Historia ya Wokovu
Jinsi Pietro
Perugino alivyochora Mateso
ya Yesu msalabani kwa mtindo wa Stabat Mater,
yaani akiwa na Bikira
Maria na Mtume Yohane chini
yake (1482). Kifo na ufufuko wa Yesu ndiyo
kilele cha historia ya wokovu kwa imani ya Ukristo.
Kwa jina hilo Wakristo wanamaanisha ufafanuzi wa mpango wa kazi ya Mungu kwa wokovu wa binadamu kadiri ya Biblia.
Yaliyomo
- 1
Maana ya historia
- 2
Maana ya wokovu
- 3
Imani kuhusu Biblia
- 4
Agano la Kale
- 4.1 Vitabu vitano vya Torati
- 4.2 Uumbaji
- 4.3 Dhambi ya asili
- 4.4 Watu walivyoishi baada ya dhambi
- 4.5 Nuhu
- 4.6 Mnara wa Babeli
- 4.7 Abrahamu (1900-1800 hivi K.K.)
- 4.8 Watoto wa Isaka: Esau na Yakobo
- 4.9 Yosefu na ndugu zake kushukia Misri (1700 hivi K.K.)
- 4.10 Utumwa wa Misri na wito wa Musa (1250 hivi K.K.)
- 4.11 Mapigo ya Wamisri
- 4.12 Safari ya kuendea Nchi ya ahadi
- 4.13 Agano la Mlima Sinai
- 4.14 Ndama ya dhahabu
- 4.15 Mungu kujifunua tena kwa Musa
- 4.16 Mambo ya Walawi
- 4.17 Hesabu
- 4.18 Kumbukumbu la Torati (Sheria)
- 4.19 Vitabu vinavyofuata Kumbukumbu la Torati (Sheria)
- 4.20 Yoshua (1210-1200 hivi K.K.)
- 4.21 Waamuzi (1200-1025 hivi K.K.)
- 4.22 Ruthu
- 4.23 Samweli (1050-1015 hivi B.C.)
- 4.24 Mfalme Sauli (1030-1010 hivi K.K.) na mfalme Daudi (1010-970
hivi K.K.)
- 4.25 Vitabu vya Wafalme
- 4.26 Mfalme Solomoni (970-931 hivi K.K.)
- 4.27 Manabii
- 4.28 Manabii Eliya na Elisha (865-790 hivi K.K.)
- 4.29 Nabii Amosi (786-746 hivi K.K.)
- 4.30 Nabii Hosea (750-725 hivi K.K.)
- 4.31 Nabii Isaya (740-700 hivi K.K.)
- 4.32 Nabii Mika (740-700 hivi K.K.)
- 4.33 Nabii Sefania (640-625 hivi K.K.)
- 4.34 Nabii Yeremia (626-585 hivi K.K.)
- 4.35 Nabii Habakuki (600 hivi K.K.)
- 4.36 Nabii Ezekieli (592-570 hivi K.K.)
- 4.37 Isaya II na III (550-500 K.K. hivi)
- 4.38 Wayahudi kuanza upya Yerusalemu chini ya Waajemi (538-333
K.K.)
- 4.39 Manabii wa mwisho wa Agano la Kale
- 4.40 Vitabu vya Hekima vya kwanza
- 4.41 Uenezi wa utamaduni wa Kiyunani (333-63 K.K.)
- 5
Agano Jipya
- 5.1 Mazingira ya Yesu
- 5.2 Maisha ya Yesu
- 5.3 Ufunuo kuendelea baada ya ufufuko wa Yesu
- 5.4 Kitabu cha Matendo ya Mitume
- 5.5 Kanisa la Yerusalemu
- 5.6 Ukristo ulivyoanza kuenea
- 5.7 Safari za kimisionari za
Paulo zilivyoanza (46-49)
- 5.8 Mtaguso wa Yerusalemu (49)
- 5.9 Barua au nyaraka
- 5.10 Safari ya pili ya Mtume Paulo (50-52)
- 5.11 Barua mbili kwa Wathesalonike
- 5.12 Safari ya tatu ya Mtume Paulo (54-58)
- 5.13 Barua kwa Wagalatia
- 5.14 Barua kwa Wafilipi
- 5.15 Barua kwa Filemoni
- 5.16 Barua mbili kwa Wakorintho
- 5.17 Barua kwa Waroma
- 5.18 Ukristo baada ya Paulo kufika Roma
- 5.19 Barua kwa Wakolosai
- 5.20 Barua kwa Waefeso
- 5.21 Barua tatu za Kichungaji
- 5.22 Barua ya kwanza ya Petro
- 5.23 Barua kwa Waebrania
- 5.24 Injili Ndugu
- 5.25 Barua ya Yakobo
- 5.26 Barua ya Yuda
- 5.27 Barua ya pili ya Petro
- 5.28 Ufunuo wa Yohane
- 5.29 Injili ya Yohane
- 5.30 Barua tatu za Yohane
Maana ya historia
Historia ni mfululizo wa habari za mambo yaliyotokea pamoja na sababu zake.
Binadamu anaziandika ili kuelewa maisha yake, yaani ametokea wapi, amepata
mafanikio gani na matatizo gani. Historia inatufundisha kuishi: kumbukumbu za
mambo ya zamani (vita, uhuru, viongozi na mengineyo) zinatuwezesha kuendelea vizuri zaidi. Lakini ni
muhimu zaidi kujua mambo makuu aliyoyatenda Mungu ili kutuokoa. Dini ya Uyahudi na ya Ukristo ni dini zinazotegemea historia kuliko maumbile: Mungu hatazamwi kama Muumba tu, bali zaidi kama Mwokozi.
Maana ya wokovu
Wokovu ni kazi ya Mungu kwa ajili yetu (1Tim 2:4; 2Tim 1:9-10). Sisi hatuwezi kujikomboa, lakini Mungu ana nguvu kuliko shetani na mabaya yote, naye anatuhurumia sisi maskini (Kol 1:13-14). Mungu Alifanya nini ili kutuokoa? Hiyo Ndiyo historia ya
wokovu. Wapo walioiandika katika Biblia ili tusadiki na kuishi upya (1Pet 1:10-12). Humo mtu hatazamwi kama nafsi ya peke yake tu, bali zaidi kama mtu wa taifa lake; hivyo Mungu anatangazwa kuwa hashughulikii wokovu wa mtu binafsi
tu, bali wa mataifa mazima pia, kuanzia lile la Israeli. Aliyowatendea wao ni hasa kuwatoa utumwani Misri, kuwapa agano na masharti yake li awafanye taifa
huru katika nchi bora. Waisraeli walijenga imani yao juu ya hayo mang’amuzi ya msingi ya wokovu kutoka kwa Mwenyezi
Mungu, halafu wakajikumbusha kwamba alikuwa ameshawaahidia mababu wao baraka kama hizo. Hatimaye tu walitafakari juu ya asili ya watu na ya ulimwengu, wakaelewa kuwa Mungu aliweza kuwaokoa kwa sababu ndiye aliyeumba
vyote: hakuna wa kushindana naye na wa kuzuia mpango wake kwa ajili ya watu.
Kwa Wakristo tukio kuu lililo msingi wa imani ni ufufuko wa Yesu, aliyetoka kaburini mzima na mtukufu, wa kwanza kati ya umati, akaingia katika nchi ya walio hai kweli.
Imani kuhusu Biblia
Biblia iliyochapwa na Johannes
Gutenberg mwaka 1455 hivi. Ndiyo ya kwanza kutonakiliwa kwa mkono.
Wakristo wanasadiki Biblia imeandikwa kwa uvuvio wa Roho
Mtakatifu (2Pet 1.20-21; 2Tim 3:16): ndiyo sababu wanaiheshimu sana. Lakini habari zake hazifuati
mpangilio wa tarehe. Wapo wataalamu waliozipanga kwa utaratibu huo unaotupendeza zaidi siku
hizi: wamejitahidi kuelewa tarehe ya matukio na ya maandiko yote ili kuyapanga
moja baada ya lingine kuanzia ya zamani za kale hadi maisha ya Yesu na ya Mitume wake. Lakini tukumbuke daima kwamba lengo la Biblia si kueleza sayansi, jiografia wala historia, bali ni kufundisha kwa ukweli njia ya wokovu. Taarifa
nyingine zinategemea ujuzi wa mtu aliyeandika na mtindo alioutumia: sheria, taratibu
za ibada, nasaba, ufafanuzi wa majina, maneno matakatifu ya mahali fulani, baraka, hadithi, simulizi, historia halisi n.k.
Sehemu kuu mbili za Biblia ni Agano la Kale na Agano
Jipya (2Kor 3:10; Eb 8:13). La Kale limeandikwa kabla ya Yesu, Jipya baada yake. Hata hivyo
Agano la Kale lina utabiri mwingi juu ya Yesu (Lk 24:27,44), na Agano Jipya linarudia na kufafanua habari nyingi za kale:
hivyo tunatakiwa kusoma daima Agano la Kale kwa mwanga wa Agano Jipya, na
kutafuta katika habari za kale mifano inayotusaidia kuelewa mambo ya Yesu na Kanisa (1Kor 10:11; Kol 2:17). Kwa kuwa ufunuo wa Mungu ulifanyika hatua kwa hatua hata ukakamilishwa na Yesu (Eb 1:1-2), hatuwezi kutegemea dondoo moja tu kuhusu jambo fulani, bali
tuzingatie jambo hilo lilivyoozungumziwa tangu mwanzo hadi mwisho wa ufunuo.
Tunahitaji kujua Biblia nzima ili kuelewa jinsi Mungu alivyo, alivyotuokoa na
anavyotaka tuishi.
Vitabu vya Biblia ni 73: yaani 46 katika
Agano la Kale na 27 katika Agano Jipya. Ndivyo vilivyokubaliwa na Kanisa Katoliki kuwa ni Neno
la Mungu. Waprotestanti wengi wanakataa vitabu 7 vya Agano la Kale (pamoja na sehemu chache za
vingine): hivyo Biblia yao inavyo 66 tu.
Mgawanyo wa vitabu hivyo si muhimu, mradi
tusiongeze wala kupunguza neno. Kwa kawaida vinapangwa kwa kuzingatia vinaleta
habari za namna gani. Hivyo katika Agano la Kale yanatofautishwa makundi manne:
Torati (yaani sheria), vitabu vya historia ya Israeli, vitabu vya manabii (waliotumwa na Mungu ili kuwaonya na kuwafariji Waisraeli), na vitabu
vya hekima (vyenye nyimbo, mashairi, mithali n.k.). Katika Agano Jipya tuna
vitabu 5 vya historia (yaani Injili 4 na Matendo
ya Mitume), barua 21 za Mitume na kitabu kimoja tu cha
kinabii (Ufunuo).
Lugha asili ziko tatu, yaani Biblia
imeandikwa sehemusehemu kwa Kiyahudi, Kiaramu (ndiyo lugha ya Yesu), na Kiyunani (yaani Kigiriki cha zamani). Ila Agano Jipya lote limeandikwa kwa Kiyunani ambacho
zamani za Yesu kilikuwa lugha ya kimataifa. Kutoka lugha hizo wataalamu wanaendelea
kutafsiri Biblia katika lugha yoyote ili Neno la Mungu liwaelee watu wote. Kati
ya tafsiri zote, mbili za zamani zina sifa za pekee, yaani tafsiri ya LXX (kwa
Kigiriki "Septuaginta", yaani sabini: ni Agano Kale kwa lugha ya Kiyunani), na ya Vulgata (Biblia nzima kwa Kilatini).
Maelezo ya Kanisa yanahitajika kwa sababu:
kwanza mwenyewe sielewi maandiko hayo yameandikwa na nani, lini, wapi, kwa
lengo lipi na katika mazingira ya namna gani. Hasa Roho Mtakatifu hakunipa Biblia peke yangu, bali ndani ya taifa lote la Mungu. Hivyo
sina haki ya kuifafanua ninavyotaka. Wasio na elimu na msimamo wanapotosha
Biblia na kupotea (2Pet 3:16).
Agano la Kale
Vitabu vya Agano la Kale
Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli
I * Samueli II * Wafalme
I * Wafalme II * Mambo
ya Nyakati I * Mambo
ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo
IDK * Wamakabayo
IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki
Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.
Vitabu vitano vya Torati
Kitabu cha Torati katika Sinagogi la Cologne, Ujerumani.
Vitabu vya kwanza vya Biblia (Mwanzo, Kutoka, Mambo
ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu
la Torati) vinaunda kwa pamoja Torati (kwa Kiyahudi
“fundisho”, yaani “sheria”). Mgawanyo wa kawaida wa Kiyahudi wa vitabu vya
Biblia katika makundi matatu (Torati, Manabii na Maandishi) unaonyesha jinsi
vitabu vitano vya kwanza vinavyotazamwa kuwa kitu kimoja, tena kiini cha Agano
la Kale lote. Ajabu la Torati ni jinsi inavyounganisha mambo mbalimbali: ibada
kwa Mungu pekee, ahadi zake, matakwa yake, uasi wa binadamu na ukombozi wa Kimungu, wito wa kujali mwanzo wa taifa la Mungu.
Humo tunakuta muhtasari wa historia kuanzia uumbaji wa ulimwengu hadi kifo cha Musa: historia ya asili (Mwa 1-11), kipindi cha mababu (Mwa 12-36), simulizi la Yosefu (Mwa 37-50), ukombozi toka Misri na safari kwenye Sinai (Kut 1-18), toleo la sheria mlimani huko (Kut 19 – Hes 10), safari hadi mabonde ya Moabu (Hes 10-36) na nyongeza (Kumb 1-34).
Zamani Musa alidhaniwa kuwa mwandishi wa
vitabu hivyo vyote. Siku hizi wataalamu wamethibitisha kuwa ndiye asili ya
kiini cha sheria za Israeli, lakini vitabu hivyo viliandikwa katika kipindi kirefu hadi mwaka 400
hivi K.K. Ndiyo sababu katika sheria za vitabu hivyo yanaonekana mabadiliko
mbalimbali yaliyofanyika karne hadi karne, k.mf. kuhusu Pasaka na umoja wa hekalu. Waliohusika na uandishi ni watu wengi wa Israeli Kaskazini na Kusini.
Hasa yameainishwa mapokeo manne tofauti: J (yaliyoandikwa katika karne X K.K. kwa kumuita Mungu YHWH), E (ya karne
IX K.K. yanayomuita Elohim), D (yanayotawala
Kumbukumbu ya Torati: ni ya karne VII K.K.) na P (yaani ya kikuhani kwa kuwa yanajali sana ibada: ni ya karne
VI K.K.). Hayo ya mwisho yalitumika kama fremu ya
mapokeo hayo yote ili kuunganisha Torati nzima katika karne V K.K. Hivyo Torati inatunza matukio ya msingi na imani ya taifa la Israeli
jinsi ilivyozidi kukomaa baada ya Musa.
UUMBAJI
Uumbaji (1896–1902), mchoro wa James
Tissot.
Uumbaji unasimuliwa katika sura mbili za kwanza za Mwanzo. Kama vile sehemu
mbalimbali za Biblia, kitabu hicho kilitungwa kwa kushona pamoja maandishi
tofauti. Ndiyo sababu tunakuta masimulizi mawili juu ya Mungu kuumba ulimwengu
na watu.
La kwanza (1:1-2:4a) linamchora Mungu
akifanya kazi kama binadamu kwa siku sita halafu kustarehe. Aliumba kila kitu
kwa Neno lake (Eb 11:3; ndiye Mwanae pekee: Yoh 1:1-18). Wengine wanaona humo hata kidokezo cha kwanza cha Roho
Mtakatifu, aliye upendo wa Mungu, katika upepo uliovuma juu ya wingi wa maji.
Mungu aliona kila alichokiumba ni chema tu, lakini alipoumba mtu katika jinsia mbili akaona ni mwema sana, ni bora kuliko vingine, akamweka kuvitawala
kwa niaba yake. Mwanamume na mwanamke wana hadhi sawa kwa kuwa wote wawili ni
sura na mfano wake, si upande wa mwili, bali hasa kwa roho yenye uwezo wa kuelewa na kupenda kwa hiari.
Muumba anataka watu washirikiane na
kusaidiana, kilele cha uhusiano wowote kati yao ni ndoa inayowafanya kuwa mwili mmoja kama Kristo na Kanisa (Ef 5:31-32).
Simulizi linalofuata (Mwa 2:2b-25) ni la zamani zaidi, nalo pia lina mafundisho makuu juu ya
Mungu na mtu, hasa kwamba huyo ndiye kiumbe bora anayeweza kushirikiana na
Mungu tofauti na vingine. Hali yake asili ilikuwa ya kupendeza kabisa kwa usafi wa moyo na uhai usio na mwisho, naye alitakiwa akubali kazi za Mungu na kufuata
maneno yake, bila ya kujiamulia nini jema, nini baya.
Michelangelo
alivyochora katika kuta za Cappella Sistina huko Vatikano dhambi ya Adamu na Eva na adhabu
iliyofuata ya kufukuzwa bustanini.
Mwanzo 3 inasimulia dhambi iliyo asili ya dhambi zote (Rom 5:12). Kwa njia hiyo tunaambiwa hali yetu mbaya haitokani na Mungu,
bali na uasi wetu na wa wazee wetu (Hek 2:23-24). Pia tunafundishwa kukataa toka mwanzo vishawishi vyetu
tukiamini maagizo yote ya Mungu yametolewa kwa upendo mkuu. Shetani ndiye aliyeanzisha kishawishi. Eva alipaswa asimsikilize. Kosa lake la kwanza ni kumjibu: hivyo shetani
akamdanganya kwamba, eti Mungu ana kijicho, hataki watu walingane naye, ndiyo sababu aliwakataza (Yoh 8:44). Tukianza kuzingatia kishawishi tunakubali shaka juu ya wema wa
Mungu kwetu katika kutuelekeza. Kwa namna hiyo walianguka watu wa kwanza
waliokuwa watakatifu; kwa urahisi zaidi tutaanguka sisi wenye tabia
mbaya kutokana na dhambi hiyo na nyingine nyingi.
