HABARI YA MSALABA.

 

 HABARI YA MSALABA.
Tuko Kanisani kwa sababu ya imani yetu tuliyonayo na hatupo ili kusheherekea, tunakusanyika hapa kwa ajili ya imani ya Yesu Kristo ambayo ilianza na Ibrahimu, ni imani gani hiyo? Ya kumwamini muumbaji.

 

Kama Biblia inasema “pasipo imani hauwezi kumpendeza Mungu” njia pekee ya kumpendeza Mungu ni kukaa katika imani; kwa nini watu wanahangaika, wanateseka na wanang’ang’ana ili wapate chakula, wapate kodi au ada ya shule? Kwa sbabau wamekosa Imani ndani yao.

Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Yupo Mungu anayekuwezesha kupata kile unacho kihitaji, lakini kama haumtumaini kamwe hautaweza kuishi vizuri hapa duniani.

 

Imani inamfanya mtu jinsi alivyo, je! Wewe unaamini nini? Tutayaona maisha yako.

Imani tuliyomo ndani yake inaanzia pale msalabani na siyo mahali pengine. Ukitaka matatizo, mateso na maumivu yote yafikie kikomo ni pale utakapolijua Neno msalaba.

1 Wakorintho 1:18-19 “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa.” tofauti hapa ni nini? Ni mtazamo, tatizo siyo msalaba bali ni mtu, je! Wewe unaona nini au unafahamu nini kuhusu msalaba? Msalaba umesababisha mimi kuwa jinsi nilivyo leo, msalaba umekufanya wewe uwe jinsi hivyo ulivyo leo, ndiyo maana unanena kwa lugha mpya kwa sababu ya msalaba.

Katika msalaba kuna vitu vingi sana sasa je! Wewe unaona nini? Mambo unayo yaona hapo ndiyo utakayo yapata, kama ukiuona wokovu basi utaupokea, kama ukiona ni upuuzi basi utapokea huo upuuzi.

 

2 Wakorintho 4:3 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;” kwa wanao potea injili imefichwa kwao, ingawa wanasikia lakini kamwe hawataelewa maana yake ni nini? Kwa wanao potea utawahubiria lakini wataona kama ani upuuzi.

Warumi 1:16 “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.” Inamaana kuwa kwa watu wengine injili ni aibu kwao hawataki kuisikia wala kuibeba, na Yesu akasema ukinionea mimi haya na mimi pia nitakuonea haya mbele ya Baba yangu, hii inamaana kuwa msalaba kwa watu wengine hauna maana kwa maana ni aibu kwao. Ndio maana unaweza kumwambia mtu kuwa nimeokoka akakucheka, waacha wacheke kwa maana kwa wao ni wana wa upotevu wewe shikiria kile unacho kiamini.

 

kupotea maana yake ni nini? kupotea maana yake ni kutokuzingatia. Imani yetu inatembea kunako kuzingatia, kama hautozingatia basi upotevu umeruhusiwa kwako.

Kwa nini watu wanang’ang’ana katika maisha? Kwa sababu hawazingatii, imani ni kuzingatia, kwa jinsi unavyo zingatia ndivyo unavyo ipata imani, hatuipati imani kwa kuomba bali kwa kuzingatia.

Ukisoma kitabu cha ufunuo kinasema “yeye aliye na sikio na asikie” hii inamaana kuwa yeyote anaye zingatia acha azingatie, kwa anini? Katika uzingatia ndipo unapo pokea baraka zako, hata katika biashara usipo zingatia basi upotevu utatokea na utaishia kupoteza fedha na biashara, kwa nini? Kwa sababu hakuna kuzingatia na hii ndiyo tunaiita Imani.

Imani haiwezi kukaa kwa mtu asiyeweza na kuzingatia.

 

Wazo la Mungu kwa wale wanaotaka kutoka upotevuni wanapaswa kuzingatia  mstari huu: Mwanzo 4:7 “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.

Imani inagharimu uweza wa mtu, ni kwa jinsi gani unazingatia mambo na kutenda sawa sawa?  hiki ndicho kinaitwa imani, unapo sikia Neno lizingatie na utende sawa sawa basi utaipata imani, lakini  kama utasikia neno na usitende sawa sawa kamwe hautaweza kuipata imani.

Mwanzo 12: 1-2 “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;” Ibrahimu alilisikia hili neno na akalizingatia pasipo kuelewa nini kitatokea mbeleni lakini yeye alizingatia amri, imani ni jinsi unavyo zingatia na siyo jinsi unavyo sikia, hicho ndicho kinacho kufanya imani yako kujengwa.

Mungu alisema na Ibrahimu katika ndoto na siyo ana kwa ana lakini Ibrahimu alizingatia na akatenda kama Mungu alivyomwambia, kwa sababu ya hiyo Mugu aliweka kituo kwake na akaishia kusema naye kama rafiki. Kwa jinsi unavyo zingatia kutakupeleka hatua kwa hatua mpaka utafikia hatua ambayo Mungu atasema na wewe ana kwa ana.

