Simba 0 Yanga 1: Yanga yailambisha Simba sakafu na kutibua sherehe za ubingwa
Simba 0 Yanga 1: Yanga yailambisha Simba sakafu na kutibua sherehe za ubingwa
Klabu ya Yanga imewachapa watani wao wa jadi Simba SC na kuizuia klabu hiyo kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania kwa msimu wa 2020/2021.
Mabingwa watetezi Simba walihitaji kupata alama tatu ili kutawazwa mabingwa kwa msimu wa nne mfululizo.
Hata hivyo goli la dakika ya 13 lililofungwa na Zawadi Mauya liliitosha Yanga kuifunga mdomo Simba na kulinda hadhi yake. Laiti Yanga ingelifungwa, maana yake watani wao wangetangazwa mabingwa kupitia mgongo wao.
Hata hivyo licha ya kufungwa bado Simba wapo katika nafasi nzuri ya kuchukua ubingwa. Simba sasa inahitaji kushinda michezo miwili kati ya minne aliyosalia nayo ili kuchukua ubingwa. Hata hivyo, ubingwa huo utakosa kionjjo muhimu cha kumfunga Yanga katika mechi zote mbili za msimu huu. Mechi ya raundi ya kwanza Simba na Yanga zilitoka sare ya goli 1-1.
Joto kali lapanda kabla ya mchezo
Kwa mujibu wa ratiba ya awali ya ligi, mechi hii ilitakiwa ichezwe mnamo Mei 8, lakini ikaakhirishwa katika mazingira ya kutatanisha.
Shirikisho la Kandanda nchini Tanzania (TFF) lilitangaza mabadiliko ya ratiba ya mchezo mchana wa Mei nane na kuisogeza mbele mechi hiyo kutoka saa 11 jjioni mpaka saa moja usiku, kwa maelezo kwamba wameamrishwa kufanya hivyo na serikali.
Klabu ya Yanga ilipinga mabadiliko hayo na kujikita kwenye kanuni ambazo zinabainisha kuwa mabadiliko ya ratiba yanatakiwa kufanyika kabla ya saa 24. Hivyo waliingiza timu uwanjani saa 11 jioni na baada ya kusubiri kwa 15 za kikanuni bila Simba kutokea uongozi wa Yanga ukaitoa timu uwanjani.
Simba wao wakaingia uwanjjani kama ilivyoelekezwa na TFF na wakati huo wapinzania wao walikuwa wamekwishaondoka muda mrefu uliopita. Kadhia hiyo ikasababisha TFF kuakhirisha mchezo huo kwa muda usiojulikana.
Suala hilo lilizua mjjadala mkubwa nchini Tanzania ambao ulihusisha vilabu hivyo viwili, TFF na serikali. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa alilizungumzia suala hilo Bungeni na kuagiza mazungumzo yafanywe kupata suluhu.
Mwishoni, bila kupia lawama upande wowote ule, kikao baina ya klabu hizo mbili, TFF na serikali kikafikia tamati ya kuwa mchezo huo urejewe tarehe ya leo Julai 3, 2021.
Maoni