Kwa nini tunasifu kama sehemu ya maombi yetu?
Sifa huja kutokana na moyo wa shukrani au
furaha, pia unaweza ukaimba katika hali ya huzuni ukitoa hisia zako za ndani
kutokana na kile unachopitia.
Kuimba na kusifu ni vya muhimu kwa mafanikio
ya ufahamu na mahusiano yako na Mungu, kabla haujaomba lazima ujiulize maswali
kuwa je mahusiano yako yakoje na yule unayetaka kumuomba.
Utimilifu wa kweli wa kiroho huja pale
tunapoelekeza maisha yetu katika muendelezo wa kusifu na kuabudu, unapoendelea
kumsifu na kumwabudu Mungu ndipo unaongeza ladha ya mahusiano yako ya kiroho na
Mungu wako.
Chanzo cha sifa zetu:
Yesu ndio chanzo cha sifa zetu kwa sababu ya
kile alichotutendea, alikufa msalabani kwa ajili yetu ili alipe deni zetu,
alifufuka kutoka kaburini ili nasi tupate kuwa hai na sasa tuna fursa na uwezo
wa kupokea miujiza mikuu ya Mungu kwa sababu ya kile alichofanya. Tunasifu na
kuabudu kuheshimu na kushukuru kile Yesu alichokifanya kwa ajili yetu.
Kuzaliwa upya kwa roho ya Mwanadamu kulikuja
kupitia kile Yesu alichokifanya; Neno la Imani li karibu sana nasi liko
kinywani na moyoni mwetu. Warumi 10:8 “Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa
chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.”
Sifa hazitoki kwenye kitabu, kinanda wala
gitaa bali huanza toka ndani ya roho ya mtu na inatawaliwa na nia ya mwanadamu.
Kwa nini nia? Kwa sababu akili ya mtu ndiyo inayoamua kuwa anataka kuimba, na
wimbo gani ataimba.
Nguvu ya sifa:
Matendo ya Mitume 16:25-26 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila
walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine
walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya
gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote
vikalegezwa.” Wakati Paulo na Sila walipo amua
kumsifu Mungu walifungua malango yao ili waweze kumsababisha mfalme wa Utukufu
kuja na kutenda kwa niaba yao.
Utakapojua jinsi ya kumpa Mungu sifa
utasababisha mambo yatokee kwako. Tunapo sema kusifu hapa sina maana ya kuimba
na waimbaji, kinanda wala gitaa bali nazungumzia moyo wa mtu ulio na sifa.
Sifa sio kwa watu wanaosahau nini kilitokea
kwao, la! Kusifu na kuabudu ni kwa wale walio na moyo wa shukrani.
Nguvu ya sifa iliwasababisha Paulo na Sila
kutoka gerezani, yeyote aliye na nguvu ya sifa haijalishi kutakuwa na vikwazo
vya aina gani kutoka kwa ibilisi kamwe havitamzuilia yeye kushindwa kumsifu
Mungu, kwa jinsi yoyote atamsifu Mungu kwa kile alichomtendea.
Tutakapo ziruhusu zaburi za sifa katika mioyo
yetu Mungu atalitimiza Neno lake kwetu na tutaona ushindi katika maisha yetu.
Kuabudu inamaana gani?
Kuabudu maana yake ni kustahili au uthamani,
kuhesabiwa wa thamani hiki ndicho tunakiita kuabudu. Unapo muabudu Mungu
inamaana kuwa unamwambia unastahili, wewe ni wa thamani kwangu.
Unamsifu Mungu kwa ajili ya kile alicho
kifanya na unamwabudu kwa maana anastahili na Yeye ni wa thamani kwako.
Kusifu kunaambatana na matoleo ya kidhabihu,
kuna tofauti kati ya sadaka na dhabihu, sadaka unatoa kitu cha thamani lakini
dhabihu inaambatana na moyo.
1 Mambo ya Nyakati 16:29 “Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Leteni
sadaka, mje mbele zake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu;”
Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya
damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu
ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” Kushindana kwetu, kupigana, kupambana si kati yangu
mimi na wewe, kama tukishinda na kupigana inamaana mmoja ni wa ibilisi na
mwingine ni wa Mungu.
Katika familia yoyote ile ukiona kuna talaka
maana yake mtu mmoja kati yao amekubali kutumiwa na ibilisi ili apate kutenda
hicho alicho kifanya. Kama ni kanisani ukaona utengano watu wanaligawanya
kanisa kwa maneno yao na mtu anasema MUNGU ameniambia nifanye hivi, la si Mungu
ni ibilisi, kwa sababu Mungu msistizo wake ni umoja na sio mgawanyo.
Ukionamgawanyo basi jua kuwa ni ibilisi yupo kazini.
Mungu aliumba mfanano wala yeye hakuleta
mgawanyo mbinguni au duniani. Hata sasa unaona kuna makabila mengi na mataifa
mengi Mungu hakuumba hayo bali ni ibilisi.
Ndio maana siku za mwisho wote waliomwamini
Mungu tutakuwa mahali pamoja Mungu mmoja Roho Mtakatifu mmoja na Yesu mmoja.
Kwa nini kuna haya yote ulimwenguni? Kwa sababu watu wamebeba maisha yao
wenyewe hivyo wana shauku au tama ya kile wanacho kitaka na sio kile Mungu
anachotaka.
Usikubali kutumiwa na ibilisi kwa kuwa mmoja
wa kuleta ugomvi au utengano mahali popote bali uwe mpatanishi pamoja na Mungu.
Kuwekwa watu huru ni jambo moja na
kuwasababisha waendelee kuwa huru ni jambo lingine, ni muhimu mno kumfundisha
mtu adumu kuwa huru pindi anapo funguliwa au kuwekwa huru.
Unadumuje katika kuwa huru? Kaa mbali na
dhambi, jifunze kuhusu Neno na maombi. Yohana 5:14 “Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu,
akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata
jambo lililo baya zaidi.”
Watu wengi wanapokea uponyaji na baada ya huo
ukombozi wanadumu nao kwa kitambo tu baada ya hapo maradhi yanarejea tena, je
ni nani anayeyarejesha hayo maradhi? Ni mtu mwenyewe. Unapowekwa huru usirejee
kule ulikokuwa mwanzo yaani usitende dhambi tena ili uweze kutunza huo uponyaji
wako.
Ibilisi ana mambo matatu anayoyafanya kwa
mtu, hasa kwa mwamini:
1.
Anakuja
ili kukuibia, kuiba nini? Chochote kilicho chema
ibilisi anataka akichukue kutoka kwako, anaweza kuchukua afya, pesa, mumeo,
kazi yako au biashara yako, ibilisi ni mwizi.
2.
Kuua; ibilisi haji kuiba tu kwako bali pia anakuja kuua,
chochote kizuri atakacho kiona atakiua, biashara yako, kazi yako au mahusiano
yako. Ukiona kitu chochote katika maisha yako kinaelekea kufa usisubiri mpaka
kife pambana.
3.
Anakuja
kuharibu, ibilisia anapokuja kwa mtu ni ili
kuharibu kitu kizuri kilichopo ndani ya mtu ili kukiondolea uzuri wake.
Biashara iliyoibiwa lazima irejeshwe, maisha
bora ambayo ibilisi alikuibia lazima yarejee, furaha ambayo ibilisi alikuibia
lazima irejeshwe kwa Jina la Yesu, lazima hayo yakatokee kwako jiadae.
Maoni