Historia ya Wokovu
Historia ya Wokovu
Jinsi Pietro
Perugino alivyochora Mateso ya
Yesu msalabani kwa mtindo wa Stabat Mater, yaani akiwa na Bikira Maria na Mtume Yohane chini yake (1482). Kifo na ufufuko wa Yesu ndiyo kilele cha
historia ya wokovu kwa imani ya Ukristo.
Kwa jina hilo Wakristo wanamaanisha ufafanuzi wa mpango wa kazi ya Mungu kwa wokovu wa binadamu kadiri ya Biblia.
Yaliyomo
- 1 Maana ya historia
- 2 Maana ya wokovu
- 3 Imani kuhusu Biblia
- 4 Agano la Kale
- 4.1 Vitabu vitano vya Torati
- 4.2 Uumbaji
- 4.3 Dhambi ya asili
- 4.4 Watu walivyoishi baada ya dhambi
- 4.5 Nuhu
- 4.6 Mnara wa Babeli
- 4.7 Abrahamu (1900-1800 hivi K.K.)
- 4.8 Watoto wa Isaka: Esau na Yakobo
- 4.9 Yosefu na ndugu zake kushukia Misri (1700
hivi K.K.)
- 4.10 Utumwa wa Misri na wito wa Musa (1250 hivi
K.K.)
- 4.11 Mapigo ya Wamisri
- 4.12 Safari ya kuendea Nchi ya ahadi
- 4.13 Agano la Mlima Sinai
- 4.14 Ndama ya dhahabu
- 4.15 Mungu kujifunua tena kwa Musa
- 4.16 Mambo ya Walawi
- 4.17 Hesabu
- 4.18 Kumbukumbu la Torati (Sheria)
- 4.19 Vitabu vinavyofuata Kumbukumbu la Torati
(Sheria)
- 4.20 Yoshua (1210-1200 hivi K.K.)
- 4.21 Waamuzi (1200-1025 hivi K.K.)
- 4.22 Ruthu
- 4.23 Samweli (1050-1015 hivi B.C.)
- 4.24 Mfalme Sauli (1030-1010 hivi K.K.) na
mfalme Daudi (1010-970 hivi K.K.)
- 4.25 Vitabu vya Wafalme
- 4.26 Mfalme Solomoni (970-931 hivi K.K.)
- 4.27 Manabii
- 4.28 Manabii Eliya na Elisha (865-790 hivi
K.K.)
- 4.29 Nabii Amosi (786-746 hivi K.K.)
- 4.30 Nabii Hosea (750-725 hivi K.K.)
- 4.31 Nabii Isaya (740-700 hivi K.K.)
- 4.32 Nabii Mika (740-700 hivi K.K.)
- 4.33 Nabii Sefania (640-625 hivi K.K.)
- 4.34 Nabii Yeremia (626-585 hivi K.K.)
- 4.35 Nabii Habakuki (600 hivi K.K.)
- 4.36 Nabii Ezekieli (592-570 hivi K.K.)
- 4.37 Isaya II na III (550-500 K.K. hivi)
- 4.38 Wayahudi kuanza upya Yerusalemu chini ya
Waajemi (538-333 K.K.)
- 4.39 Manabii wa mwisho wa Agano la Kale
- 4.40 Vitabu vya Hekima vya kwanza
- 4.41 Uenezi wa utamaduni wa Kiyunani (333-63
K.K.)
- 5 Agano Jipya
- 5.1 Mazingira ya Yesu
- 5.2 Maisha ya Yesu
- 5.3 Ufunuo kuendelea baada ya ufufuko wa Yesu
- 5.4 Kitabu cha Matendo ya Mitume
- 5.5 Kanisa la Yerusalemu
- 5.6 Ukristo ulivyoanza kuenea
- 5.7 Safari za kimisionari za Paulo zilivyoanza
(46-49)
- 5.8 Mtaguso wa Yerusalemu (49)
- 5.9 Barua au nyaraka
- 5.10 Safari ya pili ya Mtume Paulo (50-52)
- 5.11 Barua mbili kwa Wathesalonike
- 5.12 Safari ya tatu ya Mtume Paulo (54-58)
- 5.13 Barua kwa Wagalatia
- 5.14 Barua kwa Wafilipi
- 5.15 Barua kwa Filemoni
- 5.16 Barua mbili kwa Wakorintho
- 5.17 Barua kwa Waroma
- 5.18 Ukristo baada ya Paulo kufika Roma
- 5.19 Barua kwa Wakolosai
- 5.20 Barua kwa Waefeso
- 5.21 Barua tatu za Kichungaji
- 5.22 Barua ya kwanza ya Petro
- 5.23 Barua kwa Waebrania
- 5.24 Injili Ndugu
- 5.25 Barua ya Yakobo
- 5.26 Barua ya Yuda
- 5.27 Barua ya pili ya Petro
- 5.28 Ufunuo wa Yohane
- 5.29 Injili ya Yohane
- 5.30 Barua tatu za Yohane
Maana ya historia
Historia ni mfululizo wa habari za mambo yaliyotokea pamoja
na sababu zake. Binadamu anaziandika ili kuelewa maisha yake, yaani ametokea
wapi, amepata mafanikio gani na matatizo gani. Historia inatufundisha kuishi:
kumbukumbu za mambo ya zamani (vita, uhuru, viongozi na mengineyo)
zinatuwezesha kuendelea vizuri zaidi. Lakini ni muhimu zaidi kujua mambo makuu
aliyoyatenda Mungu ili kutuokoa. Dini ya Uyahudi na ya Ukristo ni dini zinazotegemea historia kuliko maumbile: Mungu hatazamwi kama Muumba tu, bali zaidi kama Mwokozi.
Maana ya wokovu
Wokovu ni kazi ya Mungu
kwa ajili yetu (1Tim 2:4; 2Tim 1:9-10). Sisi hatuwezi kujikomboa, lakini Mungu ana nguvu
kuliko shetani na mabaya yote, naye anatuhurumia sisi maskini (Kol 1:13-14). Alifanya nini
ili kutuokoa? Ndiyo historia ya wokovu. Wapo walioiandika katika Biblia ili
tusadiki na kuishi upya (1Pet 1:10-12). Humo mtu hatazamwi kama nafsi ya peke yake tu, bali
zaidi kama mtu wa taifa lake; hivyo Mungu anatangazwa kuwa hashughulikii wokovu wa
mtu binafsi tu, bali wa mataifa mazima pia, kuanzia lile la Israeli. Aliyowatendea wao ni hasa kuwatoa utumwani Misri, kuwapa agano na masharti yake li
awafanye taifa huru katika nchi bora.
Waisraeli walijenga imani yao juu ya hayo mang’amuzi ya msingi ya wokovu kutoka kwa
Mwenyezi Mungu, halafu wakajikumbusha kwamba alikuwa ameshawaahidia mababu wao baraka kama hizo. Hatimaye tu walitafakari juu ya asili ya watu
na ya ulimwengu, wakaelewa kuwa Mungu aliweza kuwaokoa kwa sababu
ndiye aliyeumba vyote: hakuna wa kushindana naye na wa kuzuia mpango wake kwa
ajili ya watu. Kwa Wakristo tukio kuu lililo msingi wa imani ni ufufuko wa Yesu, aliyetoka kaburini mzima na mtukufu, wa kwanza kati ya umati, akaingia katika nchi
ya walio hai kweli.
Imani kuhusu Biblia
Biblia iliyochapwa na Johannes Gutenberg mwaka 1455 hivi. Ndiyo ya kwanza
kutonakiliwa kwa mkono.
Wakristo wanasadiki
Biblia imeandikwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu (2Pet 1.20-21; 2Tim 3:16): ndiyo sababu
wanaiheshimu sana. Lakini habari zake hazifuati mpangilio wa tarehe. Wapo wataalamu waliozipanga kwa utaratibu huo
unaotupendeza zaidi siku hizi: wamejitahidi kuelewa tarehe ya matukio na ya
maandiko yote ili kuyapanga moja baada ya lingine kuanzia ya zamani za kale
hadi maisha ya Yesu na ya Mitume wake. Lakini tukumbuke daima kwamba lengo la Biblia si
kueleza sayansi, jiografia wala historia, bali ni kufundisha kwa ukweli njia ya
wokovu. Taarifa nyingine zinategemea ujuzi wa mtu aliyeandika na mtindo
alioutumia: sheria, taratibu za
ibada, nasaba, ufafanuzi wa majina, maneno matakatifu ya mahali fulani, baraka, hadithi, simulizi, historia halisi n.k.
Sehemu kuu mbili za
Biblia ni Agano la Kale na Agano Jipya (2Kor 3:10; Eb 8:13). La Kale limeandikwa kabla ya Yesu, Jipya baada
yake. Hata hivyo Agano la Kale lina utabiri mwingi juu ya Yesu (Lk 24:27,44), na Agano
Jipya linarudia na kufafanua habari nyingi za kale: hivyo tunatakiwa kusoma
daima Agano la Kale kwa mwanga wa Agano Jipya, na kutafuta katika habari za
kale mifano inayotusaidia kuelewa mambo ya Yesu na Kanisa (1Kor 10:11; Kol 2:17). Kwa kuwa ufunuo wa Mungu ulifanyika hatua kwa hatua hata ukakamilishwa na
Yesu (Eb 1:1-2), hatuwezi kutegemea dondoo moja tu kuhusu jambo
fulani, bali tuzingatie jambo hilo lilivyoozungumziwa tangu mwanzo hadi mwisho
wa ufunuo. Tunahitaji kujua Biblia nzima ili kuelewa jinsi Mungu alivyo, alivyotuokoa
na anavyotaka tuishi.
Vitabu vya Biblia ni 73:
yaani 46 katika Agano la Kale na 27 katika Agano Jipya. Ndivyo vilivyokubaliwa
na Kanisa Katoliki kuwa ni Neno la Mungu. Waprotestanti wengi wanakataa vitabu 7 vya Agano la Kale (pamoja
na sehemu chache za vingine): hivyo Biblia yao inavyo 66 tu.
Mgawanyo wa vitabu hivyo
si muhimu, mradi tusiongeze wala kupunguza neno. Kwa kawaida vinapangwa kwa
kuzingatia vinaleta habari za namna gani. Hivyo katika Agano la Kale
yanatofautishwa makundi manne: Torati (yaani sheria), vitabu vya historia ya Israeli, vitabu vya manabii (waliotumwa na Mungu ili kuwaonya na kuwafariji
Waisraeli), na vitabu vya hekima (vyenye nyimbo, mashairi, mithali n.k.).
Katika Agano Jipya tuna vitabu 5 vya historia (yaani Injili 4 na Matendo ya Mitume), barua 21 za Mitume na kitabu kimoja tu cha kinabii
(Ufunuo).
Lugha asili ziko tatu,
yaani Biblia imeandikwa sehemusehemu kwa Kiyahudi, Kiaramu (ndiyo lugha ya Yesu), na Kiyunani (yaani Kigiriki cha zamani). Ila Agano Jipya lote limeandikwa kwa
Kiyunani ambacho zamani za Yesu kilikuwa lugha ya kimataifa. Kutoka lugha hizo
wataalamu wanaendelea kutafsiri Biblia katika lugha yoyote ili Neno la Mungu
liwaelee watu wote. Kati ya tafsiri zote, mbili za zamani zina sifa za pekee,
yaani tafsiri ya LXX (kwa Kigiriki "Septuaginta", yaani sabini: ni Agano Kale kwa lugha ya
Kiyunani), na ya Vulgata (Biblia nzima kwa Kilatini).
Maelezo ya Kanisa yanahitajika
kwa sababu: kwanza mwenyewe sielewi maandiko hayo yameandikwa na nani, lini,
wapi, kwa lengo lipi na katika mazingira ya namna gani. Hasa Roho Mtakatifu hakunipa Biblia peke yangu, bali ndani ya taifa lote
la Mungu. Hivyo sina haki ya kuifafanua ninavyotaka. Wasio na elimu na msimamo
wanapotosha Biblia na kupotea (2Pet 3:16).
Agano la Kale
Vitabu vya Agano la Kale
Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati
II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki
Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.
Vitabu vitano vya Torati
Kitabu cha Torati katika
Sinagogi la Cologne, Ujerumani.
Vitabu vya kwanza vya
Biblia (Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la
Torati) vinaunda kwa pamoja
Torati (kwa Kiyahudi “fundisho”, yaani “sheria”). Mgawanyo wa kawaida wa
Kiyahudi wa vitabu vya Biblia katika makundi matatu (Torati, Manabii na
Maandishi) unaonyesha jinsi vitabu vitano vya kwanza vinavyotazamwa kuwa kitu
kimoja, tena kiini cha Agano la Kale lote. Ajabu la Torati ni jinsi
inavyounganisha mambo mbalimbali: ibada kwa Mungu pekee, ahadi zake, matakwa
yake, uasi wa binadamu na ukombozi wa Kimungu, wito wa kujali mwanzo wa taifa la Mungu.
Humo tunakuta muhtasari
wa historia kuanzia uumbaji wa ulimwengu hadi kifo cha Musa: historia ya asili (Mwa 1-11), kipindi cha mababu (Mwa 12-36), simulizi
la Yosefu (Mwa 37-50), ukombozi toka Misri na safari kwenye Sinai (Kut 1-18), toleo la sheria
mlimani huko (Kut 19 – Hes 10), safari hadi mabonde ya Moabu (Hes 10-36) na nyongeza
(Kumb 1-34).
Zamani Musa alidhaniwa
kuwa mwandishi wa vitabu hivyo vyote. Siku hizi wataalamu wamethibitisha kuwa
ndiye asili ya kiini cha sheria za Israeli, lakini vitabu hivyo viliandikwa katika kipindi
kirefu hadi mwaka 400 hivi K.K. Ndiyo sababu katika sheria za vitabu hivyo
yanaonekana mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika karne hadi karne, k.mf. kuhusu Pasaka na umoja wa hekalu. Waliohusika na uandishi ni watu wengi wa Israeli
Kaskazini na Kusini. Hasa yameainishwa mapokeo manne tofauti: J (yaliyoandikwa
katika karne X K.K. kwa kumuita Mungu YHWH), E (ya karne IX K.K. yanayomuita Elohim), D (yanayotawala Kumbukumbu ya
Torati: ni ya karne VII K.K.) na P (yaani ya kikuhani kwa kuwa yanajali sana ibada: ni ya karne VI K.K.). Hayo ya mwisho yalitumika kama fremu ya mapokeo
hayo yote ili kuunganisha Torati nzima katika karne V K.K. Hivyo Torati inatunza matukio ya msingi na imani ya
taifa la Israeli jinsi ilivyozidi kukomaa baada ya Musa.
Uumbaji
Uumbaji (1896–1902), mchoro wa James Tissot.
Uumbaji unasimuliwa katika sura mbili za kwanza za Mwanzo.
Kama vile sehemu mbalimbali za Biblia, kitabu hicho kilitungwa kwa kushona
pamoja maandishi tofauti. Ndiyo sababu tunakuta masimulizi mawili juu ya Mungu
kuumba ulimwengu na watu.
La kwanza (1:1-2:4a)
linamchora Mungu akifanya kazi kama binadamu kwa siku sita halafu kustarehe.
Aliumba kila kitu kwa Neno lake (Eb 11:3; ndiye Mwanae pekee:
Yoh 1:1-18). Wengine wanaona humo hata kidokezo cha kwanza cha
Roho Mtakatifu, aliye upendo wa Mungu, katika upepo uliovuma juu ya wingi wa
maji. Mungu aliona kila alichokiumba ni chema tu, lakini alipoumba mtu katika jinsia mbili akaona ni mwema sana, ni bora kuliko vingine,
akamweka kuvitawala kwa niaba yake. Mwanamume na mwanamke wana hadhi sawa kwa
kuwa wote wawili ni sura na mfano wake, si upande wa mwili, bali hasa kwa roho yenye uwezo wa kuelewa
na kupenda kwa hiari.
Muumba anataka watu
washirikiane na kusaidiana, kilele cha uhusiano wowote kati yao ni ndoa inayowafanya kuwa mwili
mmoja kama Kristo na Kanisa (Ef 5:31-32).
Simulizi linalofuata (Mwa 2:2b-25) ni la zamani
zaidi, nalo pia lina mafundisho makuu juu ya Mungu na mtu, hasa kwamba huyo
ndiye kiumbe bora anayeweza kushirikiana na Mungu tofauti na vingine. Hali yake
asili ilikuwa ya kupendeza kabisa kwa usafi wa moyo na uhai usio na mwisho, naye alitakiwa akubali kazi
za Mungu na kufuata maneno yake, bila ya kujiamulia nini jema, nini baya.
Michelangelo alivyochora katika kuta za Cappella Sistina huko Vatikano dhambi ya Adamu na Eva na adhabu iliyofuata ya kufukuzwa bustanini.
Mwa 3 inasimulia dhambi iliyo asili ya dhambi zote (Rom 5:12). Kwa njia hiyo
tunaambiwa hali yetu mbaya haitokani na Mungu, bali na uasi wetu na wa wazee
wetu (Hek 2:23-24). Pia tunafundishwa kukataa toka mwanzo vishawishi
vyetu tukiamini maagizo yote ya Mungu yametolewa kwa upendo mkuu. Shetani ndiye aliyeanzisha kishawishi. Eva alipaswa asimsikilize. Kosa lake la kwanza ni kumjibu:
hivyo shetani akamdanganya kwamba, eti Mungu ana kijicho, hataki watu walingane naye, ndiyo sababu
aliwakataza (Yoh 8:44). Tukianza kuzingatia kishawishi tunakubali shaka juu
ya wema wa Mungu kwetu katika kutuelekeza. Kwa namna hiyo walianguka watu wa
kwanza waliokuwa watakatifu; kwa urahisi zaidi tutaanguka sisi wenye tabia mbaya kutokana na dhambi hiyo
na nyingine nyingi.
Hata baada ya dhambi
Mungu anamtafuta mtu kwa upendo, ila huyo kwa aibu anamkimbia, au
akijisikia analaumiwa na dhamiri, basi anatafuta visingizio hata kumlaumu Mungu kana
kwamba ndiye aliyesababisha. Kwa utakatifu wake Mungu hawezi kuvumilia maovu, na kwa haki yake anataka makosa
yalipwe. Ndiyo sababu tunakuta matatizo maishani, kama vile uchungu wa
uzazi, kuhusiana kwa mabavu,
kupata riziki kwa shida, na hasa kufa: hayo yote ni matokeo ya dhambi. Pamoja na hayo Mungu
hapendi mtu yeyote apotee (2Pet 3:9), hivyo toka mwanzo aliahidi kwamba mzawa
wa Eva atamponda kichwa shetani. Ndiyo habari njema ya awali kuhusu wokovu
ujao.
Watu walivyoishi baada ya dhambi
Kaini na Abeli, mchoro wa karne ya 15 kutoka kitabu cha Ujerumani Speculum Humanae Salvationis.
Baada ya dhambi ya asili watu walianza kuzaa. Mwa 4:1-16 inatuchorea picha ya
Kaini na Abeli kama wazaliwa wa kwanza waliotofautiana kiadili (1Yoh 3:11-12). Toka mwanzo
mwovu na mwadilifu waliishi pamoja, wa kwanza akimdhulumu wa pili hata kumuua
bila ya kujali udugu. Ikisikitishwa
kufikiria mzaliwa wa kwanza kuwa muuaji wa mdogo wake, inafurahisha kwamba wa
kwanza kufa alikuwa mwema, kielelezo cha Yesu aliyeuawa bila ya kosa (Eb
12:24).
Toka mwanzo hao
walimuabudu Mungu kwa njia ya dini, ibada na sadaka mbalimbali. Hata hivyo Mungu akakubali zile tu
zilizotolewa kwa ukarimu (Eb 11:4). Tangu hapo
Biblia inatuonyesha jinsi alivyopendelea wadogo kuliko wakubwa.
Kuhusu Kaini
tunaonyeshwa ustawi wa
dhambi ndani mwake na uongozi
wa Mungu aliyemtaka ashinde dhambi bado mlangoni. Hata baada ya dhambi hiyo
ambayo ni kubwa kiasi cha kumlilia Mungu alipe kisasi, yeye alizidi
kumhifadhi Kaini.
Baadaye (Mwa 4:17-24)
kukawa na maendeleo ya aina mbalimbali: ujenzi, ufundi, muziki, lakini hasa dhambi. Picha yake ni Lameki, mtu wa kwanza kuwa na mitara, mkatili kama nini. Ingawa hali ilikuwa ya kukatisha
tamaa, kwa baraka ya Mungu watu wakazidi kuzaa na kati ya watoto wao
wakapatikana waadilifu kama Henoko aliyestahili kutwaliwa na Mungu. Hata hivyo ongezeko la
dhambi likasababisha maisha ya binadamu yafupike (Mwa 6:3) kwa kuwa ni kusogea
mbali na Mungu, chemchemi ya uhai.
Nuhu
Sadaka ya Nuhu ilivyochorwa na Daniel
Maclise.
Mwa 6:5-9:17
inatufundisha kwamba Mungu anachukizwa na dhambi, hivyo anataka kuondoa maovu
duniani ili nchi impendeze kama alivyokusudia alipoiumba. Kwa ajili hiyo zamani
za Nuhu alileta maji yafunike dunia na kuzamisha waovu. Lakini
alisalimisha waadilifu katika safina kubwa ya kutosha, halafu akafunga nao agano thabiti (Eb 11:7). Hasa
maji yanayokusudiwa kutakasa dunia yote ni yale ya ubatizo (1Pet 3:17-22), na safina ambayo iokoe watu ni
Kanisa, ambalo ni la lazima kwa wokovu kama vile ubatizo unaotuingiza ndani
yake.
Uso wa nchi
ulipokwishatakaswa na maji njiwa akarukaruka akachuma tawi la mzeituni unaozaa matunda ya kutengenezea mafuta. Njiwa akaonekana tena juu ya maji siku ya ubatizo wa Yesu ambapo alipakwa Roho Mtakatifu na kuyatia maji nguvu
ya kutakasa watu (Mk 1:9-11; Tito 3:3-7). Maji na mafuta ndiyo mwanzo mpya kwa binadamu.
Mara alipotoka safinani
Nuhu alimtolea Mungu sadaka iliyompendeza hata akaahidi hataangamiza tena
binadamu kila anapostahili. Sadaka hiyo ni mfano wa ile ya Yesu msalabani,
inayoadhimishwa katika ekaristi, ikituondolea adhabu nyingi na kutuletea huruma ya Mungu, yaani nafasi na neema ya kutubu (Tito 2:11-14).
Hatimaye kutakuwa na hukumu (Math 24:37-41).
Mnara wa Babeli
ulichorwa mara nyingi na wasanii kama katika picha hii ya Pieter Brueghel
Mzee.
Mwa 11:1-9 inatufundisha
kwamba kiburi na dhambi kwa jumla vinatenganisha watu wasiweze kuelewana
wala kuishi pamoja. Kinyume chake katika Agano Jipya tunasikia kwamba siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu, aliye upendo wa Mungu, aliunganisha
tena watu wa makabila mbalimbali katika kutangaza sifa zake (Mdo 2:5-12). Palipo na
upendo, tofauti za lugha na utamaduni si shida.
Abrahamu (1900-1800 hivi K.K.)
Mwanzo wa safari ya
Abrahamu ulivyochorwa na József
Molnár.
