nyota hawa 10 wa kandanda wanapigiwa upatu kutamba Ulaya
EURO 2020:nyota hawa 10 wa kandanda wanapigiwa upatu kutamba Ulaya
Kutoka juu kushoto: Jeremy Doku, Eljif Elmas, Orkun Kokcu, Becir Omeragic, Jamal Musiala na Alexander Isak, ni miongoni mwa nyota wa kuchungwa katika michuano ya Euro 2020
Kwa sasa dunia inasubiri kwa hamu kuona kizazi kipya cha nyota wa soka, baada ya kizazi cha sasa kinachoongozwa na Cristiano Ronaldo na Leonel Messi, kuelekea mwishoni.
Ukiacha kombe la dunia, ligi ya mabingwa ulaya ama ligi tano bora kubwa Ulaya, michuano mikubwa mingine inayozalisha nyota wengi wapya ni michuano ya Euro, ambayo kwa mwaka huu inaanza Ijumaa hii katika majiji 11 barani Ulaya.
Michuano hii inashirikisha nyota 622 waliothibitishwa, wapo nyota wazoefu kama kina Ronaldo, Paul Pogba, Romelu Lukaku, Robert Lewandowski, Ng'olo Kante na Gareth Bale, lakini wapo pia nyota wakali wengine vijana ambao wameibuka hivi karibuni kama Kylian Mbappe wa Ufaransa, Pedri wa Hispania, Phil Foden wa England na Billy Gilmour wa Scotland, wanaotarajia kung'ara.
Pamoja na hao dunia inatarajia kushuhudia nyota wengine vijana wapya wakiibuka kupitia michuano hiyo itakayoshirikisha mataifa 24. Wameanza kuonyesha cheche zao lakini michuano hii huenda ikaweka zaidi kwenye ramani ya soka duniani. BBC inakuletea wachezaji 10 ambao ni wakutazamwa kwa jicho la haja.Ni mshangao upi mkubwa katika historia ya mashindano ya ubingwa wa bara Ulaya?
1. Jeremy Doku (Ubelgiji)
Huyu anafahamika kama mfalme wa kukokota mipira, kutokana na uwezo wake wa kuwakabili bila uoga mabeki wa aina zote. Kama unamjua nyota mwenye kasi wa klabu ya Wolves ya England, Adama Traore, basi aina yake ya uchezaji na kasi inashabihiana kabisa na Doku. Japo hana wakati mzuri sana nchini Ufaransa tangu ajiunge na Rennes mwezi Oktoba mwaka jana kwa kitita cha £20m akitokea Anderlecht, anatazamwa kung'ara kwenye michuano hiyo.
Doku alifunga katika mchezo wake wa kwanza tu kuichezea timu ya taifa dhidi ya Iceland mwezi September na kufunga goli lingine na kutoa pasi mbili za mabao katika mchezo dhidi ya Belarus mwezi Machi.
Kocha wa Ubelgiji, Roberto Martinez ameendelea kumuamini, licha ya kukabiliwa na upinzani mkali wa nafasi ndani ya kikosi cha Ubelgiji kutokana na uwepo wa washambuliaji wegi wakali.
2. Jordan Larsson (Sweden)
Unamjua nyota aliyeng'ara na vilabu vya Fayenoord, Celtic, Barcelona, Manchester United (mkopo)? aliyeng'ara pia na timu ya taifa ya Sweden, Henrik Larsson, basi huyu ni mtoto wake. Baba yake alikua mshabiki wa nyota wa mpira wa kikapu, Michael Jordan, akaamua kumpa jina la Jordan mtoto wake huyo, badala ya kuwa mcheza kikapu, akafuata damu ya baba yake, sasa anatazwa kama nyota mkuwa ajae. Ameshaifungia Spartak Moscow mabao 15 msimu huu.
3. Jules Kounde (Ufaransa)
Vilabu vingi vya Ulaya vinamfuatilia sana nyota huyu, huenda asipate nafasi sana katika michuano hii, lakini akipata huenda akashangaza wengi. Ingawa si mrefu wa fupi sita, anatajwa kuwa mzuri zaidi kwenye mipira ya juu, wamempa jina la Cafu mpya, wakimfananisha na beki kisiki wa zaani wa Brazil, Cafu. Fikiria awe kwenye safu moja na Virgil van Dijk au Ruben Dias, utakuwa ukuta wenye ladha ya kuutazama muda wote. Manchester City walikaribia kumnasa msimu uliopita na msimu huu Arsenal wanajaribu kutupa ndoano Sevilla ili kumnasa.
4. Adam Hlozek (Czech Republic)
Anatajwa kama kipaji kikubwa zaidi kutokea nchini Czech tangu Tomas Rosicky, Hlozek maarufu kama'Golden Boy' licha ya kuwa nje kwa karibu miezi minne na nusu kwa sababu ya majeraha, amekuwa mfungaji bora wa ligi ya Czech akiwa na magoli 15 katika michezo 19 tu aliyoichezea timu yake ya Sparta Prague. Ni wa kutazamwa sana kwenye michuano ya mwaka huu.
