Nini maana ya kufunga?



Isaya 58:6-14 “Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde…….

·         Kufunga maana yake ni kuachilia matendo maovu.

·         Kufunga ni kukusababisha wewe kutimiza mapenzi ya Muumba wako,

·         Kufunga ni kumwambia Mungu mimi sistahili pasipo wewe, yaani inamaana ni kumkaribia Mungu.

·         Kufunga ni kuuita uwepo wa Mungu uwe pamoja nawe na kutembea na wewe, uwepo wake ni utukufu wake na utukufu wake ni ulinzi wako. Hivyo unapo funga ni sawa na unauambia utukufu wa Mungu uje kwako.

·         Unapo funga ni sawa na unamwambia Mungu mimi sina nguvu dhidi ya maadui zangu ninahitaji usaidizi wako.

·         Ni kumruhusu Mungu atende jambo kwa niaba yako sawa sawa na kile ulicho mueleza.

Kufunga ni jambo lenye nguvu kwa maana unamuhusisha Mungu katika maisha yako hivyo lolote utendalo utastawi. Unapo funga inamaana kuwa umeamua kuutiisha mwili wako uwe dhabihu iliyo hai mbele ya Mungu. Ni kumwambia Mungu mwili huu ni hekalu lako, utakapofanya hivyo maana yake utakuwa unaua maradhi na magonjwa katika mwili wako, kwa maana uwepo wa Bwana unakuwa ndani yako na magonjwa hayawezi kukaa katika uwepo wa Mungu. Kufunga maana yake ni kuiambia dunia kuwa umasikini hauna nafasi kwangu kwa maana uwepo  wa Mungu upo ndani yako. Ni kuruhusu kutumiwa na Mungu.

Unapo funga tarajia jambo la pekee kutokea katika maisha yako. Mfalme Yehoshefati alipokuwa na watu wake alitangaza kufunga kwa watu wake wote na baada ya hapo neno likamjia na kumwambia 2 Nyakati 20:15 “akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; Bwana awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; KWANI VITA SI YENU BALI NI YA MUNGU.” kufunga maana yake  ni  kugeuza vita iwe si yako bali iwe ni ya Bwana, unapo funga unabadilisha jinsi ulivyo.

Ni muhimu sana kwako wewe kuelewa maana ya kufunga, kufunga sio kupunguza kula chakula, usifunge  na siku nzima ukakusanya chakula kwa ajili ya jioni, huu sio mfungo bali umebadilisha tu saa za kula. Baada ya mfungo Yehoshefati hakupigana bali alipofika vitani akakuta maadui wameshapigwa na ye akateka nyara tu, mfungo unakusaidia wewe kupata vitu ambavyo haukutarajia kuvipata.

 

IMANI

1 Yohana 5:4  “Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu.” Imani inaweza kupatikana kwa wale waliozaliwa na Mungu na si wale waliozaliwa na mwanamke.  Hii inamaana kua kwa wale waliozaliwa naYesu inamaana wamezaliwa katika roho hawa ndio unaweza kukuta imani ndani yao.

Mshiriki wa imani maisha yake yanaonekana hapa: 1 Yohana  5:18  “Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi.” aliye zaliwa na Mungu hatendi dhambi, dhambi hairuhusiwi kwake na pia anajilinda na kujitunza kwa nini au anatunza nini? Hasubiri kuambiwa usifanye hiki na kile bali yeye  anajitunza na kujilinda mwenyewe, hii inamaana kuwa anatunza maisha ya Mungu ndani yake na si kutunza nguo au nyumba yake. Kujitunza mwenyewe ni pamoja na kumtunza mkewako na watoto, nyumba yako, kazi yako na biashara yako. Watu wa imani hawana hofu kwa sababu ibilisi hana nguvu juu yao, mara zote ibilisi anawaogopa. Yeyote anaye enenda katika imani yeye ni mshindi na anatembea katika ushindi kamwe ibilisi hawagusi.

Nini maana ya imani? Imani maana yeke ni:-

·         Imani ni kutumaini si katika uwezo wa wanadamu, sio kusema labda inawezekana, labda itakuwa, bali imani ni kweli.

·         Imani sio hoja ambayo inakuja kwa kufikiri, kupitia mtazamo wako wala katika namna yako ya kufikiria.

·         Imani maana yake kile Mungu amesema ni kweli, unapojua kile Mungu alichosema kuwa ni kweli hiyo ndiyo inaitwa Imani.

·         Imani huja kwa kusikia Neno na kuakisi katika ahadi za Mungu aliye juu yeye aliyesema na kile anacho kisema ndicho anachokitenda. Hakuna kitu kinacho mzuilia Mungu huku duniani.

 

Imani mara zote ipo katika Neno la Mungu, unapo litendea kazi neno inamaana kuwa unatenda katika imani; Biblia inasema “imani haiwezi kushindwa” hivyo inamaana kuwa ukitenda katika neno hautakaa ushindwe.

Mungu atakufurahia pale utakapokuwa katika imani, hii inamaana kuwa ukiwa katika Neno Mungu atakufurahia na ndio maana yeye akasema “naliangalia neno langu ili nipate kulitimiza” ukitenda katika Neno unampendeza Mungu kwa sababu yeye analiangalia Neno lake. Nani aliye na Neno? Muabuduo, Je! Wewe ni muabuduo?  Kama wewe ni muabuduo Mungu anakuangalia na kukuangalia wewe. Mungu yumo ndani ya Neno. Analipenda analiishi na kulitendea kazi Neno. Ukiwa ndani ya Neno mara zote wewe ni mtendaji;  Unaweza kutenda lolote unalopaswa kutenda.