Mtu huyo, aliyezaliwa Mesopotamia (Iraq) baada ya watu kubuni uandishi, ndiye mwanzo wa taifa teule la Mungu na baba wa
waamini wote. Aliishi kwa kuhamahama pamoja na mifugo yake: akipitia Syria alifikia nchi ya Kanaani aliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu akashukia Misri kwa muda (Mwa 12). Lakini safari yake muhimu zaidi ni ile
ya imani, kwa kuwa Abrahamu aliongozwa na Mungu siku kwa siku, katika mazuri na
magumu, akisadiki ahadi zake za ajabu (Eb 11:8-19). Mchungaji huyo alikubali
Mungu amchunge maisha yake yote, akamfuata bila ya wasiwasi, akituachia mfano
bora wa kumshika mkono Mungu daima bila ya hofu.
Mungu akimuagiza Abramu
kuhesabu nyota; mchoro wa Julius Schnorr von Carolsfeld (1860).
Hasa Mungu alimuahidia
uzao mkubwa kama nyota za mbinguni, naye akaamini ingawa alikuwa hajapata hata
mtoto mmoja: ndiyo imani iliyompendeza sana Mungu (Mwa 15:1-6).
Mwa 18 inamchora kama
mtu mkarimu sana kwa wageni, rafiki wa Mungu anayestahili kuambiwa yote, mwenye
huruma, busara na unyenyekevu katika sala. Wageni wake watatu
ambao ni kama mtu mmoja tu wanadokeza Utatu Mtakatifu. Mungu
alimdai Abrahamu asadiki kwamba anaweza yote kama atakavyomdai Bikira Maria (Lk 1:17), naye alidumu kumuomba awahurumie waovu kwa ajili ya
waadilifu (Yak 5:16).
Mwa 19 inatuchorea uovu
wa watu ambao huko Sodoma ulizidi hata kumdai Mungu alipe kisasi. Lakini kati yao
mwadilifu akaokolewa, isipokuwa mke wake akaja kuadhibiwa kwa sababu aliangalia
nyuma kinyume cha agizo la Bwana (Lk 17:28-33).
Mwa 21:1-21 inatusimulia
jinsi Mungu alivyotimiza ahadi yake kwa kumjalia Sara amzalie Abrahamu mtoto Isaka katika uzee na utasa. Isaka ni mtoto wa
imani, si wa mwili, naye ni huru, tofauti na Ishmaeli mtoto wa mtumwa ambaye hastahili kurithi pamoja na
mdogo wake. Isaka, baba wa Israeli alipata baraka kuu, naye ni mfano wa watu wa
Agano Jipya. Ishmaeli, baba wa Waarabu alibarikiwa pia kwa ajili ya baba yake, naye ni
mfano wa Agano la Kale ambapo watu wanategemea mambo ya kimwili (kutahiriwa,
kunawa, kubagua vyakula n.k.) na hivyo ni watumwa (Gal 4:21-5:1).
Mwa 22:1-19 inatuletea
habari ya kusisimua kuhusu sadaka ambayo Mungu alimdai Abrahamu, yaani
kumchinja Isaka. Ni kimoja kati ya vilele vya imani ya binadamu, imani
inayoonyeshwa kwa matendo ya utiifu (Yak 2:21-22). Abrahamu hakusita kumrudishia Mungu kile
alichopewa, akaondoka alfajiri akasafiri mpaka mahali alipoambiwa (Wayahudi wanaamini
mlima huo ndipo walipojenga hekalu la Yerusalemu). Kwa niaba ya waamini wote Abrahamu alikuwa tayari
kumchinjia Mungu mwanae pekee ampendaye. Lakini atakayemtoa kweli Mwana pekee ni Mungu Baba (Yoh 3:16). Mwanae ndiye mwanakondoo aliyeuliziwa na Isaka
na ambaye Mungu akajipatia juu ya mlima Kalivari alioupanda huku amejitwika sio kuni bali mti wa msalaba. Abrahamu aliamini uwezo wa Mungu juu ya mauti na hasa uaminifu wake kwa ahadi
alizompa: kwa hiyo akarudishiwa mwana hai kama mfano wa ufufuko, na katika yeye, yaani katika mzawa wake, watu wote
wakabarikiwa. Maisha ya imani yanadai daima sadaka, hasa ya mambo yanayopendwa
zaidi (Rom 12:1-2): ndiyo njia ya kujaliwa baraka zinazopita ubinadamu wetu.
Mwa 24 inasimulia kirefu
jinsi Abrahamu kabla hajafa alivyomfanyia mpango wa ndoa Isaka kufuatana na mila zao, ila alikataza
kabisa asirudi kwao, bali kwa vyovyote abaki katika nchi ile aliyoahidiwa na
Mungu. Hivyo imani izidi kuongoza uzao wake kama ilivyomuongoza mwenyewe.
Watoto wa Isaka: Esau na Yakobo
Matthias
Stom, Esau [kulia]
akimuuzia Yakobo haki yake kama mtoto wa kwanza au Sahani ya dengu,
(karne ya 17).
Kadiri ya Mwa 25:19-34, Rebeka alimzalia Isaka watoto pacha wenye sura na silika tofauti, Esau na Yakobo. Wa kwanza analaumiwa hasa kwa kupuuzia baraka ya Mungu
iliyokuwa haki ya kifunguamimba: kwa sahani ya dengu alikubali kukosa neema zile zote alizojitwalia
Yakobo kwa imani yake (Eb 12:16-17).
Mwa 27 inasimulia jinsi
Yakobo, akifundishwa na mama yake, alivyoweza kubarikiwa na baba. Ingawa uongo wake haukubaliki (Hos 12:3-5), Mungu
alithibitisha baraka ya Isaka kadiri ya desturi yake ya kumpendelea mdogo:
hivyo Yakobo, aliyekimbia nchi yake ana fimbo tu, alirudi miaka ishirini
baadaye ana wake 4, watoto 11 na mifugo wengi ajabu (Mwa 32). Kabla hajaingia
nchi yake Mungu alishindana naye usiku kucha akalazimika kumbariki na kumtajia
jina jipya, Israeli.
Yosefu na ndugu zake kushukia Misri (1700 hivi K.K.)
Yosefu na kaka zake
wakipokewa na Farao kadiri ya James Tissot (1900 hivi).
Kama kawaida ya mitara,
kulikuwa na upendeleo na wivu kati ya watoto wa
Yakobo. Hasa Yosefu alichukiwa na kaka zake wote, ingawa alikuwa mnyofu hata
kuwasimulia ndoto zake za ajabu (Mwa 37:2-11). Kijicho na chuki vilifikia hatua ya
kuwafanya watamani kumuua. Walipopata nafasi walifanya njama, ingawa si wote.
Mwisho uamuzi ukawa kumuacha hai lakini kumuuza kama mtumwa kwa wafanyabiashara walioelekea Misri (Mwa 37:12-36).
Lakini katika maovu ya binadamu Mungu akazidi kushughulikia taifa lake teule.
Hivyo Yosefu akawa mfano wa Yesu ambaye alichukiwa bure tu akauawa msalabani
kwa wokovu wa wadogo zake wakosefu.
Mwa 39 inaonyesha jinsi
Yosefu alivyozidi kumtiii Mungu na kukwepa dhambi. Hivyo baada ya majaribu
mbalimbali akatukuzwa kuwa liwali wa Farao kwa nchi yote, hasa kwa usimamizi wa akiba ya chakula (Mwa
41:1-49) kwa ajili ya miaka saba ya njaa aliyotabiri. Kadiri ya
mpango wa Mungu njaa hiyo ikawalazimisha kaka zake waje kumuinamia, naye
hakulipa kisasi; halafu, kama vile alivyotafsiri ndoto mbalimbali,
aliwafafanulia maana ya matukio ya maisha yao katika mpango wa Mungu: kwamba
ndiye aliyemtuma Misri kusudi awaokoe (Mwa 45:1-15).
Mwa 46:1-7 inasimulia
Yakobo na wazawa wake wote, jumla wanaume 70, walivyohamia Misri. Lakini
hawakusahau nchi waliyoahidiwa na Mungu: ndiyo sababu Yakobo na Yosefu walidai
waapiwe kuwa watakuja kuzikwa kwao (Mwa 49:29-50:26). Kabla ya kufa Yakobo
aliwabariki watoto wake 12 na kwa namna ya pekee Yuda ambaye atatawala moja kwa moja (Mwa 49:8-12).
Utumwa wa Misri na wito wa Musa (1250 hivi K.K.)
Musa akiokolewa katika
maji ya mto Nile, alivyochorwa na Nicolas
Poussin mwaka 1638.
Wanaisraeli waliishi Misri kama wageni tu zaidi ya miaka mia nne
(Mdo 7:6-16) wakiongezeka kiasi cha kuwatisha wenyeji wao: ndiyo sababu
wakaanza kudhulumiwa mwaka 1300 hivi K.K.
Hasa katika kuwakomboa
utumwani, Mungu alijionyesha mtetezi wa haki za maskini. Pamoja na kushurutishwa kufanya kazi wasioipenda,
ilitolewa amri ya kuua watoto wao wote wa kiume: lakini mpango huo
haukutekelezwa sawasawa (Kut 1:7-22).
Mmoja kati ya watoto
waliookolewa katika hatari hiyo ni Musa, wa kabila la Lawi (Kut 2:1-10; Eb 11:23; Mdo 7:17-22). Kisha kukimbia
Misri Musa akaoa Mmidiani (Kut 2:11-22; Eb 11:24-27; Mdo 7:23-29): alipokuwa
anachunga mifugo ya mkwewe kwenye mlima Sinai akaitwa na Mungu kutoka ndani ya
kichaka kinachowaka moto kisiteketee. Mungu alimchagua ingawa ana kigugumizi yaani anaonekana hafai kushindana na Farao. Mungu
akasisitiza aende mwenyewe, naye atatumia uwezo wake wa Kimungu kumlazimisha
Farao. Kadiri Musa alivyoomba, Mungu alimfunulia jina lake takatifu YHWH ambalo
linaeleweka kiasi tu, kama vile fumbo la Mungu mwenyewe (Kut
2:23-3:20; Mdo 7:30-35).
Mapigo ya Wamisri
"Maji Kugeuka
Damu" kadiri ya Tissot.
Mungu alipomtuma Musa
kwa Farao alijua tayari huyo atakataa kuwaruhusu Waisraeli waende zao, mpaka
aone mapigo yake kwa Wamisri. Kwa kuwa ulihitajika muda kuleta ukombozi,
iliwabidi Waisraeli wawe na imani na subira hadi ahadi za Mungu zitimie. Lakini binadamu hatupendi
kungojea ukombozi: hivyo Waisraeli wakaanza kunung’unika (Kut 5:1-6:1). Hata
hivyo Mungu akaendelea na mpango wake.
Maajabu aliyoyatenda
huwa yanatokea Misri lakini si yote kwa wakati mmoja wala si kwa kiasi kile
alichosababisha Musa kwa fimbo yake (Kut 6:28-7:7). Tuna orodha mbalimbali za
mapigo hayo, lakini kwa kawaida yanahesabiwa kumi: maji ya mto Naili kuwa mekundu kama damu, vyura kujaa nchi, chawa, nzi, tauni, majipu, mvua ya mawe, nzige, giza na hatimaye kifo cha wazaliwa wa kwanza
wa kiume wa watu na wa wanyama. Adhabu hizo ziliwapata Wamisri, lakini si
Waisraeli: hivyo ilikuwa wazi kuwa Mungu anabagua watu wake na watu waovu.
Katika pigo la kumi
Waisraeli waliopolewa kwa kuipaka milango yao damu ya mwanakondoo (Kut 11:1-10;
Mdo 7:36-37; Eb 11:28). Hivyo Mungu aliwaandaa watu kupokea imani kwa Yesu
Kristo, Mwanakondoo wa kweli na Mkombozi wa waliokuwa watumwa wa dhambi,
shetani na kifo (Yoh 19:36; 1Kor 5:7; 1Pet 1:18-20). Hiyo ni wazi katika ibada
iliyoagizwa ifanyike kila mwaka (Kut 12:1-14), yaani Waisraeli wale nyama ya
mwanakondoo dume asiye na hila, pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga ya majani machungu.
Yesu akaifanya ibada hiyo iwe ibada kuu ya agano jipya la milele, akiagiza
tuifanye kwa ukumbusho wake, si tena kwa ukumbusho wa kutoka Misri (1Kor
11:23-26).
Safari ya kuendea Nchi ya ahadi
"Kuvuka Bahari ya
Shamu" kadiri ya Nicholas
Poussin.
Kut 12:29-42 inasimulia
Waisraeli wote walivyokimbia Misri pamoja na mifugo yao waliposikia mayowe kutoka
nyumba za majirani wao wote. Katika safari yao wakaongozwa na Mungu kwa sura ya
wingu mchana na ya moto usiku (Kut 13:17-22; Yoh 8:12): hivyo Mungu alionyesha wazi kuwa
hawaachi hata kidogo bali anawashughulikia kwa namna tofauti kadiri ya
mahitaji.
Kut 14:5-31 inasimulia
jinsi Wamisri, kisha kuwalilia wafu wao, walivyoanza kuwatafuta Waisraeli kwa farasi na magari wakawakuta karibu na bahari ya Shamu. Lakini Waisraeli walivuka bahari kama kwamba ni nchi kavu, kwa kuwa maji yamegawanyika. Kumbe Wamisri wakazama
kwa kuwa maji yamerudi mahali pake (Eb 11:29). Asubuhi Waisraeli wakaona maiti
za Wamisri wote zikielea wakamshangilia Mungu aliyewaokoa (Kut 15:1-21
inatuletea wimbo ambao maneno yake ni kati ya yale ya kale zaidi katika
Biblia). Hivyo Mungu aliwaokoa tena watu wake katika maji, na huu pia ni mfano
wa ubatizo ambao unaadhimishwa hasa usiku wa Pasaka. Hata katika hatari ya kukandamizwa Mungu alidai Waisraeli
watulie kwa imani ya kuwa ushindi ni wake tu. Tena walitakiwa wasiyasahau kamwe
mang’amuzi hayo, kwa kuwa ndiyo msingi wa imani ya dini yao. Sisi vilevile
tunatakiwa kukumbuka daima ubatizo wetu ambapo Mungu ametuokoa.
Baada ya ushindi wa
Pasaka safari ikaendelea mpaka kufikia nchi aliyoahidi Mungu, ila Waisraeli
wakaja kusahau uweza wake na kumlalamikia
kipumbavu hata kumchosha. 1Kor 10:1-11 inatuonya tusifanye vile. Kama kawaida
malalamiko ya kwanza yalihusu kula na kunywa (Kut 15:22-17:7). Mungu
aliwakubalia kwa kuwateremshia kwale halafu mana: hasa chakula hicho
kiliwashangaza Waisraeli wakazidi kukikumbuka hata wakamdai Yesu awapatie tena
kama kweli ndiye Musa mpya. Yesu akawajibu kuwa
mwenyewe ndiye chakula cha
uzima kutoka mbinguni
kinachotulisha safarini hapa (Yoh 6:22-59). Vilevile kuhusu maji, Mungu
aliyatokeza katika mwamba huko Masa au Meriba, lakini alichukizwa sana na matendo yao (Eb 3:15-19).
Shida nyingine ya
kawaida kwa makabila ya wahamaji ni kupigana vita. Waisraeli walilazimika
kufanya hivyo na Waamaleki, wakapata ushindi si kwa nguvu zao, ila kutokana na
sala ya Musa, mwombezi wao (Kut 17:8-16). Sisi
taifa la Mungu tunatakiwa tutegemee sala kuliko uhodari wetu, na daima tuwe na
watu wenye kumuinulia Mungu mikono yao kama Musa jangwani.
Agano la Mlima Sinai
Sanamu ya Musa iliyochongwa na Michelangelo iko katika kanisa la Mt. Petro "in vinculis" mjini Roma (Italia).
Walipofikia mlima huo wa
kutisha, Mungu alimuita Musa aupande ili aseme naye, huku wengine wakibaki
chini. Hapo akampa Musa masharti ya agano lake na Waisraeli (Kut 19). Akiwa
Muumba na hasa Mkombozi wao alidai waishi kitakatifu kwa kushika amri kumi, ambazo tatu zinahusu heshima kwake na saba uhusiano
na watu wengine (Kut 20:2-17). Ndiyo mawe mawili ambayo Musa alipewa
halafu Yesu akayakamilisha katika amri kuu ya upendo kwa Mungu na
kwa jirani (Mk 12:28-34). Amri hizo zinaweza kujulikana na kukubaliwa na mtu
yeyote mwenye mapenzi mema, lakini Mungu alipenda
kutusaidia tujue kwa urahisi na hakika zaidi tufanye nini ili kumpendeza, tuwe
watu wake naye awe Mungu wetu kwelikweli. Agano hilo upande wa Mungu ni imara
kwa kuwa yeye ni mwaminifu kabisa, shida iko upande wetu tulio geugeu,
tukiahidi tusitekeleze. Ndiyo sababu likahitajika agano lingine lililofungishwa
na Yesu Kristo (2Tim 2:11-13).
Ndama ya dhahabu
The Adoration of the
Golden Calf by Nicolas
Poussin
Kut 32 inasimulia uasi
wa Waisraeli ulivyofikia kilele chake walipojitengenezea mungu wa dhahabu mwenye sura ya fahali (Biblia kwa dharau
inasema “ndama” na “mla nyasi”). Hata Haruni, kaka yake Musa, alikubali kufuata matakwa yao huku mdogo
wake akichelewa mlimani (Mdo 7:38-42). Musa akambembeleza Mungu asiwaangamize
watu wake, hivyo akawa mfano bora wa mwombezi, kwa kuwa hakujali ahadi ya Mungu
ya kumfanya chanzo cha taifa lingine kubwa. Kazi hiyo ni hasa ya Bwana Yesu ambaye aliwatetea
watu wake kwa kumwaga damu yake, na anazidi kuwaombea kwa Baba yake (Eb
7:25-27).
Mungu kujifunua tena kwa Musa
Kilele cha Mlima Sinai (mita 2,285 juu ya usawa wa bahari).
Kut 33:18-34:9
inasimulia jinsi Mungu alivyokubali kiasi ombi la Musa la kumuonyesha utukufu wake; badala ya kumuonyesha uso wake (Yoh 1:18)
alijifunua kwake kwa kulitangaza na kulifafanua jina lake: YHWH ni mwingi wa
rehema na uaminifu, anawaonea wivu watu
wake, yaani hawezi kukubali waabudu miungu mingine kwa hasara yao. Ndiyo sababu
alipoagana nao kwa kuandika tena amri zake kumi katika mawe, pamoja na kuahidi
kuwafukuza wenyeji wa nchi takatifu ili kuwapatia nafasi Waisraeli, aliwaagiza
wasichanganyikane nao wasije wakavutwa katika Upagani. Hasa alikataza ndoa za
mseto ili kulinda usafi wa imani.
Kwa namna ya pekee Kristo analipenda na kulionea wivu Kanisa lake analolitaka bikira safi katika imani na maadili (2Kor 11:2; Ef 5:25-27): hivyo tunaposhirikiana na
watu wengine tuwe macho tusifuate mawazo, maneno na matendo yao, bali
tushuhudie imani na upendo kwa maisha yetu tofauti na ya kwao (Yoh 17:15-17).
Mambo ya Walawi
Hema la
mkutano na kambi lake (mchoro wa karne ya 19).
Kitabu hicho cha tatu
kimejaa hasa sheria za ibada zenye kulenga utakatifu wa makuhani na wa sadaka.
Watu wa kabila la Lawi tu ndio walioruhusiwa kushughulikia ibada, tena kati yao
ukoo wa Haruni tu ndio makuhani kamili. Kutokana na kazi hiyo Walawi hawakupewa
sehemu ya nchi takatifu, ila Mungu mwenyewe ndiye fungu lao. Lakini taifa lote
lilitakiwa liwe takatifu kutokana na uhusiano wake na Mungu (Law 19:1).
Polepole maana ya utakatifu huo ilizidi kueleweka si kukwepa unajisi wa kiibada tu, bali unategemea hasa mwenendo
mwadilifu.
Hesabu
Kitabu cha nne kinaitwa
hivyo kwa sababu kinaleta hesabu mbalimbali, hasa ya idadi ya Waisraeli:
wanaume wa kuweza kwenda vitani walikuwa 603,500 (mbali na Walawi waliohesabiwa
peke yao: wanaume 22,000 wakiwa pamoja na watoto wa kiume); ukiongeza wanawake
na watoto mpaka umri wa miaka ishirini, basi jumla yao iliweza kufikia watu
milioni tatu, ingawa si lazima kuamini idadi hiyo ni sahihi (pengine namba hizo
hazilingani katika makala kwa kuwa ilikuwa rahisi kukosea wakati wa kunakili).
Uzito wa kazi ya
kuwaongoza watu wengi hivyo wanaonung’unika kila mara ulimchosha Musa hata
akamuomba Mungu tena ampunguzie mzigo au amuue kabisa (Hes 11:1-30). Musa
alieleza shida yake kama rafiki kwa mwenzake, kwa unyofu uleule wa watu wengine
wa Mungu katika Biblia. Mungu akamkubalia akawashirikisha watu sabini roho yake
kwa ajili ya uongozi katika ngazi mbalimbali. Huo pia ni mfano wa Agano Jipya,
ambapo askofu hawezi kuchunga waamini peke yake, bali anahitaji msaada
wa viongozi wa daraja za chini, yaani mapadri na mashemasi (Mdo 6:1-6). Katika nafasi hiyo Musa alimueleza Yoshua kwamba hawaonei kijicho kwa kupewa karama, tena angependa kama Waisraeli wote wangekuwa manabii.
Hamu hiyo ikatimia siku ya Pentekoste: katika Kanisa wote wanapewa Roho
Mtakatifu na kuwa manabii, hata wanawake na watoto (Mdo 2:16-18).
Kinyume chake Hes 12
inasimulia kijicho kilivyowafanya dada na kaka wa Musa wamseme wakijidai nao
pia ni manabii. Lakini Mungu akawaeleza kuna namna mbalimbali za unabii, na
Musa ni wa pekee. Kisha akatoa adhabu ambayo ikaondolewa kwa maombezi ya Musa
tu: ndiyo sababu anasifiwa kwa upole wake. Kijicho
kitasumbua daima taifa la Mungu, hata katika Agano Jipya (1Kor 12:1-31;
14:37-38).
Musa na wapelelezi wa
Kanaani, walivyochorwa na Giovanni
Lanfranco, J. Paul
Getty Museum, Los Angeles, Marekani.
Waisraeli walipofikia
mipakani mwa nchi takatifu walituma wapelelezi ili waivamie, nao waliporudi
walisimulia uzuri wake, lakini pia walitisha kwa kuzidisha habari za wananchi
na miji yao (Hes 13). Hapo Waisraeli wakaanza kunung’unika usiku kucha (Hes 14)
wakapanga kuwaua kwa mawe Kalebu na Yoshua waliotaka kuivamia nchi bila ya hofu kwa jina la
Bwana. Lakini Mungu akaonyesha utukufu wake na kutisha ataleta tauni ili
kuwaangamiza wote kwa ukaidi wao. Kwa maombezi ya Musa, akakubali kuwahurumia
lakini akaamua warudi jangwani na kuzungukazunguka huko mpaka wafe wote; ila
watoto wao pamoja na Kalebu na Yoshua ndio watakaoingia nchi takatifu
kuimiliki. Maana ya
kiroho ni kwamba hatutakiwi
kuzitia shaka ahadi za Mungu; hata zikionekana ngumu kupatikana, ni lazima tuwe
na moyo mkuu na imani hata tukabili vipingamizi vyovyote.