Mungu anampenda mtu anayezingatia.

Mwanzo 4:7 “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.” Inamaana Mungu anataka kila mmoja wetu apate kutenda vyema, je! Wewe unatenda vyema. Unapikaje chakula chako? Unapopika je! Watu wanafurahia mapishi yako au wanalalamika?  Unaweza kuona ni jambo dogo sana lakini linamaana.

Je! Unayawekaje maisha yako pale unapoishi? Biblia inasema tenda vyema na siyo omba vyema.  Hii inamaana kuwa kila siku chochote utendacho tenda vyema, hiki ndicho kinaitwa kuzingatia.

Je! wewe unazungumzaje? Wengine wanaweza kujishambulia kwa maneno yao mwenyewe, kivipi? Unaweza kumkuta mtu anajiambia kuwa mimi ni mjinga sana huyu hajamshambulia mtu bali kajishambulia mwenyewe. Sasa je! wewe unaongeaje?.

Wakati wa kupika pika vizuri, ukiongea ongea vizuri na hata ukitembea tembea vizuri pasipo kumgonga mwingine. Unakuta mtu kwa kuwa anagari basi anapoendesha hajali hata kuwa kuna mtu anatembea kwa mguu anammwagia maji, huko ni kutokuzingatia.

Imani siyo jinsi unavyofunga na kuomba bali ni jisi gani vile unavyotenda.  Unapo tenda vyema unapata kibali.

Mungu akiona unafanya vizuri ndipo sasa anaruhusu imani ya msalaba kufunuliwa kwako, kwa sababu hauwezi kupata siri ya msalaba kabla haujazingatia.

Kwa jinsi unavyozingatia Neno la Mungu  ndivyo ibilisi anasalimu amri kwako, lakini usipokuwa na muda na biblia  au kujifunza Neno la Mungu basi ibilisi atakuwa na muda wa kukuchezea.

Mhubiri 7:29 “Tazama, hili tu nimeliona; Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu, lakini wamebuni mavumbuzi mengi.” Mungu ametufanya sisi viumbe vyake wakamilifu sana lakini nini kimetokea? Kutokuzingatia ndiyo kumetuharibu.

Tukijifunza kuzingatia imani yetu ya msalaba itafanya maajabu. Ukiamua kuzingatia leo hii utaiona safari.

Unapoanza kuzingatia ndivyo mambo yatakavyo kwenda, unahitaji kuzingatia lakini usipo zingatia hata ukaalika waombaji wa dunia nzima wakuombee hakuna jambo litatokea kwako.

Watu wengi  wanafikiri  kuwa wakienda kuombewa na watu wanaofanya miujiza mambo yatatokea, sikia nikwambie Mungu hajibu kwa sababu umeombewa na mtu wa aina hiyo bali Mungu atakujibu maombi yako kwa sababu umezingatia.

 

NENO LA MSALABA.

 


Usichezee maisha yako ya wokovu uliyonayo kwa sababu hayo maisha yako yaligharimu uhai wa Yesu.

1 Wakoritho 1:18 “Kwa sababu Neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. ”

 

Hapa duniani iko misingi mingi ya kufanya vitu vitawale na kuinuka, lakini kwa wokovu, ukombozi, uzima wa milele, miujiza, maajabu, uponyaji na baraka kwa wanadamu Neno la msalaba ndio msingi pekee. Pasipo Neno la Msalaba miujiza na maajabu ni bure, usipokuwa na Neno la Msalaba kamwe hauwezi kuwa na muujiza wala Baraka za kudumu, hivyo inamaana kuwa msingi wa Imani yetu upo katika NENO la MSALABA.

 

Neno la Mungu linadhihirika katika Neno msalaba. Nguvu ya Msalaba ilianza katika kipindi cha Musa, Wana wa Israel walipokuwa katika safari ya kutoka Misri kwenda Kaanani, walipofika mahali nyoka wamewazingira na kila atakayeng’atwa na hao nyoka alikufa pale pale na hakukuwa na dawa yoyote ya kuwaponya. Ndipo Mungu akamwambia Musa aweka msalaba na mtu yeyote atakayeng’atwa na hao nyoka aje na kuutazama huo msalaba na atakapoutazama ataponyeka. Ndipo watu waliukimbilia huo msalaba nao waliponyeka na sumu ya nyoka haikuwadhuru.

 

Neno la msalaba linaweza kuharibu sumu ya aina yoyote ile. Wana wa Israel waliukimbilia msalaba nao wakaponyeka lakini wale waliokuwa wanaangalia zaidi kule kung’atwa na kusikilizia maumivu ya hao nyoka walikufa pale pale lakini wale waliong’atwa na nyoka na wakaanza kukimbilia ule msalaba waliponyeka.