Hata baada ya dhambi Mungu anamtafuta mtu kwa
upendo, ila huyo kwa aibu anamkimbia, au akijisikia analaumiwa na dhamiri, basi anatafuta visingizio hata kumlaumu Mungu kana kwamba ndiye
aliyesababisha. Kwa utakatifu wake Mungu hawezi kuvumilia maovu, na kwa haki yake anataka makosa yalipwe. Ndiyo sababu tunakuta matatizo maishani,
kama vile uchungu
wa uzazi, kuhusiana kwa mabavu, kupata riziki kwa
shida, na hasa kufa: hayo yote ni matokeo
ya dhambi. Pamoja na hayo Mungu hapendi mtu yeyote
apotee (2Pet 3:9), hivyo toka mwanzo aliahidi kwamba mzawa wa Eva atamponda
kichwa shetani. Ndiyo habari njema ya awali kuhusu wokovu ujao.
Watu walivyoishi baada ya dhambi
Kaini na Abeli, mchoro wa karne ya 15
kutoka kitabu cha Ujerumani Speculum Humanae Salvationis.
Baada ya dhambi ya asili watu walianza kuzaa. Mwa 4:1-16 inatuchorea picha ya Kaini na Abeli kama wazaliwa wa kwanza waliotofautiana kiadili (1Yoh 3:11-12). Toka mwanzo mwovu na mwadilifu waliishi pamoja, wa kwanza
akimdhulumu wa pili hata kumuua bila ya kujali udugu. Ikisikitishwa kufikiria mzaliwa wa kwanza kuwa muuaji wa mdogo wake,
inafurahisha kwamba wa kwanza kufa alikuwa mwema, kielelezo cha Yesu aliyeuawa
bila ya kosa (Eb 12:24).
Toka mwanzo hao walimuabudu Mungu kwa njia ya
dini, ibada na sadaka mbalimbali. Hata hivyo Mungu akakubali zile tu zilizotolewa kwa ukarimu (Eb 11:4). Tangu hapo Biblia inatuonyesha jinsi alivyopendelea wadogo
kuliko wakubwa.
Kuhusu Kaini tunaonyeshwa ustawi
wa dhambi ndani mwake na uongozi wa Mungu aliyemtaka
ashinde dhambi bado mlangoni. Hata baada ya dhambi hiyo ambayo ni kubwa kiasi
cha kumlilia Mungu alipe kisasi, yeye alizidi kumhifadhi Kaini.
Baadaye (Mwa 4:17-24) kukawa na maendeleo ya aina mbalimbali: ujenzi, ufundi, muziki, lakini hasa dhambi. Picha yake ni Lameki, mtu wa kwanza kuwa na mitara, mkatili kama nini. Ingawa hali ilikuwa ya kukatisha tamaa, kwa baraka ya Mungu watu wakazidi kuzaa na kati ya watoto wao wakapatikana waadilifu kama Henoko aliyestahili kutwaliwa na Mungu. Hata hivyo ongezeko la dhambi
likasababisha maisha ya binadamu yafupike (Mwa 6:3) kwa kuwa ni kusogea mbali
na Mungu, chemchemi ya uhai.
NUHU
Sadaka ya Nuhu ilivyochorwa na Daniel
Maclise.
Mwa 6:5-9:17 inatufundisha kwamba Mungu
anachukizwa na dhambi, hivyo anataka kuondoa maovu duniani ili nchi impendeze
kama alivyokusudia alipoiumba. Kwa ajili hiyo zamani za Nuhu alileta maji yafunike dunia na kuzamisha waovu. Lakini alisalimisha
waadilifu katika safina kubwa ya kutosha, halafu akafunga nao agano thabiti (Eb 11:7). Hasa maji yanayokusudiwa kutakasa dunia yote ni yale
ya ubatizo (1Pet 3:17-22), na safina ambayo iokoe watu ni Kanisa, ambalo ni la
lazima kwa wokovu kama vile ubatizo unaotuingiza ndani yake.
Uso wa nchi ulipokwishatakaswa na maji njiwa akarukaruka akachuma tawi la mzeituni unaozaa matunda ya kutengenezea mafuta. Njiwa akaonekana tena juu ya maji siku ya ubatizo wa Yesu ambapo alipakwa Roho Mtakatifu na kuyatia maji nguvu ya kutakasa watu (Mk 1:9-11; Tito 3:3-7). Maji na mafuta ndiyo mwanzo mpya kwa binadamu.
Mara alipotoka safinani Nuhu alimtolea Mungu
sadaka iliyompendeza hata akaahidi hataangamiza tena binadamu kila
anapostahili. Sadaka hiyo ni mfano wa ile ya Yesu msalabani, inayoadhimishwa
katika ekaristi, ikituondolea adhabu nyingi na kutuletea huruma ya Mungu, yaani nafasi na neema ya kutubu (Tito 2:11-14).
Hatimaye kutakuwa na hukumu (Math 24:37-41).
Mnara wa Babeli ulichorwa mara nyingi na wasanii kama katika picha hii
ya Pieter
Brueghel Mzee.
Mwa 11:1-9 inatufundisha kwamba kiburi na dhambi kwa jumla vinatenganisha watu wasiweze kuelewana wala kuishi
pamoja. Kinyume chake katika Agano Jipya tunasikia kwamba siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu, aliye upendo wa Mungu, aliunganisha tena watu wa
makabila mbalimbali katika kutangaza sifa zake (Mdo 2:5-12). Palipo na upendo, tofauti za lugha na utamaduni si shida.
ABRAHAMU (1900-1800 HIVI K.K.)
Mwanzo
wa safari ya Abrahamu ulivyochorwa na József Molnár.
Mtu huyo, aliyezaliwa Mesopotamia (Iraq) baada ya watu kubuni uandishi, ndiye mwanzo wa taifa
teule la Mungu na baba wa waamini wote. Aliishi
kwa kuhamahama pamoja na mifugo yake: akipitia Syria alifikia nchi ya Kanaani aliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu akashukia Misri kwa muda (Mwa 12). Lakini safari yake muhimu zaidi ni ile ya imani, kwa
kuwa Abrahamu aliongozwa na Mungu siku kwa siku, katika mazuri na magumu,
akisadiki ahadi zake za ajabu (Eb 11:8-19). Mchungaji huyo alikubali Mungu
amchunge maisha yake yote, akamfuata bila ya wasiwasi, akituachia mfano bora wa
kumshika mkono Mungu daima bila ya hofu.
Mungu
akimuagiza Abramu kuhesabu nyota; mchoro wa Julius
Schnorr von Carolsfeld (1860).
Hasa Mungu alimuahidia uzao mkubwa kama nyota za mbinguni, naye akaamini ingawa alikuwa hajapata hata mtoto mmoja:
ndiyo imani iliyompendeza sana Mungu (Mwa 15:1-6).
Mwa 18 inamchora kama mtu mkarimu sana kwa
wageni, rafiki wa Mungu anayestahili kuambiwa yote, mwenye huruma, busara na unyenyekevu katika sala. Wageni wake watatu ambao ni kama mtu mmoja tu wanadokeza Utatu Mtakatifu. Mungu alimdai Abrahamu asadiki kwamba anaweza yote kama
atakavyomdai Bikira
Maria (Lk 1:17), naye alidumu kumuomba awahurumie waovu kwa ajili ya waadilifu (Yak 5:16).
Mwa 19 inatuchorea uovu wa watu ambao huko Sodoma ulizidi hata kumdai Mungu alipe kisasi. Lakini kati yao mwadilifu
akaokolewa, isipokuwa mke wake akaja kuadhibiwa kwa sababu aliangalia nyuma
kinyume cha agizo la Bwana (Lk 17:28-33).
Mwa 21:1-21 inatusimulia jinsi Mungu
alivyotimiza ahadi yake kwa kumjalia Sara amzalie Abrahamu mtoto Isaka katika uzee na utasa. Isaka ni mtoto wa imani, si wa mwili, naye ni huru, tofauti na Ishmaeli mtoto wa mtumwa ambaye hastahili kurithi pamoja na mdogo wake. Isaka,
baba wa Israeli alipata baraka kuu, naye ni mfano wa watu wa Agano Jipya.
Ishmaeli, baba wa Waarabu alibarikiwa pia kwa ajili ya baba yake, naye ni mfano wa Agano la Kale
ambapo watu wanategemea mambo ya kimwili (kutahiriwa, kunawa, kubagua vyakula
n.k.) na hivyo ni watumwa (Gal 4:21-5:1).
Mwa 22:1-19 inatuletea habari ya kusisimua
kuhusu sadaka ambayo Mungu alimdai Abrahamu, yaani kumchinja Isaka. Ni kimoja
kati ya vilele vya imani ya binadamu, imani inayoonyeshwa kwa matendo ya utiifu (Yak 2:21-22). Abrahamu hakusita kumrudishia Mungu kile alichopewa,
akaondoka alfajiri akasafiri mpaka mahali alipoambiwa (Wayahudi wanaamini mlima
huo ndipo walipojenga hekalu la Yerusalemu). Kwa niaba ya waamini wote Abrahamu alikuwa tayari kumchinjia Mungu
mwanae pekee ampendaye. Lakini atakayemtoa kweli Mwana
pekee ni Mungu Baba (Yoh 3:16). Mwanae ndiye mwanakondoo aliyeuliziwa na Isaka na ambaye Mungu akajipatia juu ya mlima Kalivari alioupanda huku amejitwika sio kuni bali mti wa msalaba. Abrahamu aliamini uwezo wa Mungu juu ya mauti na hasa uaminifu wake kwa ahadi alizompa: kwa hiyo akarudishiwa mwana hai kama mfano wa ufufuko, na katika yeye, yaani katika mzawa wake, watu wote wakabarikiwa.
Maisha ya imani yanadai daima sadaka, hasa ya mambo yanayopendwa zaidi (Rom
12:1-2): ndiyo njia ya kujaliwa baraka zinazopita ubinadamu wetu.
Mwa 24 inasimulia kirefu jinsi Abrahamu kabla
hajafa alivyomfanyia mpango wa ndoa Isaka kufuatana na mila zao, ila alikataza kabisa asirudi kwao, bali kwa vyovyote abaki katika
nchi ile aliyoahidiwa na Mungu. Hivyo imani izidi kuongoza uzao wake kama
ilivyomuongoza mwenyewe.
WATOTO WA ISAKA: ESAU NA YAKOBO
Matthias Stom, Esau
[kulia] akimuuzia Yakobo haki yake kama mtoto wa kwanza au Sahani ya dengu, (karne
ya 17).
Kadiri ya Mwa 25:19-34, Rebeka alimzalia Isaka watoto pacha wenye sura na silika tofauti, Esau na Yakobo. Wa kwanza analaumiwa hasa kwa kupuuzia baraka ya Mungu iliyokuwa haki
ya kifunguamimba: kwa sahani ya dengu alikubali kukosa neema zile zote alizojitwalia Yakobo kwa imani yake (Eb 12:16-17).
Mwa 27 inasimulia jinsi Yakobo, akifundishwa
na mama yake, alivyoweza kubarikiwa na baba. Ingawa uongo wake haukubaliki (Hos 12:3-5), Mungu alithibitisha baraka ya Isaka kadiri ya desturi yake ya
kumpendelea mdogo: hivyo Yakobo, aliyekimbia nchi yake ana fimbo tu, alirudi
miaka ishirini baadaye ana wake 4, watoto 11 na mifugo wengi ajabu (Mwa 32).
Kabla hajaingia nchi yake Mungu alishindana naye usiku kucha akalazimika
kumbariki na kumtajia jina jipya, Israeli.
YOSEFU NA NDUGU ZAKE KUSHUKIA MISRI (1700
HIVI K.K.)
Yosefu
na kaka zake wakipokewa na Farao kadiri ya James Tissot (1900 hivi).
Kama kawaida ya mitara, kulikuwa na upendeleo
na wivu kati ya watoto wa Yakobo. Hasa Yosefu alichukiwa na kaka zake wote, ingawa alikuwa mnyofu hata kuwasimulia ndoto zake za ajabu (Mwa 37:2-11). Kijicho na chuki vilifikia hatua ya kuwafanya watamani kumuua. Walipopata nafasi
walifanya njama, ingawa si wote. Mwisho uamuzi ukawa kumuacha hai lakini
kumuuza kama mtumwa kwa wafanyabiashara walioelekea Misri (Mwa 37:12-36). Lakini katika
maovu ya binadamu Mungu akazidi kushughulikia taifa lake teule. Hivyo Yosefu
akawa mfano wa Yesu ambaye alichukiwa bure tu akauawa msalabani kwa wokovu wa
wadogo zake wakosefu.
Mwa 39 inaonyesha jinsi Yosefu alivyozidi
kumtiii Mungu na kukwepa dhambi. Hivyo baada ya majaribu mbalimbali akatukuzwa
kuwa liwali wa Farao kwa nchi yote, hasa kwa usimamizi wa akiba ya chakula (Mwa 41:1-49) kwa
ajili ya miaka saba ya njaa aliyotabiri. Kadiri ya mpango wa Mungu njaa hiyo ikawalazimisha kaka
zake waje kumuinamia, naye hakulipa kisasi; halafu, kama vile alivyotafsiri
ndoto mbalimbali, aliwafafanulia maana ya matukio ya maisha yao katika mpango
wa Mungu: kwamba ndiye aliyemtuma Misri kusudi awaokoe (Mwa 45:1-15).
Mwa 46:1-7 inasimulia Yakobo na wazawa wake
wote, jumla wanaume 70, walivyohamia Misri. Lakini hawakusahau nchi
waliyoahidiwa na Mungu: ndiyo sababu Yakobo na Yosefu walidai waapiwe kuwa
watakuja kuzikwa kwao (Mwa 49:29-50:26). Kabla ya kufa Yakobo aliwabariki
watoto wake 12 na kwa namna ya pekee Yuda ambaye atatawala moja kwa moja (Mwa 49:8-12).
UTUMWA WA MISRI NA WITO WA MUSA (1250 HIVI
K.K.)
Musa akiokolewa katika maji ya mto Nile,
alivyochorwa na Nicolas
Poussin mwaka 1638.
Wanaisraeli waliishi Misri kama wageni tu zaidi ya miaka mia nne (Mdo 7:6-16)
wakiongezeka kiasi cha kuwatisha wenyeji wao: ndiyo sababu wakaanza kudhulumiwa
mwaka 1300 hivi K.K.
Hasa katika kuwakomboa utumwani, Mungu
alijionyesha mtetezi wa haki za maskini. Pamoja na kushurutishwa kufanya kazi wasioipenda, ilitolewa amri ya
kuua watoto wao wote wa kiume: lakini mpango huo haukutekelezwa sawasawa (Kut
1:7-22).
Mmoja kati ya watoto waliookolewa katika
hatari hiyo ni Musa, wa kabila la Lawi (Kut 2:1-10; Eb 11:23; Mdo 7:17-22). Kisha kukimbia Misri Musa akaoa
Mmidiani (Kut 2:11-22; Eb 11:24-27; Mdo 7:23-29): alipokuwa anachunga mifugo ya
mkwewe kwenye mlima Sinai akaitwa na Mungu kutoka ndani ya kichaka kinachowaka
moto kisiteketee. Mungu alimchagua ingawa ana kigugumizi yaani anaonekana hafai kushindana na Farao. Mungu akasisitiza aende
mwenyewe, naye atatumia uwezo wake wa Kimungu kumlazimisha Farao. Kadiri Musa
alivyoomba, Mungu alimfunulia jina lake takatifu YHWH ambalo linaeleweka kiasi
tu, kama vile fumbo la Mungu mwenyewe (Kut 2:23-3:20; Mdo 7:30-35).
MAPIGO YA WAMISRI
"Maji
Kugeuka Damu" kadiri ya Tissot.
Mungu alipomtuma Musa kwa Farao alijua tayari
huyo atakataa kuwaruhusu Waisraeli waende zao, mpaka aone mapigo yake kwa Wamisri. Kwa kuwa ulihitajika muda kuleta ukombozi, iliwabidi Waisraeli wawe na
imani na subira hadi ahadi za Mungu zitimie. Lakini binadamu hatupendi kungojea
ukombozi: hivyo Waisraeli wakaanza kunung’unika (Kut 5:1-6:1). Hata hivyo Mungu
akaendelea na mpango wake.
Maajabu aliyoyatenda huwa yanatokea Misri
lakini si yote kwa wakati mmoja wala si kwa kiasi kile alichosababisha Musa kwa
fimbo yake (Kut 6:28-7:7). Tuna orodha mbalimbali za mapigo hayo, lakini kwa
kawaida yanahesabiwa kumi: maji ya mto Naili kuwa mekundu kama damu, vyura kujaa nchi, chawa, nzi, tauni, majipu, mvua
ya mawe, nzige, giza na hatimaye kifo cha wazaliwa wa kwanza wa kiume wa watu na wa wanyama. Adhabu hizo
ziliwapata Wamisri, lakini si Waisraeli: hivyo ilikuwa wazi kuwa Mungu anabagua
watu wake na watu waovu.
Katika pigo la kumi Waisraeli waliopolewa kwa
kuipaka milango yao damu ya mwanakondoo (Kut 11:1-10; Mdo 7:36-37; Eb 11:28).
Hivyo Mungu aliwaandaa watu kupokea imani kwa Yesu Kristo, Mwanakondoo wa kweli
na Mkombozi wa waliokuwa watumwa wa dhambi, shetani na kifo (Yoh 19:36; 1Kor
5:7; 1Pet 1:18-20). Hiyo ni wazi katika ibada iliyoagizwa ifanyike kila mwaka
(Kut 12:1-14), yaani Waisraeli wale nyama ya mwanakondoo dume asiye na hila,
pamoja na mkate usiotiwa chachu na mboga ya majani machungu. Yesu akaifanya ibada hiyo iwe ibada kuu ya agano
jipya la milele, akiagiza tuifanye kwa ukumbusho wake, si tena kwa ukumbusho wa kutoka Misri (1Kor 11:23-26).
SAFARI YA KUENDEA NCHI YA AHADI
"Kuvuka
Bahari ya Shamu" kadiri ya Nicholas
Poussin.
Kut 12:29-42 inasimulia Waisraeli wote
walivyokimbia Misri pamoja na mifugo yao waliposikia mayowe kutoka nyumba za
majirani wao wote. Katika safari yao wakaongozwa na Mungu kwa sura ya wingu mchana na ya moto usiku (Kut 13:17-22; Yoh 8:12): hivyo Mungu alionyesha wazi kuwa hawaachi
hata kidogo bali anawashughulikia kwa namna tofauti kadiri ya mahitaji.