Kinyume chake, Waisraeli
walipoamua kuivamia nchi kwa kusikitikia adhabu waliyopewa wakashindwa kabisa,
maana ni lazima tumtii Mungu kwa wakati wake. Pia kughairi kutokana na matatizo
kunaweza kukatusukuma tutende namna ambayo haimpendezi tena; ni lazima tuchukue
majukumu ya matendo yetu na kukubali adhabu au matatizo tuliyojitakia:majuto
hayo yanafaa kwa kuonyesha utiifu kwa Mungu (Zab 119:71).
Manung’uniko ya
Waisraeli katika safari yao jangwani yakawaletea adhabu nyingine, mojawapo ile
ya kugongwa na nyoka wengi wenye sumu kali. Lakini walipoomba
msamaha, Mungu akamuagiza Musa atengeneze nyoka wa
shaba na kumuinua juu ya mti
ili mtu aliyeumwa akimtazama tu apate kupona (Hes 21:4-9). Ufafanuzi wa tukio
hilo ulitolewa na Yesu mwenyewe: ndiye aliyeinuliwa juu ya mti wa msalaba ili
watakaomtazama kwa imani wapate kuishi (Yoh 3:14-15).
Kumbukumbu la Torati (Sheria)
Mchoro wa William
Blake (1780 hivi) unaomuonyesha
"Musa akipokea Sheria", Yale Center
for British Art.
Kitabu hicho cha mwisho
cha Torati kiliandikwa kama miaka 600 baada ya Musa, ingawa kina namna ya hotuba tano alizoweza kuwatolea Waisraeli kabla hajafa. Kinapitia
upya matukio ya wokovu ya wakati wa Musa kikifaidika na ujumbe wa manabii, hasa
Hosea. Kwa msingi huo, kitabu hiki kinasisitiza sana upendo kwa Mungu, uaminifu kwa agano la mlima
Sinai pamoja na tuzo na adhabu zitakazotolewa kufuatana na matendo ya
Waisraeli. Katika maneno yake yote ya kitabu hiki, maarufu ni hasa yale ya
6:4-9 ambayo Mwisraeli yeyote anayakariri kila siku katika sala na kuyashika
pengine neno kwa neno.
Maneno mengine muhimu
sana yapo 26:5-10: ni kama kanuni ya imani ambayo Mwisraeli alikuwa anaiungama mbele ya Mungu
wakati wa kumtolea malimbuko ya ardhi. Hivyo alikuwa akikiri amepewa yote na
Bwana, halafu akaweza kuyafurahia mavuno.
Baada ya hotuba hizo,
Kumb 31:1-8 inasimulia jinsi Musa alivyomuachia Yoshua uongozi wa Waisraeli
wote kwa kumwekea mikono (Hes 27:12-23). Musa alifikia mpakani mwa nchi
takatifu asikubaliwe kuiingia kama adhabu ya makosa yake, ila alionyeshwa yote
kutoka mlimani (Kumb 32:48-52) halafu akafariki (Kumb 34). Kazi aliyopangiwa
iliishia huko, mwingine akampokea na kuendeleza ukombozi wa Kimungu. Binadamu
wote ni vyombo tu vinavyotumika kwa muda fulani, halafu vinaweza kuachwa. Kumbe
Mungu ndiye mtendaji mwenyewe ambaye hasinzii wala halali, bali anazidi
kuwashughulikia watu wake. Kwa imani hiyo tuwe daima tayari kuwaachia wengine
nafasi yetu.
Vitabu vinavyofuata Kumbukumbu la Torati (Sheria)
Vitabu vinavyofuata
katika Biblia ya
Kiebrania (Yoshua, Waamuzi,
Samweli na Wafalme) vinataka kuthibitisha kwamba kweli ikawa kama hiki
kinavyosema: Waisraeli walipofuata agano (wakati wa Yoshua) waliteka nchi ya
ahadi na kuifurahia, lakini
walipozidi kuasi (wakati wa Waamuzi, Samweli na Wafalme) walikuja kunyang’anywa nchi ile yote,
kwanza sehemu nzuri zaidi (kaskazini), halafu ile hafifu zaidi (kusini). Hapo Waisraeli wote wakajikuta tena utumwani katika nchi
ya kigeni kama kabla ya Musa, wakikosa hata sanduku la agano, lililopotea wakati wa maangamizi ya Yerusalemu na hekalu lake, baada ya wao kufikia hatua ya kula watoto wao
kutokana na njaa.
Vitabu hivyo
vilikamilishwa wakati wa kukaa uhamishoni Babeli, vikiwa jibu la swali kuu
lililowakwaza huko: je, Mungu wetu ameshindwa? Waandishi walichagua matukio
mbalimbali ya historia baada ya Yoshua ili kuthibitisha kuwa aliyeshindwa ni
Israeli, si Mungu. Historia hiyo inaonyesha mfululizo wa maasi hata baada ya
Mungu kutuma waamuzi na manabii wake ili kuwaonya Waisraeli na kuwaelekeza
upya.
Lengo la waandishi
halikuwa kutunza kumbukumbu za mambo yote kwa usahihi na ukamilifu, bali
kuelekeza njia ya kupata wokovu hata baada ya Israeli kuonekana imekoma moja
kwa moja. Kama vile Biblia nzima, vitabu hivyo vinalenga wokovu wetu,
vikihakikisha kuwa Mungu anaweza kuleta mwanzo mpya hata hali ikiwa mbaya namna
gani. Ndiyo sababu habari ya mwisho kabisa ni ya kuleta tumaini: kwamba mfalme Yekonia alitolewa gerezani (alipokaa miaka 37) na kufanywa
mgeni wa kudumu mezani pa mfalme wa Babeli.
Yoshua (1210-1200 hivi K.K.)
"Wana wa Israeli
wakivuka Yordani" walivyochorwa na Gustave Doré (alifariki mwaka 1883).
Kitabu cha sita cha
Biblia kinatupasha habari za uvamizi wa nchi takatifu ambao Waisraeli
waliufanya chini ya Yoshua, ambaye ni mfano wa Yesu (hata jina lao kwa Kiyahudi
ni moja, linalotafsiriwa “Mungu anaokoa”): ndiye aliyewaingiza watu katika nchi
ya ahadi, si Musa.
Mara baada ya kushika
uongozi, Yoshua alituma wapelelezi nchini; huko Yeriko, mji wa zamani kuliko yote ya dunia, walisaidiwa na Rahabu, kahaba aliyeamini kuwa ushindi utakuwa wa Mungu wa Israeli (Yos
2): kwa hiyo akaokolewa pamoja na ndugu zake, tena akajaliwa kuwa bibi wa babu
wa mfalme Daudi, hata akatajwa na Injili kama bibi wa Yesu Kristo
(Math 1:5-6), halafu akachukuliwa kama mfano wa imani (Eb 11:31) na wa matendo
mema (Yak 2:25).
Yoshua aliwavusha
Waisraeli pakavu kati ya mto Yordani (Yos 3-4) na hivyo akawaingiza katika nchi takatifu.
Hapo ikawabidi kwanza wafunge tena agano na Mungu kwa kutahiriwa wanaume wote
na kwa kuadhimisha Pasaka ambapo kwa mara ya kwanza walikula mazao ya nchi hiyo
waliyoahidiwa: ndio mwisho wa mana na wa kipindi cha jangwani (Yos 5:1-12).
Hata sisi tutaacha kula mkate toka mbinguni tutakapoingia pale tulipoahidiwa.
Baada ya matendo hayo ya
kidini Mungu alimtokea Yoshua kama amirijeshi wa Israeli ili
kumhakikishia kwamba mwenyewe ataongoza mambo, hivyo Yoshua amtegemee
akijisikia chombo chake tu (Yos 5:13-15). Ni rahisi kwa kila binadamu
aliyeshika uongozi kujisikia mwenyewe na hivyo kuacha kumtegemea Mungu. Kumbe
Yoshua kwa kupokea ujumbe huo akaweza kushinda watu wenye maboma, nguvu na
silaha kali kuliko Waisraeli. Kwamba hiyo ni nguvu ya Mungu inaonekana wazi
hasa katika simulizi la kuteka Yeriko (Yos 6:1-21): huko Waisraeli walifanya maandamano ya ibada mpaka kuta za mji zikaanguka. Vita vyetu
vya kiroho na vya kitume vitegemee hasa sala. Baada ya vita vingi Yoshua
akayagawia makabila 12 ya Israeli nchi yote, ikiwa ni pamoja na sehemu
zilizobaki chini ya wenyeji (Yos 12:1-13:14). Huko Shekemu aliwadai wote wachague
kumtumikia YHWH au miungu mingine, akisisitiza ugumu wa kumtumikia sawasawa
Mungu aliye mtakatifu na mwenye wivu kwa watu wake. Lakini wao walikubali kwa
moyo wote kumtumikia Mungu tu, wakasimamisha jiwe kubwa kama kumbukumbu (Yos
24:1-28).
Kabla hajafa Yoshua
akawaita Waisraeli wote ili kuwaimarisha katika imani na umoja kwa kuwakumbusha
maajabu waliyotendewa na Mungu na kwa kuwahimiza wamuonyeshe shukrani (Yos 23). Kukumbuka ni
jambo muhimu ili tuishi kwa imani bila ya kudanganywa na maisha
yanayosahaulisha kwa urahisi mambo ya Kimungu.
Waamuzi (1200-1025 hivi K.K.)
"Gideoni
akimshukuru Mungu kwa muujiza wa umande", alivyochorwa na Maarten van
Heemskerck (Musée des Beaux-Arts de Strasbourg, Ufaransa).
Kitabu hiki kinaleta picha tofauti na kile cha Yoshua kuhusu hali ya nchi ya Kanaani baada ya uvamizi. Kinaonyesha kuwa Waisraeli hawakufukuza wenyeji wote, bali waliteka baadhi tu ya maeneo yao wakaishi
jirani nao.
Baada ya makabila ya
Waisraeli kugawana nchi, kila moja likaanza kujitegemea: lakini bila ya umoja
hakuna nguvu upande wa dini wala wa siasa. Upande wa dini, Waisraeli wakaanza
kuchanganyikana na wenyeji Wapagani na kufuata utamaduni wao uliostaarabika
zaidi, wakiwaiga katika yote: kuishi katika nyumba ya kudumu, kulima n.k. hata wakaabudu miungu yao ya kiume
na ya kike kwa ukahaba wa
kidini na kwa kuitolea sadaka watoto wao ili kujivutia fadhili zao, hasa mvua. Kutokana na makosa
hayo, Mungu akawaacha wapatwe na ukame, njaa na zaidi ya hayo
wanyanyaswe na makabila mbalimbali.
Mara kwa mara Waisraeli
wakamlilia yeye aliyewasikiliza walipokuwa wanaonewa Misri, naye akaitikia kwa
kuwainulia mwanamume au mwanamke ambaye awashinde maadui na kuwarudishia amani (Amu 2:6-19). Watu wa
namna hiyo wanaitwa “waamuzi”: maana ya neno hilo si wasomi wanaosikiliza kesi na kutoa hukumu kadiri ya sheria zilizotungwa na bunge la nchi, bali walikuwa
“watawala” wakati wa amani baada ya kushinda vita vya
ukombozi. Waliweza kuwa watu wa
kila aina, hata wasiotarajiwa kabisa, kwa kuwa mkombozi wa kweli alikuwa Mungu tu.
Habari za waamuzi hao 12
haziwezi kupangwa kitarehe, kwa kuwa hazina dalili zinazotusaidia kujua ipi ilitangulia na ipi ilifuata.
Waandishi wenyewe hawakujua mwaka wa matukio hayo, hivyo walikusanya kumbukumbu walizokuwanazo kama kwamba waamuzi walifuatana mmoja
baada ya mwingine kuongoza Israeli. Ukweli ni kwamba waliweza kuongoza kwa wakati mmoja
huyu huku na huyu huku, kwa kuwa kila mmoja alihusika na eneo fulani tu. Kwa
kuwapanga mmoja baada ya mwingine, waandishi waliweza kusisitiza mara 12 kwamba
Waisraeli walirudiarudia dhambi, na kwa sababu hiyo walirudiarudia kupewa na Mungu adhabu aliyoitabiri Musa. Lakini fundisho muhimu
zaidi ni kwamba Bwana, bila ya kujali ugeugeu wao, daima alikuwa
tayari kuwaokoa walipomlilia msaada.
Mwamuzi mmojawapo ni Gideoni aliyedumisha amani kwa miaka 40. Alipoitwa
na Mungu alijitetea kwa kusisitiza udogo na ufukara wake, lakini akajaliwa ishara zote alizoziomba ili kuhakikishiwa msaada (Amu
6:11-24,36-40). Sura ya 7 inasimulia Mungu alivyopunguza askari wake ili
ionekane wazi kuwa ushindi ni wa Mungu mwenyewe, hautegemei uhodari na wingi wa
watu au silaha zao. Ni kawaida ya kazi ya Mungu kuonyesha uweza wake katika
udhaifu wa binadamu. Waisraeli walipotaka Gideoni awe mfalme wao, akakataa katakata ili Bwana tu aendelee kuwatawala
(Amu 8:22-23), lakini wazo hilo likaendelea kuenea, ingawa wengine walilipinga
(Amu 9:1-21).
Nyongeza ya kitabu inaonyesha
kuwa kumwasi Mungu kulisababisha hatimaye Waisraeli kupigana wenyewe kwa
wenyewe. Ni kwamba, ukivunja amri ya kwanza unaweza kuja kuzivunja zote, na ukimkataa bab, hutakubali tena ndugu zako. Mstari wa mwisho
unaeleza sababu nyingine ya fujo hizo: kutokuwepo mfalme mmoja juu ya makabila yote 12. Kwa kusema hivyo, kitabu
kinatuandaa kusikia katika vitabu vinavyofuata jinsi ufalme wa Israeli ulivyoanzishwa kwa usimamizi wa Samweli, nabii na mwamuzi wa mwisho lakini mkuu kuliko hao 12.
Ruthu
Ruthu alivyochorwa na Antonio
Cortina Farinós.
Katika fujo ya miaka
ile, habari ya kitabu hiki kifupi inatujenga: inahusu mwanamke huyo Mpagani wa
kabila la Moabu aliyeolewa na Mwisraeli huko ng’ambo ya Yordani. Baada ya
kufiwa mume wake akafuatana na mama mkwe hadi Bethlehemu ili aolewe na ndugu wa marehemu na kumzalia mtoto
kadiri ya sheria. Huyo mtoto akawa babu wa Daudi. Hivyo kwa
uaminifu wake mwanamke huyo pia akatajwa katika Injili kama bibi wa Yesu (Math
1:5-6).
Samweli (1050-1015 hivi B.C.)
Vitabu viwili vya Biblia ya Kikristo vinaitwa kwa jina la
mtu huyo, ambaye kwa njia yake Israeli ilianza kuwa na umoja zaidi na hatimaye kuwa ufalme. Badala ya kila kabila kujitegemea, yote 12 yalikubaliana yawe na kiongozi mmoja wa kudumu ambaye cheo chake kirithiwe na
mwanae. Kwa umoja huo waliweza kushinda maadui wao.
Vitabu hivyo vimekusanya
kumbukumbu zote kuhusu mwanzo wa ufalme (1070-972 hivi K.K.), yaani kuhusu Samweli mwenyewe na wanaume wawili aliowapaka mafuta watawale Israeli kwa niaba ya Mungu: kwanza Sauli, halafu Daudi. Kumbukumbu hizo zilikuwa
nyingi na tofauti, hivyo tunakuta humo tata nyingi kuliko katika vitabu vingine
vyote vya Biblia. Hasa mna hoja za kukubali mfumo wa ufalme na hoja za
kuukataa.
Ukuu wa Samweli
ulidokezwa na uzazi wake wa ajabu, kwa kuwa mama yake alikuwa tasa akampata
baada ya kusali na kuweka nadhiri (1Sam 1). Hivyo baada ya miaka michache alihamia Shilo kwenye sanduku la agano kama mtumishi wa kuhani Eli.
1Sam 3 inasimulia wito wake: akiwa amelala
karibu na sanduku hilo akaamshwa na Mungu mara tatu mpaka akafundishwa na Eli
kumtambua na kumuitikia Mungu. Hapo akamtabiria Eli adhabu kali, na hivyo
Israeli ikajua kuwa amefanywa nabii wa Bwana.
Samweli aliwaamua
Waisraeli kwa kuwakomboa mikononi mwa Wafilisti (1Sam 7), lakini ni muhimu hasa kwa kuwaanzishia
ufalme kwa kuwaweka wakfu kwanza Sauli halafu Daudi. Kadiri ya 1Sam 8, yeye na Mungu
hawakupendezwa na jinsi Waisraeli wengi walivyotaka kuiga mtindo wa mataifa
yote: Samweli aliwaangalisha kuhusu matatizo na unyonyaji wa wafalme, naye
Mungu aliona katika ombi hilo uasi ambao Waisraeli wanamkataa asiwatawale tena,
lakini akamuagiza Samweli awakubalie.
Ukweli ni kwamba mfalme aliwekwa wakfu kwa Mungu kama mwakilishi wake akitakiwa kutimiza matakwa yake, hasa kwa
kusikiliza anamuambia nini kwa kinywa cha manabii wake. Ndiyo sababu Samweli alizidi kumuelekeza Sauli, na
hatimaye akamkataa kwa ukaidi wake. Mabishano kati ya Samweli na
Sauli ni mwanzo wa mabishano yote kati ya manabii na wafalme ambao hawakutaka
kumtii Mungu, na hatimaye wakadhulumu na kuua manabii wake. Mamlaka ya neno la Mungu lililoletwa na nabii ilitakiwa kuwa
juu ya mamlaka ya serikali na nguvu ya kijeshi alivyokuwa
navyo mfalme. Lakini mara nyingi wafalme, kwa kujivunia cheo chao, walishindwa
kumnyenyekea nabii wa Mungu, wakaona afadhali kufuata manabii wengine wengi
waliosema uongo ama kwa kudanganywa na matarajio yao ama kwa kujipendekeza
kwa mfalme na kwa taifa lote.
Mfalme Sauli (1030-1010 hivi K.K.) na mfalme Daudi
(1010-970 hivi K.K.)
Picha ndogo inayomchora Samweli
akimweka wakfu mfalme Daudi.
1Sam 9:11-10:16
inasimulia Sauli alivyoteuliwa kuwa mfalme wa kwanza. Akitawala karibu miaka
ishirini, alifanya makosa na kulaumiwa na Samweli, hata akakataliwa kabisa na
Mungu kwa kutomtii kikamilifu (1Sam 15). Ingawa akaendelea kutawala kwa muda fulani,
polepole alijitokeza kijana Daudi ambaye akaja kuanzisha ukoo wa kifalme wa
milele.
1Sam 16-17 inaanza
kutuletea mkusanyo wa hadithi juu ya Daudi ambazo zinampatia sifa aliyostahili, ingawa
nyingine zinagongana: k.mf. kama aliingia katika utumishi wa Sauli kutokana na
uhodari wake katika muziki au katika vita. Uhodari huo wote ukaendelea kusifiwa
ila Daudi aliutumia kwa utukufu wa Mungu: ndiye aliyeingiza ala mbalimbali
katika ibada na kutunga zaburi kadhaa, na ndiye aliyeeneza utawala wa Israeli
kuliko yeyote.
Kadiri alivyozidi
kupendwa na Mungu na watu, Sauli alimchukia kwa kijicho na kutaka kumuua (1Sam
18:6-16). Daudi alipolazimika kukimbia na kuunda kikosi chake akapata nafasi
rahisi ya kumuua Sauli lakini alijizuia kwa kuheshimu krisma aliyopakwa awe
mfalme (1Sam 24 na 26): hivyo ni mfano bora wa kujali wito wa Kimungu.
Baada ya kufanywa mfalme
wa kabila lake (Yuda, yaani Kusini) na ya kupigana vita na mwana wa marehemu
Sauli, Daudi akakubaliwa kuwa mfalme wa Israeli yote (yaani Kaskazini pia):
pamoja na taarifa hiyo, 2Sam 5:1-12 inatuambia alivyoteka Yerusalemu uliokuwa
bado mikononi mwa Wapagani akaifanya makao makuu ya kisiasa na ya kidini ya
taifa lote la Mungu ili aunganishe Kaskazini na Kusini katika mji huo uliopo
katikati. Kuanzia hapo Yerusalemu ukawa mji mtakatifu wa dini tatu
zinazomuabudu Mungu wa Abrahamu.
2Sam 6 inasimulia
sanduku la agano lilivyohamishiwa Yerusalemu kwa shangwe kubwa; hasa Daudi
alicheza mbele ya Mungu kwa nguvu zake zote huku amevaa nguo ndogo ya kikuhani
tu, bila ya kujijali kama kifalme. Kwa unyenyekevu wake alimpendeza Mungu
akapewa naye ahadi ya ajabu, yaani kwamba ufalme wake utadumu milele (2Sam 7).
Pamoja na hayo, Daudi akabaki kielelezo cha mfalme wa Israeli, ambaye awe
tofauti na wengine wote kwa kuwa hasa mtumishi mnyenyekevu wa Mungu bila ya
kuyumba kwa kuelekea miungu mingine. Kisha kupewa ahadi hiyo alikwenda mbele ya Mungu
na kusali vizuri kama kawaida yake hata nje ya ibada: sala yake ya sifa na
shukrani imejaa mshangao kwa ukuu wa Mungu na fadhili zake na kumalizika kwa
ombi nyenyekevu. Ingawa hakukubaliwa kumjengea Mungu hekalu la ajabu
alivyokusudia, amekuwa mwalimu wa sala kwa nyakati zote: hata leo liturujia inategemea sana zaburi zake.
Utabiri huo wa nabii Nathani ukawa chanzo cha uimara wa ufalme wa Yerusalemu kwa miaka 400 hivi, halafu ukaja kuongoza tumaini la Waisraeli hasa walipodhulumiwa, k.mf. zamani za
Yesu chini ya ukoloni wa Kirumi, ambapo wote walimtazamia mwana wa Daudi mwenye kurudisha ufalme wa Israeli. Kwa mchango wa manabii mbalimbali ujio wake ulitarajiwa kuwa hatua mpya ambapo kasoro za wafalme waliotangulia zitakoma.
Matendo mengine tofauti
yaliyoathiri sana maisha ya Daudi ni dhambi alizotenda kwa ajili ya mke wa Uria Mhiti, yaani uzinifu, unafiki, ulevyaji na uuaji wa askari huyo
mwadilifu (2Sam 11). Basi, Nathani akamuendea ili kumlaumu na kumtabiria adhabu
mbalimbali, hasa kwamba upanga hautaondoka nyumbani kwake (2Sam 12:1-25). Ikawa
hivyo hasa kwa sababu ya Absalomu mwanae ambaye alimuua kaka yake (2Sam 13:22-37) na
baada ya kusamehewa akafanya njama hata akamfukuza Daudi toka Yerusalemu (2Sam
14:28-15:29) akazini na masuria wake mahali pa wazi (2Sam 16:20-23). Hata hivyo
Daudi akazidi kumpenda na alipoambiwa amekufa akamlilia kwa namna ambayo
iliwashangaza na kuwachukiza waliompigania: yeye ambaye alijiombea na kupewa
msamaha wa Mungu hakumchukia mwanae aliyehatarisha maisha yake (2Sam
18:19-20:8).
