UVIKO 19 TANZANIA
UVIKO 19 TANZANIA
Kahama.
Kiongozi wa mbio za mwenge, Luteni Josephine Mwambashi amewataka wananchi wa Kahama mkoani Shinyanga, kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Uviko-19 ambao umerejea kwa kasi kubwa kwa awamu ya tatu ukilinganisha na wamu zilizopita.
Luteni Mwambashi alitoa kauli hiyo leo Julai 12, 2021 wakati akitoa ujumbe wa mbio za mwenge baada ya kuweka jiwe la msingi katika Shule ya Sekondari Mwakata ujenzi uliogharimu kiasi cha Sh137 milioni.
Alisema mwenge wa uhuru unakwenda sambamba na uchukuaji tahadhari juu ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (Uviko-19), kila mmoja anatakiwa kuchukua tahadhari bila kusukumwa na viongozi hivyo kwa mtu ambaye atakuwa hajavaa barakoa hatashiriki kukimbiza mwenge.
Luteni Mwambashi amesema, Wizara ya Afya imeendelea kutoa maelekezo bora ya namna ya kujikinga na ugonjwa huko na kwamba kila mmoja atatakiwa kuzingatia maelekezo hayo.
Hata hivyo amewataka kuhakikisha wanafanya usafi katika mazingira yanayowazunguka kwa kufukia madimbwi ya maji, kuua mazalia ya mbu ili kujikinga na ugonjwa wa malaria ambao kwa asilimia kubwa wanaoathirika ni watoto wadogo chini ya miaka mitano.
Luteni Mwambashi amesema takwimu za ugonjwa wa malaria zinaonyesha watoto wadogo chini ya miaka mitano wanaathirika zaidi ukilinganisha na watu wazima, hivyo mapambano dhidi ya ugonjwa huo yanaanza nasi kabla ya kutokea kwa madhara makubwa. Pia alisisitiza kuwa, miradi itakayozinduliwa na kuwekwa jiwe la msingi wahakikishe inakuwa na taarifa za kutoka kwa wahusika wa ujenzi wa miradi hiyo wanapatika ili kuondoa usumbufu ambao unaweza kujitokeza inapohitajika ufafanuzi wa kitalaam au kina juu ya mradi.
Kwa upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa ambae pia ni Mbunge wa Ushetu amesema, miradi mingi ya elimu na afya wananchi wamekuwa wakijitoa katika kuchangia na kutatua changamoto zinazowakabili kuhakikisha watoto wao wanasoma katika mazingira mazuri.
Maoni