Ayubu 22:28 “Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako.” Ukitenda sawa sawa na Neno unaishi katika Neno na ndipo utaamrisha chochote nacho kitakuwa, utakaposema nataka kujenga hauhitaji pesa bali unahitaji Neno ili hilo jambo lipate kutimia kwako.

Baba wa mbinguni anasubiri kulitendea kazi Neno lake, unapo lisoma Neno, utakapo litamka na kuliishi hilo Neno inamaana kitu chochote utakacho kitamka kitakuwa kwa maana Neno linaishi ndani yako. Kwa maana hiyo neno lolote utakalo litamka litatoka na nguvu ya Mungu kwa sababu neno linaishi ndani yako.

Wengi wenu mnatafuta tafuta mistari ya Biblia pasipo kulijua Neno lililo tamkwa. Yesu aliwatuma wanafunzi wake waende ili kuwafanya watu wawe neno lililo tamkwa. Wakikubali inamaana na wao wanakuwa neno lililo tamkwa na wakitembea wanakuwa hilo Neno na lolote watakalo tamani litakuwa kwao.Ukitembea katika Neno lililo tamkwa tangaza lolote nalo litatokea kwako.

Ukiri: Baba mimi ni Neno lililo tamkwa, nitatamka sawa sawa na jinsi nilivyo lazima nidhihirike ili kwamba ninapo tamka chochote lazima kidhihirike kwangu kwa jina laYesu.

 

NGUVU YA DAMU:

Damu ya Yesu ndiyo inayomfanya mwamini awe mtakatifu wa Mungu, hauwi mtakatifu pasipo Damu ya Yesu kukusafisha. Unahitaji damu ya Yesu kukusafisha ili uwe mtakatifu wa Mungu. Haki huja kupitia Neno lakini utakatifu huja kwa kupitia damu. Katika damu ndipo ukombozi ulipo,  huwezi kutoka kwenye dhambi na uovu ambao unaokufanya usiwe mtakatifu pasipo Damu ya Yesu, ni kwa Damu pekee ndiyo itakufanya uwe mtakatifu wa Mungu na huo utakatifu ndio unamfanya Mungu avutiwe na wewe. Utakatifu wako ndio utakao mvutia Mungu lakini ili uupate ni lazima uipate Damu ya Yesu na hapo ndipo ukombozi ulipo. Nguvu inayo fukuza dhambi zote maradhi na magonjwa ni damu ya Yesu, kupitia Damu tunao ukombozi wetu, wokovu, utakatifu, tunakuwa washiriki wa mambo ya mbinguni.

Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” tunamshinda adui, maradhi na magonjwa kwa Damu ya Yesu, imo nguvu ndani ya hiyo Damu. Katika maisha yako Damu ya Yesu ni ya muhimu sana ili uwe na ushindi na kupitia hii ndipo mwamini atashinda kila aina ya changamoto humu duniani.

Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” kuchubuliwa kwake kulisababisha damu imtoke kwa ajili yetu, kwa kupitia damu yake tunakuwa washiriki wa uzima.

 

UPAKO:

·         Upako huvunja nira,

·         Unakuondoa kunako mizimu,

·         unakukutoa kutoka katika ya kale.

·         Upako unakutoa kwenye mambo yanayo kushikiria na kuvuta nyuma.

Isaya 10:27 “Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Kama kuna nira zinazo kufuatilia iwe ni za kifamilia unahitaji upako ili kuzivunja hizo nira.

Mafuta ya upako ni nini? Ni tunda la mzaituni  ambalo kwa nyakazi za kale walikuwa wanatumia kwa matumizi yafuatayo:-

·         Yalitumika kuwasha taa hekaluni,

·         Yalitumika kama mafuta yakujipaka mwilini,

·         Yalitumika kwa ajili ya kupikia,

·         Yalitumiwa kuweka wakfu kitu kitakatifu kama nyumba au vyombo vitakavyotumika hekaluni.

·         Yalikuwa ni kwa ajili ya kusimikwa kwa watumishi wa Mungu aliye juu; lengo la kuwapaka mafuta hayo ni kuonesha kwamba mtu huyu yupo chini ya wito wa Mungu na kwa kufanya hivyo roho wa Mungu mwenye enzi yote alikuja juu ya huyo mtu ili kumuwezesha kwa ajili ya kazi takatifu za Mungu. Tunaweza kuona Musa alipofanya hivyo kwa Haruni na Samweli kwa Daudi; jambo hilo Yesu alifanya kwako wewe ambaye umeokoka, baada ya kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako roho yule yule aliyeishi kwa Yesu yumo ndani yako.

Kupitia huo upako unayo nguvu ya kufukuza mapepo, unayo nguvu ya kuponya wagonjwa na kufukuza maradhi. Kwa huo upako tunayo nguvu ya kuziharibu kazi zote za ibilisi.

Ombi:

Simama katika zamu yako na mfukuze ibilisi katika chochote alicho kuibia au kukiharibu katika maisha yako.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JINSI YA KUMSHINDA SHETANI

NGUVU YA DAMU YA YESU

VIPAJI VYA ROHO MTAKATIFU