2Sam 24 pia inatuchorea
sura yake ya kiroho: alipoadhibiwa na Mungu kwa tauni iliyoua Waisraeli wengi
baada ya yeye kuhesabu askari wote alioweza kuwategemea vitani, basi kama
mchungaji mwema aliomba adhabu imuangukie mwenyewe, lakini si kondoo zake wasio
na kosa. Mfalme wa kumpendeza Mungu ni mchungaji wa watu wake; Kristo mwana wa
Daudi anawajua kondoo zake mmojammoja kwa jina, naye amejitwisha adhabu ya
makosa yao: ndiye mfalme na mchungaji bora.
Habari za mwisho za
Daudi zinapatikana katika 1Fal 1-2 tunaposikia juu ya njama ya mtoto mwingine: Adonia alitaka kutawala akajifanya mfalme huku Daudi mkongwe hana
habari. Lakini Nathani akaingilia kati ili mwandamizi awe Solomoni, ambaye alipozaliwa na mke wa Uria alimhakikishia
Daudi msamaha wa Mungu.
Vitabu vya Wafalme
Vitabu hivyo viwili
vinapitia historia ya Israeli kuanzia mwaka 972 hadi 560 hivi K.K. vikionyesha mwenendo wa kila mfalme upande wa dini, hasa katika kutekeleza
maneno ya Kumbukumbu la
Torati, ya kwamba Mungu ni mmoja, hivyo hekalu lake liwe moja tu. Kwa kuwa wafalme wote wa kaskazini na karibu wale wote wa kusini walikwenda kinyume, vitabu hivyo vinaanza na ufalme imara na wa fahari ulioweza kumjengea
Mungu hekalu la ajabu, kumbe vinaishia na hali mbaya na ya aibu kuliko ilivyokuwa kabla
ya Musa, wafalme wakiwa wafungwa Babeli, Waisraeli wote uhamishoni na hekalu lenyewe magofu tu.
Lakini waandishi
hawakusimulia hayo ili kutunza kumbukumbu za zamani kama wanavyofanya wanahistoria, bali kwa lengo la kuonyesha tena uaminifu wa Mungu, aliyezidi
kutuma manabii wake hata baada ya kuona hawasikilizwi, bali wanadhulumiwa
hata kuuawa. Kwa kutegemea uaminifu huo, Wayahudi waliohamishiwa Babeli waliweza kutumaini mwanzo mpya.
Hasa manabii wa mwisho wa wakati huo, Yeremia na Ezekieli, waliwatia moyo kuwa Mungu atabadili mioyo yao na
kufanya nao Agano Jipya.
Mfalme Solomoni (970-931 hivi K.K.)
Solomoni katika ikulu yake (kadiri ya Ingobertus, 880 hivi).
Ufalme wake uliweza
kustawi kuliko ule wa baba yake kutokana na msingi imara aliouweka Daudi.
Lakini mwenyewe aliudhoofisha na kusababisha mara baada ya kifo chake utokee
utengano kati ya makabila ya Kaskazini na yale ya Kusini.
Kati ya kazi muhimu
alizozifanya, mojawapo ni kujenga hekalu la Yelusalemu na kuliweka wakfu kwa
sherehe kubwa ya siku saba, ambapo Mungu alionyesha kibali chake kwa kulijaza
kwa sura ya wingu (1Fal 8). Polepole hekalu hilo likaja kuwa la pekee hata
patakatifu pengine pote pakakatazwa chini ya mfalme Yosia.
Ingawa Solomoni
anasifiwa kwa hekima yake, alishindwa kukwepa majivuno na tamaa, akataka kuwapendeza wake zake waliokuwa
700 (mbali na masuria 300), wengi wao Wapagani, hata akawajengea mahali pa
kuabudia miungu yao akamchukiza Mungu hata akamtabiria mtoto wake
atanyang’anywa sehemu kubwa ya ufalme (1Fal 11:1-13) ikawa hivyo.
Baada yake, makabila ya
kaskazini yalitawaliwa na wafalme wa koo mbalimbali (931-722), kumbe yale ya
kusini yalitawaliwa na watu wa ukoo wa Daudi tu (931-587). Wafalme wote wa
kaskazini wanasemwa kuwa wabaya. Kati ya wafalme wa kusini, wema ni 2 (Ezekia na Yosia); wengine wema kiasi; wengine wabaya. Hatimaye
Waisraeli wa kaskazini walipelekwa uhamishoni Ashuru (722) wasirudi tena. Wale wa kusini walipelekwa uhamishoni
Babeli (587) lakini baadhi wakarudi (kuanzia 538).
Manabii
Nathani akimlaumu Daudi
na kumtabiria adhabu.
Tofauti na mtangulizi wake, Daudi alimpendeza Mungu, si kwa sababu
hakufanya makosa, bali kwa sababu
alikuwa tayari kumsikiliza akisema kwa njia ya manabii wake Nathani, Gadi n.k. Alikubali kukosolewa, kuonywa na kuambiwa la kufanya.
Kila mfalme baada yake alitakiwa kufanya hivyo.
Kwa kiasi kikubwa, miaka
ya wafalme wa Israeli na Yuda ni pia miaka ya manabii bora walioinuliwa na
Mungu alivyotaka ili kuwakemea au kuwafariji Waisraeli. Kazi yao kubwa haikuwa
kutabiri yatakayotokea, bali kuwa madaraja kati ya Mungu na watu wake, wakiwafahamisha
yeye anawaza na kutaka nini. “Nabii” ni hasa mtu “anayesema kwa niaba” ya
Mungu. Si lazima aandike kitu.
Njia zake za kuwasiliana
na Mungu zinafanana na zile za dini nyingine: kuota, kupata njozi, kutoka nje
ya nafsi na hata kutazamia kwa
kutumia vifaa maalumu vya kubashiria. Lakini polepole hivyo vya mwisho vikaja
kulaumiwa, kumbe Neno lenyewe likaja kushika nafasi ya kwanza kuliko dalili za
ajabu zinazoweza zikapatikana hata katika vichaa.
Kwa kuwa Roho ni wa
Bwana tu, akijalia unabii ni kama karama ipitayo: hivyo mtu yuleyule anaweza
akasema mara ukweli mara uongo. Vilevile karama hiyo haithibitishi usahihi wa
imani na uadilifu wa mhusika. Hatimaye baadhi yao wakaanza kuitwa "manabii wa uongo", kwa sababu ya kutabiri uongo kwa niaba ya
Mungu (kwa makusudi mazima au kwa kujidanganya) na zaidi kwa sababu ya
kupotosha imani na maadili ya taifa lake.
Manabii Eliya na Elisha (865-790 hivi K.K.)
Nabii Eliya alivyochorwa
na José de
Ribera.
Waisraeli walielekea dini za kandokando kwa
sababu zilikuwa zinaahidi kufanikisha maombi yao kwa ibada za hakika, wakati Mungu ana hiari ya kupokea au kukataa sadaka zao. Waisraeli walijaribu kufuata pande zote mbili kwa
pamoja, ila Mungu hakuweza kukubali, kwa kuwa ni peke yake tu. Imani yao iliyumba hasa
wakati mfalme Ahabu alipotawala Kaskazini (869-850 hivi K.K.), ambapo Yezebeli, mke wake, alifanya juhudi kubwa za kuikomesha
kabisa imani yao kwa YHWH ili wamuabudu Baali, mungu mkuu wa kwao aliyehusika
na mvua, kufuatana na sanamu mbili zilizotengenezwa na Yeroboamu I
zikiwa na sura ileile ya Baali (fahali wa dhahabu). Mezani pa malkia huyo
walikuwa wanalishwa manabii wa uongo 850 kumbe manabii wa Bwana waliuawa karibu
wote.
Hapo Mungu akamtuma
Eliya (1Fal 17-18) ambaye jina lake lina maana ya kwamba, “Mungu wangu ni YHWH” na
linajumlisha kazi yake ya kutetea kwa ari zote imani ya kweli
hata akaiokoa. Ili kuondoa utata wa kuabudu pande mbili, Eliya kwanza alizuia mvua
isinyeshe nchini miaka mitatu na nusu, ibada kwa Baali zisifanikiwe hata
kidogo, halafu akashindana na manabii hao hadhara ya Israeli yote juu ya mlima Karmeli. Tofauti na mbinu za manabii 450 wa
Baali, waliofikia kujichanja na kutoka damu ili kuvuta moto kutoka mbinguni wasifaulu, Eliya aliomba tu kwa unyofu kwamba Mungu ajitokeze
ili kugeuza mioyo ya watu wake wamrudie. Kwa kuteremsha moto toka mbinguni juu
ya sadaka yake YHWH alithibitisha kuwa ndiye Mungu pekee na kuwa anaendelea
kuwaokoa watu wake. Baada ya Eliya kuwachinja wote aliruhusu mvua inyeshe tena.
Ndiyo sababu anasifika kwa nguvu ya sala yake (Yak 5:17-18).
Hasa ni kwamba, baada ya
kukimbia hasira ya Yezebeli aliyemuapia atamuua kabla ya kesho yake, akisali pangoni juu ya mlima Sinai kama
Musa mwanzoni mwa agano la Israeli na Bwana, alijaliwa kutokewa na
kuagizwa upya na Mungu katika sauti ndogo ya upepo mtulivu akamilishe kazi yake
hasa kwa kuwafanya Elisha nabii na Yehu mfalme (1Fal 19:1-18).
Hata katika Yesu kugeuka sura mlimani akatokea pamoja na Musa ili wamshuhudie
kama wawakilishi wa Torati na Manabii (Mk 9:2-13).
Kwa jinsi alivyofanya
kazi kwa ari, na kwa kupalizwa juu ya gari la moto (2Fal 2:1-18) akalinganishwa
na moto (YbS 48:1-11) akatabiriwa atarudi kabla ya siku ya Bwana (Mal 3:23-24).
Ndiyo sababu Injili zinamtaja mara nyingi.
Elisha akimfufua mtoto
wa mwanamke Mshunami katika mchoro wa mwanzo
wa karne ya 20.
Kwa miaka zaidi ya 50
kazi yake iliendelezwa na Elisha, ambaye anasifika pia kwa miujiza yake (YbS
48:12-16) na pamoja na mwalimu wake amechukuliwa na Yesu kama mfano wa unabii
wake utakaowaokoa mataifa baada ya Israeli kumkataa (Lk 4:24-27). Elisha
alijihusisha sana na siasa akaombwa shauri na wafalme mbalimbali
hata wa nchi za nje. Kwa kumpaka mafuta Yehu alianzisha mapinduzi dhidi ya ukoo wa Ahabu na kukomesha upotoshaji wake wa imani.
Mapinduzi hayo yakaenea kusini kwa kumuua Atalia, dada (au binti) wa Ahabu, aliyetawala miaka saba kisha
kuua watu wote wa ukoo wa Daudi (mtoto Yoashi tu alinusurika).
Nabii Amosi (786-746 hivi K.K.)
Nabii Amosi kadiri ya
Gustave Doré.
Mungu aliendelea kukazania ufalme wa
kaskazini kabla haujaangamizwa
kabisa: tahadhari kabla ya hatari. Ndiyo sababu alimtuma
huko Amosi kutoka ufalme wa
kusini, alipokuwa mfugaji karibu na jangwa. Amosi aliona maendeleo makubwa ya kaskazini chini ya mfalme Yeroboamu II, lakini hakudanganywa nayo, bali alitabiri yatakoma
mapema. Aliona Waisraeli wanaoshika sabato na ibada mbalimbali, lakini wananyanyasa wenzao maskini: hapo akapiga kelele kudai kwanza haki itiririke kama maji ya mto ili ibada ziwe na
maana. Hatimaye alikatazwa asiendelee kuhubiri, pia kwa sababu alikuwa mtu wa
kusini, hivyo walifikiri anasema kwa kijicho tu.
Tofauti na Eliya na Elisha wasioacha maandishi, nabii huyo ana kitabu chenye
mafundisho yake aliyoyatoa Kaskazini ingawa alikuwa mtu wa Kusini. Hakutarajia
kutumwa na Mungu, ila ilimbidi akubali kutabiri kwa niaba yake (7:10-17), hasa
kuwa Israeli itaangamizwa na kutekwa na Waashuru utumwani kwa makosa dhidi ya
imani na ya haki pamoja na anasa (5-6). Waisraeli wakakataa maneno yake hata
wakatendwa alivyowatabiria (2Fal 17:5-23).
Nabii Hosea (750-725 hivi K.K.)
Picha ya nabii Hosea ya karne ya 18, monasteri ya Kizhi, Karelia, Russia.
Muda mfupi baada ya Amosi, nabii Hosea alianza
kazi yake katika ufalme wa kaskazini pia, akaweza kuendelea nayo kwa muda mrefu
akiwa mwenyeji. Yeye hakufundisha kwa
maneno tu, bali hasa kwa maisha yake: mtindo wa kufikirisha kwa matendo ya kushangaza ulitumiwa
na manabii wengi, hata na Yesu.
Aliitwa kuoa kahaba ili awaonyeshe Waisraeli katika matatizo ya ndoa yake jinsi Mungu alivyopenda taifa hilo ingawa linapenda
kufuata miungu mingine badala ya kuwa aminifu kwake tu. Kwa mfano hai wa Hosea,
Mungu alitaka waelewe kwamba kwa kuwapenda na pengine kuwaadhibu analenga tu
hatimaye wampende kwa moyo wote.
Sura 1-3 zinasimulia
Hosea alivyompenda mke wake aliyemzalia watoto wa uzinzi, hata hivyo akaendelea
kumpenda na kumtafuta hata baada ya kumfukuza, akamkomboa na kumrudisha ili
ambembeleze zaidi na hatimaye amfanye amrudishie upendo kama wakati wa uchumba. Hivyo adhabu yenyewe ilitokana na upendo na kulenga umoja wa dhati.
Hata Mungu, baada ya
kuacha Israeli ishindwe na Waashuru, ataendelea na upendo wake kwa wenzao wa kusini,
akiwabakiza kama mbegu (ndio “mabaki ya Israeli” yaliyozungumziwa kwanza na
Amosi): mpango wa Bwana unapitia hatua mbalimbali lakini
haukatiki kamwe.
Mfano huo wa upendo wa
Mungu kwa bibiarusi asiye mwaminifu uligusa
sana watu ukazidi kuzingatiwa mpaka katika Agano Jipya na kuchangia uimara wa ndoa iliyofikiriwa
upya kama upendo mwaminifu, si kama uhusiano wa kisheria au wa
kimwili tu ambao udumu mpaka utakapoendelea kuleta faida. Zaidi ya hayo,
uliwaelekeza Waisraeli kupokea fundisho la Yesu kwamba dini ni suala la upendo, si ibada
wala sheria tu.
Nabii Isaya (740-700 hivi K.K.)
Wakati wa Hosea kufanya unabii kaskazini, Mungu aliita wengine kusini; kati yao muhimu
zaidi ni Isaya, kuhani wa Yerusalemu mwenye elimu nzuri ambayealizaliwa
Kusini mwaka 765 hivi, akatabiri kwa muda usiopungua miaka 40 akiingilia kati
matukio yote ya siasa, ambayo yalikuwa ya kutisha kutokana na nguvu za Waashuru ambao waliangamiza Israeli na kukaribia kufuta hata
ufalme wa Kusini.
Maandishi yake
yanapendeza kuliko yote, hasa upande wa ushairi. Lakini ukuu wa Isaya uko hasa upande wa
imani.
Kuanzia wito wake alioupata
hekaluni, alipong’amua kwamba Mungu ni mtakatifu kabisa, yaani tofauti mno na
yeyote na chochote (6), alitawaliwa na wazo la utukufu wa Mungu na la unyonge wa binadamu anayehitaji
kutakaswa naye. Kwa msingi huo alidai wafalme na wananchi wote wa Yuda
wamtegemee Mungu tu, si mataifa yenye nguvu, hata upande wa siasa na mbele ya hatari kubwa namna gani.
Lakini toka mwanzo
aliambiwa hatasikilizwa, hivyo ikambidi atabiri adhabu. Kweli hali haikuwa shwari, ndiyo sababu wengi
walishindwa kuamini na kutulia, wakaendelea kujifanyia mipango na kutafuta msaada kutoka kwa binadamu, hasa Farao wa Misri. Hapo Mungu alimuagiza
Isaya atembee uchi mwaka mmoja unusu ili kudokeza kuwa Wamisri watafanywa watumwa wa Waashuru wasiweze kusaidia kitu (20:1-6).
Katika kutuliza watu
alimtabiria mfalme Ahazi kwamba mwanamwali atamzaa mtoto wa kiume
atakayethibitisha uwepo wa Mungu pamoja na watu wake, jina lake Emanueli linavyomaanisha. (7:1-17) Kweli mke wa Ahazi alimzaa Hezekia atakayeendeleza ufalme wa ukoo wa Daudi, lakini utabiri huo ulimlenga zaidi Yesu, mwana wa Bikira (walivyoelewa watafsiri wa kwanza wa Biblia katika Kigiriki) ambaye kweli ni Mungu pamoja nasi, na ni mwana wa
Daudi ambaye atatawala milele kwa amani na haki (11:1-9).
Hivyo, pamoja na adhabu
kwa utovu wao wa imani (22:1-14),
Isaya aliwatabiria watu wa Yuda kuwa Mungu hataangamiza
kabisa taifa lake, bali ataacha mabaki yake ambayo yataleta wokovu (10:20-23):
katika mabaki hayo Bikira atamzaa Masiya ambaye ni Mungu pamoja nasi, mwana wa
Daudi ambaye ataleta amani na haki duniani.
Nafasi ya mwisho kwa
Isaya kutuliza watu ilikuwa mwaka 701 K.K. ambapo jeshi kubwa la Waashuru
lilizingira Yerusalemu na kutamka maneno ya kumkufuru Mungu. Isaya
aliwarudishia jibu la dharau, nao kweli wakakimbia
haraka baada ya kupatwa na tauni.
Isaya ni maarufu pia kwa
ubora wa mashairi yake yaliyofanya ujumbe wake upendeze na uguse zaidi. Kwa
sababu hiyo wengi walipenda kuyakariri na kuyasoma na hata kuiga mtindo wake:
ndiyo maana kitabu chake kiliongezewa maandishi mengine mengi mpaka miaka mingi
baada ya mwenyewe kuuawa kwa kukatwa kwa msumeno.
Nabii Mika (740-700 hivi K.K.)
Nabii Mika kadiri ya Gustave Doré.
Wakati mmoja na Isaya
alifanya kazi nabii Mika ambaye pia alitetea haki za wanyonge (2:1-11) na
kutabiri adhabu. Vilevile alitabiri juu ya Masiya kwamba atazaliwa Bethlehemu (5:1-3).
Baada ya hapo hatujui
vizuri kilichoendelea kwa miaka 60: au Mungu hakutuma manabii kwa sababu maangamizi ya ufalme wa kaskazini
yameshatokea na yale ya kusini yako bado mbali, au mfalme Manase aliyetawala karibu
miaka 50 aliwaua wote akitaka watu wake wafuate dini ya Waashuru ili
kuwapendeza mabwana hao. Kumbe chini ya mjukuu wake, mfalme mwema Yosia, manabii wakatokea tena
mfululizo kabla ya maangamizi ya Yerusalemu yaliyochangiwa na watoto wake ambao
hawakufaa kitu hata wakasababisha ukoo wa Daudi kukoma kutawala (586 K.K.).
Nabii Sefania (640-625 hivi K.K.)
Sefania akiwahubiria
watu (mchoro wa huko Ufaransa, karne ya 16.
Mtu huyo wa Yerusalemu
alihubiri kwa nguvu mwanzoni mwa ufalme wa Yosia, kabla huyo hajaanza
urekebisho wake wa kidini uliofuata kuvumbua hekaluni maandiko ya Kumbukumbu ya
Sheria. Pamoja na kutisha kwa matabiri yake, aliahidi wokovu kwa mabaki ya
Israeli, akisema watakuwa watu maskini na walionewa (3:9-20). Ndio mwanzo wa
imani ya kuwa wapenzi wa Mungu ni hasa mafukara, ambayo taratibu ilitia mizizi
katika Israeli hadi ilipokuja kukaziwa na Yesu (Lk 6:20-21).
Nabii Yeremia (626-585 hivi K.K.)
Mchoro wa Rembrandt van Rijn, "Yeremia Akililia
Maangamizi ya Yerusalemu", mwaka 1630 hivi.
Akiwa bado kijana, kuhani huyo mpole aliitwa na Mungu awe nabii katika kipindi cha misukosuko huko Mashariki ya Kati, ambapo Wakaldayo wa Babeli waliwashinda Waashuru na kueneza utawala wao hadi kuteketeza Yerusalemu na hekalu lake. Katikati ya matukio hayo yote, Yeremia alipewa kazi
ngumu ya kuonya na kutisha watu wa ufalme wa Yuda kwa kutabiri maangamizi hayo ili wamrudie kweli
Mungu wasipatwe na adhabu kali kama wenzao wa kaskazini. Lakini wao hawakuwa tayari kufanya hivyo,
wakijiamini hawatakoma kwa kuwa, tofauti na hao, wanatawaliwa na ukoo halali wa Daudi ulioahidiwa kudumu milele, tena wanatunza hekalu pekee la Mungu na sanduku la agano analokalia. Walidanganywa na manabii wa uongo waamini hivyo, kumbe walitakiwa kujirekebisha na
kufuata kweli masharti ya agano lenyewe.
Hivyo Yeremia
alilazimika kupambana na wote: wafalme, makuhani na manabii wenzake, ndugu wa ukoo wake na
wananchi kwa jumla. Ilimbidi ashindane nao kinyume cha silika yake ya upole iliyomfanya apende
kuelewana na watu. Upweke wake ulizidiwa na useja alioitiwa na Mungu ili
aonye hata kwa njia hiyo kwamba mambo yajayo ni magumu na ya kutisha hata iwe
afadhali kutozaa watoto.
Katika miaka yote 40 na
zaidi ya unabii wake kipindi kizuri ni miaka ile 13 tu (622 - 609 K.K.) ambapo Yosia alifanya urekebisho wa
kidini kuanzia Yerusalemu hadi kwa mabaki ya Waisraeli wa kaskazini, akizuia wote wasiabudu miungu mingine
wala wasimtolee Mungu sadaka nje ya hekalu la
Yerusalemu. Kipindi hicho mji mkuu
wa Ashuru uliangamizwa alivyotabiri kwa furaha Nahumu (612 hivi K.K.).
Lakini Yosia alipokufa vitani kabla ya wakati mambo
yakaharibika haraka sana, kwa sababu urekebisho ulitokana zaidi na juhudi zake binafsi. Basi,
ikambidi Yeremia awakaripie wafalme waliomrithi mmoja baada ya mwingine waache siasa yao ili kumtegemea
Mungu tu. Aliwakaripia pia wananchi wasifanye dini kisingizio cha kuendelea na
maovu badala ya kutubu (7:1-15; 19:1-13).
Aliwakaripia vilevile
manabii wa uongo waliotumainisha watu bure (20:1-6). Ndipo alipoanza kupigwa,
kufungwa na kuhukumiwa, akawa mfano wa Yesu, yeye ambaye peke yake katika Agano
la Kale aliishi bila ya ndoa kwa agizo la Mungu; lakini hakuuawa (26:1-19). Kwa
hofu akajificha, ila hakuacha kutabiri maangamizi kwa maandishi kwa njia ya
karani wake Baruku (36).
Basi, mfalme Nabukadreza II wa Babeli akazidi kuwa na nguvu: mwaka 602 K.K.
akamtiisha mfalme Yehoyakimu wa Yuda, na mwaka 598 K.K. akazingira Yerusalemu
akawahamishia Babeli mfalme Yekonia na viongozi wengine 8000. Hapo Yeremia akawaandikia
wasikate tamaa ila wasitarajie kurudi upesi kwa kuwa watabaki uhamishoni miaka
70 (29:4-23). Lakini katika mpango wa Mungu hao ndio wa kutegemewa, sio
walioachwa Yerusalemu (24). Nabukadreza alipohusuru mji huo mara ya pili,
mfalme na viongozi wengine walikataa shauri la Yeremia la kusalimu amri,
wakamfunga pabaya sana mpaka siku ya Yerusalemu kutekwa na kuteketezwa (37-38).