Haijalishi upo mbali kiasi gani lakini katika uweza wa ufahamu wako ukatambua kuwa kuna msalaba mahali nawe ukaamua kuutazama utaponyeka.

1 Wakoritho 1:18 “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. ”

Wana wa Israel wakati wanaukimbilia ule msalaba ile nguvu iliyokuwa kwenye msalaba ilikuwa inawaponya, je wewe unafahamu nini kwenye msalaba?

Wana wa Israel walioamini kuwa katika msalaba kuna nguvu, uponyaji na ukombozi uliwajia kwenye miili yao nao walikombolewa.

Ili kuipata Nguvu ya msalaba inategemea jinsi ulivyoelewa siyo tu kwa jinsi unavyoongea bali unafahamu nini.

Nguvu ya msalaba ni ya muhimu sana zaidi ya ombi lolote lile, kwa nini? Kwa sababu ombi lolote haliwezi kusikiwa pasipo Neno la msalaba, kwa sababu Neno la msalaba lilituleta karibu na Mungu na hilo Neno la msalaba likatusababisha tusikiwe na tukubaliwe. Neno la msalaba limetusababisha sisi tupate kibali, tuwe wa thamani machoni pa Mungu, pasipo Neno la Msalaba sisi si kitu machoni pa Mungu, lakini kupitia Msalaba sisi ni wa thamani.

• Neno la msalaba limetufanya sisi tuwe washiriki wa vitu vya Mungu.

• Neno la msalaba limetufanya tuwe ni watu wa pekee, watu wenye maana tuliyoondoka kwenye upumbavu.

• Neno la msalaba lilibadilisha mtazamo na mawazo yetu na tukawa wenye hekima. Ni neno la msalaba pekee linaloweza kukufanya kuwa mwenye hekima.

• Neno la msalaba limeleta upatanisho kati yako na Mungu na kati yako na wenzako kwa sababu katika hilo unaweza kusema nampenda Mungu na Mungu ananipenda.

• Neno la msalaba limefanya dhambi yako kusamehewa na sasa uko chini ya Rehema za Mungu.

• Neno la msalaba limekufanya uwe mshiriki wa Neema ya Mungu, haijalishi una upumbavu wa aina gani au ulitenda uovu kwa kiasi gani lakini kwa kuukubali msalaba unatakaswa na kusafishwa nawe unakuwa mweupe kama theluji.

• Kwa sababu ya neno la msalaba unakuwa huru na hukumu na hakuna mwenye nguvu ya kukuhukumu kwa sababu Neno la msalaba limeiondoa hukumu yako.

• Neno la msalaba linakutoa nyuma na kukupeleka mbele, hakuna kushindwa tena bali kuna ushindi tele.

• Neno la msalaba linakuondoa kwenye laana na kukuingiza kunako Baraka za Mungu.

• Neno la msalaba linakuondoa kwenye uadui na Mungu mpaka kukuingiza kwenye uwana.

• Neno la msalaba linakutoa kwenye kifo na kukuingiza kwenye uzima.

• Neno la msalaba linakufanya wewe uwe mshiriki wa mambo ya rohoni pamoja na Mungu, yaani unakuwa na uwezo wa kushiriki nguvu ya Mungu.

Ikiwa umeitambua nafasi yako kwa sababu ya msalaba basi unaweza kubadilisha kila kitu na kuwa vile unavyotaka uwe.

Kwa nini watu wanakuwa na mapepo wakati wamezaliwa mara ya pili? Sielewi kwa nini watu bado wanahangaika au wanasumbuliwa na wachawi wakati watu hao wamezaliwa mara ya pili? Nimekuja kutambua kwamba hawaelewi Nguvu iliyopo ndani ya msalaba.

Siku ulipomjua Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yako kuna mambo mawili yalitokea:

1. Yesu alifanyika kuwa Bwana kwako wewe,

2. Yesu akawa Mfalme wa wafalme, akitawala mbingu na nchi hivyo Yeye ni amiri jeshi mkuu mbinguni na duniani, akiamrisha kila kitu kipate kwenda. Yeye akafanyike kuwa Mfalme wa wafalme kwako wewe, kupitia msalaba unapaswa kufahamu hilo. Kwa sababu katika msalaba tunafahamu nguvu ya ufalme.

Kupitia msalaba umesamehewa, ikiwa kuna hukumu, laana, lalamiko lolote au jambo la kudhuru lolote kwa sababu ya huo msalaba wewe siyo sehemu ya hayo. Haijalishi watu wanasema nini au wanafanya nini hakitakudhuru, ukilitambua hilo katika akili yako uko huru. Ibilisi anaogopa ufahamu wako na siyo maombi yako, je! Unajua nini? Kile unachokijua kitakufanya wewe kuwa mwenye nguvu na siyo kwa jinsi gani unafunga na kuomba, kwa sababu unaweza ukafunga lakini bado uko kwenye mateso na funga yako ikawa haina maana.