Kut 14:5-31 inasimulia jinsi Wamisri, kisha
kuwalilia wafu wao, walivyoanza kuwatafuta Waisraeli kwa farasi na magari wakawakuta karibu na bahari ya Shamu. Lakini Waisraeli walivuka bahari kama kwamba ni nchi kavu, kwa kuwa maji yamegawanyika. Kumbe Wamisri wakazama kwa kuwa maji
yamerudi mahali pake (Eb 11:29). Asubuhi Waisraeli wakaona maiti za Wamisri
wote zikielea wakamshangilia Mungu aliyewaokoa (Kut 15:1-21 inatuletea wimbo ambao maneno yake ni kati ya yale ya kale zaidi katika Biblia). Hivyo
Mungu aliwaokoa tena watu wake katika maji, na huu pia ni mfano wa ubatizo
ambao unaadhimishwa hasa usiku wa Pasaka. Hata katika hatari ya kukandamizwa Mungu alidai Waisraeli watulie kwa
imani ya kuwa ushindi ni wake tu. Tena walitakiwa wasiyasahau kamwe mang’amuzi hayo, kwa kuwa
ndiyo msingi wa imani ya dini yao. Sisi vilevile tunatakiwa kukumbuka daima
ubatizo wetu ambapo Mungu ametuokoa.
Baada ya ushindi wa Pasaka safari ikaendelea
mpaka kufikia nchi aliyoahidi Mungu, ila Waisraeli wakaja kusahau uweza wake na kumlalamikia kipumbavu hata kumchosha. 1Kor 10:1-11 inatuonya
tusifanye vile. Kama kawaida malalamiko ya kwanza yalihusu kula na kunywa (Kut
15:22-17:7). Mungu aliwakubalia kwa kuwateremshia kwale halafu mana: hasa chakula hicho kiliwashangaza Waisraeli wakazidi kukikumbuka hata
wakamdai Yesu awapatie tena kama kweli ndiye Musa
mpya. Yesu akawajibu kuwa mwenyewe ndiye chakula
cha uzima kutoka mbinguni kinachotulisha safarini hapa
(Yoh 6:22-59). Vilevile kuhusu maji, Mungu aliyatokeza katika mwamba huko Masa au Meriba, lakini alichukizwa sana na matendo yao (Eb 3:15-19).
Shida nyingine ya kawaida kwa makabila ya
wahamaji ni kupigana vita. Waisraeli walilazimika kufanya hivyo na Waamaleki, wakapata ushindi si kwa nguvu zao, ila kutokana na sala ya Musa, mwombezi wao (Kut 17:8-16). Sisi taifa la Mungu tunatakiwa tutegemee sala kuliko
uhodari wetu, na daima tuwe na watu wenye kumuinulia Mungu mikono yao kama Musa
jangwani.
AGANO LA MLIMA SINAI
Sanamu ya Musa iliyochongwa na Michelangelo iko katika kanisa la Mt.
Petro "in vinculis" mjini Roma (Italia).
Walipofikia mlima huo wa kutisha, Mungu
alimuita Musa aupande ili aseme naye, huku wengine wakibaki chini. Hapo akampa
Musa masharti ya agano lake na Waisraeli (Kut 19). Akiwa Muumba na hasa
Mkombozi wao alidai waishi kitakatifu kwa kushika amri kumi, ambazo tatu zinahusu heshima kwake na saba uhusiano na watu wengine
(Kut 20:2-17). Ndiyo mawe
mawili ambayo Musa alipewa halafu Yesu
akayakamilisha katika amri
kuu ya upendo kwa Mungu na kwa jirani (Mk
12:28-34). Amri hizo zinaweza kujulikana na kukubaliwa na mtu yeyote mwenye mapenzi
mema, lakini Mungu alipenda kutusaidia tujue kwa
urahisi na hakika zaidi tufanye nini ili kumpendeza, tuwe watu wake naye awe
Mungu wetu kwelikweli. Agano hilo upande wa Mungu ni imara kwa kuwa yeye ni
mwaminifu kabisa, shida iko upande wetu tulio geugeu, tukiahidi tusitekeleze.
Ndiyo sababu likahitajika agano lingine lililofungishwa na Yesu Kristo (2Tim
2:11-13).
NDAMA YA DHAHABU.
Ndama ya dhahabu
Kut 32 inasimulia uasi wa Waisraeli
ulivyofikia kilele chake walipojitengenezea mungu wa dhahabu mwenye sura ya fahali (Biblia kwa dharau inasema “ndama” na “mla nyasi”). Hata Haruni, kaka yake Musa, alikubali kufuata matakwa yao huku mdogo wake
akichelewa mlimani (Mdo 7:38-42). Musa akambembeleza Mungu asiwaangamize watu
wake, hivyo akawa mfano bora wa mwombezi, kwa kuwa hakujali ahadi ya Mungu ya
kumfanya chanzo cha taifa lingine kubwa. Kazi hiyo ni hasa ya Bwana Yesu ambaye aliwatetea watu wake kwa kumwaga damu yake, na anazidi
kuwaombea kwa Baba yake (Eb 7:25-27).
Mungu kujifunua tena kwa Musa
Kilele cha Mlima Sinai (mita 2,285 juu ya usawa wa bahari).
Kut 33:18-34:9 inasimulia jinsi Mungu
alivyokubali kiasi ombi la Musa la kumuonyesha utukufu wake; badala ya kumuonyesha uso wake (Yoh 1:18) alijifunua kwake kwa kulitangaza na kulifafanua jina lake: YHWH ni mwingi wa rehema na uaminifu, anawaonea wivu watu wake, yaani hawezi kukubali waabudu miungu mingine
kwa hasara yao. Ndiyo sababu alipoagana nao kwa kuandika tena amri zake kumi
katika mawe, pamoja na kuahidi kuwafukuza wenyeji wa nchi takatifu ili kuwapatia nafasi Waisraeli, aliwaagiza wasichanganyikane nao wasije
wakavutwa katika Upagani. Hasa alikataza ndoa
za mseto ili kulinda usafi wa imani. Kwa namna ya
pekee Kristo analipenda na kulionea wivu Kanisa lake analolitaka bikira safi katika imani na maadili (2Kor 11:2; Ef 5:25-27): hivyo tunaposhirikiana na watu wengine tuwe
macho tusifuate mawazo, maneno na matendo yao, bali tushuhudie imani na upendo
kwa maisha yetu tofauti na ya kwao (Yoh 17:15-17).
Mambo ya Walawi
Hema
la mkutano na kambi lake (mchoro wa karne
ya 19).
Kitabu hicho cha tatu kimejaa hasa sheria za
ibada zenye kulenga utakatifu wa makuhani na wa sadaka. Watu wa kabila la Lawi
tu ndio walioruhusiwa kushughulikia ibada, tena kati yao ukoo wa Haruni tu ndio
makuhani kamili. Kutokana na kazi hiyo Walawi hawakupewa sehemu ya nchi
takatifu, ila Mungu mwenyewe ndiye fungu lao. Lakini taifa lote lilitakiwa liwe
takatifu kutokana na uhusiano wake na Mungu (Law 19:1). Polepole maana ya
utakatifu huo ilizidi kueleweka si kukwepa unajisi wa kiibada tu, bali unategemea hasa mwenendo mwadilifu.
Hesabu
Kitabu cha nne kinaitwa hivyo kwa sababu
kinaleta hesabu mbalimbali, hasa ya idadi ya Waisraeli: wanaume wa kuweza
kwenda vitani walikuwa 603,500 (mbali na Walawi waliohesabiwa peke yao: wanaume
22,000 wakiwa pamoja na watoto wa kiume); ukiongeza wanawake na watoto mpaka
umri wa miaka ishirini, basi jumla yao iliweza kufikia watu milioni tatu,
ingawa si lazima kuamini idadi hiyo ni sahihi (pengine namba hizo hazilingani
katika makala kwa kuwa ilikuwa rahisi kukosea wakati wa kunakili).
Uzito wa kazi ya kuwaongoza watu wengi hivyo
wanaonung’unika kila mara ulimchosha Musa hata akamuomba Mungu tena ampunguzie
mzigo au amuue kabisa (Hes 11:1-30). Musa alieleza shida yake kama rafiki kwa
mwenzake, kwa unyofu uleule wa watu wengine wa Mungu katika Biblia. Mungu
akamkubalia akawashirikisha watu sabini roho yake kwa ajili ya uongozi katika
ngazi mbalimbali. Huo pia ni mfano wa Agano Jipya, ambapo askofu hawezi kuchunga waamini peke yake, bali anahitaji msaada wa viongozi wa
daraja za chini, yaani mapadri na mashemasi (Mdo 6:1-6). Katika nafasi hiyo Musa alimueleza Yoshua kwamba hawaonei kijicho kwa kupewa karama, tena angependa kama Waisraeli wote wangekuwa manabii. Hamu hiyo
ikatimia siku ya Pentekoste: katika Kanisa wote wanapewa Roho Mtakatifu na kuwa
manabii, hata wanawake na watoto (Mdo 2:16-18).
Kinyume chake Hes 12 inasimulia kijicho
kilivyowafanya dada na kaka wa Musa wamseme wakijidai nao pia ni manabii.
Lakini Mungu akawaeleza kuna namna mbalimbali za unabii, na Musa ni wa pekee.
Kisha akatoa adhabu ambayo ikaondolewa kwa maombezi ya Musa tu: ndiyo sababu
anasifiwa kwa upole wake. Kijicho kitasumbua daima taifa la Mungu, hata katika Agano Jipya
(1Kor 12:1-31; 14:37-38).
Musa na wapelelezi wa Kanaani, walivyochorwa na Giovanni
Lanfranco, J.
Paul Getty Museum, Los Angeles, Marekani.
Waisraeli walipofikia mipakani mwa nchi
takatifu walituma wapelelezi ili waivamie, nao waliporudi walisimulia uzuri
wake, lakini pia walitisha kwa kuzidisha habari za wananchi na miji yao (Hes
13). Hapo Waisraeli wakaanza kunung’unika usiku kucha (Hes 14) wakapanga kuwaua
kwa mawe Kalebu na Yoshua waliotaka kuivamia nchi bila ya hofu kwa jina la Bwana.
Lakini Mungu akaonyesha utukufu wake na kutisha ataleta tauni ili kuwaangamiza
wote kwa ukaidi wao. Kwa maombezi ya Musa, akakubali kuwahurumia lakini akaamua
warudi jangwani na kuzungukazunguka huko mpaka wafe wote; ila watoto wao pamoja
na Kalebu na Yoshua ndio watakaoingia nchi takatifu kuimiliki. Maana
ya kiroho ni kwamba hatutakiwi kuzitia shaka ahadi za
Mungu; hata zikionekana ngumu kupatikana, ni lazima tuwe na moyo mkuu na imani hata tukabili vipingamizi vyovyote.
Kinyume chake, Waisraeli walipoamua kuivamia
nchi kwa kusikitikia adhabu waliyopewa wakashindwa kabisa, maana ni lazima
tumtii Mungu kwa wakati wake. Pia kughairi kutokana na matatizo kunaweza
kukatusukuma tutende namna ambayo haimpendezi tena; ni lazima tuchukue majukumu
ya matendo yetu na kukubali adhabu au matatizo tuliyojitakia:majuto hayo
yanafaa kwa kuonyesha utiifu kwa Mungu (Zab 119:71).
Manung’uniko ya Waisraeli katika safari yao
jangwani yakawaletea adhabu nyingine, mojawapo ile ya kugongwa na nyoka wengi wenye sumu kali. Lakini walipoomba msamaha, Mungu akamuagiza Musa atengeneze nyoka
wa shaba na kumuinua juu ya mti ili mtu aliyeumwa
akimtazama tu apate kupona (Hes 21:4-9). Ufafanuzi wa tukio hilo ulitolewa na
Yesu mwenyewe: ndiye aliyeinuliwa juu ya mti wa msalaba ili watakaomtazama kwa
imani wapate kuishi (Yoh 3:14-15).
Kumbukumbu la Torati (Sheria)
Mchoro wa William
Blake (1780 hivi) unaomuonyesha "Musa akipokea Sheria", Yale Center for British Art.
Kitabu hicho cha mwisho cha Torati
kiliandikwa kama miaka 600 baada ya Musa, ingawa kina namna ya hotuba tano alizoweza kuwatolea Waisraeli kabla hajafa. Kinapitia upya matukio
ya wokovu ya wakati wa Musa kikifaidika na ujumbe wa manabii, hasa Hosea. Kwa msingi huo, kitabu hiki kinasisitiza sana upendo kwa Mungu, uaminifu kwa agano la mlima Sinai pamoja na tuzo na adhabu zitakazotolewa
kufuatana na matendo ya Waisraeli. Katika maneno yake yote ya kitabu hiki,
maarufu ni hasa yale ya 6:4-9 ambayo Mwisraeli yeyote anayakariri kila siku
katika sala na kuyashika pengine neno kwa neno.
Maneno mengine muhimu sana yapo 26:5-10: ni
kama kanuni
ya imani ambayo Mwisraeli alikuwa anaiungama mbele ya
Mungu wakati wa kumtolea malimbuko ya ardhi. Hivyo alikuwa akikiri amepewa yote
na Bwana, halafu akaweza kuyafurahia mavuno.
Baada ya hotuba hizo, Kumb 31:1-8 inasimulia
jinsi Musa alivyomuachia Yoshua uongozi wa Waisraeli wote kwa kumwekea mikono
(Hes 27:12-23). Musa alifikia mpakani mwa nchi takatifu asikubaliwe kuiingia
kama adhabu ya makosa yake, ila alionyeshwa yote kutoka mlimani (Kumb 32:48-52)
halafu akafariki (Kumb 34). Kazi aliyopangiwa iliishia huko, mwingine akampokea
na kuendeleza ukombozi wa Kimungu. Binadamu wote ni vyombo tu vinavyotumika kwa
muda fulani, halafu vinaweza kuachwa. Kumbe Mungu ndiye mtendaji mwenyewe
ambaye hasinzii wala halali, bali anazidi kuwashughulikia watu wake. Kwa imani
hiyo tuwe daima tayari kuwaachia wengine nafasi yetu.
Vitabu vinavyofuata Kumbukumbu la Torati
(Sheria)
Vitabu vinavyofuata katika Biblia
ya Kiebrania (Yoshua, Waamuzi, Samweli na Wafalme)
vinataka kuthibitisha kwamba kweli ikawa kama hiki kinavyosema: Waisraeli
walipofuata agano (wakati wa Yoshua) waliteka nchi
ya ahadi na kuifurahia, lakini walipozidi kuasi
(wakati wa Waamuzi, Samweli na Wafalme) walikuja kunyang’anywa nchi ile yote, kwanza sehemu nzuri
zaidi (kaskazini), halafu ile hafifu zaidi (kusini). Hapo Waisraeli wote wakajikuta tena utumwani katika nchi ya kigeni
kama kabla ya Musa, wakikosa hata sanduku la agano, lililopotea wakati wa maangamizi ya Yerusalemu na hekalu lake, baada ya wao kufikia hatua ya kula watoto wao kutokana na njaa.
Vitabu hivyo vilikamilishwa wakati wa kukaa
uhamishoni Babeli, vikiwa jibu la swali kuu lililowakwaza huko: je, Mungu wetu
ameshindwa? Waandishi walichagua matukio mbalimbali ya historia baada ya Yoshua
ili kuthibitisha kuwa aliyeshindwa ni Israeli, si Mungu. Historia hiyo
inaonyesha mfululizo wa maasi hata baada ya Mungu kutuma waamuzi na manabii
wake ili kuwaonya Waisraeli na kuwaelekeza upya.
Lengo la waandishi halikuwa kutunza
kumbukumbu za mambo yote kwa usahihi na ukamilifu, bali kuelekeza njia ya
kupata wokovu hata baada ya Israeli kuonekana imekoma moja kwa moja. Kama vile
Biblia nzima, vitabu hivyo vinalenga wokovu wetu, vikihakikisha kuwa Mungu
anaweza kuleta mwanzo mpya hata hali ikiwa mbaya namna gani. Ndiyo sababu
habari ya mwisho kabisa ni ya kuleta tumaini: kwamba mfalme Yekonia alitolewa gerezani (alipokaa miaka 37) na kufanywa mgeni wa kudumu
mezani pa mfalme wa Babeli.
Yoshua (1210-1200 hivi K.K.)
"Wana wa Israeli wakivuka Yordani" walivyochorwa na Gustave Doré (alifariki mwaka 1883).
Kitabu cha sita cha Biblia kinatupasha habari
za uvamizi wa nchi takatifu ambao Waisraeli waliufanya chini ya Yoshua, ambaye
ni mfano wa Yesu (hata jina lao kwa Kiyahudi ni moja, linalotafsiriwa “Mungu
anaokoa”): ndiye aliyewaingiza watu katika nchi ya ahadi, si Musa.
Mara baada ya kushika uongozi, Yoshua alituma
wapelelezi nchini; huko Yeriko, mji wa zamani kuliko yote ya dunia, walisaidiwa na Rahabu, kahaba aliyeamini kuwa ushindi utakuwa wa Mungu wa Israeli (Yos 2): kwa hiyo
akaokolewa pamoja na ndugu zake, tena akajaliwa kuwa bibi wa babu wa mfalme Daudi, hata akatajwa na Injili kama bibi wa Yesu Kristo (Math 1:5-6), halafu
akachukuliwa kama mfano wa imani (Eb 11:31) na wa matendo mema (Yak 2:25).
Yoshua aliwavusha Waisraeli pakavu kati ya mto Yordani (Yos 3-4) na hivyo akawaingiza katika nchi takatifu. Hapo ikawabidi
kwanza wafunge tena agano na Mungu kwa kutahiriwa wanaume wote na kwa
kuadhimisha Pasaka ambapo kwa mara ya kwanza walikula mazao ya nchi hiyo
waliyoahidiwa: ndio mwisho wa mana na wa kipindi cha jangwani (Yos 5:1-12).
Hata sisi tutaacha kula mkate toka mbinguni tutakapoingia pale tulipoahidiwa.