Yeye alishuhudia hayo
yote kwa huzuni kubwa na kati ya dhuluma nyingi hata akamlalamikia sana Mungu kwa kumuumba
awe mtu wa mateso. Toka mwanzo alitaka
kukataa wito wa unabii, na baadaye akafikia hatua ya kukata tamaa. Lakini Mungu
alimuita kwa mpango wa milele, Yeremia asiweze kukataa (15:10-21; 20:7-18). Unyofu wa maneno yake katika sala (Maungamo ya
Yeremia) unatuwezesha kumfahamu
mpaka ndani kuliko mtu yeyote wa Agano la Kale. Lakini mateso hayo hayakuwa bure, bali kwa njia
yake alizidi kuelewa dini kama suala la moyo. Ni hivyo kwamba aliona
agano lililoandikwa katika mbao za mawe limeshindikana, na tohara inayohitajika ni ile ya masikio na moyo. Basi, kwa
kutambua uaminifu wa Mungu, alitabiri
agano litakaloandikwa katika mioyo ya watu, ambao hapo wataweza kulishika na
kumfahamu kweli Bwana.
Kwa kawaida Yeremia
alitabiri kinyume cha matazamio madanganyifu ya watu, lakini walipokata tamaa
akawatuliza na kutabiri heri. Basi, kilele cha mafundisho yake na ya Agano la Kale lote ni kwamba Mungu atafunga na Israeli yote Agano
Jipya (31:31-34).
Baada ya Yerusalemu
kuteketezwa (587 K.K.) Yeremia alichagua kubaki nchini pamoja na mafukara
badala ya kuhamia Babeli kwa heshima ya pekee (39:8-40:6), ila ukatokea uasi
akalazimishwa na Waisraeli wenzake kuwafuata Misri: huko akawaonya wasifuate
Upagani lakini wakakataa tena kumsikiliza (42-44).
Hatimaye, kadiri ya mapokeo ya Wayahudi, akauawa nao huko. Ingawa alionekana kufeli kabisa, sadaka yake ilizidi kuzaa, kwa kuwa wengi walizingatia mafundisho
yake bora.
Kama nyongeza ya kitabu
cha Yeremia tuna Maombolezo matano juu ya
Yerusalemu ulioteketezwa, ambamo inaonekana toba halisi baada ya tukio hilo.
Hatujui yametungwa na nani.
Nabii Habakuki (600 hivi K.K.)
Sanamu ya
Habakuki iliyotengenezwa na Donatello, Museo dell'Opera del Duomo, Florence.
Wakati huo aliishi pia Habakuki, aliyeandika kitabu kifupi ambamo alithubutu
kumuuliza Mungu kwa nini anaadhibu Israeli vikali hivyo kwa mikono ya watu wabaya
kuliko wao. Jibu ni kwamba Mungu ana njia zake ambazo anaandaa ushindi wa haki:
hivyo mwadilifu ataishi kwa imani yake (1:12-2:4). Usemi huo ukaja kutumika
sana katika Agano Jipya.
Nabii Ezekieli (592-570 hivi K.K.)
Ezekieli, alivyochorwa na Pierre Paul
Rubens (1609-1610), Musée du
Louvre, Paris.
Polepole waliohamishiwa
Babeli waliweza kujitafutia kazi (kwanza kilimo, halafu biashara), wakafaulu
sana, hata wengine wakawa watumishi wa serikali. Lakini upande wa dini walikuwa
hatarini, kwa sababu imani ya Mwisraeli inategemea taifa, nchi na hekalu ambavyo
vyote vilikuwa vimeharibika.
Kwa ajili yao Mungu
akatuma tena manabii, hasa Ezekieli ambaye alihamishwa mapema mwaka 598 K.K.. Habari zake tunazipata katika kitabu chake tu, anapotajwa kwa jina mara tatu, kumbe kwa kawaida
Mungu anamuita “binadamu”. Kabla hajahamishwa aliweza kumfahamu Yeremia, na kweli aliathiriwa na ujumbe wake ambao aliuunga
mkono na kuuendeleza. Alifanya unabii wake hukohuko uhamishoni, ingawa ujumbe wake uliwalenga waliobaki Yuda pia. Kwanza aliwatolea
maneno ya hukumu ili watubu kabla hawajaangamia, lakini baadaye akawapa maneno ya faraja wasikate tamaa. Katika
kuwahakikishia kuwa wataanza upya nchini kwao aliwapa maelekezo yote kwa ajili
hiyo. Kwa namna ya pekee, akiwa kuhani, kama vile Yeremia, katika kitabu chake
alishughulika sana na hekalu na mambo ya ibada.
Upande mwingine
alianzisha mtindo mpya wa unabii ambao unaitwa wa Kiapokaliptiko (kilele chake
ni Ufunuo wa Yohane) na ambao hauhusu tena matukio madogomadogo ya
siasa, bali kwa njozi za ajabuajabu unaonyesha maana ya historia yote mpaka mwisho. Njozi 4 anazozisimulia
kinaganaga na zisizosahaulika (utukufu wa Mungu kuhama hekalu, utukufu huo kurudi hekaluni, hekalu kutokwa na maji yenye uwezo wa kuponya
hata Bahari ya Kifo, hatimaye mifupa mikavu kusimama na kuishi tena)
zinachukua nafasi kubwa katika kitabu chake na kwa mafumbo yake yanavutia ubunifu wetu ujitahidi kuelewa yaliyofichika katika mifano, tarakimu, rangi n.k.
Dini ya Kiyahudi mpaka leo inategemea sana kazi aliyoifanya Ezekieli ya
kukazia utekelezaji wa Torati hata pasipo uhuru wa
kisiasa. Muhimu kwake ni kwamba
Wayahudi popote walipo wamtukuze Mungu kwa kufuata sheria yake. Tena alitabiri kuwa Mungu tu atawawezesha kufanya
hivyo kwa kugeuza mioyo yao migumu kama mawe yadunde kama ile ya nyama, au vizuri zaidi kwa
kuwatia moyo mpya na roho mpya wazishike amri zake (11:17-20; 36:26).
Mungu atawaokoa kabla hawajatubu ili jina lake litukuzwe katika watu wake:
wokovu anaouleta hautegemei matendo mema ya binadamu, bali muungano wa Mungu na
wale walioitwa kwa jina lake (16:58-63). Hakuna kitabu kinachosisitiza utukufu
wa Mungu kuliko hicho.
Isaya II na III (550-500 K.K. hivi)
Ingawa Ezekieli alifanya kazi nzuri, waliokuwa uhamishoni waliendelea kuzoea na
kufurahia mazingira mapya yenye ustawi wa kiuchumi wakazidi
kupotewa na hamu na tumaini la kurudi Yerusalemu. Ndiyo sababu Mungu aliwatumia nabii mwingine mkubwa:
hatujui jina lake, lakini tunamuita Isaya II kwa kuwa alifuata mapokeo ya Isaya na kulingana naye kwa ufasaha wa mashairi aliyoyatumia kutolea ujumbe wake; hivyo maandiko yake yamepangwa katika kitabu cha Isaya (40-55). Sehemu hiyo inaitwa pia kitabu cha faraja ya Israeli kwa sababu ililenga kuwatia moyo Wayahudi wenzake huko Babeli kwamba Mungu atawarudisha kwao akitumia kama chombo chake mfalme Mpagani, kwa kuwa yeye anatawala watu wote pamoja na mioyo
yao (Is 40:1-11). Hivyo akawafanya watamani kurudi badala ya kukwama katika
kujitafutia maendeleo ya kidunia.
Kwa uchangamfu wa hali ya juu Isaya II
alitabiri ukombozi na mwanzo mpya wa taifa kama ajabu kubwa kuliko lile la mababu wao kutoka Misri chini ya Musa. Alilifananisha na uumbaji mpya utakaowezekana kwa sababu Mungu wa Israeli si
mmoja kati ya wengi, walivyodhani kwa muda mrefu, bali kweli ni peke yake, hakuna
mwingine: ndiyo sababu anaweza yote. Imani hiyo ilizidi kutia
mizizi kati ya Wayahudi na kuwaimarisha dhidi ya kishawishi cha kuabudu wengine.
Pamoja na hayo, katikasura hizo mna mashairi manne
bora kuhusu mtumishi
mteswa wa Bwana ambayo ndiyo utabiri bora juu ya Yesu na juu ya wokovu atakaoleta kwa kuteseka mwenyewe ili kufidia dhambi za wote (42:1-4; 49:1-6; 50:4-9; 52:13-53:12). Hatimaye
Isaya II ndiye aliyeandaa dini ya Kiyahudi kupokea mataifa yote.
Isaya 56 66 ni sura za
baadaye tena (Isaya III, mwaka 500 hivi K.K.) ambazo zinawakaribisha watu wa mataifa yote kujiunga na Israeli katika kumuabudu Mungu pekee. Kiini chake ni 61:1-3.
Wayahudi kuanza upya Yerusalemu chini ya Waajemi
(538-333 K.K.)
Koreshi Mkuu akiruhusu
Wayahudi kurudi Yerusalemu kutoka Babuloni (mchoro mdogo wa Jean Fouquet, 1470-1475 hivi).
Utabiri wa Isaya II
ulitimia mwaka 538 K.K. ambapo mfalme Koreshi Mkuu wa Uajemi, mwaka mmoja baada ya kuteka Babeli, aliwaruhusu Wayahudi
warudi Yerusalemu pamoja na vitu vilivyotekwa nyara toka hekalu lake
ili kuvijenga upya. Wengi hawakukubali kwa sababu walilinganisha mazingira hayo tofauti. Waliorudi walikuwa kama elfu tano tu na familia zao, lakini wote wenye imani na nia thabiti, wakiwemo makuhani na Walawi wengi waliorithi katika ukoo wao upendo kwa ibada za hekaluni.
Kama kawaida, imani yao ilitakiwa
kupitia majaribu mbalimbali, kuanzia
mazingira magumu, kwa sababu hali waliyoikuta ilikuwa
mbaya kuliko ile ya kabla ya uhamisho: majengo na mashamba yalikuwa yameharibika kwa kukaa miaka 48 bila ya watu,
tena makabila ya jirani hawakupenda Wayahudi warudi, hivyo waliwazuia kwa namna mbalimbali. Wasamaria, mchanganyiko wa mabaki
ya Israeli kaskazini na watu wa mataifa walioletwa na Waashuru waishi nao, walitaka kusaidia ujenzi wa hekalu, lakini walipokataliwa wakawa maadui moja kwa moja.
Hata hivyo utabiri
ulitimia, na kwa msaada wa Mungu kupitia watu wake mbalimbali, kuanzia manabii Hagai na Zekaria, kundi hilo dogo likawa mwanzo mpya wa taifa la
Mungu: walimuabudu kwa bidii katika hekalu jipya ingawa dogo (Ezra 3:10-13), walijipatia
usalama kwa kujenga tena kuta za Yerusalemu (Neh 4:13-23; 12:27) na
walijitenga kabisa na Wapagani: waliokuwa wameoa wake wa kigeni walilazimishwa
kuwafukuza pamoja na watoto waliowazaa kwa njia yao (Ezra 9-10; Neh 9-10).
Gustave Doré, Nehemia Akikagua Magofu ya Ngome ya Yerusalemu,
1866.
Habari hizo zinapatikana
hasa katika vitabu vya Ezra na Nehemia, mfululizo wa vile vya Mambo ya Nyakati. Waandishi wa vitabu hivyo vinne waliishi miaka mia hivi
baada ya matukio: ndiyo sababu waliweza wakachanganya habari za hao watu wawili
ambao walifanya juhudi mpya tena kali, wa kwanza upande wa dini, wa pili upande
wa siasa, labda kwa nyakati tofauti. Nehemia alipokuwa liwali wa mkoa wa Yuda
wakazi walikuwa hamsini elfu tu, na eneo lao lilikuwa dogo sana. Kuhani Ezra
anasifiwa zaidi kutokana na mchango wake mkubwa katika kulipatia taifa teule
sura ya kudumu, kama watu wanaoambatana kabisa na Torati, ambayo toleo lake la
mwisho lilipitishwa na mfalme wa Uajemi wakati huo kuwa sheria kuu ya Wayahudi
(Ezra 7:1-28). Hivyo dini yao ikawa “dini ya
kitabu” hata leo.
Manabii wa mwisho wa Agano la Kale
Katika karne mbili za utawala wa Waajemi unabii ulizidi kufifia ukiacha nafasi kwa aina nyingine za uongozi wa
kiroho: wataalamu wa Torati na watu wenye hekima waliotunga vitabu kwa uvuvio wa Mungu bila ya kupatwa na hali za pekee kama manabii.
Manabii wa mwisho walikuwa Hagai, Zekaria, mwandishi wa Kitabu cha Malaki, Obadia, na Yoeli, mbali na wengine ambao hatuwafahamu, lakini walihakiki na
kuchangia vitabu vya manabii waliotangulia.
Mwaka 520 K.K. Hagai alihimiza ujenzi wa hekalu jipya kama njia ya
kujipatia baraka za Mungu katika hali ngumu ya miaka ya kwanza baada ya kurudi
Yerusalemu (1:3-11). Hasa alitabiri kuwa siku za mbele utukufu wa hekalu hilo utakuwa mkubwa kuliko ule wa hekalu
la Solomoni: ikawa hivyo kwa sababu ya upanuzi na urembaji ulioanza chini ya Herode Mkuu, lakini zaidi kwa sababu Yesu alilitakasa na
kufundisha humo na hatimaye mwili wake mtukufu ukashika nafasi yake.
Wakati huohuo Zekaria
naye alitamani ujenzi huo lakini pamoja na toba ili ibada na makuhani wampendeze Mungu (1:3-6). Baada ya kumaliza ujenzi wa
hekalu (515 K.K.), taratibu za ibada ziliendelea moja kwa moja,
lakini tarajio la wengi la kuona
mapema taifa la Mungu lina hali tukufu halikutimia. Hivyo ilitokea tena hali
ya kukata tamaa iliyowafanya makuhani
na Wayahudi kwa jumla wamtumikie kwa uzembe.
Ndipo alipotumwa nabii
Malaki kukaripia makosa yao katika kumuabudu, akijibu hoja zao na kutabiri ujio wa
mjumbe wa Agano na wa mjumbe mwingine atakayemuandalia njia; hapo maadili na
ibada vitaratibishwa tena (3:1-5) na kila mahali itatolewa sadaka safi kwa
Mungu (1:11). Katika wajumbe hao wawili Wakristo waliwatambua kwa urahisi Yesu
na Yohane Mbatizaji.
Baada ya kazi za Ezra na Nehemia, nabii Obadia aliishia kutangaza kifupi adhabu ya Mungu kwa Waedomu, kielelezo cha maadui wa taifa la
Mungu, siku yake itakapofika.
Muhimu zaidi ni unabii wa Yoeli aliyetangaza vivyo hivyo siku ya Bwana akichukua mfano hai wa uvamizi wa nzige wengi uliolazimisha
Wayahudi wote kufanya toba, lakini alitabiri pia mmiminiko wa Roho wa Bwana juu ya watu wake wa
kila aina (2:28-32) alivyoomba Musa na utakavyowatokea
wanafunzi wa Yesu siku ya Pentekoste (Mdo 2:16-21). Hivyo tapo la unabii kabla
halijakoma lilitabiri kipindi kingine cha unabii chenye kustawi kuliko cha
awali.
Vitabu vya Hekima vya kwanza
Pengine ni wakati wa Waajemi kwamba, baada ya muda mrefu wa mapokeo ya
sauti, vilianza kuandikwa vitabu vya hekima (Kitabu cha Methali, Kitabu cha Ayubu) na vinginevyo (Wimbo Ulio Bora, Zaburi nyingi). Wenye hekima ni watu wanaopatikana katika makabila yote, hasa kati ya wazee wenye mang’amuzi mengi. Toka zamani watu
wa namna hiyo walitegemewa kwa malezi ya vijana ili wajue jinsi ya kukabili vizuri maisha. Mbali na mithali na mafundisho yaliyotolewa kwa sauti, baada ya uandishi kubuniwa hata vitabu vya namna hiyo vilianza
kutungwa katika lugha mbalimbali. Waisraeli walifaidika na hekima ya nchi jirani zilizostaarabika zaidi, kwa namna ya pekee Mesopotamia na Misri. Hasa wakati wa amani na ustawi uliopatikana chini ya mfalme Solomoni, wenye hekima waliweza kujitokeza katika Israeli,
kuanzia mwenyewe: ndiyo sababu aliendelea kuchukuliwa kama kielelezo cha
hekima.
Ingawa vinafanana na
vile vya makabila ya jirani, vitabu vya hekima vilivyomo katika Biblia vinafikiria maisha kwa mwanga wa imani katika Mungu aliye
mmoja tu, hasa kwa kuzingatia uzima na kifo, uchungu, mwenendo, heri n.k.
Mithali ndicho kitabu cha kwanza cha aina hiyo, hivyo kinatuletea mawazo na maneno
ya zamani zaidi na ya kwamba Mungu anamtuza mwadilifu na kumuadhibu mwovu hapa
duniani.
Mtazamo huo ulianza
kupingwa na kitabu cha Ayubu kinakataa mtazamo huo kwa kuonyesha hali halisi,
yaani kuwa duniani mara nyingi mwadilifu ndiye anayeteseka; hata hivyo kinasema
binadamu hawezi kujua ni kwa nini: basi amuachie Mungu na kumuabudu katika
fumbo lake linalozidi akili yetu (42:1-6).
Wimbo ulio Bora haumtaji
Mungu wala dini: ulihusu mapenzi ya wachumba, lakini ukaja kufafanuliwa kama
mapenzi ya Mungu na Israeli wanaotafutana ili kuungana kabisa. Zaburi, ambazo
zilitungwa na kurekebishwa polepole kwa muda unaokaribia miaka elfu, yaani muda
ule wote uliotumika kutunga vitabu vingine vyote vya Agano la Kale, ndizo sala
za kishairi au nyimbo ambazo katika hali ya sifa, ibada, shukrani na dua
zinajumlisha Biblia nzima.
Uenezi wa utamaduni wa Kiyunani (333-63 K.K.)
Mchoro wa Antonio
Ciseri, Kifodini cha Watoto
Saba (1863), unamuonyesha mama kati ya maiti za watoto wake 7
waliokubali kuuawa kikatili ili wasiasi dini ya Kiyahudi.
Kwa muda mfupi sana Aleksanda Mkuu wa Makedonia (Ulaya Kusini Mashariki) aliteka Asia (mpaka India) na Misri. Kuanzia hapo
utamaduni na lugha ya Kiyunani vikaenea pote, hata kwa Wayahudi wengi, hasa
walioishi nje ya nchi yao. Chini ya utawala wa Kiyunani unabii ukaja kwisha
(1Mak 9:27): badala yake yalitolewa maandiko ya kiapokaliptiko (hasa kitabu cha Danieli ambacho ni kama Ufunuo
wa Agano la Kale), hadithi (Yona, Tobiti, Esta, Yudithi) na vitabu vingine vya hekima (Mhubiri, Yoshua bin Sira, Hekima).
Humo tunaona maendeleo
ya ufunuo, hasa kwa sababu Wayahudi wengi walianza kusadiki ufufuko wa wafu na
mengineyo. Nguvu ya imani hiyo iliwasaidia kukabili dhuluma na kifo (2Mak 7:1-41) chini ya Antioko Epifane (175-164 K.K.) aliyetaka kuwalazimisha waache
kufuata Torati ili wajilinganishe na watu wengine. Tena akijidai kuwa tokeo la
Mungu Mkuu alijenga altare kwa mungu wake ndani ya hekalu la Yerusalemu. Hapo
Wayahudi wakaanza kupigania uhuru wao wa kidini na wa kisiasa chini ya ukoo wa Wamakabayo, ambao kwa imani na ushujaa mkubwa wakafaulu
kushinda majeshi ya kutisha (1Mak 3:18-22), kutakasa hekalu (1Mak 4:36-61) na
kurudisha ufalme wa Israeli mpaka baada ya Warumi kuweka Uyahudi chini ya himaya yao (63 K.K.). Habari hizo
zinapatikana katika vitabu viwili vya Wamakabayo ambavyo havifuatani kwa kuwa
viliandikwa na watu tofauti katika karne II K.K.
Matukio hayo ndiyo asili
ya kundi la Mafarisayo (yaani “waliojitenga”), walioshika kwa bidii Torati
kadiri ya mapokeo ya walimu wa sheria, wengi wao wakiwa walei. Kwa jumla
walileta uamsho wa kiroho kati ya Wayahudi, lakini walidharau wenzao wasiojua
Maandiko Matakatifu. Pia walishindana sana na Masadukayo kuhusu masuala ya dini na ya siasa hata kusababisha
mauaji; kwa kuwa Masadukayo (waliokuwa na nguvu kati ya makuhani) walikataa
mafundisho hayo mapya huku wakishika Torati tu.
Yona ni simulizi
lililowahimiza Wayahudi waachane na ukabila kwa sababu Mungu anawahurumia watu
wote (3-4). Kitabu cha Tobiti kinachora uadilifu wa Kiyahudi: uaminifu kwa
Torati, upendo katika familia, sadaka kwa maskini, heshima kwa marehemu,
utakatifu wa ndoa (12:6-22). Vitabu vya Esta na Yudithi vinahadithia ushujaa wa
wanawake hao ili kuhimiza msimamo wa kufaa kwa wakati vilipoandikwa ambao
ulikuwa mgumu kwa watu wa Mungu (Est 3:13a-g; Yudithi 13:11-20). Mhubiri
alisisitiza ubatili wa malimwengu yote (1:1-11) akimuunga mkono mwandishi wa
Ayubu: mang’amuzi yanaonyesha matarajio ya kidunia hayana maana (8:10-17).
Yoshua bin Sira alikabili pia masuala hayo (15:11-16:23), akituelekeza tutafute
jibu katika siku ya mwisho. Kitabu cha Hekima kinakisiwa kuwa cha mwisho
kuandikwa katika Agano la Kale kwa kuwa kilitungwa miaka 50 tu K.K. huko Misri
katika lugha na utamaduni wa Kiyunani. Kina mpango mzuri sana na kutoa jibu
wazi kuhusu suala la haki ya Mungu kwa waadilifu na waovu, kikifundisha uzima
wa milele (2:23-3:10) hata kuliko kilivyowahi kufanya kitabu cha Danieli
(12:1-4). Mbali na sehemu ya kitabu hicho na ya Esta, vile vyote vilivyoandikwa
karne mbili za mwisho K.K. na kutunzwa kwa lugha ya Kiyunani vikaja kukataliwa
na Wayahudi katika kubishana na Wakristo waliovitumia (mwaka 80 hivi B.K.),
halafu na Waprotestanti wengi. Vinaitwa deuterokanoni (yaani “orodha ya pili”).