Wokovu ulikufanya wewe usamehewe na huo msamaha umesababisha ukaponyeka, ukilijua hilo uponyaji utatiririka mwilini mwako.

Usipojua Neno la msalaba utahangaika huku na kule ili kukusanya maombi, utatafuta unabii ili upate kujua Mungu amesema nini kuhusu wewe unasahau kuwa wewe ni msemaji wa Mungu.

Msalaba umekufanya kuwa mwakilishi na balozi wa Mungu hapa duniani, jitambue na uishi katika huo utayaona maajabu ya Mungu.

Nani alikwambia wewe si kitu? Ni kwa sababu ya ujinga wako ndiyo maana ibilisi akachukua nafasi ya kukupeleka huku na kule, kwa sababu haujajua nguvu iliyopo ndani ya msalaba.

Nguvu ya msalaba inaondoa uovu kwako, ukiwepo uovu wa aina yoyote ile wewe unakuwa huru kwa huo, hivyo usimuache ibilisi akulaumu kwa mambo yaliyopita. Usimuache ibilisi akwambie kuwa ulikuwa unaenda kwa wachawi hadi unalala huko au ulifanya hiki na kile, mwambie kuna mtu mmoja (Yesu) alimalizana na hayo , alilipa deni zangu zote za dhambi sidaiwi tena, mimi ni mrithi wa mambo ya Mungu.

Fahamu msingi wa imani na wokovu wako, ni upi huo? Msalaba.

Unapoujua msalaba basi kuhangaika kwako kumekoma, nguvu ya msalaba itakuondoa kwenye kuhangaika mpaka kukufikisha mahali penye vitu vyenye mashiko.

Yeyote anayejifungamanisha na huo msalaba maisha yake yanabadilishwa, unapojifungamanisha na msalaba maisha ya kung’ang’ana yanakoma na sasa unakuwa mshindi.

KIRI:

• Kuanzia sasa nakataa kujua mambo mengi mpaka pale nitakapojua siri ya nguvu iliyopo katika msalaba.

• Nitatumia nguvu zangu zote kujifunza siri iliyopo ndani ya msalaba kwa sababu nataka nilete badiliko juu ya maisha yangu.

Msalaba unakuletea mambo yaliyokuwa mbali na kuyasogeza karibu na wewe.

Kupitia msalaba kung’ang’ana kwako kunakoma, unachotakiwa kujua ni kwamba Yesu alilipia mahitaji yako yote hakuna kilichosalia. Chakula chako, nyuba yako, gari yako, ada ya shule, namna ya maisha yako yamekwisha kulipiwa.

JE! UNAPATAJE UNACHOKIHITAJI?

1.      Jifungamanishe msalabani, kwa jinsi gani? 1 Petro 2:1-2 “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;”   Kubali kwamba wewe ni mtoto na uanzie kutoka hapo.

·         Mtoto lazima ajifunze kula, kutembea, kusema n.k, hivyo unapo zaliwa mara ya pili ni lazima ujifunze jinsi ya kuenenda kiroho na msamiati wa kiroho kama vile mtoto ajifunzaye lugha ya mama na wewe pia lazima ujifunze lugha ya mbinguni, hapa haina maana kunena kwa lugha, hapana! bali inamaana ni kusema mambo ya Mungu na kulisema Neno.

·         Jifunze kula, kwa jinsi gani? Kusoma Biblia na vitabu vya watumishi wa Mungu waliyotiwa mafuta.

·         Jifunze namna ya kuenenda, hii inamaana kuwa acha kwenda pale ulipopazoelea bali nenda pale Neno linapohubiriwa.

·         Mwana hutamani kumsikia mama yake, na wewe pia tamani kumsikia mtumishiwa Mungu ili upate kusikia Neno la Mungu.

·         Jifunze kuzingatia maelekezo,

Unapookoka unatakiwa kufanya kazi ya kujiugamanisha, unajiungamanishaje? 1 Petro 2:1-2 “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;

WALIOPOTEA NA WALIOOKOLEWA.

 


1 Wakorintho 1:17-18 “Maana Kristo hakunituma ili nibatize, bali niihubiri Habari Njema; wala si kwa hekima ya maneno, msalaba wa Kristo usije ukabatilika. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.”

Neno la msalaba kwa wanaopotea ni upuuzi lakini kwa wale waliookolewa ni nguvu ya Mungu.

 

Wanaopotea inamaana ni kupoteza, anafifia, hayupo tena, haonekani, yaani hapatikani tena, kwake yeye Neno la Msalaba ni upuuzi kwa maana kapotea na haonekani. Kwa wale wanaopotea ambao hawawezi kuonekana wala kuwepo Neno la Msalaba ni upuuzi.

Je! wewe umepotea? Kama unaliona neno la Mungu ni upuuzi inamaana kuwa umepotea, amua kurejea katika nafasi yako ili uweze kumuona Mungu.

