Lissu kurejea Tanzania kudai katiba mpya
Lissu kurejea Tanzania kudai katiba mpya
Licha ya Rais Samia Suluhu wa Tanzania kuweka wazi kwamba kwa wakati huu hayuko tayari kuanzisha mchakato wa katiba mpya, wapinzani wameendelea kupaza sauti kuongeza shinikizo la kudai katiba mpya.
Chama kikuu cha upinzani Tanzania, CHADEMA, kimezinduwa rasmi Alhamis vuguvugu lake la madai ya Katiba Mpya na haki za kisiasa.
Kauli hiyo ya Rais Samia, ambaye aliwahi kuwa makamu mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, inaonekana kama vile imeamsha ari ya wapinzani hao pamoja na wanaharakati wanaotumia majukwaa mbalimbali kupeperusha ujumbe wa kudai katiba mpya.
Chadema hakitarudi nyuma katika kutaka katiba mpya
Chadema, ambayo ilianza hivi karibuni kwa kufanya mikutano ya ndani katika takribani mikoa yote ya Tanzania Bara, sasa inaonekana kugeuza muelekeo na kuanzisha makongamano ya ndani yenye shabaha hiyo hiyo ya kushajiisha umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya.
Katika kongamano lake la kwanza lenye dhima hiyo hapo jana, chama hicho kilisema hakitarudi nyuma katika mkakati wake wa kutaka kuwepo kwa katiba mpya na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akatoa mapendekezo kadhaa kwa Rais Samia, ukiwemo ushauri wa kuunda tume ya katiba ili kusimamia mchakato wa kupata katiba mpya.
Na kwenye suala la zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, Mbowe alisema wazi kwamba hawatangojea tena, na badala yake ameitisha mikutano nchi nzima kwa ajili ya kupeleka ujumbe kudai katiba mpya.
Viongozi wa kidini nao wamekuwa wakilijadili suala la katiba mpya
Kikiweka msukumo juu ya hilo, makamu mwenyekiti wake aliyeko ugaibuni, Tundu Lissu, aliyezungumza kwa njia ya mtandao katika kongaamano hilo la kudai katiba mpya, lililofanyika kando kidogo ya kitovu cha jiji la Dar es Salaam, aliashiria utayari wake wa kurejea nchini kushiriki vuguvugu la kudai katiba mpya.
Maoni