Baada ya Torati kuzidi
kuzingatiwa na Wayahudi, wataalamu wake pia walizidi kuheshimiwa kama watu wa
Neno la Mungu, wanaoleta mwanga wake katika maisha ya jamii. Hekima,
iliyotafutwa hasa chini ya Wagiriki, ilipotambulika kuwa inapatikana katika
Torati, wataalamu hao wakaja kushika nafasi ya watu wa hekima kama vile hao
walivyoziba pengo lililoachwa na manabii. Wayahudi walizoea hali hiyo kiasi
kwamba wakaona vigumu kumkubali Yesu ambaye hafafanui Torati kwa kufuata
mapokeo ya wataalamu, bali kwa kujiamini kama manabii waliojiona wabebaji wa
Neno la Mungu. Kweli ndiye Hekima ya milele ambaye ndani yake tunamjua Mungu,
hivyo mwenendo wake na mafundisho yake haviwezi kuishia mambo yaliyozoeleka,
kwa sababu kila mara ya Mungu yanapindua ya binadamu. La kufanya ni kujitahidi
kufuata halafu kuelewa: ndiyo wongofu ambao Yesu aliudai pamoja na imani.
Agano Jipya
Mazingira ya Yesu
Palestina katika karne ya 1 BK.
Nchi ambayo Yesu
alizaliwa akafundisha ni nchi ileile ambayo Mungu aliwaahidia Waisraeli tangu
zamani za Abrahamu, ni nchi ileile waliyoiteka chini ya Yoshua, ni nchi ileile
waliyoirudia kutoka utumwani Babeli. Lakini wakati wote wa Agano Jipya, yaani
tangu Yesu alipozaliwa hadi mwisho wa maisha ya mitume wake, nchi hiyo haikuwa
huru, bali chini ya himaya ya Warumi, ingawa pengine hao waliwakabidhi vibaraka, yaani watawala wenyeji
waliowekwa na wakoloni. Vibaraka hao ni Herode Mkuu (37-4 K.K.) na wazawa wake, ambao tena hawakuwa
Waisraeli halisi bali Waedomu ingawa kabila lao lililazimishwa kuingia dini ya
Kiyahudi karne iliyotangulia. Ukoo huo unajulikana kwa ukatili, uchu wa
madaraka na uzinifu wake.
Vilevile maliwali wa
Kirumi waliowekwa pengine kutawala nchi au sehemu fulani walionyesha mara
nyingi ukatili na dharau kwa Waisraeli na dini yao, hata kusababisha chuki na
mapigano kati ya jeshi na wananchi. Mfano mmojawapo ni Ponsyo Pilato aliyesimamia Uyahudi kuanzia mwaka 26 hadi 36 B.K.
Mbali na hayo, utawala wa Roma, ulioenea Ulaya Magharibi na Kusini, Afrika Kaskazini na nchi za Mashariki ya Kati kupakana na Iraq ya
leo, kwa jumla ulihakikisha hali ya amani kwa muda wote wa Agano Jipya na karne
za kwanza za Kanisa. Hali hiyo, pamoja na umoja wa dola hilo lote, na urahisi
wa mawasiliano kwa njia ya barabara zilizotengenezwa na Warumi, na uenezi wa
lugha ya kimataifa (Kiyunani), ilichangia kasi ya uenezaji Injili. Lugha hiyo
ndiyo iliyotumiwa na waandishi wote wa Agano Jipya ili vitabu vyao viwafaidishe
watu wengi zaidi, ingawa baadhi yao hawakuijua vizuri.
Lugha asili ya Yesu na
ya Mitume ilikuwa Kiaramu ambacho ni jamii ya Kiyahudi na ambacho polepole
kilishika nafasi yake kati ya Wayahudi kuanzia karne VI K.K. Hao wote walitokea
mkoa wa Galilaya, uliokuwa na mchanganyiko wa watu (Waisraeli na
mataifa), kiasi kwamba huko Wayahudi wenyewe walifuata kwa urahisi desturi za
Kiyunani hata wakadharauliwa na wenzao wa Kusini (Yerusalemu na mkoa wa Yudea).
Kati ya mikoa hiyo miwili ulienea mkoa wa Samaria ambao wakazi wake walijenga uadui mkubwa na Wayahudi
baada ya uhamisho wa Babeli, walipokataliwa kuchangia ujenzi wa hekalu la pili
la Yerusalemu.
Maisha ya Yesu
Dionisi Mdogo, mmonaki aliyeanzisha (mwaka 533 hivi) mtindo wa kuhesabu
miaka kuanzia kuzaliwa Yesu kurudi nyuma (K.K.) au kwenda mbele (B.K.), alikosea hesabu zake.
Leo tunakisia Yesu alizaliwa mwaka 6 hivi K.K. kwa sababu alizaliwa Bethlehemu
chini ya Herode Mkuu aliyefariki mwaka 4 K.K. Huyo alipojaribu kumuua mtoto
Yesu, familia takatifu ilikimbilia Misri mpaka baada ya kufa kwake. Hapo
ikarudi Galilaya hata Yesu akajulikana kwa jina la kijiji cha Nazareti kilichodharauliwa na Wagalilaya pia. Ndipo
alipokulia na kuishi akifanya kazi ya ufundi.
Nazareti katika kadi ya zamani ya Fadil
Saba.
Yohane Mbaptizaji kadiri ya Bartolomeo
Veneto, karne ya 16.
Yesu akimponya mtu
aliyepooza ni kati ya picha zake za zamani zaidi (karne ya 2); iko katika ukuta wa sinagogi la Dura Europos.
Mwaka 26 hivi B.K. ndugu
yake Yohane Mbatizaji aliacha maisha ya jangwani na kuanza kuhubiri toba
kandokando ya mto Yordani. Kwa kuwa Waisraeli walikosa manabii kwa muda mrefu,
na walitamani sana ukombozi, walimuendea kwa wingi hata wakamtia hofu Herode Antipa. Ingawa huyo akamfunga mapema akamuua, kazi ya
Yohane ilikuwa imetimia kwa sababu aliweza kuwaandaa Waisraeli wengi (hasa watu
wadogo na wakosefu) wampokee Yesu aliyebatizwa naye. Katika nafasi hiyo Yohane
alimtambulisha kama Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu.
Ndipo Yesu naye
alipoanza kuhubiri, lakini pia kutenda miujiza ya kila aina, akapata haraka
wafuasi wengi. Kati yao akachagua mitume wake 12 kama msingi mpya wa taifa la Mungu.
Alifanya kazi hizo
kuanzia Galilaya, akitangaza ujio wa ufalme wa Mungu, kwa maana ya kwamba ufalme uliotazamiwa na Wayahudi
umewajia kwa njia yake.
Ingawa hakupitia shule
yoyote ya Biblia, Yesu alionekana anafundisha vizuri kuliko walimu wa sheria wa
kawaida, kama mtu mwenye mamlaka juu ya Torati. Mafundisho yake yalilingana na
yale ya Mafarisayo kuliko na yale ya Masadukayo, lakini alishindana pia na hao
wa kwanza.
Kijicho na upinzani
vikazidi hasa Yerusalemu, walipoanza kufanya njama za kumuua. Ingawa Yesu
alijua hayo, alijikaza kwenda katika mji mtakatifu autangazie habari njema na
kufia huko. Baada ya kupokewa kwa shangwe kabla ya sherehe ya Pasaka ya mwaka
30 (au 33) akakamatwa na baraza la
Israeli kwa tuhuma ya kufuru ya kujilinganisha na
Mungu, halafu akakabidhiwa kwa liwali wa Kirumi aliyekuwa na mamlaka ya kutoa
adhabu ya kifo. Baada ya kikao ambapo Wayahudi walitafuta kisingizio cha
kisiasa, Ponsyo Pilato akalazimika kuagiza Yesu asulubiwe, na kisha kufa kwake
kaburi lilindwe na askari.
Hata hivyo siku ya tatu kaburi likaonekana tupu, na Yesu akaanza kuwatokea wanafunzi wake
wa kike na wa kiume kwa muda wa siku arubaini, halafu akapaa mbinguni mbele ya
macho yao.
Habari hizo zikatangazwa
kwa sauti tu kwa miaka kadhaa, halafu zikaanza kuandikwa.
Ufunuo kuendelea baada ya ufufuko wa Yesu
Kurasa 4 za Injili ya Luka zilizonakiliwa katika karne ya 3 katika nyasi zilizopondwa.
Kifo na ufufuko wa Yesu si mwisho wa ufunuo wa Mungu: ni lazima tupokee vilevile kama mpango wake yale
yaliyojitokeza wakati wa Mitume wake. Miaka hiyo 70 hivi iliona Kanisa likizidi kusogea mbali na dini ya Kiyahudi na kuwa la kimataifa kweli pamoja na kupata muundo wa kudumu wa uongozi. Sambamba na hilo, makao yake makuu yalihamia Roma kutoka Yerusalemu uliokuja kuangamizwa tena mwaka 70. Ni wakati huohuo
kwamba lilipata vitabu
vitakatifu vya kwake
vilivyokamilisha vile vya Agano la Kale. Kanisa linaheshimu kwa namna ya pekee, kama
ushuhuda mkuu juu ya maisha na mafundisho ya Yesu na kama moyo wa Maandiko
matakatifu yote, Injili nne zilizoandikwa na Marko, Mathayo, Luka na Yohane kati ya mwaka 65 na 100 hivi.
Mabadiliko hayo yaliyokusudiwa na
Mungu hayakutokea bila ya matatizo, hasa kwa sababu
yalikuwa magumu kueleweka kwa Wayahudi, ambao mwanzoni walikuwa wengi kati ya Wakristo, na hata kwa Mitume. Lakini Roho Mtakatifu aliwaongoza taratibu wakubali fumbo hilo lililofunuliwa
hasa kwa Mtume Paulo. Suala gumu zaidi lilikuwa
nafasi ya Torati katika Ukristo, hasa kwa waliojiunga nao moja kwa moja bila ya kutahiriwa kwanza ili wawe Wayahudi.
Katika Agano Jipya inajitokeza misimamo 4 tofauti, na ni ajabu kwamba
haikuvunja ushirika wa imani. 1. Wakristo wenye
asili ya Kiyahudi, hasa ya Kifarisayo, walitaka watu wa mataifa watahiriwe kabla hawajabatizwa, halafu wafuate masharti yote ya Torati ili waweze
kuokoka. 2. Wengine, kama Mtume Petro na Yakobo Mdogo, walitaka washike walau baadhi ya masharti hayo ili
wasiwe chukizo kwa Wakristo wa
Kiyahudi, hasa wakati wa kula pamoja ekaristi. 3. Paulo alikataa kupunguza uhuru wa
Kiinjili kwa kudhani wokovu unategemea Torati kuliko msalaba wa Yesu; hata hivyo alisisitiza upendo kama tunu bora ya kuzingatiwa ili
mtu asikwaze na kupoteza wengine dhaifu kama hao Wakristo wa Kifarisayo. 4.
Hatimaye ulijitokeza msimamo mkali zaidi, wa
kupuuzia kwa kiasi fulani Torati kama kitu kilichopitwa na wakati. Misimamo
hiyo ya mwisho ulizidi kupata nguvu kadiri Wayahudi na Wakristo walivyozidi
kutengana, lakini hata ule wa kwanza uliacha athari yake ya kudumu katika
Kanisa hasa kupitia Injili ya Mathayo na Barua ya Yakobo.
Kitabu cha Matendo ya Mitume
Kati ya Wainjili, Luka hakuishia kuandika habari za Yesu tu, bali
alizikamilisha kwa kuandika kitabu cha pili chenye historia ya mwanzo wa
Kanisa. Kinajulikana kwa jina la Matendo ya Mitume, kwa kuwa kinawatokeza hasa watu wawili ambao Luka
aliwafahamu, yaani Mtume Petro mpaka sura ya 12, halafu Mtume Paulo. Kwa namna ya pekee alikuwa mwanafunzi wa Paulo
akamfuata mpaka kifo chake: hivyo si ajabu kwamba alipenda kushuhudia kazi zake
na mateso yake kwa ajili ya Kristo na uenezi wa imani.
Mpangilio wa kitabu
hicho unaelezwa katika 1:8, yaani kuonyesha jinsi imani hiyo ilivyoshuhudiwa
toka Yerusalemu hadi mwisho wa dunia upande wa magharibi. Ndiyo sababu kitabu
kinaishia na habari za Paulo kufikia Roma na kuanza utume huko
mwaka 61, ingawa kuandikwa kiliandikwa kama miaka 20 baadaye.
Kuanzia Injili yake,
Luka anaonekana alivyojitahidi kuzingatia ukweli wa historia, lakini pia jiografia: katika Injili mambo yote yanaelekea Yerusalemu,
ambapo Yesu alikwenda kufa na kufufuka, na katika Matendo ya Mitume mambo yote
yanaanzia Yerusalemu, ambapo Roho Mtakatifu aliwashukia. Tukipenda kujua
historia ya wokovu ilivyoendelea baadaye, hatuna budi kufuata kitabu hicho
tukilinganisha habari zake na zile tunazozipata hasa katika barua za mitume.
Kwa namna ya pekee zile za Paulo tunaweza kuzipanga kwa faida katika mfululizo
wa habari za maisha yake alizotuachia Luka, ingawa kuna utatanishi fulani.
Kanisa la Yerusalemu
Pentekoste ilivyochorwa
na Duccio di
Buoninsegna juu ya ubao (1308).
Kabla ya kusimulia
uenezi wa Ukristo, Luka aliandika habari za Kanisa mama, yaani lile la
Yerusalemu. Katika msingi wake tunaona mitume wakiwa wanasali pamoja na mama wa
Yesu na waamini wengine. Majina ya hao 11 yameorodheshwa tena, halafu pengo
lililoachwa na msaliti Yuda Iskarioti likazibwa ili idadi muhimu ya 12 ikamilike tena.
Aliyeamua ifanyike hivyo ni Petro akitumia tayari mamlaka aliyoachiwa na Yesu,
na akiweka masharti kwa mapendekezo ya watu, hasa kwamba mteule awe shahidi wa
utume na ufufuko wa Yesu (Mdo 1).
Baada ya idadi hiyo
kukamilika tena, Roho Mtakatifu akawashukia wote katika nafasi maalumu, yaani
sikukuu ya Pentekoste, iliyotimiza Pasaka siku 50 baada yake (Mdo 2:1-41).
Safari hiyo alijitokeza kama upepo wa nguvu kubwa ajabu uliojaza nyumba nzima
(yaani Kanisa lote) na kama ndimi za moto zilizowashukia mojamoja kila mwamini
aliyekuwemo (kwa kuwa karama zake ni mbalimbali). Hapo hao waoga, waliojifungia
ndani kwa usalama, wakatoka nje na kuhubiria umati wa watu waliokusanyika kwa
kufuata upepo. Kwa kuwa siku hiyo ni ya hija walikuwepo Wayahudi na waongofu
kutoka sehemu nyingi za ulimwengu, lakini kila mmoja aliwaelewa mitume kwa
lugha yake mwenyewe. Hivyo umoja wa binadamu uliovunjika Babeli katika kujenga
mnara wa kiburi ukapatikana tena Yerusalemu kwa nguvu ya Yule aliye upendo wa
Mungu. Toka mwanzo Kanisa si la kabila la Yuda tu au la lugha ya Kiaramu tu,
bali ni Kanisa Katoliki, yaani la mataifa yote na la lugha zote. Bila ya
shaka aliyesimama kwa niaba yake lote atoe hotuba ya kwanza na kufafanua
matukio hayo pamoja na kumshuhudia Kristo mfufuka ni Petro. Maneno yake
yaliwachoma moyo wasikilizaji hata wakamuuliza wafanye nini. Jibu likawa watubu
na kubatizwa ili wapate msamaha na Roho Mtakatifu. Siku hiyo ya kwanza waamini
wakawa hawapungui elfu tatu.
Luka ametuachia picha ya
Kanisa mama hasa katika mihtasari mitatu (Mdo 2:42-47; 4:32-35; 5:12-16) ambayo
inachora maisha ya Wakristo wa kwanza kama kielelezo kwa wale wote
watakaofuata. Kweli katika historia yote ya Kanisa wengi wakaja kujipima kwa
kuangalia kielelezo hicho cha umoja katika roho na katika mali. Hasa watawa
wengi wakaja kujaribu kutekeleza tena umoja huo mashirikani mwao na hivyo
kuwachochea waamini wenzao wote. Umoja huo ndio sifa ya kwanza ya Kanisa na
mpango wa Mungu kwa watu wote.
Mwanzoni umoja
ulifanikiwa kwa namna ya pekee, ingawa hapo pia ulikuwa na kasoro tunavyosoma
katika Mdo 5:1-11; 6:1 na katika vitabu vingine vyote vya Agano Jipya. Kutokana
na malalamiko ndani ya jumuia, mitume waliamua kuwashirikisha kazi yao katika
ngazi ya chini watu saba: idadi hiyo katika Biblia inamaanisha mataifa, na
kweli wote walikuwa na majina ya Kigiriki (Mdo 6:2-6). Tofauti za waamini hasa
upande wa lugha na utamaduni zinadai daima ubunifu na nia njema zisije
zikavuruga umoja. Shida iliyotokea hapo ni utangulizi wa habari nyingine kuhusu
Wakristo wa Kiyahudi kuwabana wenzao wenye asili ya Kipagani.
Katika Mdo 6-8 hao
viongozi 7 wapya wanajitokeza kama mashujaa katika utume, ambao mwisho wake kwa
Stefano ulikuwa ni kifodini. Katika kusimulia tukio hilo la mwaka 36 hivi, Luka
alisisitiza kuwa mashtaka ya Wayahudi dhidi ya Stefano ni yaleyale yaliyomhusu Yesu: yaani upinzani dhidi
ya mwalimu unaendelea dhidi ya wanafunzi wake. Vilevile Stefano akakabili
mateso kama alivyofanya Yesu akimkabidhi Bwana roho yake na kuwaombea watesi
wake. Kabla ya hapo Wakristo walikuwa wamedhulumiwa katika nafasi mbalimbali,
lakini dhuluma hiyo ya tatu ikawa kubwa zaidi na kusababisha wengi wakimbie
Yerusalemu. Lakini kwa mpango wa Mungu mtawanyiko huo ulichangia kueneza
Injili.
Ukristo ulivyoanza kuenea
Rembrandt, Ubatizo wa
towashi, (1626 hivi).
Kufuatana na mpangilio
wa kitabu, Mdo 8 inaeleza jinsi Mungu alivyoongoza uenezi wa Kanisa kwa watu
wasiokubaliwa na Israeli, yaani kwanza kwa Wasamaria waliokuwa maadui wakuu wa
taifa teule, halafu towashi (yaani mwanamume mbovu) toka Ethiopia. Katika nafasi hizo zote mbili Luka alisisitiza
furaha iliyotokea kama dalili ya wokovu. Juhudi za Filipo mwinjilisti zikaja kuthibitishwa na
mitume kwa kuwawekea mikono Wakristo wapya wa Samaria.
Wakati uleule likatukia
jambo lingine, la ajabu kabisa, ambalo kwa umuhimu wake limesimuliwa na Luka
mara tatu, yaani uongofu wa Saulo/Paulo aliyekuwa mtesi mkuu wa Stefano na
Wakristo wengine. Ndiye aliyechaguliwa na Mungu awe mwenezi mkuu wa imani ya
Kikristo, mtetezi mkuu wa uhuru wa Wakristo wa mataifa kuhusu sheria za
Kiyahudi, tena mwandishi mkuu wa Agano Jipya, mwenye kufafanua mafumbo ya imani
kwa undani kabisa. Mungu alimteua awe chombo chake kiteule ili kuleta jina lake
kwa mataifa (Gal 1:13-24; Mdo 9:1-31; Mdo 22:17-21): katika historia yote ya
Kanisa baada ya Pentekoste hadi leo hakuna tukio lingine muhimu zaidi.
Ukubwa na ubora wa
mchango wa Paulo unaeleweka tukizingatia kwamba alifanya kazi na kuandika kabla
ya vitabu vya Agano Jipya kupatikana. Ndiye aliyeanza kuliandika akipanua
mawazo aliyoyapokea katika Kanisa kwa kuzingatia Agano la Kale na mang’amuzi yake mwenyewe. Hapo
alifafanua vizuri ajabu maisha ya Kikristo kama neema ya kumshiriki Yesu kwa imani, sakramenti na juhudi za kushinda umimi hadi kugeuka sadaka hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu. Wokovu huo, utakaokamilika katika ufufuko wa mwili, unapatikana katika
Kanisa, ambalo Paulo alilitambulisha kama bibiarusi wa Kristo na mwili
wake.
Lakini, kabla Luka
hajasimulia umisionari wake, aliandika habari nyingine ya ajabu ambayo pia
inapatikana mara tatu katika Matendo ya Mitume, yaani uongofu wa Kornelio na nyumba yake (Mdo
10). Wapagani hao walijaliwa Roho Mtakatifu kabla hawajabatizwa, wakimsikiliza
tu mtume Petro. Hivyo Mungu alimuonyesha mkuu wa mitume nia yake kuhusu wokovu
wa mataifa, naye Petro akalitangazia Kanisa kwamba Wapagani wasilazimishwe
kufuata sheria za Kiyahudi. Uamuzi huo uliofuata hiyo Pentekoste ya mataifa
ilimfungulia Paulo mlango wa umisionari wake unaotawala Mdo 13-28. Ingawa
Wakristo wenye msimamo mkali wa Kiyahudi walikubali maneno ya Petro (Mdo
11:1-18), hawakuweza kumuunga mkono Paulo aliposisitiza kwamba wokovu
unategemea imani kuliko utekelezaji wa sheria. Basi, mvutano juu ya suala hilo
ukaendelea kuvuruga maisha ya Kanisa kwa miaka mingi ya mbele.
Ni baada tu ya Petro
kufungua mlango kwamba Mdo 11:19-26 inasimulia jinsi waliotawanyika baada ya
uuaji wa Stefano walivyoeneza Ukristo huko walikohamia nje ya nchi takatifu, wakiwahubiria
kwanza Wayahudi wenzao, halafu Wapagani. Kitabu kizima kinafuata utaratibu huo:
Paulo mwenyewe kila alipofika aliwaelekea Wapagani baada tu ya Wayahudi kukataa
Injili.
Kati ya miji ambapo
ilianzishwa jumuia ya waamini wengiwengi, muhimu zaidi ni Antiokia (mpakani kwa Sirya na Uturuki wa leo): huko wafuasi wa Yesu walikuwa mchanganyiko
mkubwa wa Wayahudi na mataifa, hivyo wakapewa jina jipya maalumu la Kiyunani (Wakristo). Ndipo walipofanya kazi Barnaba aliyetumwa na mitume, Paulo aliyeitwa naye
kumsaidia, pamoja na manabii na walimu wengine.
Wakati huohuo (mwaka 44
hivi) Herode Agripa alimuua Yakobo Mkubwa (mtume wa kwanza kumfia Yesu) akakusudia kumuua hata
Petro, lakini huyo akahama Yerusalemu (Mdo 12:1-17) akafanya kazi huko na huko
kabla hajahamia moja kwa moja Roma akiuletea mamlaka yake.
Safari za kimisionari za Paulo zilivyoanza (46-49)
Kanisa changa na
motomoto la Antiokia likawa kituo cha umisionari kuanzia mwaka 46; kwa mara
nyingine Roho Mtakatifu ndiye aliyechochea juhudi za kitume na kuteua watu wa
kutumwa, yaani Barnaba na Paulo (Mdo 13:1-3). Safari yao ya kwanza ilichukua
miaka 3 katika kisiwa cha Kupro na mikoa ya kusini ya Uturuki wa leo (Mdo 13:16-51;
14:19-23). Ilikuwa kawaida yao kuanzisha Kanisa katika miji mikubwa ili toka
huko ujumbe ufike hadi vijijini.