Baada ya matendo hayo ya kidini Mungu
alimtokea Yoshua kama amirijeshi wa Israeli ili kumhakikishia kwamba mwenyewe ataongoza mambo, hivyo
Yoshua amtegemee akijisikia chombo chake tu (Yos 5:13-15). Ni rahisi kwa kila
binadamu aliyeshika uongozi kujisikia mwenyewe na hivyo kuacha kumtegemea
Mungu. Kumbe Yoshua kwa kupokea ujumbe huo akaweza kushinda watu wenye maboma,
nguvu na silaha kali kuliko Waisraeli. Kwamba hiyo ni nguvu ya Mungu inaonekana
wazi hasa katika simulizi la kuteka Yeriko (Yos 6:1-21): huko Waisraeli
walifanya maandamano ya ibada mpaka kuta za mji zikaanguka. Vita vyetu vya kiroho na vya
kitume vitegemee hasa sala. Baada ya vita vingi Yoshua akayagawia makabila 12 ya Israeli nchi yote, ikiwa ni pamoja na sehemu zilizobaki chini ya
wenyeji (Yos 12:1-13:14). Huko Shekemu aliwadai wote wachague kumtumikia YHWH au miungu mingine, akisisitiza
ugumu wa kumtumikia sawasawa Mungu aliye mtakatifu na mwenye wivu kwa watu
wake. Lakini wao walikubali kwa moyo wote kumtumikia Mungu tu, wakasimamisha
jiwe kubwa kama kumbukumbu (Yos 24:1-28).
Kabla hajafa Yoshua akawaita Waisraeli wote
ili kuwaimarisha katika imani na umoja kwa kuwakumbusha maajabu waliyotendewa na Mungu na kwa kuwahimiza
wamuonyeshe shukrani (Yos 23). Kukumbuka ni jambo muhimu ili tuishi kwa imani bila ya
kudanganywa na maisha yanayosahaulisha kwa urahisi mambo ya Kimungu.
Waamuzi (1200-1025 hivi K.K.)
"Gideoni akimshukuru Mungu kwa muujiza wa umande",
alivyochorwa na Maarten
van Heemskerck (Musée des Beaux-Arts de
Strasbourg, Ufaransa).
Kitabu hiki kinaleta picha tofauti na kile cha Yoshua kuhusu hali ya nchi ya Kanaani baada ya uvamizi. Kinaonyesha kuwa Waisraeli hawakufukuza wenyeji wote, bali waliteka baadhi tu ya maeneo yao wakaishi jirani nao.
Baada ya makabila ya Waisraeli kugawana nchi,
kila moja likaanza kujitegemea: lakini bila ya umoja hakuna nguvu upande wa
dini wala wa siasa. Upande wa dini, Waisraeli wakaanza kuchanganyikana na
wenyeji Wapagani na kufuata utamaduni wao uliostaarabika zaidi, wakiwaiga
katika yote: kuishi katika nyumba ya kudumu, kulima n.k. hata wakaabudu miungu yao ya kiume na ya kike
kwa ukahaba
wa kidini na kwa kuitolea sadaka watoto wao ili kujivutia fadhili zao, hasa mvua. Kutokana na makosa hayo, Mungu akawaacha wapatwe na ukame, njaa na zaidi ya hayo wanyanyaswe na makabila mbalimbali.
Mara kwa mara Waisraeli wakamlilia yeye
aliyewasikiliza walipokuwa wanaonewa Misri, naye akaitikia kwa kuwainulia mwanamume au mwanamke ambaye awashinde maadui na kuwarudishia amani (Amu 2:6-19). Watu wa namna hiyo wanaitwa “waamuzi”: maana ya neno hilo
si wasomi wanaosikiliza kesi na kutoa hukumu kadiri ya sheria zilizotungwa na bunge la nchi, bali walikuwa “watawala” wakati wa amani baada ya kushinda vita
vya ukombozi. Waliweza kuwa watu wa kila aina, hata
wasiotarajiwa kabisa, kwa kuwa mkombozi wa kweli alikuwa Mungu tu.
Habari za waamuzi hao 12 haziwezi kupangwa
kitarehe, kwa kuwa hazina dalili zinazotusaidia kujua ipi ilitangulia na ipi ilifuata. Waandishi wenyewe
hawakujua mwaka wa matukio hayo, hivyo walikusanya kumbukumbu walizokuwanazo kama kwamba waamuzi walifuatana mmoja baada ya mwingine
kuongoza Israeli. Ukweli ni kwamba waliweza kuongoza kwa wakati mmoja huyu huku na huyu
huku, kwa kuwa kila mmoja alihusika na eneo fulani tu. Kwa kuwapanga mmoja
baada ya mwingine, waandishi waliweza kusisitiza mara 12 kwamba Waisraeli
walirudiarudia dhambi, na kwa sababu hiyo walirudiarudia kupewa na Mungu adhabu aliyoitabiri Musa. Lakini fundisho muhimu zaidi ni kwamba Bwana, bila ya kujali ugeugeu wao, daima alikuwa tayari kuwaokoa walipomlilia msaada.
Mwamuzi mmojawapo ni Gideoni aliyedumisha amani kwa miaka 40. Alipoitwa na Mungu alijitetea kwa kusisitiza udogo na ufukara wake, lakini akajaliwa ishara zote alizoziomba ili kuhakikishiwa msaada (Amu 6:11-24,36-40). Sura ya
7 inasimulia Mungu alivyopunguza askari wake ili ionekane wazi kuwa ushindi ni
wa Mungu mwenyewe, hautegemei uhodari na wingi wa watu au silaha zao. Ni
kawaida ya kazi ya Mungu kuonyesha uweza wake katika udhaifu wa binadamu.
Waisraeli walipotaka Gideoni awe mfalme wao, akakataa katakata ili Bwana tu aendelee kuwatawala (Amu 8:22-23), lakini
wazo hilo likaendelea kuenea, ingawa wengine walilipinga (Amu 9:1-21).
Nyongeza ya kitabu inaonyesha kuwa kumwasi Mungu kulisababisha hatimaye
Waisraeli kupigana wenyewe kwa wenyewe. Ni kwamba, ukivunja amri ya kwanza unaweza kuja kuzivunja zote, na ukimkataa bab, hutakubali tena ndugu zako. Mstari wa mwisho unaeleza sababu nyingine ya fujo hizo: kutokuwepo mfalme mmoja juu ya makabila yote 12. Kwa kusema hivyo, kitabu kinatuandaa
kusikia katika vitabu vinavyofuata jinsi ufalme wa Israeli ulivyoanzishwa kwa usimamizi wa Samweli, nabii na mwamuzi wa mwisho lakini mkuu kuliko hao 12.
Ruthu
Ruthu alivyochorwa na Antonio Cortina Farinós.
Katika fujo ya miaka ile, habari ya kitabu
hiki kifupi inatujenga: inahusu mwanamke huyo Mpagani wa kabila la Moabu aliyeolewa na Mwisraeli huko ng’ambo ya Yordani. Baada ya kufiwa mume
wake akafuatana na mama
mkwe hadi Bethlehemu ili aolewe na ndugu wa marehemu na kumzalia mtoto kadiri ya sheria. Huyo mtoto akawa babu wa Daudi. Hivyo kwa uaminifu wake mwanamke huyo pia akatajwa katika
Injili kama bibi wa Yesu (Math 1:5-6).
Samweli (1050-1015 hivi B.C.)
Vitabu viwili vya Biblia
ya Kikristo vinaitwa kwa jina la mtu huyo, ambaye kwa
njia yake Israeli ilianza kuwa na umoja zaidi na hatimaye kuwa ufalme. Badala ya kila kabila kujitegemea, yote 12 yalikubaliana yawe na kiongozi mmoja wa kudumu ambaye cheo chake kirithiwe na mwanae. Kwa umoja huo waliweza kushinda maadui wao.
Vitabu hivyo vimekusanya kumbukumbu zote kuhusu mwanzo wa ufalme (1070-972 hivi K.K.), yaani kuhusu Samweli mwenyewe na wanaume wawili aliowapaka mafuta watawale Israeli kwa niaba ya Mungu: kwanza Sauli, halafu Daudi. Kumbukumbu hizo zilikuwa nyingi na tofauti, hivyo tunakuta humo tata
nyingi kuliko katika vitabu vingine vyote vya Biblia. Hasa mna hoja za kukubali mfumo wa ufalme na hoja za kuukataa.
Ukuu wa Samweli ulidokezwa na uzazi wake wa
ajabu, kwa kuwa mama yake alikuwa tasa akampata baada ya kusali na kuweka nadhiri (1Sam 1). Hivyo baada ya miaka michache alihamia Shilo kwenye sanduku
la agano kama mtumishi wa kuhani Eli.
1Sam 3 inasimulia wito wake: akiwa amelala karibu na sanduku hilo akaamshwa na Mungu mara tatu
mpaka akafundishwa na Eli kumtambua na kumuitikia Mungu. Hapo akamtabiria Eli
adhabu kali, na hivyo Israeli ikajua kuwa amefanywa nabii wa Bwana.
Samweli aliwaamua Waisraeli kwa kuwakomboa
mikononi mwa Wafilisti (1Sam 7), lakini ni muhimu hasa kwa kuwaanzishia ufalme kwa kuwaweka wakfu kwanza Sauli halafu Daudi. Kadiri ya 1Sam 8, yeye na Mungu hawakupendezwa na jinsi
Waisraeli wengi walivyotaka kuiga mtindo wa mataifa yote: Samweli
aliwaangalisha kuhusu matatizo na unyonyaji wa wafalme, naye Mungu aliona
katika ombi hilo uasi ambao Waisraeli wanamkataa asiwatawale tena, lakini
akamuagiza Samweli awakubalie.
Ukweli ni kwamba mfalme aliwekwa wakfu kwa Mungu kama mwakilishi wake akitakiwa kutimiza matakwa yake, hasa kwa kusikiliza anamuambia nini kwa kinywa cha manabii wake. Ndiyo sababu Samweli alizidi kumuelekeza Sauli, na hatimaye
akamkataa kwa ukaidi wake. Mabishano kati ya Samweli na Sauli ni mwanzo wa mabishano yote kati ya manabii na
wafalme ambao hawakutaka kumtii Mungu, na hatimaye wakadhulumu na kuua manabii
wake. Mamlaka ya neno la Mungu lililoletwa na nabii ilitakiwa kuwa juu ya mamlaka ya serikali na nguvu ya kijeshi alivyokuwa navyo mfalme. Lakini mara nyingi wafalme, kwa
kujivunia cheo chao, walishindwa kumnyenyekea nabii wa Mungu, wakaona afadhali
kufuata manabii wengine wengi waliosema uongo ama kwa kudanganywa na matarajio yao ama kwa kujipendekeza kwa mfalme
na kwa taifa lote.
Mfalme Sauli (1030-1010 hivi K.K.) na mfalme
Daudi (1010-970 hivi K.K.)
Picha
ndogo inayomchora Samweli akimweka wakfu mfalme Daudi.
1Sam 9:11-10:16 inasimulia Sauli
alivyoteuliwa kuwa mfalme wa kwanza. Akitawala karibu miaka ishirini, alifanya
makosa na kulaumiwa na Samweli, hata akakataliwa kabisa na Mungu kwa kutomtii
kikamilifu (1Sam 15). Ingawa akaendelea kutawala kwa muda fulani, polepole
alijitokeza kijana Daudi ambaye akaja kuanzisha ukoo wa kifalme wa milele.
1Sam 16-17 inaanza kutuletea mkusanyo wa hadithi juu ya Daudi ambazo zinampatia sifa aliyostahili, ingawa nyingine
zinagongana: k.mf. kama aliingia katika utumishi wa Sauli kutokana na uhodari
wake katika muziki au katika vita. Uhodari huo wote ukaendelea kusifiwa ila
Daudi aliutumia kwa utukufu wa Mungu: ndiye aliyeingiza ala mbalimbali katika
ibada na kutunga zaburi kadhaa, na ndiye aliyeeneza utawala wa Israeli kuliko
yeyote.
Kadiri alivyozidi kupendwa na Mungu na watu,
Sauli alimchukia kwa kijicho na kutaka kumuua (1Sam 18:6-16). Daudi
alipolazimika kukimbia na kuunda kikosi chake akapata nafasi rahisi ya kumuua
Sauli lakini alijizuia kwa kuheshimu krisma aliyopakwa awe mfalme (1Sam 24 na
26): hivyo ni mfano bora wa kujali wito wa Kimungu.
Baada ya kufanywa mfalme wa kabila lake
(Yuda, yaani Kusini) na ya kupigana vita na mwana wa marehemu Sauli, Daudi
akakubaliwa kuwa mfalme wa Israeli yote (yaani Kaskazini pia): pamoja na
taarifa hiyo, 2Sam 5:1-12 inatuambia alivyoteka Yerusalemu uliokuwa bado
mikononi mwa Wapagani akaifanya makao makuu ya kisiasa na ya kidini ya taifa
lote la Mungu ili aunganishe Kaskazini na Kusini katika mji huo uliopo
katikati. Kuanzia hapo Yerusalemu ukawa mji mtakatifu wa dini tatu
zinazomuabudu Mungu wa Abrahamu.
2Sam 6 inasimulia sanduku la agano
lilivyohamishiwa Yerusalemu kwa shangwe kubwa; hasa Daudi alicheza mbele ya
Mungu kwa nguvu zake zote huku amevaa nguo ndogo ya kikuhani tu, bila ya
kujijali kama kifalme. Kwa unyenyekevu wake alimpendeza Mungu akapewa naye
ahadi ya ajabu, yaani kwamba ufalme wake utadumu milele (2Sam 7). Pamoja na
hayo, Daudi akabaki kielelezo cha mfalme wa Israeli, ambaye awe tofauti na
wengine wote kwa kuwa hasa mtumishi mnyenyekevu wa Mungu bila ya kuyumba kwa
kuelekea miungu mingine. Kisha kupewa ahadi hiyo alikwenda mbele ya Mungu na kusali
vizuri kama kawaida yake hata nje ya ibada: sala yake ya sifa na shukrani
imejaa mshangao kwa ukuu wa Mungu na fadhili zake na kumalizika kwa ombi
nyenyekevu. Ingawa hakukubaliwa kumjengea Mungu hekalu la ajabu alivyokusudia,
amekuwa mwalimu wa sala kwa nyakati zote: hata leo liturujia inategemea sana zaburi zake.
Utabiri huo wa nabii
Nathani ukawa chanzo cha uimara wa ufalme wa Yerusalemu kwa miaka 400 hivi, halafu ukaja kuongoza tumaini la Waisraeli hasa walipodhulumiwa, k.mf. zamani za Yesu chini ya ukoloni wa Kirumi, ambapo wote walimtazamia mwana wa Daudi mwenye kurudisha ufalme wa Israeli. Kwa mchango wa manabii mbalimbali ujio wake ulitarajiwa kuwa hatua mpya ambapo kasoro za wafalme waliotangulia zitakoma.
Matendo mengine tofauti yaliyoathiri sana
maisha ya Daudi ni dhambi alizotenda kwa ajili ya mke wa Uria Mhiti, yaani uzinifu, unafiki, ulevyaji na uuaji wa askari huyo mwadilifu (2Sam 11). Basi, Nathani akamuendea ili
kumlaumu na kumtabiria adhabu mbalimbali, hasa kwamba upanga hautaondoka
nyumbani kwake (2Sam 12:1-25). Ikawa hivyo hasa kwa sababu ya Absalomu mwanae ambaye alimuua kaka yake (2Sam 13:22-37) na baada ya kusamehewa
akafanya njama hata akamfukuza Daudi toka Yerusalemu (2Sam 14:28-15:29) akazini
na masuria wake mahali pa wazi (2Sam 16:20-23). Hata hivyo Daudi akazidi
kumpenda na alipoambiwa amekufa akamlilia kwa namna ambayo iliwashangaza na
kuwachukiza waliompigania: yeye ambaye alijiombea na kupewa msamaha wa Mungu
hakumchukia mwanae aliyehatarisha maisha yake (2Sam 18:19-20:8).
2Sam 24 pia inatuchorea sura yake ya kiroho:
alipoadhibiwa na Mungu kwa tauni iliyoua Waisraeli wengi baada ya yeye kuhesabu
askari wote alioweza kuwategemea vitani, basi kama mchungaji mwema aliomba
adhabu imuangukie mwenyewe, lakini si kondoo zake wasio na kosa. Mfalme wa
kumpendeza Mungu ni mchungaji wa watu wake; Kristo mwana wa Daudi anawajua
kondoo zake mmojammoja kwa jina, naye amejitwisha adhabu ya makosa yao: ndiye
mfalme na mchungaji bora.
Habari za mwisho za Daudi zinapatikana katika
1Fal 1-2 tunaposikia juu ya njama ya mtoto mwingine: Adonia alitaka kutawala akajifanya mfalme huku Daudi mkongwe hana habari.
Lakini Nathani akaingilia kati ili mwandamizi awe Solomoni, ambaye alipozaliwa na mke wa Uria alimhakikishia Daudi msamaha wa
Mungu.
Vitabu vya Wafalme
Vitabu hivyo viwili vinapitia historia ya Israeli kuanzia mwaka 972 hadi 560 hivi K.K. vikionyesha mwenendo wa kila mfalme upande wa dini, hasa katika kutekeleza maneno ya Kumbukumbu
la Torati, ya kwamba Mungu ni mmoja, hivyo hekalu lake liwe moja tu. Kwa kuwa wafalme wote wa kaskazini na karibu wale wote wa kusini walikwenda kinyume, vitabu hivyo vinaanza na ufalme imara na wa fahari ulioweza kumjengea Mungu hekalu la ajabu, kumbe vinaishia na hali mbaya na ya aibu kuliko ilivyokuwa kabla ya Musa, wafalme wakiwa wafungwa Babeli, Waisraeli wote uhamishoni na hekalu lenyewe magofu tu.
Lakini waandishi hawakusimulia hayo ili
kutunza kumbukumbu za zamani kama wanavyofanya wanahistoria, bali kwa lengo la kuonyesha tena uaminifu wa Mungu, aliyezidi kutuma manabii wake hata baada ya kuona hawasikilizwi, bali wanadhulumiwa hata kuuawa.
Kwa kutegemea uaminifu huo, Wayahudi waliohamishiwa Babeli waliweza kutumaini mwanzo mpya. Hasa manabii wa
mwisho wa wakati huo, Yeremia na Ezekieli, waliwatia moyo kuwa Mungu atabadili mioyo yao na kufanya nao Agano Jipya.
Mfalme Solomoni (970-931 hivi K.K.)
Solomoni katika ikulu yake (kadiri ya Ingobertus, 880 hivi).
Ufalme wake uliweza kustawi kuliko ule wa
baba yake kutokana na msingi imara aliouweka Daudi. Lakini mwenyewe
aliudhoofisha na kusababisha mara baada ya kifo chake utokee utengano kati ya
makabila ya Kaskazini na yale ya Kusini.
