezwa ili kufuta wiki na Jumapili
pamoja na sikukuu za
Kikristo. Monasteri zote
zilibomolewa, wengi waliuawa au kufukuzwa nchini kwa sababu ya imani yao. Mali
za Kanisa zilitaifishwa na mapadri walidaiwa kula kiapo cha kufuata serikali
badala ya Papa. Mnamo 1799 Papa Pius VI alitekwa hadi Ufaransa na hatimaye kufa kifungoni.
Kiongozi wa Ufaransa, Napoleon Bonaparte, alizidi kueneza
misimamo mipya katika sehemu kubwa ya Ulaya aliyoiteka.
Hata Waorthodoksi
walipata shida za namna hiyo hasa Urusi, ambapo mwaka 1721 Kaisari Petro I alifuta Upatriarki nchini na kuweka Kanisa
moja kwa moja chini ya serikali.
Ukristo katika karne ya 19
Pius IX, Papa
aliyeongoza Kanisa kwa muda mrefu kuliko wote (1846-1878).
Baada ya Ufaransa wa
Napoleon kushindwa (1815), nchi za Ulaya zilikubaliana kurudisha hali ilivyokuwa
kabla ya mapinduzi, lakini haikuwa rahisi. Umati wa watu ulizidi
kusogea mbali na dini.
Baada ya mateso yao, Papa na Kanisa
Katoliki walipewa tena heshima, lakini siasa iliendelea kuwa dhidi
yao.
Kilele chake ni Kulturkampf (kwa Kijerumani: vita vya utamaduni) iliyotangazwa na Chansela Bismarck ili kuzuia umoja wa Wakatoliki wa Ujerumani na Papa.
Majimbo na parokia nyingi vilibaki bila mchungaji, mapadri wengi
walifungwa n.k.
Kabla ya hapo, Papa Pius IX alikutanisha maaskofu mjini Roma kwa Mtaguso wa kwanza
wa Vatikano (1869-1870) uliotangaza dogma ya karama ya Papa kutokosea anapotoa mafundisho ya moja kwa moja
"ex cathedra".
Mtaguso ulikatishwa na
jeshi la Italia lililovamia Roma na kuuteka moja kwa moja, likikomesha Dola la Papa (1870). Tukio hilo lilimkomboa Papa kutoka majukumu
ya kisiasa na kumwezesha kuimarisha mamlaka yake ya kiroho duniani kote dhidi
ya utaifa uliotesa Kanisa kwa karne kadhaa.
Karne ya 19 iliona pia
Wakatoliki kuchangamkia tena umisionari, kuanzia Wafaransa.
Jambo lingine la pekee
katika Kanisa Katoliki la karne hiyo ni uundaji wa mashirika ya kitawa ya kike
na ya kiume zaidi ya 2000 yaliyolenga huduma maalumu, k.mf. kuhubiri vijijini, kulea vijana, kufundisha mafukara, kuuguza wagonjwa, kuanzisha misheni, kushughulikia upashanaji
habari. Mara nyingi mashirika
hayo yanafanana ingawa yalianzishwa wakati na mahali tofauti, kwa kawaida chini
ya askofu wa jimbo, baada ya mashirika ya zamani kuzuiwa na serikali.
Kati ya waanzilishi
muhimu zaidi wakumbukwe Karolo Yosefu
Mazenod (1782-1861), Vinsenti Pallotti (1795-1850), Antoni Maria
Claret (1807-1870), Yohane Bosco (1815-1888), Daniele Comboni (1831-1881), Arnold Janssen (1837-1909). Kati ya wanawake, Yoana Antida
Thouret (1765-1826), Magdalena wa
Canossa (1774-1835), Visensya Gerosa (1784-1847) pamoja na Bartolomea
Capitanio (1807-1833), Fransiska Saveri Cabrini (1850-1917).
Uprotestanti uliendelea
kufaidika na uamsho, ingawa huko Marekani walifikia hatua ya kuanzisha
madhehebu mengi ya aina mpya, yaliyojaribu kuanza kila kitu upya kwa msingi wa
Biblia, yakidharau historia yote ya Kanisa kama upotoshaji wa imani.
Miaka ya mwisho ya karne
ya 19 iliona ustawi wa elimu ya
Biblia iliyoongozwa na mawazo
mapya kabisa yaliyoyumbisha imani ya wengi kwa kukanusha mambo yapitayo maumbile (teolojia ya Usasa).
Karne ya 20
Papa Yohane Paulo II (1978-2005) anahesabiwa na
wanahistoria kadhaa kama mtu aliyeathiri ulimwengu kuliko watu wote wa karne ya 20, hasa kwa
kusambaratisha Ukomunisti na kumaliza vita baridi.
Wakati Ulaya ulipozidi
kuachana na dini, Ukristo ulienea kwa kasi ya ajabu katika bara la Afrika, na
kwa kiasi tofauti katika maeneo mengine yasiyokuwa na mapokeo hayo.
Mang'amuzi ya
kimisionari yalifanya Wakristo watambue upya haja ya umoja kati yao. Walianza
Waprotestanti (Kongamano la
Edinburgh, 1910), halafu Waorthodoksi
na Wakatoliki.
Masomo ya liturujia na
uchungaji pamoja na uchunguzi wa maandishi ya mababu wa Kanisa vilileta pumzi
mpya katika madhehebu mbalimbali.
Mtaguso wa pili wa
Vatikano (1962-1965) ulioitishwa na Papa Yohane XXIII ulielekeza Kanisa Katoliki kukabili vema ulimwengu
wa kisasa badala ya kuulaumu tu.
Lakini karne ya 20
inakumbukwa hasa kwa dhuluma za kidini zisizowahi kutokea: hasa Ukomunisti, ulioteka Urusi ukaenea polepole hadi kutawala theluthi moja ya binadamu wote, ulipiga vita dini kwa namna
zote na kuua mamilioni ya waamini, hasa Waorthodoksi.
Hatimaye, chini ya Papa Yohane Paulo
II, wa kwanza kutoka
mataifa ya Kislavi, Wapolandi walifaulu kuangusha serikali ya Kikomunisti,
wakifuata na wenzao wa nchi zote za Ulaya Mashariki.
Baada ya hapo, Ukristo
uliamka upya katika nchi hizo.
Maoni