Mtaguso wa Yerusalemu (49)
Yakobo Mdogo, kiongozi wa Wakristo wa
Kiyahudi mjini Yerusalemu, aliyekubali Wakristo wa
mataifa wasilazimishwe kushika Torati.
Waliporudi Antiokia
walipaswa kupambana na Wakristo wa
Kiyahudi kuhusu uwezekano wa
mataifa kuokoka pasipo kutahiriwa. Hatimaye suala likapelekwa Yerusalemu kwa
Kanisa mama. Baada ya majadiliano marefu Petro akatoa neno la mwisho kwamba
Wapagani wanaomuamini Yesu wasitwishwe mzigo usiobebeka wa kufuata sheria za
Kiyahudi (Mdo 15:1-12). Katika Gal 2:1-10 Paulo pia ametuachia kumbukumbu ya
mtaguso huo akisisitiza kuwa mitume waliokuwepo (Yakobo Mdogo, Petro na Yohane) walitambua rasmi karama ya
kimisionari ya kwake na ya Barnaba na uhalali wake, wakiwaomba tu wachangishe
pesa kati ya Wakristo wa mbali kwa ajili ya wenzao wa Yerusalemu wwnye hali
ngumu. Hiyo ilikuwa namna mpya ya kutekeleza upendo wa kidugu na kudumisha
umoja wa Kanisa baada ya uenezi wake.
Masuala hayo yakadai
uamuzi mwingine ili Wakristo wa Kiyahudi waweze kuendelea kushirikiana na
wenzao wa mataifa pasipo kuogopa unajisi ambao ungewazuia wasifuate ibada zao.
Gal 2:11-14 inaeleza shida iliyotokea Antiokia: ingawa Paulo alimheshimu sana
Petro, alipoona hafuati kwa unyofu uamuzi wa mtaguso hakusita kumkosoa kidugu
hadharani ili aliepushe Kanisa na upotovu kuhusu suala la wokovu. Basi, kadiri
ya Mdo 15:13-35, Yakobo Mdogo aliyeachiwa uongozi wa Kanisa la Yerusalemu
alichagua makatazo makuu manne kutoka Mambo ya Walawi akidai Wakristo wote
wayashike kama mambo mazito kwa dhamiri ya Kiyahudi. Uamuzi huo uliarifiwa kwa
Wakristo wa Antiokia na mikoa ya jirani kwa wajumbe na barua. Barua zikaendelea
kuandikwa hata leo kwa lengo la kudumisha umoja na amani katika Kanisa, kwa
kuwa ni kazi ngumu kuelewana kwa watu tofauti kama hao waliozoea kudharauliana
kwa matusi kama “mbwa”.
Barua au nyaraka
Kati ya vitabu 27 vya Agano Jipya, 21 vina mtindo wa barua au nyaraka. Hiyo ni tofauti kabisa na Agano la Kale, ambamo vitabu kadhaa vinazileta, lakini si kitabu kizima hata kimoja. Mtume Paulo ndiye aliyetumia zaidi mtindo huo ili afikie na ujumbe na mamlaka yake pale asipoweza kufikia kimwili. Barua 14
zinahusishwa na yeye kwa namna moja au nyingine, wakati nyingine 7 zinahusishwa
na Yakobo Mdogo, Mtume Petro, Mtume Yohane na Yuda Tadei. Hii haina maana kwamba ziliandikwa zilivyo na
Mitume hao. Kwanza, tokea awali watu waliweza kuandika barua kwa mkono wao, au kwa kumuongoza karani aandike maneno yao wenyewe, au kwa kumpa maelekezo ya
jumla kuhusu namna ya kuandika kama si kumuachia aandike anavyoona inafaa. Zaidi
ya hayo, wakati wa Mitume ilikuwa kawaida kuandika kwa kutumia jina la marehemu fulani maarufu kama kwa
kumwezesha aendelee kutoa ujumbe aliokuwa anautoa maishani. Pengine aliyeandika
hivyo alikuwa na uhusiano wa pekee na marehemu huyo kama mwanafunzi au mwandamizi wake.
Pengine maandishi hayo
hayakuwa tu barua fupi za kuwasiliana kuhusu shida fulani, bali hati au insha ndefu kuhusu mada fulani: ndizo
zinazostahili kuitwa nyaraka. Ingawa tofauti kati ya barua na waraka inaeleweka
kinadharia, pengine ni vigumu kugawa vitabu hivyo vya Agano
Jipya katika makundi mawili: kwa hakika Eb ni waraka na 3Yoh ni barua, lakini
nyingine ziko katikati. Barua saba zisizohusishwa na Paulo zinaitwa Katoliki, maana zimekubaliwa na Kanisa lote, ingawa maana asili ya neno hilo ilikuwa kwamba ni
kwa ajili ya watu wote, jambo ambalo si kweli.
Katika Biblia barua hazikupangwa kufuatana na tarehe za kuandikwa, bali zinatangulia zile za Paulo, na kati ya
hizo zinatangulia zile kwa makanisa 7, zinafuata zile kwa watu binafsi 3 na
mwisho waraka kwa
Waebrania ambao haumtaji Paulo.
Ndani ya makundi hayo, zinatangulia zile ndefu zaidi hadi zile fupi. Sisi,
tukitaka kuelewa zaidi ujumbe na maendeleo yake, ni afadhali tuzisome kwa mpangilio wa tarehe kadiri tunavyoweza kuikadiria. 2Pet, ambayo inafikiriwa
kuwa ya mwisho kuandikwa, inashuhudia kwamba tayari barua za Paulo zilikuwa
zimekusanywa na kuheshimiwa kama Maandiko
Matakatifu.
Safari ya pili ya Mtume Paulo (50-52)
Mtume Paulo akitoa Hotuba ya
Areopago huko Athene, kadiri ya Raffaello Sanzio, 1515.
Mdo 15:36-39 inasimulia
ugomvi kati ya Paulo na Barnaba walipotaka kufunga safari tena (mwaka uleule
49). Mungu hakuzuia ugomvi huo kusudi hao wawili waeneze zaidi neno lake
wakienda sehemu tofauti. Barnaba na Marko walielekea Kupro, kumbe Paulo
alimchukua Sila na kufunga safari iliyodumu miaka mitatu, akielekea kwanza
jumuia zile za bara alizoziunda miaka iliyopita (Mdo 15:40-16:5).
Paulo ni maarufu kwa
juhudi zake za kueneza Ukristo mahali pengi palipokuwa bado, lakini pia tunajua
upendo wake kwa watu aliowatangazia habari njema, na bidii zake kwa makanisa
aliyoanzisha: alikuwa akiwaombea usiku na mchana, akiwaka hamu ya kuwatembelea,
akiwaandikia barua za kusisimua ili kuwatia moyo au kuwakosoa, kutatua matatizo
yao na kujibu maswali mbalimbali. Pengine aliwatumia watu alioongozana nao:
kati yao alimpendelea Timotheo akashirikiana naye mpaka kufa.
Kadiri ya Mdo 16:6-15,
katika safari hiyohiyo kwenye mikoa mbalimbali ya Uturuki wa leo, huenda Luka
pia akajiunga na msafara akifuatana na Paulo hadi kufa kwake. Yeye anatia
maanani uongozi wa Mungu ambaye kwanza aliwazuia mara mbili wasielekee
walikokusudia, halafu kwa njozi alionyesha ni mapenzi yake wavukie Ulaya katika
Ugiriki wa leo.
Inavyojulikana, Wayunani
walikuwa na hamu kubwa ya kupata maarifa kuliko wengine, halafu kubishana nao
kwa ufasaha na kuwashinda. Katika mazingira hayo, falsafa na dini zilikuwa mada
kuu na kuingiliana na hadithi za ajabuajabu kuhusu miungu, malaika na wengineo.
Karibu barua zote za mitume zilikabili hatari hiyo, ambayo ikazidi kuwa kubwa
na kuleta mafarakano katika Kanisa hasa katika karne II, ilipoitwa “Gnosis” (= ujuzi). Hasa Paulo
alijitahidi kuishinda mapema iwezekanavyo.
Huko Ugiriki wakaanzisha
Kanisa kwanza Filipi, halafu Thesalonike. Kutokana na dhuluma za Wayahudi, Paulo alilazimika
kuondoka akafika Athene, mji mkuu wa falsafa, akajaribu kutangaza Injili kwa ufasaha wa maneno
ili kuwavuta hao watu wa elimu; kumbe akashindwa kabisa (Mdo 17). Ndipo
alipoelewa kuwa imani haitegemei akili na elimu, akaamua kuhubiri kwa unyofu tu mafumbo ya imani
(1Kor 1:17-2:5).
Mdo 18:1-11 inasimulia
mang’amuzi mengine aliyoyapata katika jiji la Korintho, lenye bandari mbili
katika bahari tofauti zilizoleta urahisi wa kuvusha bidhaa toka moja hadi nyingine badala ya kuzisafirisha kwa meli kandokando ya rasi. Kutokana na umuhimu
huo na wa kuwa makao makuu ya mkoa wa Akaya (Ugiriki kusini),
pamoja na biashara kubwa, kulikuwa na mchanganyiko wa watu, wakiwemo watumwa na
makahaba wengi. Huko alikaa mwaka mmoja na nusu kutokana na kufunuliwa na Yesu
kwamba ana wateule wengi jijini. Kweli utume wa Paulo ukazaa sana, ingawa kabla
hajafika walikuwepo tayari Wakristo kadhaa kama Akula na Priska waliofukuzwa na kaisari Klaudio mwaka 49 watoke Roma pamoja na Wayahudi wote hasa
kutokana na mabishano yao kuhusu Kristo.
Barua mbili kwa Wathesalonike
Paulo Akiandika Nyaraka
Zake, karne ya 17.
Mtume Paulo alikuwa amekimbia Thesalonike baada ya wiki 3 tu za utume, hivyo aliogopa kwamba
huenda dhuluma zikawakatisha wanafunzi tamaa. Kumbe, akina Timotheo
walipofika Korintho toka Thesalonike, walimpa Paulo ripoti kuhusu hali ya
Kanisa la kule na kumuondolea wasiwasi: dhuluma zilikuwa zikiendelea lakini
Wakristo wachanga wa huko ni imara katika imani yao mpya, isipokuwa
hawaelewi vizuri mambo fulanifulani, hasa kuhusu vikomo vya
binadamu. Hapo Paulo
akawaandikia kwa furaha barua tuliyonayo mpaka leo ili kuwahimiza na kuwaelimisha
zaidi: ndiyo andiko la kwanza la Agano Jipya kwa kuwa ni wa mwaka 51 hivi. Barua hiyo haina mafundisho mazito
isipokuwa kuhusu mambo ya mwisho (hali ya marehemu na ujio wa pili wa Bwana). Ni tulivu na ya kirafiki, ingawa inatoa
maonyo upande wa maadili (1Thes 1:1-3:13; 4:13-17; 5:1-11; 5:16-28).
Miezi michache baadaye
akarudia kuwaandikia kutokana na taarifa nyingine zilizomtia tena wasiwasi.
Akawafafanulia zaidi ujio wa Bwana na dalili zake, akiwahimiza hasa kufanya
kazi kwa bidii na kuwajibika wakati wa kungojea ujio wa pili wa Yesu badala ya kuiacha kwa
kisingizio cha kwamba, eti Kristo amesharudi (2Thes 2:1-15; 3:6-15). Mpangilio
wa barua hizo ni uleule wa barua zitakazofuata: baada ya salamu na shukrani kwa
Mungu, yanafuata mafundisho ya imani, halafu maadili, na hatimaye salamu
nyingine.
Mwaka 52 Paulo aliondoka
kwa hiari Korintho kuelekea Yerusalemu na Antiokia. Njiani alihubiri kidogo Efeso, makao makuu ya mkoa wa
Asia Ndogo (Uturuki Magharibi wa leo), lakini hakukubali kubaki
muda mrefu zaidi, ila aliwaacha huko Priska na mumewe akiahidi kurudi, Mungu
akipenda (Mdo 18:18-22). Huo ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya mseja na
watu wa ndoa katika utume.
Mdo 18:24-28 inasimulia
kwamba, baada ya Paulo kuondoka, alifika Myahudi wa Aleksandria, jina lake Apolo. Kama vile wenzake
wengi wa Misri alikuwa na elimu ya Kiyunani na ujuzi wa Biblia.
Tena alikuwa motomoto
katika kufundisha habari za Yesu, ingawa hazijui sawasawa, hasa hana habari ya
ubatizo wake mpya (kasoro hiyo ikaendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa sababu
baadhi ya wanafunzi wa Yohane Mbatizaji hawakumuamini Yesu, hivyo wakaendeleza
ujumbe wa mwalimu wao).
Priska na mumewe
wakamuelimisha zaidi, halafu wakampa barua ya kumtambulisha kwa Wakristo wa
Korintho alipokwenda kuhubiri. Wamisionari wa namna hiyo wakazidi kustawisha na
kuvuruga makanisa walau mpaka mwisho wa wakati wa mitume.
Safari ya tatu ya Mtume Paulo (54-58)
Baada ya kukaa Antiokia
mwaka mmoja na nusu Paulo akafunga tena safari akiyapitia makanisa ya Galatia na Frigia ili kuyathibitisha (Mdo 18:23). Hatimaye akafika Efeso
ambapo akabaki tangu mwaka 54 hadi 57, akifundisha kila siku na kueneza sana
Injili katika mkoa mzima (Mdo 19:1-10). Pamoja na hayo aliandika barua kadhaa,
ambazo baadhi zimepotea, nyingine tunazo hadi leo (kwa Wagalatia, kwa Wafilipi, ile ya kwanza kwa
Wakorintho, inawezekana Filemoni pia).
Barua hiyo iliandikwa na Paulo akiwa Efeso. Tofauti na zile kwa
Wathesalonike, hii ni kali sana kwa kuwa Paulo aliiandika (mwaka 54 hivi) mara baada ya
kusikia kwa mshangao na huzuni kwamba wanafunzi wake
wa mkoa wa Galatia wanataka kupotoshwa na Wakristo wengine
wanaosisitiza haja ya kushika Torati ili kupata wokovu. Ili kumpinga Paulo na mafundisho yake kuhusu neema, wazushi hao
walikanusha pia mamlaka yake kama mtume, eti, hajawahi kumuona Yesu, na anarahisisha
masharti ya dini ili ajipatie wafuasi na heshima.
Basi, ilimbidi ajitetee
na kusimulia baadhi ya matukio ya maisha yake yanayotusaidia kumfahamu zaidi na kutambua kwamba msimamo wake wa awali kama Farisayo haukumuelekeza hata kidogo kupuuzia Torati. Ni tukio
la ghafla la kutokewa na Mfufuka tu lililoweza kupindua mtazamo wake. Baada ya
hapo, msimamo wake mpya ulikubaliwa na viongozi wa Kanisa mama la Yerusalemu waliotambua karama yake ya pekee kwa uongofu wa mataifa. Akitetea uhuru wao kuhusu masharti ya
Torati, Paulo hakukosa kueleza kwamba hauruhusu kufuata udhaifu wa kibinadamu
(unaowakilishwa na mwili), bali ni kwa ajili ya kufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu ambao ni wa juu kuliko Torati na hatimaye unazaa tunda lake bora.
Akiandika kwa hasira takatifu ili kuzuia Injili isibadilishwe wala msalaba usibatilishwe - kwa sababu wokovu ukipatikana kwa
kushika Torati, Kristo amekufa bure - mara baada ya salamu akashambulia kwa nguvu
wazushi hao na kuonyesha kwa Biblia kuwa haiwezekani kujipatia uadilifu kwa
kujaribu kufuata sheria za Musa walivyotaka wao. Kinyume chake uadilifu wetu
unatokana na imani kwa Kristo na msalaba wake.
Ilimbidi kwanza ajitetee
kuwa mtume halisi anayefundisha kulingana na mitume wengine, halafu aonyeshe
tunavyookolewa kwa imani, si kwa kufuata sheria, hatimaye atoe mawaidha kuhusu uhuru wa
Kikristo, kwamba unategemea
kumfuata Roho Mtakatifu si tamaa za dunia (Gal 1:1-12; 2:15-3:14; 4:4-20; 5;
6:7-18).
Luka hakusimulia mateso
yote ya Paulo, kwa mfano alivyohukumiwa mwaka 56 hivi hukohuko Efeso (1Kor
15:32; 2Kor 1:8-9). Akiwa kifungoni alifikiwa na mjumbe toka Filipi aliyemletea
msaada wa pesa na wa huduma kwa niaba ya Wakristo wa mji huo. Paulo kabla
hajamrudisha alipenda kuwaandikia barua nzuri ya shukrani pamoja na kuwaeleza
sababu ya kufungwa (Fil 4:10-20). Barua ni nzuri pia kutokana na uhusiano wa
upendo kati ya Paulo na Wakristo hao, ambao kati yao wanawake walishika nafasi
ya pekee toka mwanzo. Tunaona wazi Paulo alivyokuwa na furaha hata kifungoni,
kwa kuwa alizoea kuridhika na kila hali. Kwake muhimu ilikuwa tu kumfikia
Kristo.
Kama kawaida mawaidha
hayakosekani, lakini si makali: hasa alihimiza umoja kwa kufuata mfano wa Yesu
aliyejishusha kutoka Umungu wake hadi kifo cha msalabani. Kwa ajili hiyo
alitumia maneno ya wimbo ambao unadhihirisha imani kamili katika umungu wa
Kristo, ingawa ni kati ya zile za kwanzakwanza kutungwa (Fil 1:12-3:1a; 4:4-7).
Lakini kuna sehemu kali
kuhusu wazushi ambayo inaanza ghafla (Fil 3:1b-4:1) na kufanya baadhi ya
wataalamu wadhani kuwa barua jinsi ilivyo tangu karne I ni mshono wa barua
mbili au tatu za mtume kwa Wafilipi.
Paulo akiwa kifungoni
(labda Efeso mwaka 56 au 57) alimuandikia Filemoni. Tofauti na barua zote zilizotangulia, hiyo
haikuandikwa kwa kanisa fulani, bali kwa Mkristo binafsi, tajiri, pengine wa Kolosai. Ingawa si muhimu upande wa teolojia, inaonyesha upendo wa mtume kwa wale aliowaongoa, na
jinsi udugu wa Kikristo ulivyoanza kutikisa utumwa.
Barua mbili kwa Wakorintho
Kutoka Korintho habari
za kusikitisha zilimfikia Paulo akiwa Efeso (pengine mwaka 57): katika Kanisa
hilo ambalo alilianzisha na kulipenda sana kulikuwa na shaka kuhusu imani,
mafarakano, upinzani wa Wakristo wa Kiyahudi dhidi yake, na makwazo.
Kilichohatarisha zaidi
jumuia hiyo ni karama mbalimbali ambazo hao Wakristo wachanga walizijali mno na
hatimaye wakajivunia kuwa nazo. Vilevile walivutiwa kumfuata mtu kama Apolo,
mwenye ujuzi na ufasaha mkubwa, mambo yaliyopendwa sana na Wagiriki. Ilimbidi
Paulo arekebishe hali hiyo ili kuokoa hasa umoja wa Kanisa na heshima kwa
viongozi wake halali.
Basi mwaka mzima akawa
na mahangaiko kwa Wakorintho akawaandikia walau barua nne au tano, ingawa sisi
tunazo mbili tu; pengine sehemu za baadhi yake zimeshonwa ndani ya 2Kor.
Mpangilio wa barua ya
kwanza una salamu na shukrani,
halafu hukumu juu ya matatizo ya Wakristo hasa kufarakana (1Kor 1:10-16;
2:1-4:16), kuzini na kushtakiana mahakamani (1Kor 5-6). Baada ya hapo akaanza
kujibu maswali yao mbalimbali: kuhusu ndoa na useja (1Kor 7), nyama
zilizotolewa sadaka kwa miungu (1Kor 8:1-11:1), mwenendo katika ibada na karama
(1Kor 11:20-33; 12:4-13:13; 14:18-40), na hatimaye ufufuko wa wafu (1Kor
15:1-28,33-49).
Mwishoni kuna maagizo,
taarifa na salamu mbalimbali (1Kor 16:1-4). Ndiyo sababu barua ni ndefu na
inagusa mambo mengi ambayo Paulo aliyatazama kwa hekima ya juu inayotokana na
msalaba wa Kristo. Kati ya mambo mengi muhimu zaidi, barua hiyo inatunza
simulizi la kwanza la karamu ya mwisho ya Bwana Yesu (11:23-25) na kanuni ya imani ya
kwanza inayoorodhesha pia matokeo ya Kristo Mfufuka (15:3-8).
Mdo 19:21-20:1
inasimulia alivyohama Efeso kutokana na matatizo kuzidi, akaelekea Makedonia na
Ugiriki. Toka huko alipata nafasi ya kuhubiri huko Iliriko, yaani Albania ya leo kwenda kaskazini (Rom 15:19). Wakati huo
alipata habari tofauti kabisa kuhusu Wakorintho, akawaandikia tena na tena
kabla hajawaendea kwa mara ya tatu. Labda kwa kuwa ni mshono wa barua hizo
mbalimbali, mpangilio wa Waraka wa pili kwa
Wakorintho haueleweki, ingawa ina
salamu na shukrani mwanzoni, na salamu nyingine mwishoni kama kawaida. Katikati
mada kuu ni tatu: kujitetea, mchango na mashambulizi dhidi ya wapinzani. Barua
hiyo inatusaidia hasa kumjua Paulo mwenyewe (2Kor 11:1-12:13).
Mitume Petro na Paulo
kadiri ya El Greco.
Ingawa Paulo alikaa
Efeso miaka mitatu, moyo wake wa kimisionari haukutulia kwa sababu alikumbuka
alivyotabiriwa atafanya kazi hata mbali zaidi. Ndiyo maana alitaka kwenda Ulaya
magharibi, yaani Roma na halafu Hispania, nchi iliyohesabika kuwa mwisho wa dunia. Ila kabla ya
kwenda huko alipanga kuleta mchango wa Wakristo wa mataifa kwa wenzao wa
Yerusalemu.
Basi, mwishoni mwa miezi
mitatu aliyokaa Korintho (Mdo 20:2-3) akijiandaa kupanda meli, yaani mwanzoni mwa
mwaka 58, Paulo aliwaandikia Wakristo wa Roma ili kuandaa utume atakaoufanya katika jiji hilo.
Huko Ukristo uliingia toka mwanzo kabisa, ukiletwa na baadhi ya Wayahudi wengi walioishi Roma ambao walibatizwa Yerusalemu kwenye Pentekoste ya mwaka 30.
Wayahudi wote
walipofukuzwa na Kaisari Klaudio (49), Wakristo wa mataifa mengine wakabaki ndio wengi, nao
wakaachana na masharti mbalimbali za Kiyahudi, kama yale kuhusu vyakula.
Muda mfupi baada ya Klaudio kufa (54), Wayahudi walianza
kurudi, kumbe wakakuta mabadiliko hayo makubwa ndani ya Kanisa, nao wakajiona wamewekwa pembeni kidogo, kama si
kudharauliwa na Wakristo wa mataifa.
Mtume Paulo akijua umuhimu wa Roma, mji mkuu wa ulimwengu wa zamani hizo, aliwaandikia Wakristo wa huko barua ndefu tena nzito kuliko
zote. Alitaka kuwaeleza kwa maandishi ya mpango mafundisho yake kuhusu wokovu, kwa sababu walikuwa wamesikia habari tofautitofauti juu
yake bila ya kukutana naye.
