Katiba Mpya Tanzania: Ni mtego kwa Rais Samia?
Katiba Mpya Tanzania: Ni mtego kwa Rais Samia?
Jaji Warioba
Safari ya mchakato wa kupata katiba mpya ya Tanzania ulianza tangu mwaka 2010, wakati Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete alipoamua kuutangazia umma dhamira na nia ya serikali ya kuanzisha mchakato wa kupata katiba mpya.
Mchakato ukaanza rasmi mwaka 2011 kwa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 83/2011 na baadaye ikatungwa Sheria nyingine ya Kura ya Maoni Na. 11/2013.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilitamka kuanzishwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilianzishwa chini ya Waziri mkuu wa zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba, ikaratibu mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya kwanza ya katiba ambayo kupitia uhariri wa Mabaraza ya Katiba ikapatikana Rasimu ya Pili ya Katiba.
Rasimu hii ya pili ambayo ni maarufu kama Rasimu ya Warioba ikawasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba (BMK) ambalo kwa kiasi kikubwa lilikuwa na wajumbe wengi kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi -Zanzibar. Kwenye bunge hili la Katiba, ambalo Makamu Mweyekiti wake alikua Samia Suluhu, ambaye ni ndiye Rais wa Tanzania kwa sasa, ndiko joto na mivutano mikali kuhusu masuala kadhaa yaliyomo kwenye katiba ilipoanzia. Baadhi ya wajumbe wa bunge hilo hasa kutoka upinzani waliamua kujitoa na kususia mchakato.
Hata hivyo waliobaki waliendela na ikapatikana Katiba pendekezwa ambayo wengi waliiona kama imekosa muafaka na maridhiano ambayo yanaonekana kama ndio msingi wa kupata Katiba bora ya kitaifa yenye kukubalika na wengi. Mchakato ukaishia hapo, ilikuwa mwaka 2014, na mpaka leo kumekuwa na mkwamo usiojulikana ni lini utakoma.
Rais wa awamu ya nne wa Tanzania, Jakaya Mrisho, ambaye mwishoni mwa mwaka 2010 aliutangazia umma dhamira ya Tanzania kuandika katika mpya na kuruhusu mchakato kuanza
Kwa nini msukumo wa kutaka Katiba mpya Tanzania umerudi kwa kasi sasa?
Kumeanza kufanyika harakati tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia za kutaka mchakato wa Katiba mpya ufufuliwe. mfano chama cha upinzani cha CHADEMA kimeitisha mkutano mkubwa kuhusu Katiba mpya, huku harakati zingine zikiendelea kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ikihusisha baadhi ya wanaharakati, wanasiasa, wasomi na watu wa kawaida.
Zipo sababu nyingi za kubashirika kuhusu kwa nini nchi iamue kuandika upya Katiba yake, moja kubwa ni kupitwa kwa baadhi ya mambo ambayo hayaonekani kwenda na maisha ya sasa wa wananchi husika, lakini pia kujitokeza masuala ambayo yanahitaji kuwekewa misingi ya kikatiba.
Katiba ya sasa ya Tanzania ina umri wa karibu miaka 41 sasa, ilitungwa mwaka mwaka 1977. Kwa sababu Katiba hii na katiba zote tano zilizopita tangu katiba ya uhuru ya mwaka 1961, ikaja ya 1962,ya 1964, 1965 mpaka katiba ya kudumu ya mwaka 1977, pamoja na marekebisho yake yote 14 kumekuwa na malalamiko kwamba wananchi hawakushirikishwa kikamilifu kuzitunga katiba hizo wakati zinahusu maisha yao. Hivyo ukaundwa mfumo ambao ungeruhusu ushiriki wa wananchi katika kupata katiba bora ambao umeishia njiani.
Kwa wanaotaka sasa Katiba mpya baada ya kukwama kwa zaidi ya miaka 6 ukiwauliza watakwambia wanataka kwa sababu ni hitaji lao kama wananchi wakisema kuna masuala muhimu ya ayopaswa kuwepo katika katiba yao ama kurekebishwa, na katika hilo hawahitaji hisani kutoka kwa mtu yoyote wakiwemo viongozi.
' Katiba hitaji kuu, katiba bora ni msingi imara wa maendeleo endelevu, Rais Samia bila katiba bora hutaweza kujenga uchumi imara Tanzania' aliandika mwanaharakati Ananilea Nkya, ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi mtendaji wa chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA).
Mwisho wa Twitter ujumbe, 1
Wengine wanasema Katiba ya sasa iliundwa wakati wa mfumo wa chama kimoja lakini sasa nchi iko kwenye mfumo wa vyama vingi hivyo, katiba ya mwaka 1977 haiwezi kuwa muafaka wa kitaifa wa vyama vingi, kwa sababu ilisimamia misingi ya muafaka wa chama kimoja, lakini sasa kuna misingi ya vyama vingi, kuna mahitaji mapya ya kisiasa, mazingira mapya ya kisiasa na zipo changamoto mpya.
Kwa mantiki hiyo ili kuleta muafaka wa kitaifa, katiba mpya itakayopatikana inapaswa kuwa ndiyo medani ya kuleta muafaka wa kitaifa.
Ujio wa awamu ya Tano ya Serikali, ulionyeshakwa kauli kwamba mchakato wa mabadiliko ya Katiba sio kipaumbele cha Serikali ya awamu hiyo, kauli ambayo pia imerejewa na Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu alipozungumza na wanahabari wiki hii, akisema "Nipeni muda tuimarishe uchumi kwanza kisha tuyashughulikie mambo ya katiba na mengine ya siasa'.