Kati ya kazi muhimu alizozifanya, mojawapo ni
kujenga hekalu la Yelusalemu na kuliweka wakfu kwa sherehe kubwa ya siku saba,
ambapo Mungu alionyesha kibali chake kwa kulijaza kwa sura ya wingu (1Fal 8).
Polepole hekalu hilo likaja kuwa la pekee hata patakatifu pengine pote
pakakatazwa chini ya mfalme Yosia.
Ingawa Solomoni anasifiwa kwa hekima yake, alishindwa kukwepa majivuno na tamaa, akataka kuwapendeza wake zake waliokuwa 700 (mbali na masuria
300), wengi wao Wapagani, hata akawajengea mahali pa kuabudia miungu yao
akamchukiza Mungu hata akamtabiria mtoto wake atanyang’anywa sehemu kubwa ya
ufalme (1Fal 11:1-13) ikawa hivyo.
Baada yake, makabila ya kaskazini
yalitawaliwa na wafalme wa koo mbalimbali (931-722), kumbe yale ya kusini
yalitawaliwa na watu wa ukoo wa Daudi tu (931-587). Wafalme wote wa kaskazini
wanasemwa kuwa wabaya. Kati ya wafalme wa kusini, wema ni 2 (Ezekia na Yosia); wengine wema kiasi; wengine wabaya. Hatimaye Waisraeli wa
kaskazini walipelekwa uhamishoni Ashuru (722) wasirudi tena. Wale wa kusini walipelekwa uhamishoni Babeli (587)
lakini baadhi wakarudi (kuanzia 538).
Manabii
Nathani akimlaumu Daudi na kumtabiria adhabu.
Tofauti na mtangulizi wake, Daudi alimpendeza Mungu, si kwa sababu hakufanya makosa, bali kwa sababu alikuwa tayari kumsikiliza akisema kwa njia ya manabii wake Nathani, Gadi n.k. Alikubali kukosolewa, kuonywa na kuambiwa la kufanya. Kila mfalme baada yake alitakiwa kufanya hivyo.
Kwa kiasi kikubwa, miaka ya wafalme wa
Israeli na Yuda ni pia miaka ya manabii bora walioinuliwa na Mungu alivyotaka
ili kuwakemea au kuwafariji Waisraeli. Kazi yao kubwa haikuwa kutabiri
yatakayotokea, bali kuwa madaraja kati ya Mungu na watu wake, wakiwafahamisha yeye
anawaza na kutaka nini. “Nabii” ni hasa mtu “anayesema kwa niaba” ya Mungu. Si
lazima aandike kitu.
Njia zake za kuwasiliana na Mungu zinafanana
na zile za dini nyingine: kuota, kupata njozi, kutoka
nje ya nafsi na hata kutazamia kwa kutumia vifaa maalumu
vya kubashiria. Lakini polepole hivyo vya mwisho vikaja kulaumiwa, kumbe Neno
lenyewe likaja kushika nafasi ya kwanza kuliko dalili za ajabu zinazoweza
zikapatikana hata katika vichaa.
Kwa kuwa Roho ni wa Bwana tu, akijalia unabii
ni kama karama ipitayo: hivyo mtu yuleyule anaweza akasema mara ukweli mara
uongo. Vilevile karama hiyo haithibitishi usahihi wa imani na uadilifu wa
mhusika. Hatimaye baadhi yao wakaanza kuitwa "manabii wa uongo", kwa sababu ya kutabiri uongo kwa niaba ya Mungu (kwa makusudi
mazima au kwa kujidanganya) na zaidi kwa sababu ya kupotosha imani na maadili
ya taifa lake.
Manabii Eliya na Elisha (865-790 hivi K.K.)
Nabii Eliya alivyochorwa na José
de Ribera.
Waisraeli walielekea dini za kandokando kwa sababu zilikuwa zinaahidi kufanikisha maombi yao kwa ibada za hakika, wakati Mungu ana hiari ya kupokea au kukataa sadaka zao. Waisraeli walijaribu kufuata pande zote mbili kwa pamoja, ila
Mungu hakuweza kukubali, kwa kuwa ni peke yake tu. Imani yao iliyumba hasa wakati mfalme Ahabu alipotawala Kaskazini (869-850
hivi K.K.), ambapo Yezebeli, mke wake, alifanya juhudi kubwa za kuikomesha kabisa imani yao kwa YHWH ili wamuabudu Baali,
mungu mkuu wa kwao aliyehusika na mvua, kufuatana na sanamu mbili zilizotengenezwa na Yeroboamu I zikiwa na
sura ileile ya Baali (fahali wa dhahabu). Mezani pa malkia huyo walikuwa
wanalishwa manabii wa uongo 850 kumbe manabii wa Bwana waliuawa karibu wote.
Hapo Mungu akamtuma Eliya (1Fal 17-18) ambaye
jina lake lina maana ya kwamba, “Mungu wangu ni YHWH” na linajumlisha kazi yake ya kutetea kwa ari zote imani ya kweli hata akaiokoa. Ili kuondoa utata wa kuabudu pande mbili, Eliya kwanza alizuia mvua isinyeshe nchini
miaka mitatu na nusu, ibada kwa Baali zisifanikiwe hata kidogo, halafu
akashindana na manabii hao hadhara ya Israeli yote juu ya mlima Karmeli. Tofauti na mbinu za manabii 450 wa Baali, waliofikia kujichanja na kutoka damu ili kuvuta moto kutoka mbinguni wasifaulu, Eliya aliomba tu kwa unyofu kwamba Mungu ajitokeze ili kugeuza mioyo ya watu wake wamrudie. Kwa
kuteremsha moto toka mbinguni juu ya sadaka yake YHWH alithibitisha kuwa ndiye
Mungu pekee na kuwa anaendelea kuwaokoa watu wake. Baada ya Eliya kuwachinja
wote aliruhusu mvua inyeshe tena. Ndiyo sababu anasifika kwa nguvu ya sala yake
(Yak 5:17-18).
Hasa ni kwamba, baada ya kukimbia hasira ya Yezebeli aliyemuapia atamuua kabla ya kesho yake, akisali pangoni juu ya mlima Sinai kama Musa mwanzoni mwa agano la Israeli na Bwana, alijaliwa kutokewa na kuagizwa upya na Mungu katika sauti ndogo ya
upepo mtulivu akamilishe kazi yake hasa kwa kuwafanya Elisha nabii na Yehu mfalme (1Fal 19:1-18). Hata katika Yesu kugeuka sura mlimani akatokea
pamoja na Musa ili wamshuhudie kama wawakilishi wa Torati na Manabii (Mk
9:2-13).
Kwa jinsi alivyofanya kazi kwa ari, na kwa
kupalizwa juu ya gari la moto (2Fal 2:1-18) akalinganishwa na moto (YbS
48:1-11) akatabiriwa atarudi kabla ya siku ya Bwana (Mal 3:23-24). Ndiyo sababu
Injili zinamtaja mara nyingi.
Elisha akimfufua mtoto wa mwanamke Mshunami katika mchoro wa mwanzo wa karne ya 20.
Kwa miaka zaidi ya 50 kazi yake iliendelezwa
na Elisha, ambaye anasifika pia kwa miujiza yake (YbS 48:12-16) na pamoja na
mwalimu wake amechukuliwa na Yesu kama mfano wa unabii wake utakaowaokoa
mataifa baada ya Israeli kumkataa (Lk 4:24-27). Elisha alijihusisha sana na siasa akaombwa shauri na wafalme mbalimbali hata wa nchi
za nje. Kwa kumpaka mafuta Yehu alianzisha mapinduzi dhidi ya ukoo wa Ahabu na kukomesha upotoshaji wake wa imani. Mapinduzi hayo yakaenea kusini kwa kumuua Atalia, dada (au binti) wa Ahabu, aliyetawala miaka saba kisha kuua watu wote
wa ukoo wa Daudi (mtoto Yoashi tu alinusurika).
Nabii Amosi (786-746 hivi K.K.)
Nabii Amosi kadiri ya Gustave Doré.
Mungu aliendelea kukazania ufalme
wa kaskazini kabla haujaangamizwa kabisa: tahadhari kabla ya hatari. Ndiyo sababu alimtuma huko Amosi kutoka ufalme
wa kusini, alipokuwa mfugaji karibu na jangwa. Amosi aliona maendeleo makubwa ya kaskazini chini ya mfalme Yeroboamu
II, lakini hakudanganywa nayo, bali alitabiri
yatakoma mapema. Aliona Waisraeli wanaoshika sabato na ibada mbalimbali, lakini wananyanyasa wenzao maskini: hapo akapiga kelele kudai kwanza haki itiririke kama maji ya mto ili ibada ziwe na maana. Hatimaye alikatazwa asiendelee kuhubiri, pia
kwa sababu alikuwa mtu wa kusini, hivyo walifikiri anasema kwa kijicho tu.
Tofauti na Eliya na Elisha wasioacha maandishi, nabii huyo ana kitabu chenye mafundisho yake
aliyoyatoa Kaskazini ingawa alikuwa mtu wa Kusini. Hakutarajia kutumwa na
Mungu, ila ilimbidi akubali kutabiri kwa niaba yake (7:10-17), hasa kuwa
Israeli itaangamizwa na kutekwa na Waashuru utumwani kwa makosa dhidi ya imani
na ya haki pamoja na anasa (5-6). Waisraeli wakakataa maneno yake hata
wakatendwa alivyowatabiria (2Fal 17:5-23).
Nabii Hosea (750-725 hivi K.K.)
Picha ya nabii Hosea ya karne ya 18, monasteri ya Kizhi, Karelia, Russia.
Muda mfupi baada ya Amosi, nabii Hosea alianza kazi yake katika ufalme wa kaskazini pia, akaweza
kuendelea nayo kwa muda mrefu akiwa mwenyeji. Yeye hakufundisha kwa maneno tu, bali hasa kwa maisha yake: mtindo wa kufikirisha kwa matendo ya kushangaza ulitumiwa na
manabii wengi, hata na Yesu.
Aliitwa kuoa kahaba ili awaonyeshe Waisraeli katika matatizo ya ndoa yake jinsi Mungu alivyopenda taifa hilo ingawa linapenda kufuata miungu mingine badala ya kuwa aminifu
kwake tu. Kwa mfano hai wa Hosea, Mungu alitaka waelewe kwamba kwa kuwapenda na
pengine kuwaadhibu analenga tu hatimaye wampende kwa moyo wote.
Sura 1-3 zinasimulia Hosea alivyompenda mke
wake aliyemzalia watoto wa uzinzi, hata hivyo akaendelea kumpenda na kumtafuta hata baada ya kumfukuza,
akamkomboa na kumrudisha ili ambembeleze zaidi na hatimaye amfanye amrudishie upendo kama wakati wa uchumba. Hivyo adhabu yenyewe ilitokana na upendo na kulenga umoja wa dhati.
Hata Mungu, baada ya kuacha Israeli ishindwe
na Waashuru, ataendelea na upendo wake kwa wenzao wa kusini, akiwabakiza kama mbegu (ndio “mabaki ya Israeli” yaliyozungumziwa kwanza na Amosi): mpango wa Bwana unapitia hatua mbalimbali lakini haukatiki kamwe.
Mfano huo wa upendo wa Mungu kwa bibiarusi asiye mwaminifu uligusa sana watu ukazidi kuzingatiwa mpaka katika Agano Jipya na kuchangia uimara wa ndoa iliyofikiriwa upya kama upendo mwaminifu, si kama uhusiano wa kisheria au wa kimwili tu ambao udumu mpaka utakapoendelea kuleta faida. Zaidi ya hayo, uliwaelekeza Waisraeli kupokea fundisho la Yesu kwamba dini ni suala la upendo, si ibada wala sheria tu.
Nabii Isaya (740-700 hivi K.K.)
Wakati wa Hosea kufanya unabii kaskazini, Mungu aliita wengine kusini; kati yao muhimu zaidi ni Isaya,
kuhani wa Yerusalemu mwenye elimu nzuri ambayealizaliwa Kusini mwaka 765 hivi, akatabiri kwa muda
usiopungua miaka 40 akiingilia kati matukio yote ya siasa, ambayo yalikuwa ya
kutisha kutokana na nguvu za Waashuru ambao waliangamiza Israeli na kukaribia kufuta hata ufalme wa Kusini.
Maandishi yake yanapendeza kuliko yote, hasa
upande wa ushairi. Lakini ukuu wa Isaya uko hasa upande wa imani.
Kuanzia wito wake alioupata hekaluni, alipong’amua kwamba Mungu ni mtakatifu kabisa,
yaani tofauti mno na yeyote na chochote (6), alitawaliwa na wazo la utukufu wa Mungu na la unyonge wa binadamu anayehitaji kutakaswa naye. Kwa msingi huo alidai wafalme
na wananchi wote wa Yuda wamtegemee Mungu tu, si mataifa yenye nguvu, hata
upande wa siasa na mbele ya hatari kubwa namna gani.
Lakini toka mwanzo aliambiwa hatasikilizwa,
hivyo ikambidi atabiri adhabu. Kweli hali haikuwa shwari, ndiyo sababu wengi walishindwa kuamini na kutulia, wakaendelea
kujifanyia mipango na kutafuta msaada kutoka kwa binadamu, hasa Farao wa Misri. Hapo Mungu alimuagiza Isaya atembee uchi mwaka mmoja unusu ili kudokeza kuwa Wamisri watafanywa watumwa wa Waashuru wasiweze kusaidia kitu (20:1-6).
Katika kutuliza watu alimtabiria mfalme Ahazi kwamba mwanamwali atamzaa mtoto wa kiume atakayethibitisha uwepo wa Mungu pamoja na watu wake, jina lake Emanueli linavyomaanisha. (7:1-17) Kweli mke wa Ahazi alimzaa Hezekia atakayeendeleza ufalme wa ukoo wa Daudi, lakini utabiri huo ulimlenga zaidi Yesu, mwana wa Bikira (walivyoelewa watafsiri wa kwanza wa Biblia katika Kigiriki) ambaye kweli ni Mungu pamoja nasi, na ni mwana wa Daudi ambaye
atatawala milele kwa amani na haki (11:1-9).
Hivyo, pamoja na adhabu kwa utovu wao wa imani (22:1-14), Isaya aliwatabiria watu wa Yuda kuwa Mungu hataangamiza kabisa taifa lake, bali ataacha mabaki yake
ambayo yataleta wokovu (10:20-23): katika mabaki hayo Bikira atamzaa Masiya
ambaye ni Mungu pamoja nasi, mwana wa Daudi ambaye ataleta amani na haki
duniani.
Nafasi ya mwisho kwa Isaya kutuliza watu
ilikuwa mwaka 701
K.K. ambapo jeshi kubwa la Waashuru lilizingira Yerusalemu na kutamka maneno ya kumkufuru
Mungu. Isaya aliwarudishia jibu la dharau, nao kweli wakakimbia haraka baada ya kupatwa na tauni.
Isaya ni maarufu pia kwa ubora wa mashairi yake yaliyofanya ujumbe wake upendeze na uguse zaidi. Kwa sababu hiyo
wengi walipenda kuyakariri na kuyasoma na hata kuiga mtindo wake: ndiyo maana
kitabu chake kiliongezewa maandishi mengine mengi mpaka miaka mingi baada ya
mwenyewe kuuawa kwa kukatwa kwa msumeno.
Nabii Mika (740-700 hivi K.K.)
Nabii Mika kadiri ya Gustave Doré.
Wakati mmoja na Isaya alifanya kazi nabii Mika ambaye pia alitetea haki za wanyonge (2:1-11) na kutabiri adhabu.
Vilevile alitabiri juu ya Masiya kwamba atazaliwa Bethlehemu (5:1-3).
Baada ya hapo hatujui vizuri kilichoendelea
kwa miaka 60: au Mungu hakutuma manabii kwa sababu maangamizi ya ufalme wa kaskazini yameshatokea na yale ya kusini yako bado mbali,
au mfalme Manase aliyetawala karibu miaka 50 aliwaua wote akitaka watu wake wafuate dini
ya Waashuru ili kuwapendeza mabwana hao. Kumbe chini ya mjukuu wake, mfalme mwema Yosia, manabii wakatokea tena mfululizo kabla ya maangamizi ya Yerusalemu
yaliyochangiwa na watoto wake ambao hawakufaa kitu hata wakasababisha ukoo wa
Daudi kukoma kutawala (586
K.K.).
Nabii Sefania (640-625 hivi K.K.)
Sefania akiwahubiria watu (mchoro wa huko Ufaransa, karne
ya 16.
Mtu huyo wa Yerusalemu alihubiri kwa nguvu
mwanzoni mwa ufalme wa Yosia, kabla huyo hajaanza urekebisho wake wa kidini
uliofuata kuvumbua hekaluni maandiko ya Kumbukumbu ya Sheria. Pamoja na kutisha
kwa matabiri yake, aliahidi wokovu kwa mabaki ya Israeli, akisema watakuwa watu
maskini na walionewa (3:9-20). Ndio mwanzo wa imani ya kuwa wapenzi wa Mungu ni
hasa mafukara, ambayo taratibu ilitia mizizi katika Israeli hadi ilipokuja
kukaziwa na Yesu (Lk 6:20-21).
Nabii Yeremia (626-585 hivi K.K.)
Mchoro wa Rembrandt
van Rijn, "Yeremia Akililia Maangamizi ya
Yerusalemu", mwaka 1630 hivi.
Akiwa bado kijana, kuhani huyo mpole aliitwa na Mungu awe nabii katika kipindi cha misukosuko huko Mashariki
ya Kati, ambapo Wakaldayo wa Babeli waliwashinda Waashuru na kueneza utawala wao hadi kuteketeza Yerusalemu na hekalu lake. Katikati ya matukio hayo yote, Yeremia alipewa kazi ngumu ya
kuonya na kutisha watu wa ufalme wa Yuda kwa kutabiri maangamizi hayo ili wamrudie kweli Mungu wasipatwe na adhabu kali kama wenzao wa kaskazini. Lakini wao hawakuwa tayari kufanya hivyo, wakijiamini hawatakoma kwa
kuwa, tofauti na hao, wanatawaliwa na ukoo halali wa Daudi ulioahidiwa kudumu milele, tena wanatunza hekalu pekee la Mungu na sanduku la agano analokalia. Walidanganywa na manabii wa uongo waamini hivyo, kumbe walitakiwa kujirekebisha na kufuata kweli masharti
ya agano lenyewe.