Pamoja na kuwaandaa
hivyo wampokee vizuri, alichukua nafasi ya kuimarisha umoja wao ulioingia dosari. Akiandika kwa utulivu mkubwa kuhusu mambo
aliyokwishawaongelea kwa hasira Wagalatia, Paulo aliweza kuinua pande zote mbili za Kanisa hilo zielewe zaidi fumbo la mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wote,
na hivyo ziheshimiane kwa upendo, ulio utimilifu wa Torati.
Hasa aliwaonya Wakristo
wa mataifa wasidharau Wayahudi, kwa sababu hao bado ni wateule wa Mungu.
Mtume Paulo akijua
umuhimu wa Roma, mji mkuu wa ulimwengu wa zamani hizo, aliwaandikia Wakristo wa
huko barua ndefu tena nzito kuliko zote.
Ingawa haina mafundisho
yote ya Paulo, barua hii imechangia teolojia ya Kikristo kwa kiasi kikubwa, hasa upande wa magharibi.
Kwa namna ya pekee
inajibu kinaganaga maswali kuhusu wokovu: unapatikana kwa njia gani? Kwa nini Wayahudi wengi
walishindwa kumuamini Yesu ili kuupata? Kwa nini mataifa yameupokea badala yao?
Aliyepata wokovu anaishi vipi? Je, Wayahudi wametupwa moja kwa moja?
Ndiyo sehemu kuu ya
barua (Rom 1:16-32; 2:1-29; 3:9-20; 3:21-31; 4:1-8; 4:23-25; 5:1-21;
6:1-14; 7:7-25; 8:1-39; 9:1-5; 11:1-36), ambayo inafuata salamu (1:1-8) na shukrani.
Paulo alisisitiza kwamba
wote ni wakosefu na wanaweza kuokolewa na Mungu tu: hiyo ni neema tupu, maana hakuna
anayeweza kuistahili kwa juhudi zake.
Neema hiyo tunaipata kwa
kumuamini Yesu ambaye alikufa akafufuka kwa ajili yetu ili sisi tuishi
upya kwa ajili yake tukiongozwa na Roho Mtakatifu.
Chini yake Mkristo
atafanya mema mengi na makubwa kuliko yale yanayodaiwa na Torati, ambayo ni
njema lakini haitutii nguvu ya kuitekeleza.
Upande wa mataifa, toka
mwanzo Mungu aliwapa mwongozo mwingine wa maisha, yaani dhamiri.
Hata hivyo pande zote
mbili zilishindwa kufaidika na miongozo hiyo wakahitaji msaada bora zaidi ili kumpendeza Mungu.
Uadilifu sasa unapatikana kwa imani na ubatizo katika kifo na ufufuko wa Yesu.
Hiyo njia mpya ya Mungu
kuwaokoa watu wote haiendi kinyume cha ahadi zake kwa Israeli ya Kale. Paulo
anathibitisha hilo kwa hatua nne akitumia madondoo mengi ya Agano la Kale.
Hamzungumzii Myahudi mmojammoja, bali wote jumla; wala hazungumzii jukumu lao
kuhusu kifo cha Yesu.
Maadili mema yatafuata kama matunda, na Paulo, kama kawaida
ya Wakristo wa kwanza, baada ya ujumbe au fundisho la imani, anayaeleza hasa katika
sehemu ya pili ambayo ina mawaidha mbalimbali (Rom 12:1-2,9-21;
13:8-14), yakifuatwa na taarifa, salamu na doksolojia.
Kwa kuwa Paulo
hakuwafahamu vizuri Wakristo wa Roma, maneno yake ni ya jumla na si ya mpango.
Hasa ni kwamba madai ya Torati hayawezi kuongoza mwenendo wa Mkristo, lakini huyo
anatakiwa kuzingatia anavyodaiwa hasa upendo kwa wote.
Maisha ya Mkristo yawe ibada kwa Mungu katika Roho Mtakatifu. Umoja wa
Kanisa unamdai ajitahidi
kushinda mabaya kwa mema. Kila kiungo cha mwili huo mmoja anadaiwa juhudi kwa ajili ya ustawi wa
wote ili maisha yawe sadaka kwa Mungu.
Akigusa zaidi maisha ya Kanisa la Roma ya wakati huo, yaliyovurugwa na masuala madogomadogo
kuhusu vyakula na sikukuu, Paulo alidai wenye nguvu watekeleze upendo kwa
walio dhaifu zaidi, pamoja na busara, uelewa, mfano wa Yesu na uaminifu kwake.
Maelekezo hayo yanaweza
kusaidia daima kukabili mvutano wowote kati ya wenye mitazamo tofauti (finyu na
mpana, au wa kizamani na wa kisasa zaidi). Lengo ni ule umoja uliofundishwa katika sura nane za kwanza.
Ukristo baada ya Paulo kufika Roma
Kusulubiwa kwa Mt. Petro
kadiri ya Caravaggio.
Paulo kupeleka mchango Yerusalemu (Mdo 20:16-21:36) ndio
mwisho wa kipindi cha utume wake mkubwa zaidi. Sura tisa za mwisho za Matendo
ya Mitume zinatusimulia kinaganaga habari zake kuanzia 58 hadi 63, ambapo
karibu miaka yote alikaa kifungoni akisubiri kesi (Mdo 23:12-24; 24:22-25:22;
28:11-16,23:30). Bila ya shaka ilikuwa ya majaribu makubwa kwake, lakini ilimpa
nafasi ya kutafakari mafumbo ya wokovu kwa undani zaidi tena, na ya kumshuhudia
Kristo mbele ya wafalme (Agripa II na
nyumba ya Kaisari)
alivyotabiriwa. Kwa Luka ni muhimu sana kwamba Paulo alifika Roma na kuanza
huko kazi yake ya utume, kiasi kwamba hakuendelea kuandika kilichofuata.
Hasa kwamba mwaka 64 mfalme Nero
alianza dhuluma za serikali dhidi ya Wakristo zilizoendelea mpaka 313, ingawa
si mfululizo. Petro na Paulo waliuawa mjini Roma kati ya mwaka huo na mwaka 68,
wakiliachia Kanisa la mji huo usimamizi wa makanisa yote. Kuhusu kipindi hicho
tuna ushahidi wa vitabu mbalimbali vya Kipagani, vya Kiyahudi na vya Kikristo.
Baadhi yake ni vile vya mwisho vya Agano Jipya ambavyo tunataka kuendelea
kuvichambua. Waandishi wake pengine walitumia majina ya mitume ili kuyapa nguvu
maandiko yao: inawezekana walikuwa warithi wa mamlaka yao na kuendeleza kazi
zao. Mkazo wa vitabu hivyo unaelekea miundo ya Kanisa (uchungaji) kuliko umisionari (uvuvi).
Katika hiyo miaka ya mwisho ya ufunuo,
Wakristo wa mataifa wakazidi kuwapita wale wa Kiyahudi kwa idadi na kwa
umuhimu. Nafasi ya Yerusalemu katika Kanisa ulizidi kupungua kutokana na hali
ya nchi, yaani vurugu kati ya Wayahudi, Wayunani na serikali ya kikoloni. Mwaka
62 Yakobo, ndugu wa Bwana na kiongozi wa Kanisa la huko, aliuawa na Wayahudi.
Tangu mwaka 66 hadi 73 hao walipigania uhuru wakashindwa; mwaka 70 Yerusalemu
ulitekwa tena na Waroma na kuteketezwa pamoja na hekalu lake. Kuanzia hapo hadi
leo dini ya Kiyahudi imebaki haina ukuhani wala
sadaka; nguvu yake ni katika masinagogi inapofanyika ibada ya Neno la Mungu
chini ya walimu wa sheria. Maangamizi hayo yalizidi
kutenganisha Wakristo na Wayahudi, hasa kwa sababu Wakristo wa Yerusalemu
walikimbilia ng’ambo ya Yordani badala ya kupigania uhuru, halafu wakarudi
mjini mpaka vita vya pili vya Kiyahudi (132-135) ambapo Waroma wakabomoa tena
Yerusalemu na kuwafukuza Wayahudi wote wasiweze hata kuingia wilayani na kuona
kwa mbali mlima wake.
Kanisa la mji huo wa biashara karibu
na Efeso lilianzishwa na mwanafunzi wa Paulo, labda Epafra,
halafu likaingiwa na mafundisho ya ajabuajabu yaliyochanganya mambo ya Kiyahudi
na ya Kipagani na yaliyozingatia mno ukuu wa malaika
juu ya ulimwengu.
Ndiyo sababu huenda Paulo, akiwa
kifungoni Roma kati ya miaka 61 na 63, akawajibika kuliandikia barua
inayoonyesha kuwa Kristo ni mkuu kuliko wote: vyote kabisa viliumbwa kwa njia
yake na kwa ajili yake, tena katika ubinadamu wake umo utimilifu wote wa Mungu.
Yeye ndiye “fumbo” kwa kuwa Mungu ametimiza mpango wa wokovu kwa njia yake.
Hakuna sababu ya kutafuta kwingine hekima na maarifa, wala ya kujiwekea
masharti ya kibinadamu yasiyosaidia kuokoka (Kol 1:13-29; 2:6-3:4; 3:5-17).
Mpangilio wa barua ni kama kawaida:
utangulizi, mafundisho ya imani, maonyo kuhusu uzushi, mawaidha na hatima.
Paulo aliweza kuandika barua hii akiwa
kifungoni Roma kati ya miaka 61 na 63 ili isomwe katika makanisa yote ya mkoa
wa Asia Ndogo, wenye makao makuu Efeso. Mafundisho yake yanalingana na yale ya
barua kwa Wakolosai ila yamechimbwa zaidi, kiasi kwamba barua hii inaonekana
kuwa kilele cha teolojia ya Paulo. Pamoja na kuchambua fumbo la wokovu katika
Kristo, inachambua hasa fumbo la Kanisa kama mwili wa Kristo ambamo kichwa kinaeneza wokovu
ulimwenguni kote. Kwa msingi huo inasisitiza na kudai umoja kamili kati ya
waamini (Ef 1:1-2; 1:17-23; 2:11-22; 3:1-21; 4:1-16).
Jina hilo linajumlisha barua moja kwa Tito na
mbili kwa Timotheo, ambao walikuwa washiriki wakuu wa utume wa Paulo, wakawa
waandamizi wake. Wataalamu wanabishana sana kuhusu mtunzi wa barua hizo, wengi
wakidhani zimeandikwa na mfuasi wa Paulo mwaka 95 hivi, huku wengine
wakishikilia aliziandika mwenyewe, kwa msaada wa karani fulani, miaka ya mwisho
ya maisha yake (63-67), ambapo baada ya kufunguliwa aliweza kusafiri tena
mashariki (Ugiriki na nchi za kandokando) na pengine hata magharibi (Hispania).
Barua ya pili kwa Timotheo inaonekana kama wasia wake alioandika kifungoni
akisubiri kuuawa.
Barua hizo zinaitwa za kichungaji kwa
kuwa ziliandikwa kwa maaskofu hao ili kuwasaidia kufanya vizuri kazi zao, hasa
kwa kushika imani sahihi, kupinga uzushi, kuchagua vizuri viongozi ambao
wawawekee mikono, kuchunga vema Wakristo wa aina mbalimbali, kuwa na mwongozo
kuhusu ibada, n.k. Ndiyo sababu ni muhimu sana kwa miundo ya Kanisa iliyokuwa
mbioni kupata sura yake ya kudumu. Pamoja na hayo zinahimiza kukubali mateso
kwa ajili ya Injili: ndio msimamo wa Mchungaji mwema (Tito 1:5-9; 2; 1Tim
1:18-2:10; 3:1-4:16; 6:2b-21; 2Tim. 1:3-14; 2:1-18; 3:14-17; 4:1-8).
Mtume Paulo alipokaribia kumaliza kazi
yake, wengine kati ya mitume na wanafunzi wao walianza kuandika kwa uvuvio wa
Roho Mtakatifu. Mmojawao ni Petro, kwa msaada wa Sila, akiwa Roma karibu na
kuuawa. Baada ya kufanya utume Antiokia, aliweza kwa urahisi kutembelea mikoa
ya Uturuki Kaskazini wa leo. Wakristo wa huko ndio walioandikiwa barua hii
yenye mafundisho na ibada kuhusu ubatizo na Pasaka. Pamoja na hayo walihimizwa
wasiogope maneno ya watu wengine wasiopendezwa na uongofu wao: hali ngumu ni
fursa ya kulingana zaidi na Yesu mpole na mteswa (1Pet 1:1-12; 2:19-25; 3:13-5:14).
Miaka hiyohiyo ya 60 Mkristo mwingine,
mwenye asili ya Kiyahudi na elimu ya Kiyunani, aliwaandikia Wakristo wa
Kiyahudi wenzake si barua hasa bali hotuba kamili iliyoambatanishwa na kipande
cha barua. Hali iliyosababisha uandishi ni baadhi yao kuvutiwa tena na dini yao
asili na ibada zake hekaluni: kishawishi kilikuwa kikubwa hasa kwa sababu
Kanisa lilikuwa bado mwanzoni, bila ya mahali maalumu pa kusali wala ibada za
fahari. Mwandishi aliwaonya kuwa wakimuasi Yesu hawamrudii Mungu aliye hai,
aliyejifunua hasa katika Mwanae, bali wanamsulubisha tena kwa makusudi mazima
na kustahili tu moto wa milele.
Sehemu kubwa ya maandishi hayo
inalinganisha Yesu na ukuhani wake katika hekalu la mbinguni upande mmoja, na
ukuhani wa Agano la Kale huko Yerusalemu upande mwingine. Hivyo mwandishi
alielekeza safari ya kiroho katika imani inayofanana na ile
ya watakatifu wa Agano la Kale.
Kwa kuwa lengo halikuwa la kinadharia,
bali kuhimiza uaminifu, kila baada ya kuchambua ukweli fulani aliongeza
mawaidha ya kufaa. Ubora wake ni kulinganisha mambo ya kale na utimilifu wake
katika Agano Jipya, pia kuthibitisha ukuu wa Kristo kama kuhani wa milele (Eb
1:1-2:4; 4:11-5:10; 7:1-8:13; 10:19-11:40; 13:22-25).
Tulivyoona, kwa muda wa miaka 30 na
zaidi Wakristo walitangaza habari za Yesu hasa kwa midomo, halafu kwa barua na
maandishi mengineyo. Lakini wakati huohuo (miaka ya 50?) baadhi yao walianza
kukusanya kwa maandishi ushuhuda wa mitume na wengineo kuhusu mafundisho na
maisha ya Yesu, kama vile mifano aliyoitoa, mabishano yake na Mafarisayo, na
hasa mateso yake. Kati yao tunaambiwa Mathayo aliandika kwa Kiaramu, ingawa
hatuna hata kipande cha kitabu chake na cha vinginevyo. Ila Wainjili wetu
walivisoma na kuvitumia kwa kutunga vya kwao. Baada ya Injili zao nne
kupatikana, Kanisa likaacha vitabu vya kwanzakwanza hata vikapotea.
Wataalamu wengi wanakubaliana kusema
Marko ndiye aliyetangulia kuandika kitabu kamili juu ya maisha na mafundisho ya
Yesu kuanzia utume wa Yohane Mbatizaji hadi ufufuko wake. Ndiye aliyekiita
kitabu cha namna hiyo Injili, hata neno hilo, lililokuwa na maana ya ujumbe
kuhusu Yesu, likaja kuwa na maana mpya ya kitabu cha habari za Yesu. Marko
aliandika akiwa Roma mwaka 65 hivi, mara baada ya serikali kuanza kuwatesa
Wakristo, na akiwa na nia ya kuwaimarisha katika dhuluma.
Baada ya Marko, watu wawili tena
waliandika vitabu kama cha kwake, wakikitegemea kwa kiasi kikubwa na kukipanua
kwa habari za utoto wa Yesu, mafundisho mengi zaidi n.k. Wataalamu wanaona
Injili hizo za Mathayo na Luka ziliandikwa kati ya miaka 80 na 90, hata hatujui
ipi imetangulia. Mazingira ni yaleyale ya Mashariki ya Kati, labda Antiokia,
ila walengwa ni tofauti. Injili ya Mathayo iliandikwa kwa ajili ya Wakristo wa Kiyahudi
wakati mabishano kati ya Kanisa na Israeli yalipozidi, na ina lengo la
kuwaimarisha katika imani yao kuwa Yesu ndiye Masiya, ndiye Musa mpya. Kumbe
Luka ambaye alikuwa Mpagani kwanza aliwaandikia hasa Wakristo wa mataifa
akisisitiza upendo wa Yesu kwa wote, na kwa namna ya pekee kwa maskini,
wakosefu na wengine waliodharauliwa.
Injili hizo tatu zinaitwa “ndugu” kwa
jinsi zinavyofanana katika mpangilio, katika habari na pengine katika maneno
yenyewe; kwa Kigiriki zinaitwa “sunoptiki”, yaani zinazotazamika kwa pamoja.
Kama tulivyoeleza, Luka aliiongezea Injili yake kitabu cha pili, yaani Matendo
ya Mitume, kama mwendelezo wake, kwa kuwa aliona kazi ya Kristo inakamilishwa
na Roho Mtakatifu katika ile ya Kanisa.
Kitabu kingine ambacho labda
kiliandikwa miaka ya 80 kina jina la Yakobo,
lakini wataalamu hawapatani kuhusu huyo ni nani, aliandika wapi na lini. Kwa
hakika walengwa wa kitabu ni Wakristo wa Kiyahudi wenzake, lakini si barua
halisi, bali ni mchanganyiko wa mawaidha yanayofuata mtindo wa vitabu vya
hekima. Lengo lake ni kuhakikisha Ukristo usiishie katika mawazo mazuri, bali
imani ijitokeze katika matendo mema. Lengo lingine ni kuwakuza mafukara na
kuwakemea matajiri, kadiri ya mwelekeo wa Kanisa la Yerusalemu (Yak 1:1-2:26;
4:1-5:6).
Hatujui vizuri mwandishi wa barua hii
ni nani (ingawa anajiita ndugu wa Yakobo), wala aliandika lini (wengi wanakisia
miaka ya 80), wala aliwaandikia akina nani (barua ni kwa wote, ingawa baadhi
wanahisi walengwa kuwa ni Wakristo wa Kiyahudi walio nje ya Israeli). Ujumbe ni
kujihadhari na wazushi wanaobunibuni mafundisho mapya badala ya kushika imani
ile iliyofunuliwa mara moja na ikatosha; ujumbe huo ulitolewa kwa kuwatukana na
kuwalaani wazushi hao (Yuda
1-4, 17-25).
Siku hizi wataalamu wanakubaliana
kukanusha barua hiyo kuwa imeandikwa kweli na Mtume Petro,
wakisema ni kitabu cha mwisho kuandikwa katika Biblia (labda Roma mwaka 100
hivi). Kwa hakika iliandikwa baada ya barua ya Yuda, kwa sababu inatumia maneno
yake mengi. Inawezekana mwandishi alitumia vilevile maneno ya Petro ambayo sasa
yamepotea; kwa vyovyote aliandika kwa mamlaka yake kwa makanisa yote ili
kuthibitisha mapokeo. Pamoja na kupinga uzushi, lengo la barua ni kueleza
sababu gani Bwana anachelewa kurudi. Mafundisho mengine muhimu yaliyomo
yanahusu uvuvio wa Roho Mtakatifu juu ya waandishi wa Biblia (Paulo mmojawao),
wito wetu wa kushiriki umungu, uwepo wa ulimwengu mpya baada ya huu wa sasa
kuangamizwa (2Pet 1:3-11,19 21; 3:8-18).
Kundi la mwisho la vitabu vya Agano
Jipya linajulikana kwa jina la Yohane, kwa kuwa Injili ya nne, barua tatu na
kitabu cha Ufunuo viliandikwa na mtume huyo na wanafunzi wake. Akiwa kijana
kuliko mitume wenzake, Yohane alijaliwa kuishi miaka mingi na kuandika hadi
miaka 70 hivi baada ya Yesu kwenda mbinguni. Miaka hiyo yote alizidi kutafakari
na kuhubiri maneno na matendo ya Bwana akitambua mafumbo mengi yaliyofichika
ndani yake. Pengine alirekebisharekebisha maandiko yake mpaka mwishoni, halafu
akawaachia wanafunzi wake kuyakamilisha na kuyaeneza kati ya Wakristo wa mkoa
wa Efeso ambapo Yohane aliongoza Kanisa miaka mingi.
Ufunuo ni kitabu pekee cha kinabii
katika Agano Jipya; kilikamilika mwaka 95 hivi; lengo lake ni kuwaimarisha
katika tumaini Wakristo waliozidi kudhulumiwa na serikali ya Roma. Kimejaa
mafumbo kama kawaida ya mtindo wa kiapokaliptiko. Mtindo huo ni mgumu kueleweka
kwa sababu mwandishi hakuweza kutamka wazi watesi watakaoangamizwa ni akina
nani. Tena alipenda kusisitiza anatoboa siri za Mungu alizojaliwa kuzijua kwa
njia za ajabu (njozi, malaika n.k.). Tunahitaji kutafsiri mifano mingi (vitu,
viungo, rangi n.k.) na tarakimu (saba, kumi na mbili n.k.). Kwa ajili hiyo ni
muhimu kujua maana zake katika Biblia (Ufunuo umejaa madondoo ya Agano la Kale:
mistari 274 kwa 404!).
Mpangilio wake kwanza una barua saba
kwa makanisa ya mkoa wa Efeso, halafu sura 4-22 zina unabii kuhusu mambo
yajayo, yaani vita vikali zaidi na zaidi kati ya Kristo na shetani ambaye
anatumia dini na serikali za Kipagani. Ushindi utakuwa wa Kristo na Kanisa,
ambao hatimaye wanachorwa kama bwanaarusi na bibiarusi katika utukufu wa Mungu.
(Ufu 1;4-5; 12; 21-22).
Injili ya Yohane
Injili hiyo ni tofauti sana na zile
ndugu kwa mtindo na kwa mpangilio, kwa mafundisho na kwa habari zenyewe. Labda
Yohane alisoma walau mojawapo, asipende kurudia habari zilezile, bali
kuzikamilisha na kuzisahihisha akiwa ni shahidi bora kati ya mitume wote. Hata
hivyo hakutaka kuandika kitabu cha historia tu, bali habari njema hasa kwa
kuchimba ishara alizozitenda Yesu zinazotufumbulia fumbo lake mwenyewe na
sakramenti zake. Lengo ni kuwafanya wasomaji wamuamini kuwa ni Mwana wa Mungu
na kwa kumuamini wapate uzima wa milele. Injili hiyo inatudai tukomae katika
maisha ya sala na kutafakari, tukizidi kumuuliza Yesu, “Wewe ni nani?”. Katika
Injili hiyo atatupa jibu moja baada ya lingine. Kitabu kilikaribia kukamilika
mwaka 90 hivi; toleo la mwisho na sura ya 21 ni kazi ya wanafunzi wa Yohane
miaka kama 10 baadaye (Yoh. 20:30-31; 21:24-25).
Barua tatu za Yohane
Ziliandikwa kati ya mwaka 90 na 100,
wakati ambapo jumuia za wafuasi wa Yohane zilianza kusambaratika. Mafundisho na
lugha vinalingana na Injili ya nne. Barua ya tatu na ya pili hazina mafundisho muhimu, tofauti na
ile ya kwanza inayodai imani sahihi na
maisha matakatifu ili mtu astahili kuitwa Mkristo kweli. Inakaza umwilisho wa
Mwana wa Mungu na haja ya kuishi kwa uadilifu,
na hasa kwa upendo (1Yoh 1:1-4; 2:3-11; 3:11-4:21; 2Yoh 7-13).
Maoni