Yeyote aliyepotea ni mjinga, kwa nini? Kwa sababu kama angekuwa na hekima usingepotea bali angeijua njia ambayo anatakiwa kuiendea.

Kupotea haina maana ya kupotea kimwili bali ni kiakili, akili yako ikiwa imepotea tutajua kwa kuutazama mwili wako. Warumi 1:28 “Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.”

Waliopotea ni watu wanao kataa au kuzira kazi. Ukimkataa Mungu na Yeye atakukataa pia, lakini ukimkubali haijalishi wewe ni mdhambi kiasi gani Mungu atakukubali kwa sababu umekubali kumfuata Yeye.

Waliopotea wana akili mbovu na ya kipumbavu na akili zao zimeharibika tayari kwa sababu wamemkataa Mungu katika akili zao. Utajuaje? Kwa sababu kunakuwa hakuna muendelezo katika maisha yao hivyo wanakua wamepotea.

Mara zote na wakati wote waliyopotea wana mateso mengi, waliopotea hawafanyi chochote, Yohana 15:5 “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.

Unaweza ukawa umezaliwa mara ya pili (Umeokoka) lakini umepotea, unasema kwa kinywa chako kwamba umezaliwa mara ya pili lakini bado unafanya kinyume na yale unayoelekezwa kwa nini? Kwa sababu Biblia inasema “pasipo mimi ninyi hamuwezi neno lolote” waliopotea hawawezi kufanya chochote, hawamvutii mtu yeyote wala kumsaidia yeyote Kwa sababu wamepotea.

Kama haumvutii wala kumsaidia yeyote na haufanyi chochote basi wewe umepotea, unapaswa ufahamu kwamba kupotea au upotevu upo kwenye akili.

Ukikubali Bwana atakubaliana na wewe kwa sababu yeyote aliyekubali ni mtii lakini ukikataa au kupinga basi wewe umepotea na aliyepotea hafanyi lolote lakini kama unafanya jambo basi haujapotea na kama haujapotea inamaana kuwa Mungu yupo pamoja nawe.

Kama haujapotea hii ndiyo ishara Daniel 11:32b “lakini watu wamjuao Mungu wao watakuwa hodari, na kutenda mambo makuu.” Wale wanaomjua Mungu wao ambao hawajapotea watakuwa hodari, majasiri, wanahekima na watakuwa ni werevu, hii inamaana kuwa wale waliopotea ni wajinga, hawafanyi chochote na kamwe hautawaona.

Na kutenda mambo makuu” Je! wewe unafanya nini ambacho ni kikuu? Watu wamjuao Mungu wao ni watu madhubuti, watu wakuu na wanajulikana, kwa nini? Kwa sababu matendo yao yanatangulia mbele yao.

Wao ni watu wakuu wanao saidia wengine na wanamjua Mungu wao. Usiseme unamjua Mungu wakati wewe ni mpumbavu, maskini, mgonjwa na unamilikiwa na mapepo ya kila aina.

Mungu wetu hadhihakiwi, chochote apandacho mtu atavuna, kama ukimkataa Mungu na YEYE atakukataa lakini ukimkubali na YEYE atakukubali, ukimpenda na YEYE atakupenda, ukiyatoa maisha yako kwake na YEYE atayatoa naisha yake kwa ajili yako, ukimpa pesa na YEYE anakupa pesa zake, ukiitoa nguvu yako kwa ajili yake na YEYE atautoa uhai wake kwa ajili yako hivyo kamwe hautakaa uugue, maradhi na magonjwa hayatakupata, chochote utakachopanda ndicho utakachovuna. Je! Wewe unampa Mungu nini katika maisha yako?.

Waliyopotea wameshindwa, hakuna chochote huku duniani kwa wanadamu ambacho ni hatari kama kushindwa, dhambi haina nguvu kama kushindwa, ibilisi hana nguvu kama kushindwa, lakini kushindwa kunakuwa na nguvu sana kwako kama wewe umepotea. Hakuna kinachoweza kuharibu watu na maisha yao kama kushindwa.

Hakuna kitu huku duniani kinaweza kuabisha watu kama kushindwa, kama wewe ni mtu wa kushindwa basi kudhihakiwa, matusi n.k, ni yako.

Hauwezi kumdhihaki mshindi bali utamsifu na kumpongeza na tena utampa na zawadi, lakini hauwezi kufanya hivyo kwa walioshindwa na ndiyo maana wao ni masikini.

Utajiri na mali ni sehemu ya zawadi na ndiyo maana wanazipata wale waliyoshinda. Hauwezi kuongeza faida kwa aliyeshindwa, aliyeshindwa hapandi daraja.

Umebaki katika nafasi hiyo hiyo uliyonayo kwa sababu umeshindwa, upo kwenye cheo kile kile miaka nenda rudi kwa sababu umeshindwa, na haya yote yanatokea kwako kwa sababu umekataa katika akili yako kuwa na Mungu.