Hivyo Yeremia alilazimika kupambana na wote:
wafalme, makuhani na manabii wenzake, ndugu wa ukoo wake na wananchi kwa jumla. Ilimbidi ashindane nao kinyume cha silika yake ya upole iliyomfanya apende kuelewana na watu. Upweke wake ulizidiwa na useja alioitiwa na Mungu ili aonye hata kwa njia hiyo kwamba mambo yajayo ni
magumu na ya kutisha hata iwe afadhali kutozaa watoto.
Katika miaka yote 40 na zaidi ya unabii wake kipindi kizuri ni miaka ile 13 tu (622 - 609
K.K.) ambapo Yosia alifanya urekebisho wa kidini kuanzia Yerusalemu hadi kwa mabaki ya Waisraeli wa kaskazini, akizuia wote wasiabudu miungu mingine wala wasimtolee
Mungu sadaka nje ya hekalu
la Yerusalemu. Kipindi hicho mji mkuu wa Ashuru
uliangamizwa alivyotabiri kwa furaha Nahumu (612 hivi K.K.).
Lakini Yosia alipokufa vitani kabla ya wakati mambo yakaharibika haraka sana, kwa sababu urekebisho
ulitokana zaidi na juhudi zake binafsi. Basi, ikambidi Yeremia awakaripie wafalme waliomrithi
mmoja baada ya mwingine waache siasa yao ili kumtegemea Mungu tu. Aliwakaripia pia wananchi wasifanye dini
kisingizio cha kuendelea na maovu badala ya kutubu (7:1-15; 19:1-13).
Aliwakaripia vilevile manabii wa uongo
waliotumainisha watu bure (20:1-6). Ndipo alipoanza kupigwa, kufungwa na
kuhukumiwa, akawa mfano wa Yesu, yeye ambaye peke yake katika Agano la Kale
aliishi bila ya ndoa kwa agizo la Mungu; lakini hakuuawa (26:1-19). Kwa hofu
akajificha, ila hakuacha kutabiri maangamizi kwa maandishi kwa njia ya karani
wake Baruku (36).
Basi, mfalme Nabukadreza II wa Babeli akazidi kuwa na nguvu: mwaka 602 K.K. akamtiisha mfalme Yehoyakimu wa Yuda, na mwaka 598 K.K. akazingira Yerusalemu akawahamishia Babeli
mfalme Yekonia na viongozi wengine 8000. Hapo Yeremia akawaandikia wasikate tamaa ila
wasitarajie kurudi upesi kwa kuwa watabaki uhamishoni miaka 70 (29:4-23). Lakini
katika mpango wa Mungu hao ndio wa kutegemewa, sio walioachwa Yerusalemu (24).
Nabukadreza alipohusuru mji huo mara ya pili, mfalme na viongozi wengine
walikataa shauri la Yeremia la kusalimu amri, wakamfunga pabaya sana mpaka siku
ya Yerusalemu kutekwa na kuteketezwa (37-38).
Yeye alishuhudia hayo yote kwa huzuni kubwa na kati ya dhuluma nyingi hata akamlalamikia sana Mungu kwa kumuumba awe mtu wa mateso. Toka mwanzo alitaka kukataa wito wa unabii, na baadaye akafikia hatua ya kukata tamaa. Lakini Mungu alimuita kwa
mpango wa milele, Yeremia asiweze kukataa (15:10-21; 20:7-18). Unyofu wa maneno yake katika sala (Maungamo
ya Yeremia) unatuwezesha kumfahamu mpaka ndani kuliko
mtu yeyote wa Agano
la Kale. Lakini mateso hayo hayakuwa bure, bali kwa
njia yake alizidi kuelewa dini kama suala la moyo. Ni hivyo kwamba aliona agano lililoandikwa katika mbao za mawe limeshindikana, na tohara inayohitajika ni ile ya masikio na moyo. Basi, kwa kutambua uaminifu wa Mungu, alitabiri agano litakaloandikwa katika mioyo ya watu, ambao
hapo wataweza kulishika na kumfahamu kweli Bwana.
Kwa kawaida Yeremia alitabiri kinyume cha
matazamio madanganyifu ya watu, lakini walipokata tamaa akawatuliza na kutabiri
heri. Basi, kilele cha mafundisho yake na ya Agano la Kale lote ni kwamba Mungu atafunga na Israeli yote Agano Jipya (31:31-34).
Baada ya Yerusalemu kuteketezwa (587 K.K.)
Yeremia alichagua kubaki nchini pamoja na mafukara badala ya kuhamia Babeli kwa
heshima ya pekee (39:8-40:6), ila ukatokea uasi akalazimishwa na Waisraeli
wenzake kuwafuata Misri: huko akawaonya wasifuate Upagani lakini wakakataa tena
kumsikiliza (42-44).
Hatimaye, kadiri ya mapokeo ya Wayahudi, akauawa nao huko. Ingawa alionekana kufeli kabisa, sadaka yake ilizidi kuzaa, kwa kuwa wengi walizingatia mafundisho yake bora.
Kama nyongeza ya kitabu cha Yeremia tuna Maombolezo matano juu ya Yerusalemu ulioteketezwa, ambamo inaonekana toba halisi
baada ya tukio hilo. Hatujui yametungwa na nani.
Nabii Habakuki (600 hivi K.K.)
Sanamu
ya Habakuki iliyotengenezwa na Donatello, Museo dell'Opera del Duomo, Florence.
Wakati huo aliishi pia Habakuki, aliyeandika kitabu kifupi ambamo alithubutu kumuuliza Mungu kwa nini
anaadhibu Israeli vikali hivyo kwa mikono ya watu wabaya kuliko wao. Jibu ni
kwamba Mungu ana njia zake ambazo anaandaa ushindi wa haki: hivyo mwadilifu
ataishi kwa imani yake (1:12-2:4). Usemi huo ukaja kutumika sana katika Agano
Jipya.
Nabii Ezekieli (592-570 hivi K.K.)
Ezekieli,
alivyochorwa na Pierre
Paul Rubens (1609-1610), Musée
du Louvre, Paris.
Polepole waliohamishiwa Babeli waliweza
kujitafutia kazi (kwanza kilimo, halafu biashara), wakafaulu sana, hata wengine
wakawa watumishi wa serikali. Lakini upande wa dini walikuwa hatarini, kwa
sababu imani ya Mwisraeli inategemea taifa, nchi na hekalu ambavyo vyote
vilikuwa vimeharibika.
Kwa ajili yao Mungu akatuma tena manabii,
hasa Ezekieli ambaye alihamishwa mapema mwaka 598 K.K.. Habari zake tunazipata katika kitabu chake tu, anapotajwa kwa jina mara tatu, kumbe kwa kawaida Mungu anamuita “binadamu”. Kabla hajahamishwa aliweza kumfahamu Yeremia, na kweli aliathiriwa na ujumbe wake ambao aliuunga mkono na
kuuendeleza. Alifanya unabii wake hukohuko uhamishoni, ingawa ujumbe wake uliwalenga waliobaki Yuda pia. Kwanza aliwatolea maneno ya hukumu ili watubu kabla hawajaangamia, lakini baadaye akawapa maneno ya faraja wasikate tamaa. Katika kuwahakikishia kuwa wataanza upya nchini kwao
aliwapa maelekezo yote kwa ajili hiyo. Kwa namna ya pekee, akiwa kuhani, kama
vile Yeremia, katika kitabu chake alishughulika sana na hekalu na mambo ya
ibada.
Upande mwingine alianzisha mtindo mpya wa
unabii ambao unaitwa wa Kiapokaliptiko (kilele chake ni Ufunuo wa Yohane) na ambao hauhusu tena matukio madogomadogo ya siasa, bali kwa njozi za ajabuajabu unaonyesha maana ya historia yote mpaka mwisho. Njozi 4 anazozisimulia kinaganaga na zisizosahaulika (utukufu wa Mungu kuhama hekalu, utukufu huo kurudi hekaluni, hekalu kutokwa na maji yenye uwezo wa kuponya hata Bahari ya Kifo, hatimaye mifupa mikavu kusimama na kuishi tena) zinachukua nafasi
kubwa katika kitabu chake na kwa mafumbo yake yanavutia ubunifu wetu ujitahidi kuelewa yaliyofichika katika mifano, tarakimu, rangi n.k.
Dini
ya Kiyahudi mpaka leo inategemea sana kazi aliyoifanya Ezekieli ya kukazia utekelezaji wa Torati hata pasipo uhuru
wa kisiasa. Muhimu kwake ni kwamba Wayahudi popote
walipo wamtukuze Mungu kwa kufuata sheria yake. Tena alitabiri kuwa Mungu tu atawawezesha kufanya hivyo kwa
kugeuza mioyo yao migumu kama mawe yadunde kama ile ya nyama, au vizuri zaidi kwa kuwatia moyo mpya na roho mpya wazishike amri zake (11:17-20; 36:26). Mungu atawaokoa kabla hawajatubu ili jina lake
litukuzwe katika watu wake: wokovu anaouleta hautegemei matendo mema ya
binadamu, bali muungano wa Mungu na wale walioitwa kwa jina lake (16:58-63).
Hakuna kitabu kinachosisitiza utukufu wa Mungu kuliko hicho.
Isaya II na III (550-500 K.K. hivi)
Ingawa Ezekieli alifanya kazi nzuri, waliokuwa uhamishoni waliendelea kuzoea na kufurahia mazingira mapya yenye ustawi wa kiuchumi wakazidi kupotewa na hamu na tumaini la kurudi Yerusalemu. Ndiyo sababu Mungu aliwatumia nabii mwingine mkubwa: hatujui jina lake, lakini tunamuita Isaya II kwa kuwa alifuata mapokeo ya Isaya na kulingana naye kwa ufasaha wa mashairi aliyoyatumia kutolea ujumbe wake; hivyo maandiko yake yamepangwa katika kitabu cha Isaya (40-55). Sehemu hiyo inaitwa pia kitabu cha faraja ya Israeli kwa sababu ililenga kuwatia moyo Wayahudi wenzake huko Babeli kwamba Mungu atawarudisha kwao akitumia kama chombo chake mfalme Mpagani, kwa kuwa yeye anatawala watu wote pamoja na mioyo yao (Is 40:1-11).
Hivyo akawafanya watamani kurudi badala ya kukwama katika kujitafutia maendeleo ya kidunia.
Kwa uchangamfu wa hali ya juu Isaya II alitabiri ukombozi na mwanzo mpya wa taifa kama ajabu kubwa kuliko lile la mababu wao kutoka Misri chini ya Musa. Alilifananisha na uumbaji mpya utakaowezekana kwa sababu Mungu wa Israeli si mmoja kati ya wengi,
walivyodhani kwa muda mrefu, bali kweli ni peke yake, hakuna mwingine: ndiyo sababu
anaweza yote. Imani hiyo ilizidi kutia mizizi kati ya Wayahudi na kuwaimarisha dhidi ya kishawishi cha kuabudu wengine.
Pamoja na hayo, katikasura hizo mna mashairi manne bora kuhusu mtumishi
mteswa wa Bwana ambayo ndiyo utabiri bora juu ya Yesu na juu ya wokovu atakaoleta kwa kuteseka mwenyewe ili kufidia dhambi za wote (42:1-4; 49:1-6; 50:4-9; 52:13-53:12). Hatimaye Isaya II ndiye
aliyeandaa dini ya Kiyahudi kupokea mataifa yote.
Isaya 56 66 ni sura za baadaye tena (Isaya III, mwaka 500 hivi K.K.) ambazo zinawakaribisha watu wa mataifa yote kujiunga na Israeli katika kumuabudu Mungu pekee. Kiini chake ni 61:1-3.
Wayahudi kuanza upya Yerusalemu chini ya
Waajemi (538-333 K.K.)
Koreshi Mkuu akiruhusu Wayahudi kurudi Yerusalemu kutoka Babuloni (mchoro mdogo wa Jean
Fouquet, 1470-1475 hivi).
Utabiri wa Isaya II ulitimia mwaka 538 K.K.
ambapo mfalme Koreshi
Mkuu wa Uajemi, mwaka mmoja baada ya kuteka Babeli, aliwaruhusu Wayahudi warudi Yerusalemu pamoja na vitu vilivyotekwa nyara toka hekalu lake ili kuvijenga upya.
Wengi hawakukubali kwa sababu walilinganisha mazingira hayo tofauti. Waliorudi walikuwa kama elfu tano tu na familia zao, lakini wote wenye imani na nia thabiti, wakiwemo makuhani na Walawi wengi waliorithi katika ukoo wao upendo kwa ibada za hekaluni.
Kama kawaida, imani yao ilitakiwa kupitia majaribu mbalimbali, kuanzia mazingira magumu, kwa sababu hali waliyoikuta ilikuwa mbaya kuliko ile ya kabla ya uhamisho: majengo na mashamba yalikuwa yameharibika kwa kukaa miaka 48 bila ya watu, tena makabila ya jirani hawakupenda Wayahudi warudi, hivyo waliwazuia kwa namna mbalimbali. Wasamaria, mchanganyiko wa mabaki ya Israeli kaskazini na watu wa mataifa walioletwa na Waashuru waishi nao, walitaka kusaidia ujenzi wa hekalu, lakini walipokataliwa wakawa maadui moja kwa moja.
Hata hivyo utabiri ulitimia, na kwa msaada wa Mungu kupitia watu wake mbalimbali, kuanzia manabii Hagai na Zekaria, kundi hilo dogo likawa mwanzo mpya wa taifa la Mungu: walimuabudu kwa
bidii katika hekalu jipya ingawa dogo (Ezra 3:10-13), walijipatia usalama kwa kujenga tena kuta za Yerusalemu (Neh 4:13-23; 12:27) na walijitenga kabisa na Wapagani: waliokuwa wameoa
wake wa kigeni walilazimishwa kuwafukuza pamoja na watoto waliowazaa kwa njia
yao (Ezra 9-10; Neh 9-10).
Gustave
Doré, Nehemia
Akikagua Magofu ya Ngome ya Yerusalemu, 1866.
Habari hizo zinapatikana hasa katika vitabu
vya Ezra na Nehemia, mfululizo wa vile vya Mambo ya Nyakati. Waandishi wa vitabu hivyo vinne waliishi miaka mia hivi baada ya
matukio: ndiyo sababu waliweza wakachanganya habari za hao watu wawili ambao
walifanya juhudi mpya tena kali, wa kwanza upande wa dini, wa pili upande wa
siasa, labda kwa nyakati tofauti. Nehemia alipokuwa liwali wa mkoa wa Yuda
wakazi walikuwa hamsini elfu tu, na eneo lao lilikuwa dogo sana. Kuhani Ezra
anasifiwa zaidi kutokana na mchango wake mkubwa katika kulipatia taifa teule
sura ya kudumu, kama watu wanaoambatana kabisa na Torati, ambayo toleo lake la
mwisho lilipitishwa na mfalme wa Uajemi wakati huo kuwa sheria kuu ya Wayahudi
(Ezra 7:1-28). Hivyo dini yao ikawa “dini
ya kitabu” hata leo.
Manabii wa mwisho wa Agano la Kale
Katika karne mbili za utawala wa Waajemi unabii ulizidi kufifia ukiacha nafasi kwa aina nyingine za uongozi
wa kiroho: wataalamu wa Torati na watu wenye hekima waliotunga vitabu kwa uvuvio wa Mungu bila ya kupatwa na hali za pekee kama manabii. Manabii wa mwisho walikuwa Hagai, Zekaria,
mwandishi wa Kitabu
cha Malaki, Obadia, na Yoeli, mbali na wengine ambao hatuwafahamu, lakini walihakiki na kuchangia
vitabu vya manabii waliotangulia.
Mwaka 520 K.K. Hagai alihimiza ujenzi wa hekalu jipya kama njia ya kujipatia baraka za
Mungu katika hali ngumu ya miaka ya kwanza baada ya kurudi Yerusalemu (1:3-11).
Hasa alitabiri kuwa siku za mbele utukufu wa hekalu hilo utakuwa mkubwa kuliko ule wa hekalu la Solomoni: ikawa hivyo kwa sababu ya upanuzi na urembaji ulioanza chini ya Herode Mkuu, lakini zaidi kwa sababu Yesu alilitakasa na kufundisha humo na hatimaye mwili wake mtukufu ukashika nafasi yake.
Wakati huohuo Zekaria naye alitamani ujenzi
huo lakini pamoja na toba ili ibada na makuhani wampendeze Mungu (1:3-6). Baada ya kumaliza ujenzi wa hekalu (515 K.K.), taratibu za ibada ziliendelea moja kwa moja, lakini tarajio la wengi la kuona mapema taifa la Mungu lina hali tukufu halikutimia. Hivyo ilitokea tena hali ya kukata
tamaa iliyowafanya makuhani na Wayahudi kwa jumla wamtumikie kwa uzembe.
Ndipo alipotumwa nabii Malaki kukaripia
makosa yao katika kumuabudu, akijibu hoja zao na kutabiri ujio wa mjumbe wa Agano na wa mjumbe mwingine
atakayemuandalia njia; hapo maadili na ibada vitaratibishwa tena (3:1-5) na
kila mahali itatolewa sadaka safi kwa Mungu (1:11). Katika wajumbe hao wawili
Wakristo waliwatambua kwa urahisi Yesu na Yohane Mbatizaji.
Baada ya kazi za Ezra na Nehemia, nabii
Obadia aliishia kutangaza kifupi adhabu ya Mungu
kwa Waedomu, kielelezo cha maadui wa taifa la Mungu, siku yake itakapofika.
Muhimu zaidi ni unabii wa Yoeli aliyetangaza vivyo hivyo siku ya Bwana akichukua mfano hai wa uvamizi wa nzige wengi uliolazimisha Wayahudi wote kufanya toba, lakini alitabiri pia mmiminiko wa Roho wa Bwana juu ya watu wake wa kila aina (2:28-32) alivyoomba Musa na utakavyowatokea wanafunzi wa Yesu siku ya Pentekoste (Mdo 2:16-21). Hivyo tapo la unabii kabla halijakoma lilitabiri kipindi kingine cha unabii chenye
kustawi kuliko cha awali.