Kauli hii imeibua hisia tofauti miongoni mwa watu wanaounga mkono kuanzishwa ama kuendelezwa kwa mchakato wa katiba mpya, ambo waliamini kuingia madarakani kwa Rais Samia kungebadili uelekeo wa serikali ya awamu ya tano na kuifanya katiba kuwa miongoni mwa vipaumbele muhimu.
Uhuru wa watu kujieleza uliodhihirika katika siku 100 za kwanza za utawala wa Rais Samia, pia unatajwa kuchagiza kurejesha mjadala kuhusu katiba mpya, ingawa wapo wachache wanaoosema uongozi wa awamu iliyopita chini ya Rais John Magufuli, umeonyesha ilivyo muhimu kupunguza mamlaka ya Rais, kwa sababu Katiba ya sasa inampa Rais Mamlaka makubwa Zaidi.
Katiba mpya kusalia kuwa kaa la moto kwa Rais Samia?
Wajumbe wa Bunge la Katika wakitoka nje ya ukumbi baada ya kuibuka vurugu ziizosababisha bunge hilo kusitishwa kwa muda
Rais Samia alikuwa Makamu mwenyekiti wa Bunge la Katiba, lililochakata rasimu ya katiba (rasimu ya Warioba) na kupatikana kwa Katiba pendekezwa ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni na Maelekezo ya Tume ya Uchaguzi (NEC), zoezi la kura ya maoni lilipaswa kufanyika tarehe 30 Aprili 2015. Lakini kutokana na sababu mbalimbali zoezi hilo halikufanyika.
Anafahamu kinagaubaga kila linalohusu mchakato huo, yakiwepo masuala yaliyoleta mijadala mikubwa kwenye Bunge la Katiba aliloliongoza yeye na Mwenyekiti wake, Marehemu Samuel Sitta. Mchakato wa kuendelea ama kutoendelea na mchakato wa Katiba utasalia kuwa jambo litakalozunguka kichwani kwake kwa muda wote atakaokuwa madarakani.
Mchakato huu wa Katiba mpya ukihuishwa tena je ni wapi pa kuanzia?
Kuna swali kubwa ambalo wengi wanajiuliza na kwa namna ya kawaida Rais Samia pia huenda na yeye amewahi kujiuliza. Je mchakato uanze upya kabisa? Kama utaanza upya mzigo wa gharama ataubeba nani? Pengine hiyo ndiyo sababu ya kutaka apewe muda ili ajenge uchumi wa nchi na masuala mengine ambayo yatahitaji uchumi imara yaendelee. Ingawa wanaopinga hoja hiyo wanasema Uchumi na Katiba bora ni kama ndugu wanaoendana, ukitaka kuwa na uchumi bora inakupaswa uwe na Katiba bora itakayoleta utulivu, itakayovutia wawekezaji na itakayosimamia mamlaka na rasimili mali za nchi.
Rais Samia, wakati huo akiongoza bunge la maalumu la Katiba kama Makamu Mwenyekiti wa bunge hilo
Maswali mengine yanayozaliwa hapa ni Je mchakato uanzie alipoishia Jaji Warioba, kwa kuileta rasimu ya Katiba na kuunda Bunge jipya la Katiba ili kuichakata na kupatikana upya kwa Katiba Pendekezwa? Au mchakato uaanzie lilipoishia Bunge maalumu la Katiba alilolongoza Rais Samia na na mwenyekiti wake Sitta, kwa kuitisha tu zoezi la kura ya maoni ili kuipigia kura Katiba pendekezwa iliyopendekezwa na bunge hilo mwaka 2014.
Wanaopinga hatua ya kuendelea kwa mchakato kwa kupigia kura katiba inayopendekezwa wanasema, katiba hiyo haitokani na maoni ya wananchi, kwa sababu mambo kadhaa wanayoyaona muhimu na yaliyopendekezwa na wananchi wengi yaliondolewa ama kubadilishwa kupitia Bunge maalumu la Katiba ambalo lilisusiwa na wajumbe wa upinzani.
Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa chama cha wananchi (CUF) na Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, walikuwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge maaluum la Katiba kutoka Upinzani
Licha ya kupitishwa na Bunge maalumu la Katiba masuala yafuatayo yalikuwa hayajapata muafaka wa kitaifa, kwa sababu lipo kundi lililoona kama maoni yake yamewekwa kando.
Masuala hayo baadhi ni;
-Masuala ya Muungano
-Tume huru ya uchaguzi
-Mamlaka yanayotajwa kuwa makubwa ya Rais
-Madaraka ya umma
-Haki za binadamu na Utawala bora
-Uwepo wa Mgombea binafsi
-Na Mgawanyo wa madaraka ya mihimili mitatu (Serikali, bunge na Mahakama) na uhuru wa Bunge na Mahakama
Japo siri ya uamuzi wowote atakaouchukua baadae hata baada ya kukamilika kwa dhamira yake ya kuifungua nchi hiyo na kujenga uchumi, itabaki moyoni kwake, laki Rais Samia anasalia kuwa na karata ya muhimu ya turufu ya ama kufufua mchakato wa katiba ama kuuzika kabisa, uamuzi ambao ni kama kaa la moto atakaloendelea kukaa nalo wakati wote atakapokuwa madarakani.
Maoni