Watu wote waliyoshindwa ni wezi, kwa nini? Kwa sababu hawana chakwao hivyo wanaiba.

Aliyeshindwa hafanyi lolote na hawezi kuzalisha chochote, anaweza akafungua duka lakini hilo duka lazima life, kwa nini? Kwa sababu ameshindwa.

Magonjwa siku zote hayamtafuti mshindi bali yanamtafuta aliyeshindwa,

Wewe unamagonjwa kama kisukri na presha je! umeshindwa ndiyo, umechelewa kuolewa au kuoa kwa sababu umeshindwa, umempa taraka mke wako kwa sababu umeshindwa, kwa maana kama wewe ni mshindi usingefanya hivyo, kwa nini? Biblia inasema “yote yawezekana kwake yeye aaminiye” na tena akasema; “nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”, umeshindwa kwa sababu hauna Mungu hichi ndiyo namba moja, kwa maana YEYE amesema pasipo YEYE sisi hatuwezi lolote.

Kushindwa ni kitu hatari sana kuliko kitu chochote huku duniani na yeye ndiye adui yako mkubwa kuliko kitu chochote.

Kushindwa mara moja kutafungulia mlango mwingine wa kushindwa zaidi, haijalishi unafunga na kuomba kwa kiasi gani.  Mara zote aliyeshindwa ana ubishi na kulalamika kwingi kwa sababu kashindwa.

Aliyeshindwa anamaneno mengi lakini hafanyi lolote. Aliyeshindwa hana maono na mara zote anahitaji mtu wa kumsimamia kwa maana hawezi kujisimamia mwenyewe.

Aliyeshindwa anatembea pamoja na ibilisi kwa sababu ibilisi ni wakushindwa namba moja na kamwe hawezi kushinda.  Kwa sababu umepotea na ndiyo maana unaishia kushindwa, unashindwa kwenye ndoa, biashara kwa sababu umeshindwa.

Kama umezaliwa mara ya pili je! Umepata msaada gani na huo wokovu? Watu wengi wameokoka lakini wako vile vile na wengine wamekuwa ni wakushindwa zaidi kuliko hata walivyokuwa hawajaokoka.

Kama umezaliwa na mtu aliyeshindwa lazima hiyo roho ikupate wewe kwa sababu kushindwa kunakuwa kupo katika akili yako kwa sababu akili yako ni sehemu ya akili ya baba yako.

Kushindwa sio kwa ajili yako kwa sababu umeamua kumsikiliza Mungu, Mungu ameahidi kuwatoa watu wake kunako mahangaiko, na kwa sababu umeamua kumsikiliza Mungu na Yeye anakutoa kunako kushindwa, kushindwa sio kwako, kamwe hutaangamia kama Baba yako au mama yako, hautaangamia kama maskini, kuna jambo linatokea kwako, kata hali ya kushindwa.

Utapata kile unachokihitaji, haijalishi madaktari walitamka nini juu yako tambua kuwa utaponyeka, haijaishi umri wako umeenda lakini utapata mtoto, haijalishi umetamkiwa nini nyumbani kwenu labda wamesema kuwa  hautaolewa utakwenda kuolewa kwa Jina la Yesu.

Uponyaji wako ni leo na sio kesho hivyo pokea huo uponyaji wako, uponyaji ni wako, umeishi na maradhi kwa muda mrefu wewe sio mshindwa Yesu alikufa kwa ajili yako ili upate ushindi.

Tangaza: Sitaangamia kwa magonjwa, roho ya kushindwa sio yangu, ibilisi mimi sio sehemu yako bali mimi ni wa Yesu aliyekushinda na roho ya ushindi inaishi ndani yangu.

 

JINSI GANI UNAWEZA KUTOKA KWENYE KUSHINDWA

Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”  Hapa panazungumzia namna ya kushinda kutoka kwenye kushindwa, unashinda kwa kupitia:-

·         Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo”Unaweza kushinda kwa damu ya Yesu, hii inamaana kuwa tunatakiwa kutubu.

·         “Kwa neno la ushuhuda wao;” tumia maneno ya kinywa chako kama shuhuda na siyo kutamka maumivu bali kwa kutamka ushuhuda wako, upi huo? Ushindi wa Kristo Yesu, huu ndiyo unatakiwa kuusema, matamshi yako ni yamuhimu sana.

Usizungumzie kushindwa na madhaifu yako kwa sababu ukiuzungumzia ushindi wa Yesu unauweka kama mbegu ndani yako, ni mbegu ipi hiyo? Ya ushindi, lakini ukiongea madhaifu yako yanakuwa kama mbegu ya kushindwa ndani yako hivyo usiyaongelee hayo. Ndiyo wakati mwingine umezungukwa na hayo lakini usiyaseme bali yapuuze kama vile hayapo.