Vitabu vya Hekima vya kwanza
Pengine ni wakati wa Waajemi kwamba, baada ya muda mrefu wa mapokeo
ya sauti, vilianza kuandikwa vitabu vya hekima (Kitabu
cha Methali, Kitabu cha Ayubu) na vinginevyo (Wimbo Ulio Bora, Zaburi nyingi). Wenye hekima ni watu wanaopatikana katika makabila yote, hasa kati ya wazee wenye mang’amuzi mengi. Toka zamani watu wa namna hiyo walitegemewa kwa malezi ya vijana ili wajue jinsi ya kukabili vizuri maisha. Mbali na mithali na mafundisho yaliyotolewa kwa sauti, baada ya uandishi kubuniwa hata vitabu vya namna hiyo vilianza kutungwa katika lugha mbalimbali. Waisraeli walifaidika na hekima ya nchi jirani zilizostaarabika zaidi, kwa namna ya pekee Mesopotamia na Misri. Hasa wakati wa amani na ustawi uliopatikana chini ya mfalme Solomoni, wenye hekima waliweza kujitokeza katika Israeli, kuanzia mwenyewe:
ndiyo sababu aliendelea kuchukuliwa kama kielelezo cha hekima.
Ingawa vinafanana na vile vya makabila ya
jirani, vitabu vya hekima vilivyomo katika Biblia vinafikiria maisha kwa mwanga wa imani katika Mungu aliye mmoja tu,
hasa kwa kuzingatia uzima na kifo, uchungu, mwenendo, heri n.k. Mithali ndicho
kitabu cha kwanza cha aina hiyo, hivyo kinatuletea mawazo na maneno ya zamani
zaidi na ya kwamba Mungu anamtuza mwadilifu na kumuadhibu mwovu hapa duniani.
Mtazamo huo ulianza kupingwa na kitabu cha
Ayubu kinakataa mtazamo huo kwa kuonyesha hali halisi, yaani kuwa duniani mara
nyingi mwadilifu ndiye anayeteseka; hata hivyo kinasema binadamu hawezi kujua
ni kwa nini: basi amuachie Mungu na kumuabudu katika fumbo lake linalozidi akili yetu (42:1-6).
Wimbo ulio Bora haumtaji Mungu wala dini:
ulihusu mapenzi ya wachumba, lakini ukaja kufafanuliwa kama mapenzi ya Mungu na
Israeli wanaotafutana ili kuungana kabisa. Zaburi, ambazo zilitungwa na
kurekebishwa polepole kwa muda unaokaribia miaka elfu, yaani muda ule wote
uliotumika kutunga vitabu vingine vyote vya Agano la Kale, ndizo sala za
kishairi au nyimbo ambazo katika hali ya sifa, ibada, shukrani na dua
zinajumlisha Biblia nzima.
Uenezi wa utamaduni wa Kiyunani (333-63 K.K.)
Mchoro wa Antonio
Ciseri, Kifodini
cha Watoto Saba (1863), unamuonyesha mama kati ya maiti za watoto wake 7 waliokubali kuuawa
kikatili ili wasiasi dini ya Kiyahudi.
Kwa muda mfupi sana Aleksanda Mkuu wa Makedonia (Ulaya Kusini Mashariki) aliteka Asia (mpaka India) na Misri. Kuanzia hapo utamaduni na lugha ya Kiyunani vikaenea pote, hata kwa Wayahudi wengi, hasa walioishi nje ya nchi yao.
Chini ya utawala wa Kiyunani unabii ukaja kwisha (1Mak 9:27): badala yake
yalitolewa maandiko ya kiapokaliptiko (hasa kitabu
cha Danieli ambacho ni kama Ufunuo wa Agano la Kale),
hadithi (Yona, Tobiti, Esta, Yudithi) na vitabu vingine vya hekima (Mhubiri, Yoshua
bin Sira, Hekima).
Humo tunaona maendeleo ya ufunuo, hasa kwa
sababu Wayahudi wengi walianza kusadiki ufufuko wa wafu na mengineyo. Nguvu ya
imani hiyo iliwasaidia kukabili dhuluma na kifo (2Mak 7:1-41) chini ya Antioko Epifane (175-164 K.K.) aliyetaka kuwalazimisha waache kufuata Torati ili
wajilinganishe na watu wengine. Tena akijidai kuwa tokeo la Mungu Mkuu alijenga
altare kwa mungu wake ndani ya hekalu la Yerusalemu. Hapo Wayahudi wakaanza
kupigania uhuru wao wa kidini na wa kisiasa chini ya ukoo wa Wamakabayo, ambao kwa imani na ushujaa mkubwa wakafaulu kushinda majeshi ya
kutisha (1Mak 3:18-22), kutakasa hekalu (1Mak 4:36-61) na kurudisha ufalme wa
Israeli mpaka baada ya Warumi kuweka Uyahudi chini ya himaya yao (63 K.K.). Habari hizo zinapatikana
katika vitabu viwili vya Wamakabayo ambavyo havifuatani kwa kuwa viliandikwa na
watu tofauti katika karne II K.K.
Matukio hayo ndiyo asili ya kundi la Mafarisayo (yaani “waliojitenga”), walioshika kwa bidii Torati kadiri ya mapokeo
ya walimu wa sheria, wengi wao wakiwa walei. Kwa jumla walileta uamsho wa
kiroho kati ya Wayahudi, lakini walidharau wenzao wasiojua Maandiko Matakatifu.
Pia walishindana sana na Masadukayo kuhusu masuala ya dini na ya siasa hata kusababisha mauaji; kwa kuwa
Masadukayo (waliokuwa na nguvu kati ya makuhani) walikataa mafundisho hayo
mapya huku wakishika Torati tu.
Yona ni simulizi lililowahimiza Wayahudi
waachane na ukabila kwa sababu Mungu anawahurumia watu wote (3-4). Kitabu cha
Tobiti kinachora uadilifu wa Kiyahudi: uaminifu kwa Torati, upendo katika
familia, sadaka kwa maskini, heshima kwa marehemu, utakatifu wa ndoa (12:6-22).
Vitabu vya Esta na Yudithi vinahadithia ushujaa wa wanawake hao ili kuhimiza
msimamo wa kufaa kwa wakati vilipoandikwa ambao ulikuwa mgumu kwa watu wa Mungu
(Est 3:13a-g; Yudithi 13:11-20). Mhubiri alisisitiza ubatili wa malimwengu yote
(1:1-11) akimuunga mkono mwandishi wa Ayubu: mang’amuzi yanaonyesha matarajio
ya kidunia hayana maana (8:10-17). Yoshua bin Sira alikabili pia masuala hayo
(15:11-16:23), akituelekeza tutafute jibu katika siku ya mwisho. Kitabu cha
Hekima kinakisiwa kuwa cha mwisho kuandikwa katika Agano la Kale kwa kuwa
kilitungwa miaka 50 tu K.K. huko Misri katika lugha na utamaduni wa Kiyunani.
Kina mpango mzuri sana na kutoa jibu wazi kuhusu suala la haki ya Mungu kwa
waadilifu na waovu, kikifundisha uzima wa milele (2:23-3:10) hata kuliko
kilivyowahi kufanya kitabu cha Danieli (12:1-4). Mbali na sehemu ya kitabu
hicho na ya Esta, vile vyote vilivyoandikwa karne mbili za mwisho K.K. na
kutunzwa kwa lugha ya Kiyunani vikaja kukataliwa na Wayahudi katika kubishana
na Wakristo waliovitumia (mwaka 80 hivi B.K.), halafu na Waprotestanti wengi.
Vinaitwa deuterokanoni (yaani “orodha ya pili”).
Baada ya Torati kuzidi kuzingatiwa na
Wayahudi, wataalamu wake pia walizidi kuheshimiwa kama watu wa Neno la Mungu,
wanaoleta mwanga wake katika maisha ya jamii. Hekima, iliyotafutwa hasa chini
ya Wagiriki, ilipotambulika kuwa inapatikana katika Torati, wataalamu hao
wakaja kushika nafasi ya watu wa hekima kama vile hao walivyoziba pengo
lililoachwa na manabii. Wayahudi walizoea hali hiyo kiasi kwamba wakaona vigumu
kumkubali Yesu ambaye hafafanui Torati kwa kufuata mapokeo ya wataalamu, bali
kwa kujiamini kama manabii waliojiona wabebaji wa Neno la Mungu. Kweli ndiye
Hekima ya milele ambaye ndani yake tunamjua Mungu, hivyo mwenendo wake na
mafundisho yake haviwezi kuishia mambo yaliyozoeleka, kwa sababu kila mara ya
Mungu yanapindua ya binadamu. La kufanya ni kujitahidi kufuata halafu kuelewa:
ndiyo wongofu ambao Yesu aliudai pamoja na imani.
Agano Jipya
Mazingira ya Yesu
Palestina katika karne ya 1 BK.
Nchi ambayo Yesu alizaliwa akafundisha ni
nchi ileile ambayo Mungu aliwaahidia Waisraeli tangu zamani za Abrahamu, ni
nchi ileile waliyoiteka chini ya Yoshua, ni nchi ileile waliyoirudia kutoka
utumwani Babeli. Lakini wakati wote wa Agano Jipya, yaani tangu Yesu
alipozaliwa hadi mwisho wa maisha ya mitume wake, nchi hiyo haikuwa huru, bali
chini ya himaya ya Warumi, ingawa pengine hao waliwakabidhi vibaraka, yaani watawala wenyeji waliowekwa na wakoloni. Vibaraka hao ni Herode Mkuu (37-4 K.K.) na wazawa wake, ambao tena hawakuwa Waisraeli halisi bali Waedomu ingawa kabila lao lililazimishwa kuingia dini ya Kiyahudi karne
iliyotangulia. Ukoo huo unajulikana kwa ukatili, uchu wa madaraka na uzinifu wake.
Vilevile maliwali wa Kirumi waliowekwa
pengine kutawala nchi au sehemu fulani walionyesha mara nyingi ukatili na
dharau kwa Waisraeli na dini yao, hata kusababisha chuki na mapigano kati ya
jeshi na wananchi. Mfano mmojawapo ni Ponsyo Pilato aliyesimamia Uyahudi kuanzia mwaka 26 hadi 36 B.K. Mbali na hayo,
utawala wa Roma, ulioenea Ulaya Magharibi na Kusini, Afrika Kaskazini na nchi za Mashariki ya Kati kupakana na Iraq ya leo, kwa
jumla ulihakikisha hali ya amani kwa muda wote wa Agano Jipya na karne za
kwanza za Kanisa. Hali hiyo, pamoja na umoja wa dola hilo lote, na urahisi wa
mawasiliano kwa njia ya barabara zilizotengenezwa na Warumi, na uenezi wa lugha
ya kimataifa (Kiyunani), ilichangia kasi ya uenezaji Injili. Lugha hiyo ndiyo
iliyotumiwa na waandishi wote wa Agano Jipya ili vitabu vyao viwafaidishe watu
wengi zaidi, ingawa baadhi yao hawakuijua vizuri.
Lugha asili ya Yesu na ya Mitume ilikuwa
Kiaramu ambacho ni jamii ya Kiyahudi na ambacho polepole kilishika nafasi yake
kati ya Wayahudi kuanzia karne VI K.K. Hao wote walitokea mkoa wa Galilaya, uliokuwa na mchanganyiko wa watu (Waisraeli na mataifa), kiasi kwamba
huko Wayahudi wenyewe walifuata kwa urahisi desturi za Kiyunani hata
wakadharauliwa na wenzao wa Kusini (Yerusalemu na mkoa wa Yudea). Kati ya mikoa
hiyo miwili ulienea mkoa wa Samaria ambao wakazi wake walijenga uadui mkubwa na Wayahudi baada ya uhamisho
wa Babeli, walipokataliwa kuchangia ujenzi wa hekalu la pili la Yerusalemu.
Maisha ya Yesu
Dionisi
Mdogo, mmonaki aliyeanzisha (mwaka 533 hivi) mtindo wa kuhesabu miaka kuanzia kuzaliwa
Yesu kurudi nyuma (K.K.) au kwenda mbele (B.K.), alikosea hesabu zake. Leo tunakisia Yesu alizaliwa mwaka 6 hivi K.K.
kwa sababu alizaliwa Bethlehemu chini ya Herode Mkuu aliyefariki mwaka 4 K.K.
Huyo alipojaribu kumuua mtoto Yesu, familia takatifu ilikimbilia Misri mpaka
baada ya kufa kwake. Hapo ikarudi Galilaya hata Yesu akajulikana kwa jina la
kijiji cha Nazareti kilichodharauliwa na Wagalilaya pia. Ndipo alipokulia na kuishi
akifanya kazi ya ufundi.
Nazareti katika kadi ya zamani ya Fadil Saba.
Yohane Mbaptizaji kadiri ya Bartolomeo
Veneto, karne ya 16.
Yesu akimponya mtu aliyepooza ni kati ya picha zake za zamani zaidi (karne ya 2); iko katika ukuta wa sinagogi la Dura
Europos.
Mwaka 26 hivi B.K. ndugu yake Yohane Mbatizaji aliacha maisha ya jangwani na kuanza kuhubiri toba kandokando ya mto
Yordani. Kwa kuwa Waisraeli walikosa manabii kwa muda mrefu, na walitamani sana
ukombozi, walimuendea kwa wingi hata wakamtia hofu Herode Antipa. Ingawa huyo akamfunga mapema akamuua, kazi ya Yohane ilikuwa imetimia
kwa sababu aliweza kuwaandaa Waisraeli wengi (hasa watu wadogo na wakosefu)
wampokee Yesu aliyebatizwa naye. Katika nafasi hiyo Yohane alimtambulisha kama
Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu.
Ndipo Yesu naye alipoanza kuhubiri, lakini
pia kutenda miujiza ya kila aina, akapata haraka wafuasi wengi. Kati yao
akachagua mitume wake 12 kama msingi mpya wa taifa la Mungu.
Alifanya kazi hizo kuanzia Galilaya, akitangaza
ujio wa ufalme
wa Mungu, kwa maana ya kwamba ufalme uliotazamiwa na
Wayahudi umewajia kwa njia yake.
Ingawa hakupitia shule yoyote ya Biblia, Yesu
alionekana anafundisha vizuri kuliko walimu wa sheria wa kawaida, kama mtu
mwenye mamlaka juu ya Torati. Mafundisho yake yalilingana na yale ya Mafarisayo
kuliko na yale ya Masadukayo, lakini alishindana pia na hao wa kwanza.
Kijicho na upinzani vikazidi hasa Yerusalemu,
walipoanza kufanya njama za kumuua. Ingawa Yesu alijua hayo, alijikaza kwenda
katika mji mtakatifu autangazie habari njema na kufia huko. Baada ya kupokewa
kwa shangwe kabla ya sherehe ya Pasaka ya mwaka 30 (au 33) akakamatwa na baraza
la Israeli kwa tuhuma ya kufuru ya kujilinganisha na Mungu, halafu akakabidhiwa kwa liwali wa Kirumi
aliyekuwa na mamlaka ya kutoa adhabu ya kifo. Baada ya kikao ambapo Wayahudi
walitafuta kisingizio cha kisiasa, Ponsyo Pilato akalazimika kuagiza Yesu
asulubiwe, na kisha kufa kwake kaburi lilindwe na askari.
Hata hivyo siku ya tatu kaburi likaonekana tupu, na Yesu akaanza kuwatokea wanafunzi wake wa kike na
wa kiume kwa muda wa siku arubaini, halafu akapaa mbinguni mbele ya macho yao.
Habari hizo zikatangazwa kwa sauti tu kwa
miaka kadhaa, halafu zikaanza kuandikwa.
Ufunuo kuendelea baada ya ufufuko wa Yesu
Kurasa 4 za Injili
ya Luka zilizonakiliwa katika karne ya 3 katika nyasi zilizopondwa.
Kifo na ufufuko
wa Yesu si mwisho wa ufunuo wa Mungu: ni lazima tupokee vilevile kama mpango wake yale yaliyojitokeza wakati
wa Mitume wake. Miaka hiyo 70 hivi iliona Kanisa likizidi kusogea mbali na dini ya Kiyahudi na kuwa la kimataifa kweli pamoja na kupata muundo wa kudumu wa uongozi. Sambamba na hilo, makao yake makuu yalihamia Roma kutoka Yerusalemu uliokuja kuangamizwa tena mwaka 70. Ni wakati huohuo kwamba lilipata vitabu
vitakatifu vya kwake vilivyokamilisha vile vya Agano la Kale. Kanisa linaheshimu kwa namna ya pekee, kama ushuhuda mkuu juu ya
maisha na mafundisho ya Yesu na kama moyo wa Maandiko matakatifu yote, Injili
nne zilizoandikwa na Marko, Mathayo, Luka na Yohane kati ya mwaka 65 na 100 hivi.
Mabadiliko hayo yaliyokusudiwa na Mungu hayakutokea bila ya matatizo, hasa kwa sababu yalikuwa magumu kueleweka kwa Wayahudi, ambao mwanzoni walikuwa wengi kati ya Wakristo, na hata kwa Mitume. Lakini Roho Mtakatifu aliwaongoza taratibu wakubali fumbo hilo lililofunuliwa hasa kwa Mtume Paulo. Suala gumu zaidi lilikuwa nafasi ya Torati katika Ukristo, hasa kwa waliojiunga nao moja kwa moja bila ya kutahiriwa kwanza ili wawe Wayahudi.
Katika Agano Jipya inajitokeza misimamo 4 tofauti, na ni ajabu kwamba haikuvunja ushirika wa imani. 1. Wakristo wenye asili ya Kiyahudi, hasa ya Kifarisayo, walitaka watu wa mataifa watahiriwe kabla hawajabatizwa, halafu wafuate masharti yote ya Torati ili waweze kuokoka. 2. Wengine,
kama Mtume
Petro na Yakobo Mdogo, walitaka washike walau baadhi ya masharti hayo ili wasiwe chukizo kwa Wakristo wa Kiyahudi, hasa wakati wa kula pamoja ekaristi. 3. Paulo alikataa kupunguza uhuru
wa Kiinjili kwa kudhani wokovu unategemea Torati kuliko msalaba wa Yesu; hata hivyo alisisitiza upendo kama tunu bora ya kuzingatiwa ili mtu asikwaze na kupoteza wengine dhaifu kama
hao Wakristo wa Kifarisayo. 4. Hatimaye ulijitokeza msimamo mkali zaidi, wa kupuuzia kwa kiasi fulani Torati kama kitu kilichopitwa
na wakati. Misimamo hiyo ya mwisho ulizidi kupata nguvu kadiri Wayahudi na
Wakristo walivyozidi kutengana, lakini hata ule wa kwanza uliacha athari yake ya kudumu katika Kanisa hasa kupitia Injili ya Mathayo na Barua
ya Yakobo.
