Katiba ya sasa inatoa nafuu kwa CCM?


 Mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya nchini Tanzania ulianza rasmi mwaka 2011 wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete. Miaka mitatu baadaye yaani mwaka 2014, wakati huo Kikwete akimalizia muda wake madarakani mchakato huo ulikwama ukiwa katika hatua ya mwisho ya upigaji kura wa katiba inayopendekezwa.

Wengi walidhani baada ya kuingia madarakani John Pombe Magufuli, mchakato huu ungepewa kipaumbele lakini mbele ya waandishi wa habari alieleza katiba mpya haikuwa kipaumbele cha utawala wake.

Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 - 2020, iliiweka hoja ya kuendelea na mchakato wa kupata katiba mpya. Baadaye hoja hiyo iliondolewa katika ilani iliyofuata. Na haikuwa tena kipau mbele kwa chama hicho.

Kutoka wakati huo hadi sasa kuna upinzani kuhusu kuendeleza gurudumu la katiba mpya kutoka CCM. Mchakato wa katiba umegeuzwa danadana kuanzia mwendazake Magufuli na Rais wa sasa Samia Suluhu Hasssan. Kutoka kuwa jambo lililoachisha watu shughuli zao kuliandaa, pesa nyingi kutumika, vikao kadhaa kulijadili, hadi kugeuka na kuwa jambo lisilo na umuhimu kwa takribani miaka saba sasa.

Na kwa namna linavyoonekana ni jambo linaloweza kusubiri, kuna maswali mengi na tafrisi na hoja tofauti zinaibuka miongoni mwa watu, wanaharakati na taasisi hasa za kisiasa.

Rais Samia Suluhu Hasan alieleza katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari, kwamba kipaumbele chake kwa sasa ni kuweka uchumi wa nchi vizuri hadi utengemae ndipo swala la katiba litakuja.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alingongelea msumari kabati la katiba siku chache baadaye kwa kueleza Katiba ya sasa ya Tanzania ni nzuri, inapaswa kuheshimiwa kwa kuwa imeivusha nchi katika kipindi kigumu.

Akaenda mbali kwa kueleza kuwa inalinda haki za kiraia, kisiasa, uchumi na za kiutamaduni na ndiyo maana Serikali imeridhia kwanza Katiba hiyo.

Rais Samia ndiye aliyekuwa makamu mwenyekiti katika Bunge Maalum la katiba. Profesa Kabudi alikuwa mjumbe katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba.Na Kabudi alikuwa miongoni mwa wajumbe waliokuwa mstari wa mbele kupita huku na kule nchi nzima kueleza kuhusu rasimu ya Katiba mpya chini ya Tume ya Jaji Joseph Warioba. Kwa kuzingatia maneno yao rasimu hiyo kwa sasa itaendelea kubaki kabatini kwa muda usiojuulikana.

Nilimuuliza kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, hoja ya kuuweka mchakato wa katiba mpya pembeni ili kushughulikia uchumi wa nchi kwanza; kwanini anaamini ni hoja isiyo na msingi?

"Hiyo sio hoja, ni kiroja cha kuwaondoa watu katika mjadala. Hakuna mahusiano yoyote kati ya kuendelea na mchakato wa katiba na shughuli za kiuchumi. Katiba ya sasa ipo miaka mingi na huo uchumi mbona haujajengwa kwa kiwango hicho kinachozungumzwa."

Wakati serikali na chama tawala wakiendelea kuhubiri uchumi kwanza kuliko katiba. Vuguvugu la kutaka mchakato huo uendelee linazidi kukua kila uchao. Haijulikana ikiwa harakati hizo zitaufanya utawala wa Rais Samia kubadili msimamo au zitakuwa ni kelele za chura zisizomkera tembo.

Ni ukweli uliowazi katiba ya sasa ina mapungufu mengi kwa kuzingatia maendeleo ya demokrasia na siasa katika mataifa mengine. Watetezi wa katiba mpya wanaamini katiba mpya ni muhimu ili kuboresha namna nchi inavyoendeshwa, wananchi kuwa na mamlaka zaidi na kumaliza kero za muungano.

 Zitto Kabwe anasma "Ni katiba ambayo inatoa faida kwa chama tawala, hata kikiwa ni Chadema, ACT Wazalendo ama chama chochote. Kikishinda dola kitakuwa kama CCM. Ni katiba inayoweka urais wa kifalme na kunyima haki za watu."

Miongoni mwa vitu ilivyonavyo katiba ya sasa ni Rais kuwa na madaraka makubwa ya kiutendaji, nguvu ya uteuzi katika safu mbalimbali na kubwa zaidi ni uteuzi wa Tume ya Uchaguzi.

Aina ya tume iliopo sasa ni ile ambayo Mwenyekiti na watendaji wake huteuliwa na Rais wa nchi. Ikumbukwe kuwa Rais anayetawaka kwa utamaduni wa CCM anakuwa ndiye mwenyekiti wa Chama hicho, naye huwa mgombea wa kiti hicho unapofika uchaguzi baada ya miaka mitano.Wagombea wa upinzani hawana uwezo wa kuchagua Mwenyekiti wa Tume. Uteuzi wa Mwenyekiti na watu wake huleta ukakasi ikiwa kweli wanaweza kusimamia uchaguzi huru na haki au husimama kwa maslahi ya aliyewachagua!