5. Pedri (Hispania)
Ana historia ya kuburudisha, alisajiliwa na Barcelona mwaka 2019, baada ya kuichezea Las Palmas michezo mitatu tu. Wengi waliamini nyota huyo wa zamani wa Tenerife amesajiliwa kwa ajili ya kutumika baadae sana, lakini akawastaajabisha kwa kuwa mchezaji wa pili kuicheza michezo 50 Barcelona, kwa muda mfupi nyuma ya Lionel Messi.
Luis Enrique akampa nafasi timu ya taifa Hispania mwezi Machi, sifa yake kubwa ni kusoma mchezo na uwezo wake wa kulazimisha kuingia kwenye eneo la hatari. Anatarajiwa kufanya makubwa kwenye Euro mwaka huu.
6. Alexander Isak (Sweden)
Akiwa na mabao 17 na klabu yake ya Real Sociedad kwenye ligi kuu ya Hispania 'La Liga' msimu huu, Isak ameifanya uamuzi wa Borussia Dortmund kumruhusu kuondoka mwaka 2019 kuonekana kama uamuzi wa kushagaza. Yeye ndio mfungaji mdogo wa Sweden kuwahi kutokea , alipoifungia chi hiyo dhidi ya Slovakia miaka mine iliyopita. Barcelona wanamfuatilia kwa ukaribu, licha ya Sociedad kumuwekea thamani ya juu ya €70 million kwa klabu inayomtaka.
7. Nuno Mendes (Ureno)
Mendes, mlinzi wa kushoto wa Sporting CP ya Ureno, anaviumiza vichwa vilabu vikubwa vikiwemo vya Manchester City, Manchester United na Chelsea. Kupata namba kwenye kikosi hicho nas kubeba ubingwa wa ligi akiwana miaka 18 tu inatoa picha tosha ya ukali wa kinda huyu. Lakini ana uwezo wake unamfanya wengi kuamini anaweza kucheza winga wa kushoto au hata kiungo mshambuliaji
8. Tomas Suslov (Slovakia)
Suslov (kulia) , amecheza nafasi saba tofauti msimu huu akiwa na timu yake ya Groningen msimu huu. Kwa timu yake ya taifa ya Slovakia, anatarajiwa kucheza winga ya kulia.
Alikuwa mchezaji mdogo zaidi kuichezea timu ya taifa ya Slovakia, alipoichezea timu hiyo akiwa na umri wa miaka 18 tu. Wanamuita David Silva wa Slovakia wakimfananisha na Mhispania huyo aliyewahi kuichezea Manchester City. Kwa sasa anaichezea klabu ya Groningen, katika ligi ku ya Uholanzi, pamoja na mkongwe Arjen Robben, mwenye miaka 37.
9: Jamal Musiala (Ujerumani)
Musiala amezaliwa Stuttgart (kushoto) mama yake ni mjerumani na baba yake ni Mnigeria. Alihamia England akiwa na miaka saba akiichezea timu ya watoto ya Chelsea, kabla ya mwaka 2019 kuhamia Bayern akiwa na miaka 16.
Musiala ni kiungo mshambuliaji ambaye ametimiza miaka 18 mwezi February mwaka huu, pamoja na umri huo ameshaonyesha makali yake akiwa na timu ya Bayern Munich hasa kwenye klabu bingwa Ulaya.
Akiwa na miaka 17 tu alifunga goli lake la kwanza kwenye Klabu bingwa Ulaya dhidi ya Lazio. Musialaanatazamwa kufanya makubwa kwenye Euro mwaka huu, kama atapata nafasi.
10. Sasa Kalajdzic (Austria)
Kalajdzic (mwenye jezi nyekundu) anafananishwa na Zlatan Ibrahimovich na Peter Crouch kutokana na urefu wake wa karibu futi sita.
Wanamwita Ibrahimovich, wakimfananisha na mkongwe huyo, wa Sweden aliyewahi kutamba na vilabu vikubwa Ulaya. Ameshaifungia Stuttgart mabao 17 msim huu, kitu kinachoashiria ukali wake wa kutazamwa katika michuano ya Euro mwaka huu.
Ukiacha hao wapo wengine ambao wanapaswa kutazamwa sana kwenye michuano ya mwaka huu ya Euro, wakiwemo Eljif Elmas (North Macedonia), Becir Omeragic (Switzerland) na Ryan Gravenberch (Netherlands).
Wegine ni Orkun Kokcu (Turkey), Alex Kral (Czech Republic), Halil Dervisoglu (Turkey), Christoph Baumgartner (Austria) , Kamil Piatkowski (Poland), Josko Gvardiol (Croatia) na Onni Valakari (Finland).
Maoni