Tunatakiwa tuseme yale yasiyoonekana kwa maana yake yasiyoonekana yana nguvu kuliko yanayoonekana, ongelea kuhusu ushindi wa Yesu, unapoongea hauuoni lakini chochote unachotamka kupitia huo ushindi kinakuwa.

·         Ambao hawakupenda maisha yao hata kufa” Hii inamaana kuwa jitoe, nguvu zako, pesa yako na mwili wako kwa ajili ya ushindi wa Kristo.

Nani tunatakiwa tumshinde?

Isaya 14:12  “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!” jina lake ni lucifer yeye ni yule aliyeanguka, hii inamaana pia hata ibilisi alishindwa na kushindwa. Hii inamaana kuwa kushindwa kuna nguvu kuliko hata ibilisi mwenyewe kwa maana hata yeye alikutwa na ile nguvu ya kushindwa, alitaka kuinuka juu lakini ile nguvu ya kushindwa ilimchukua na kumshusha chini, roho ya kushindwa ni hatari sana.  Usiipuuze hiyo nguvu ni hatari sana kwa sababu kushindwa mara moja kutakupelekea kushindwa kwingine na kwingine, haijalishi wewe ni mwelevu kiasi gani utaishia kupoteza.

Mungu akakuondolee hali ya kushindwa.

Kushinda na kushindwa.

Chochote ufanyacho hakikisha unafanya kwa UAMINIFU na UPENDO na Mungu atakuwa pamoja na wewe.

Leo hii unaona watu wengi wanaacha kazi ya Mungu na kufuata matakwa yao wenyewe wengine ni wachungaji kabisa hii ni kwa sababu ule mwisho umekaribia. Yesu anakaribia sana kurudi hivyo hakikisha chochote hakikutoi kwake, wewe uliyeamua kumfuata Mungu usibadilike, zingatia kunako Mungu utapewa thawabu siku moja utakapofika Mbinguni.

Adamu alipoumbwa aliumbwa na ushindi ndani yake, kwa sababu aliumbwa na kushinda akawa ni kiumbe cha tofauti kuliko vyote vilivyoumbwa na ndiyo maana hata Mungu alipoumba wanyama alimletea ili awape majina.

Wakati Adamu anaumbwa hakuumbiwa kushindwa bali aliumbiwa ushindi ndani yake, tunapo zungumzia kushinda maana yake ni uwezesho au ile hali ya kuweza.

Mwanadamu huyo aliyeumbwa aliwekwa mahali hakuna jembe, nyumba wala kitu chochote lakini kwa sababu aliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na ile roho ya ushindi iko ndani yake na vitu vyote aliviweka ndani yake, yaani Mungu alikuwa na maana huyo mwanadamu afanye kama Mungu.

Mwanzo1: 26-27 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. ”

Lakini pamoja na kuwa huyo mtu alitoka katika udongo Mungu aliweka uungu wake kwa huyo mtu ili aweze kuwa na uwezesho wa kufanya kama Mungu, hiki ndicho kinaitwa ushindi. Hivyo hauwezi kushinda chochote kama Mungu hajakuwezesha.

Ukienda ukamuibia, ukamuua au kumdhulumu mtu siyo kwamba wewe ni mshindi, hapana bali wewe umeruhusiwa kufanya hivyo kwa hukumu yako maana yake ni kuwa Mungu amekukasirikia na ameruhusu ufanye hivyo ili akuhukumu.

Mithali 16:4 “Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake; Naam, hata wabaya kwa siku ya ubaya.” Tazama Mungu amefanya kila kitu kwa makusudi, ukiona umemfanyia ubaya mtu na ukafanikiwa usishangilie maana Bwana amefanya hivyo ili apate kukuhukumu kwa maana ndani yako kuna uovu.

Wewe uliumbwa ukiwa na ushindi ndani yako na ushindi huu hauanzi leo bali unaanzia siku ulipoingia tumboni mwa mama yako. Kwa maana kuna mbegu nyingi zinazoingia lakini wewe ulifanikiwa kushinda na kuingia katika tumbo la uzazi kwa sababu ulikuwa na roho ya ushindi. Wewe uliweza kudumu katika tumbo la mama yako pamoja na misukosuko mingi lakini mimba yako haikuharibika ni kwa sababu ulikuwa na roho ya ushindi.

Kiumbe chochote kilichoumbwa kiliumbwa na ushindi, mfano Kuku anataga mayai yake kisha anayaatamia, kuku hayapasui mayai yake mwenyewe ili kifaranga chake kitoke bali kifaranga chenyewe kikifika wakati wa kutoka kinapasua yai lake chenyewe kisha kinatoka, ni kwa sababu ndani yake kuna nguvu ya ushindi. Mungu ndiye anayeweka ushindi ndani ya mtu au kiumbe.

Ushindi ni roho toka kwa Mungu, ukishinda jambo lolote mrudishie Mungu utukufu kwa maana siyo kwa uweza wala nguvu zako.