Hayati Magufuli aliwahi kunukuliwa, "haiwezekani Mkurugenzi (wa tume ya uchaguzi) nikuteue Mimi, nikupe mshahara, nikupe posho, nyumba na gari halafu uende huko umtangaze mpinzani kuwa ameshinda."

Uchaguzi uliopita ulikumbwa na mizengwe na malalamiko mengi. Wagombewa wa upinzani walienguliwa kwa sababu ambazo huko nyuma usingeweza hata kuzisikia mtu akitamka, mawakala wa vyama vya upinzani waliondolewa na wapo wanaomini kauli hiyo ya Magufuli ilichangia pakubwa uchaguzi wa Oktoba 2020 kuendeshwa kisongombingo. Pamoja na hilo Tume ya Uchaguzi wakati wote ilijitokeza na kusema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

Rasimu ya Katiba mpya ilipendekeza uwepo wa serikali tatu katika muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano uliogubikwa na kero tangu kuundwa kwake. Lakini ndani ya CCM kinachoelezwa kuungwa mkoono ni serikali mbili kuelekea moja.

Wabunge wa CCM kwa wingi wao katika Bunge maalum walifanikiwa kushinikiza kuondolewa kipengele cha serikali tatu na kubakisha mbili kama ilivyo sasa. Licha ya maoni ya Watanzania kutaka mabadiliko katika kipengele hicho.

Kwa Katiba ya sasa hakuna mwenye uwezo wa kuhoji matokeo ya Urais mahakamani. CCM ndio mtawala; kwa miaka mingi katiba hii imetoa ahueni kwa chama hicho baada ya uchaguzi. Hata ikiwa matokeo ya Urais yamekumbwa na kasoro hakuna mwenye uwezo wa kuyahoji kisheria. Ni kama farasi bandani, akitoka ndio ametoka.

Hayo ni machache kati ya mengi yaliyopo katika katiba ya sasa, ambayo kwa tafsiri ya kisiasa yanaonekana kukinufaisha chama kilichopo madarakani. Bila ya kujali ikiwa ni CCM au chama kingine chochote.

Msimamo wa CCM kuhuhu Katiba mpya ni upi hasa?

Msimamo wa CCM uliotolewa na mwenyekiti wake, Samia Suluhu upo wazi kwamba, Katiba ni muhimu lakini si kipaumbele kwa sasa, kipaumbele cha sasa ni kujenga uchumi na kuifungua nchi. Msimamo huo umepakwa rangi na viongozi wengi wa chama hicho akiwemo Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi Ndg Shaka Hamdu akisema kipaumbele zaidi kimewekwa katika kujenga nchi kwa ukamilishaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, kupambana na umasikini, kuboresha huduma za kijamii, kuboresha mazingira ya biashara, kuzidisha ustawi wa demokrasia, kusimamia utawala bora, kulinda sambamba na kuheshimu haki za binadamu.

'Ajenda ya Katiba mpya sio ajenda ya Chama cha mapinduzi kwa muda huu, na wala hatutatoka kwenye mstari tukacheza ngoma ambayo inataka kuturudisha nyuma kuweza kwenda hatua kubwa zaidi kimaendeleo', alisema Shaka

 Faraja Kristomus aliiambia BBC kuwa "CCM ina mtazamo tofauti kuhusu muundo wa muungano, ukubwa wa Bunge na mfumo mzima wa uendeshaji wa nchi. Katiba ya sasa inakipendelea zaidi chama tawala, kuliko katiba mpya iliyopendekezwa. "CCM inaogopa mchakato wa katiba kwa sasa kwa sababu wananchi wangependelea zaidi maoni yaliyotolewa katika tume ya Jaji Warioba, iwe ndio msimamo halisi wa katiba mpya ambayo wananchi wanaitaka."

Kwa mitizamo ya wanaounga mkono kuendelea kwa katiba ya sasa, wanaeleza uzuri wa katiba hiyo kupitia mfano wa namna ilivyotumika kwenye suala la kifo cha Magufuli kilichotokea mwezi Machi mwaka huu na kuingia kwa Rais Samia. Kwamba hakukua na vurugu, kulikua na hali tulivu kwa kuwa katiba ilikuwa wazi kwamba akifa Rais, basi makamu wa Rais anaapishwa kuchukua nafasi yake.

Kadhalika Mabadiliko ya kumi na mbili yalitokea mwaka 1995 yameweka ukomo wa Rais wa vipindi viwili vya miaka mitano mitano, utaratibu ambao unaleta shida kwa viongozi wengi wa Afrika. Na kingine kinachopigiwa chapuo kwenye katiba ya sasa ni kwmaba inawapa kipaumbele wanawake kwa kuwaongezea idadi ya viti maalumu kufikia asilimia 30 na kuboresha haki mbalimbali ikiwa ni pamoja na haki ya kutoa maoni, kushiriki na watu wengine na haki ya kuabudu.

Pomoja na uzuri huo, bado Katiba ya sasa haijaweza kuendana na mabadiliko ya kimfumo hasa mfumo wa vyama vingi vya siasa na maendeleo ya demokrasia. Hali inayotoa mwanya kwa chama kinachotawala kuwa katika wakati mzuri zaidi kimizania kuliko vyama vilivyo nje ya utawala.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JINSI YA KUMSHINDA SHETANI

NGUVU YA DAMU YA YESU

VIPAJI VYA ROHO MTAKATIFU