Katika ulimwengu huu kama kuna gumzo au mpambano mkubwa ni kati ya kushinda na kushindwa.

Mashindano yoyote yanayofanyika huku duniani wanatafuta nini? Wanataka kuona mshindi na aliyeshindwa, kama kuna mtihani wowote ule ni kwa sababu wanataka kuona mambo haya mawili tu mshindi na mshindwa, kama kuna mapigano katika uwanja wa mapambano wanatafuta nini? Wanataka kuona mshindwa na mshindi.

Hata katika hospitali wauguzi na madaktari wanafanya vipimo ili nini? Wanafanya ili kuona mshindi na mshindwa na ndiyo maana wanapima damu n.k wanataka kuona ni kipi kimeshindwa katika mwili wako ili wakifanye kishinde.

Ibilisi hana nguvu, bali yeye anachokifanya ni kumtafuta aliyeshindwa ili apate kumtumia, ibilisi hana nguvu ya kufanya chochote huku duniani bali anawatafuta watu waliyoshindwa ili awatumie. Ibilisi hakutupelekea kwenye hukumu ya kifo bali Hawa ndiye alifanya hivyo na ndiyo maana ukiangalia wakati Mungu anatoa hukumu hakumuangalia ibilisi bali alimuangalia Adam na Hawa kwa sababu hao ndio chanzo cha hiyo vurugu.

Ibilisi yeye alifanya nini ? Alimuendea Hawa na akatafuta udhaifu wake ili apate kusababisha kushindwa ili yeye achukue nafasi, ibilisi aliona udhaifu wa Hawa na akamtumia ili kusababisha kushindwa ili aweze kushambulia kizazi cha wanadamu.

Ibilisi yeye hakula lile tunda bali Hawa na Adamu ndio waliokula, ibilisi hana nguvu ya kukushusha chini bali atatumia udhaifu wako.

Mungu hatafanya chochote kwako mpaka atakapoiona imani yako na siyo udhaifu wako, kama ibilisi akiuona udhaifu wako na akiona kuwa hauwezi kuushinda huo udhaifu basi atakutumia. Kuna watu wengine wana udhaifu mahali fulani lakini hawaruhusu kushindwa na huo udhaifu wao. Kamwe usimruhusu ibilisi atumie udhaifu wako ili kukushusha chini.

Nguvu ya USHINDI inatoka kwa Yesu Kristo na nguvu ya kushindwa inatoka kwa ibilisi.

Yohana 1:5 “Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Nuru ni Neno na hilo Neno ni Yesu Kristo. Nuru ina Nguvu ambayo tunaiita ushindi nguvu hiyo imo ndani ya hiyo Nuru.

Kushindwa ni nini? Ufunuo 12:7-9 “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.”

Ibilisi alikuwa ameshindwa toka mwanzo, mshindwa mara zote atadumu kuwa mshindwa, ni nani huyo? Ni ibilisi, ibilisi ameshindwa; ameshindwa na nini? Na nguvu ya USHINDI.

Kama una NGUVU ya USHINDI ibilisi kwako anakuwa mshindwa na kamwe hatakaa akushinde bali atabakia kuwa mshindwa kwako milele.

Mshindwa kamwe hataweza kushinda kitu chochote na ndiyo maana unaweza kuona mtu anashindwa katika kila kitu anachokifanya anashindwa kwa nini? Kwa sababu yeye ni mshindwa. Washindwa wote ni wa ibilisi na hawaendi mbinguni.

Kama ulishawahi kushindwa amua kugeukia nguvu ya kushinda ili uondokane na kushindwa.

UTAKUWAJE MSHINDI?

1. Kama haujawahi kuwa mshindi kwa lolote ambalo unataka kuwa mshindi, tafuta toba ya kweli.

2. Tunza na utimize yale yote uliyo tamka kwa sababu wengi wanasema kingine na wanafanya tofauti na ndiyo maana wanakuwa wa kushindwa wakati wote. Kumbukumbu 23:23 “Yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya; kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, ni sadaka ya hiari uliyoahidi kwa kinywa chako.” Mambo unayotamka ni kama sadaka, fanya kwa moyo na uyatimize.

Tii neno lako na heshimu neno lako, 1 Timotheo 4:16 “Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia.” Ni namna ya kujiokoa mwenyewe na madhara kwa sababu kinywa chako kinaweza kukutia katika madhara hivyo linda kinywa chako na ujaribu kutimiza kile unachonena na hivi ndivyo utakuwa mshindi.

3. Ishi maisha ya kukubali na kumtii Mungu. Isaya 1:19 “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi;

4. Ishi kwa kuzingatia upate ukufanya vizuri maana utamshinda huyo akuviziaye. Mwanzo 4:7 “Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JINSI YA KUMSHINDA SHETANI

NGUVU YA DAMU YA YESU

VIPAJI VYA ROHO MTAKATIFU