Kitabu cha Matendo ya Mitume
Kati ya Wainjili, Luka hakuishia kuandika habari za Yesu tu, bali alizikamilisha kwa
kuandika kitabu cha pili chenye historia ya mwanzo wa Kanisa. Kinajulikana kwa
jina la Matendo
ya Mitume, kwa kuwa kinawatokeza hasa watu wawili
ambao Luka aliwafahamu, yaani Mtume Petro mpaka sura ya 12, halafu Mtume Paulo. Kwa namna ya pekee alikuwa mwanafunzi wa Paulo akamfuata mpaka kifo
chake: hivyo si ajabu kwamba alipenda kushuhudia kazi zake na mateso yake kwa
ajili ya Kristo na uenezi wa imani.
Mpangilio wa kitabu hicho unaelezwa katika
1:8, yaani kuonyesha jinsi imani hiyo ilivyoshuhudiwa toka Yerusalemu hadi
mwisho wa dunia upande wa magharibi. Ndiyo sababu kitabu kinaishia na habari za
Paulo kufikia Roma na kuanza utume huko mwaka 61, ingawa kuandikwa kiliandikwa kama miaka
20 baadaye.
Kuanzia Injili yake, Luka anaonekana
alivyojitahidi kuzingatia ukweli wa historia, lakini pia jiografia: katika Injili mambo yote yanaelekea Yerusalemu, ambapo Yesu alikwenda
kufa na kufufuka, na katika Matendo ya Mitume mambo yote yanaanzia Yerusalemu,
ambapo Roho Mtakatifu aliwashukia. Tukipenda kujua historia ya wokovu
ilivyoendelea baadaye, hatuna budi kufuata kitabu hicho tukilinganisha habari
zake na zile tunazozipata hasa katika barua za mitume. Kwa namna ya pekee zile
za Paulo tunaweza kuzipanga kwa faida katika mfululizo wa habari za maisha yake
alizotuachia Luka, ingawa kuna utatanishi fulani.
Kanisa la Yerusalemu
Pentekoste ilivyochorwa na Duccio
di Buoninsegna juu ya ubao (1308).
Kabla ya kusimulia uenezi wa Ukristo, Luka
aliandika habari za Kanisa mama, yaani lile la Yerusalemu. Katika msingi wake
tunaona mitume wakiwa wanasali pamoja na mama wa Yesu na waamini wengine.
Majina ya hao 11 yameorodheshwa tena, halafu pengo lililoachwa na msaliti Yuda Iskarioti likazibwa ili idadi muhimu ya 12 ikamilike tena. Aliyeamua ifanyike
hivyo ni Petro akitumia tayari mamlaka aliyoachiwa na Yesu, na akiweka masharti
kwa mapendekezo ya watu, hasa kwamba mteule awe shahidi wa utume na ufufuko wa
Yesu (Mdo 1).
Baada ya idadi hiyo kukamilika tena, Roho
Mtakatifu akawashukia wote katika nafasi maalumu, yaani sikukuu ya Pentekoste,
iliyotimiza Pasaka siku 50 baada yake (Mdo 2:1-41). Safari hiyo alijitokeza
kama upepo wa nguvu kubwa ajabu uliojaza nyumba nzima (yaani Kanisa lote) na
kama ndimi za moto zilizowashukia mojamoja kila mwamini aliyekuwemo (kwa kuwa
karama zake ni mbalimbali). Hapo hao waoga, waliojifungia ndani kwa usalama,
wakatoka nje na kuhubiria umati wa watu waliokusanyika kwa kufuata upepo. Kwa
kuwa siku hiyo ni ya hija walikuwepo Wayahudi na waongofu kutoka sehemu nyingi
za ulimwengu, lakini kila mmoja aliwaelewa mitume kwa lugha yake mwenyewe. Hivyo
umoja wa binadamu uliovunjika Babeli katika kujenga mnara wa kiburi ukapatikana
tena Yerusalemu kwa nguvu ya Yule aliye upendo wa Mungu. Toka mwanzo Kanisa si
la kabila la Yuda tu au la lugha ya Kiaramu tu, bali ni Kanisa Katoliki, yaani la mataifa yote na la lugha zote. Bila ya shaka aliyesimama kwa
niaba yake lote atoe hotuba ya kwanza na kufafanua matukio hayo pamoja na
kumshuhudia Kristo mfufuka ni Petro. Maneno yake yaliwachoma moyo wasikilizaji
hata wakamuuliza wafanye nini. Jibu likawa watubu na kubatizwa ili wapate
msamaha na Roho Mtakatifu. Siku hiyo ya kwanza waamini wakawa hawapungui elfu
tatu.
Luka ametuachia picha ya Kanisa mama hasa
katika mihtasari mitatu (Mdo 2:42-47; 4:32-35; 5:12-16) ambayo inachora maisha
ya Wakristo wa kwanza kama kielelezo kwa wale wote watakaofuata. Kweli katika
historia yote ya Kanisa wengi wakaja kujipima kwa kuangalia kielelezo hicho cha
umoja katika roho na katika mali. Hasa watawa wengi wakaja kujaribu kutekeleza
tena umoja huo mashirikani mwao na hivyo kuwachochea waamini wenzao wote. Umoja
huo ndio sifa ya kwanza ya Kanisa na mpango wa Mungu kwa watu wote.
Mwanzoni umoja ulifanikiwa kwa namna ya
pekee, ingawa hapo pia ulikuwa na kasoro tunavyosoma katika Mdo 5:1-11; 6:1 na
katika vitabu vingine vyote vya Agano Jipya. Kutokana na malalamiko ndani ya
jumuia, mitume waliamua kuwashirikisha kazi yao katika ngazi ya chini watu
saba: idadi hiyo katika Biblia inamaanisha mataifa, na kweli wote walikuwa na
majina ya Kigiriki (Mdo 6:2-6). Tofauti za waamini hasa upande wa lugha na
utamaduni zinadai daima ubunifu na nia njema zisije zikavuruga umoja. Shida
iliyotokea hapo ni utangulizi wa habari nyingine kuhusu Wakristo wa Kiyahudi
kuwabana wenzao wenye asili ya Kipagani.
Katika Mdo 6-8 hao viongozi 7 wapya
wanajitokeza kama mashujaa katika utume, ambao mwisho wake kwa Stefano ulikuwa
ni kifodini. Katika kusimulia tukio hilo la mwaka 36 hivi, Luka alisisitiza
kuwa mashtaka ya Wayahudi dhidi ya Stefano ni yaleyale yaliyomhusu Yesu: yaani upinzani dhidi ya mwalimu
unaendelea dhidi ya wanafunzi wake. Vilevile Stefano akakabili mateso kama
alivyofanya Yesu akimkabidhi Bwana roho yake na kuwaombea watesi wake. Kabla ya
hapo Wakristo walikuwa wamedhulumiwa katika nafasi mbalimbali, lakini dhuluma
hiyo ya tatu ikawa kubwa zaidi na kusababisha wengi wakimbie Yerusalemu. Lakini
kwa mpango wa Mungu mtawanyiko huo ulichangia kueneza Injili.
Ukristo ulivyoanza kuenea
Rembrandt, Ubatizo wa towashi, (1626
hivi).
Kufuatana na mpangilio wa kitabu, Mdo 8
inaeleza jinsi Mungu alivyoongoza uenezi wa Kanisa kwa watu wasiokubaliwa na
Israeli, yaani kwanza kwa Wasamaria waliokuwa maadui wakuu wa taifa teule,
halafu towashi (yaani mwanamume mbovu) toka Ethiopia. Katika nafasi hizo zote mbili Luka alisisitiza furaha iliyotokea kama
dalili ya wokovu. Juhudi za Filipo
mwinjilisti zikaja kuthibitishwa na mitume kwa kuwawekea
mikono Wakristo wapya wa Samaria.
Wakati uleule likatukia jambo lingine, la
ajabu kabisa, ambalo kwa umuhimu wake limesimuliwa na Luka mara tatu, yaani
uongofu wa Saulo/Paulo aliyekuwa mtesi mkuu wa Stefano na Wakristo wengine.
Ndiye aliyechaguliwa na Mungu awe mwenezi mkuu wa imani ya Kikristo, mtetezi
mkuu wa uhuru wa Wakristo wa mataifa kuhusu sheria za Kiyahudi, tena mwandishi
mkuu wa Agano Jipya, mwenye kufafanua mafumbo ya imani kwa undani kabisa. Mungu
alimteua awe chombo chake kiteule ili kuleta jina lake kwa mataifa (Gal
1:13-24; Mdo 9:1-31; Mdo 22:17-21): katika historia yote ya Kanisa baada ya
Pentekoste hadi leo hakuna tukio lingine muhimu zaidi.
Ukubwa na ubora wa mchango wa Paulo
unaeleweka tukizingatia kwamba alifanya kazi na kuandika kabla ya vitabu vya
Agano Jipya kupatikana. Ndiye aliyeanza kuliandika akipanua mawazo aliyoyapokea
katika Kanisa kwa kuzingatia Agano la Kale na mang’amuzi yake mwenyewe. Hapo alifafanua vizuri ajabu maisha ya Kikristo kama
neema ya kumshiriki Yesu kwa imani, sakramenti na juhudi za kushinda umimi hadi kugeuka sadaka hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu. Wokovu huo, utakaokamilika katika ufufuko wa mwili, unapatikana katika Kanisa, ambalo Paulo alilitambulisha kama bibiarusi wa Kristo na mwili wake.
Lakini, kabla Luka hajasimulia umisionari wake, aliandika habari nyingine ya ajabu ambayo pia inapatikana mara
tatu katika Matendo ya Mitume, yaani uongofu wa Kornelio na nyumba yake (Mdo 10). Wapagani hao walijaliwa Roho Mtakatifu kabla
hawajabatizwa, wakimsikiliza tu mtume Petro. Hivyo Mungu alimuonyesha mkuu wa
mitume nia yake kuhusu wokovu wa mataifa, naye Petro akalitangazia Kanisa
kwamba Wapagani wasilazimishwe kufuata sheria za Kiyahudi. Uamuzi huo uliofuata
hiyo Pentekoste ya mataifa ilimfungulia Paulo mlango wa umisionari wake
unaotawala Mdo 13-28. Ingawa Wakristo wenye msimamo mkali wa Kiyahudi
walikubali maneno ya Petro (Mdo 11:1-18), hawakuweza kumuunga mkono Paulo
aliposisitiza kwamba wokovu unategemea imani kuliko utekelezaji wa sheria.
Basi, mvutano juu ya suala hilo ukaendelea kuvuruga maisha ya Kanisa kwa miaka
mingi ya mbele.
Ni baada tu ya Petro kufungua mlango kwamba
Mdo 11:19-26 inasimulia jinsi waliotawanyika baada ya uuaji wa Stefano
walivyoeneza Ukristo huko walikohamia nje ya nchi takatifu, wakiwahubiria kwanza Wayahudi
wenzao, halafu Wapagani. Kitabu kizima kinafuata utaratibu huo: Paulo mwenyewe
kila alipofika aliwaelekea Wapagani baada tu ya Wayahudi kukataa Injili.
Kati ya miji ambapo ilianzishwa jumuia ya
waamini wengiwengi, muhimu zaidi ni Antiokia (mpakani kwa Sirya na Uturuki wa leo): huko wafuasi wa Yesu walikuwa mchanganyiko mkubwa wa Wayahudi
na mataifa, hivyo wakapewa jina jipya maalumu la Kiyunani (Wakristo). Ndipo walipofanya kazi Barnaba aliyetumwa na mitume, Paulo aliyeitwa naye kumsaidia, pamoja na manabii
na walimu wengine.
Wakati huohuo (mwaka 44 hivi) Herode Agripa alimuua Yakobo
Mkubwa (mtume wa kwanza kumfia Yesu) akakusudia
kumuua hata Petro, lakini huyo akahama Yerusalemu (Mdo 12:1-17) akafanya kazi
huko na huko kabla hajahamia moja kwa moja Roma akiuletea mamlaka yake.
Safari za kimisionari za Paulo zilivyoanza
(46-49)
Kanisa changa na motomoto la Antiokia likawa
kituo cha umisionari kuanzia mwaka 46; kwa mara nyingine Roho Mtakatifu ndiye
aliyechochea juhudi za kitume na kuteua watu wa kutumwa, yaani Barnaba na Paulo
(Mdo 13:1-3). Safari yao ya kwanza ilichukua miaka 3 katika kisiwa cha Kupro na mikoa ya kusini ya Uturuki wa leo (Mdo 13:16-51; 14:19-23). Ilikuwa
kawaida yao kuanzisha Kanisa katika miji mikubwa ili toka huko ujumbe ufike
hadi vijijini.
Mtaguso wa Yerusalemu (49)
Yakobo
Mdogo, kiongozi wa Wakristo
wa Kiyahudi mjini Yerusalemu,
aliyekubali Wakristo
wa mataifa wasilazimishwe kushika Torati.
Waliporudi Antiokia walipaswa kupambana na Wakristo
wa Kiyahudi kuhusu uwezekano wa mataifa kuokoka pasipo
kutahiriwa. Hatimaye suala likapelekwa Yerusalemu kwa Kanisa mama. Baada ya
majadiliano marefu Petro akatoa neno la mwisho kwamba Wapagani wanaomuamini
Yesu wasitwishwe mzigo usiobebeka wa kufuata sheria za Kiyahudi (Mdo 15:1-12).
Katika Gal 2:1-10 Paulo pia ametuachia kumbukumbu ya mtaguso huo akisisitiza kuwa
mitume waliokuwepo (Yakobo
Mdogo, Petro na Yohane) walitambua rasmi karama ya
kimisionari ya kwake na ya Barnaba na uhalali wake, wakiwaomba tu wachangishe
pesa kati ya Wakristo wa mbali kwa ajili ya wenzao wa Yerusalemu wwnye hali
ngumu. Hiyo ilikuwa namna mpya ya kutekeleza upendo wa kidugu na kudumisha
umoja wa Kanisa baada ya uenezi wake.
Masuala hayo yakadai uamuzi mwingine ili
Wakristo wa Kiyahudi waweze kuendelea kushirikiana na wenzao wa mataifa pasipo
kuogopa unajisi ambao ungewazuia wasifuate ibada zao. Gal 2:11-14 inaeleza
shida iliyotokea Antiokia: ingawa Paulo alimheshimu sana Petro, alipoona
hafuati kwa unyofu uamuzi wa mtaguso hakusita kumkosoa kidugu hadharani ili
aliepushe Kanisa na upotovu kuhusu suala la wokovu. Basi, kadiri ya Mdo
15:13-35, Yakobo Mdogo aliyeachiwa uongozi wa Kanisa la Yerusalemu alichagua
makatazo makuu manne kutoka Mambo ya Walawi akidai Wakristo wote wayashike kama
mambo mazito kwa dhamiri ya Kiyahudi. Uamuzi huo uliarifiwa kwa Wakristo wa
Antiokia na mikoa ya jirani kwa wajumbe na barua. Barua zikaendelea kuandikwa
hata leo kwa lengo la kudumisha umoja na amani katika Kanisa, kwa kuwa ni kazi
ngumu kuelewana kwa watu tofauti kama hao waliozoea kudharauliana kwa matusi
kama “mbwa”.
Barua au nyaraka
Kati ya vitabu 27 vya Agano Jipya, 21 vina mtindo wa barua au nyaraka. Hiyo ni tofauti kabisa na Agano la Kale, ambamo vitabu kadhaa vinazileta, lakini si kitabu kizima hata kimoja. Mtume Paulo ndiye aliyetumia zaidi mtindo huo ili afikie na ujumbe na mamlaka yake pale asipoweza kufikia kimwili. Barua 14 zinahusishwa na yeye kwa
namna moja au nyingine, wakati nyingine 7 zinahusishwa na Yakobo Mdogo, Mtume
Petro, Mtume Yohane na Yuda
Tadei. Hii haina maana kwamba ziliandikwa zilivyo
na Mitume hao. Kwanza, tokea awali watu waliweza kuandika barua kwa mkono wao, au kwa kumuongoza karani aandike maneno yao wenyewe, au kwa kumpa maelekezo ya jumla kuhusu
namna ya kuandika kama si kumuachia aandike anavyoona inafaa. Zaidi ya hayo,
wakati wa Mitume ilikuwa kawaida kuandika kwa kutumia jina la marehemu fulani maarufu kama kwa kumwezesha aendelee kutoa ujumbe aliokuwa
anautoa maishani. Pengine aliyeandika hivyo alikuwa na uhusiano wa pekee na
marehemu huyo kama mwanafunzi au mwandamizi wake.
Pengine maandishi hayo hayakuwa tu barua fupi
za kuwasiliana kuhusu shida fulani, bali hati au insha ndefu kuhusu mada fulani: ndizo zinazostahili kuitwa nyaraka. Ingawa tofauti kati ya
barua na waraka inaeleweka kinadharia, pengine ni vigumu kugawa vitabu hivyo vya Agano Jipya katika makundi
mawili: kwa hakika Eb ni waraka na 3Yoh ni barua, lakini nyingine ziko katikati. Barua saba zisizohusishwa na
Paulo zinaitwa Katoliki, maana zimekubaliwa na Kanisa lote, ingawa maana asili ya neno hilo ilikuwa kwamba ni kwa ajili ya watu wote, jambo ambalo si kweli.
Katika Biblia barua hazikupangwa kufuatana na tarehe za kuandikwa, bali zinatangulia zile za Paulo, na kati ya hizo
zinatangulia zile kwa makanisa 7, zinafuata zile kwa watu binafsi 3 na mwisho waraka
kwa Waebrania ambao haumtaji Paulo. Ndani ya makundi hayo,
zinatangulia zile ndefu zaidi hadi zile fupi. Sisi, tukitaka kuelewa zaidi ujumbe na maendeleo yake, ni afadhali tuzisome kwa mpangilio wa tarehe kadiri tunavyoweza kuikadiria. 2Pet, ambayo inafikiriwa kuwa ya mwisho kuandikwa, inashuhudia kwamba tayari
barua za Paulo zilikuwa zimekusanywa na kuheshimiwa kama Maandiko
Matakatifu.
Safari ya pili ya Mtume Paulo (50-52)
Mtume Paulo akitoa Hotuba ya Areopago huko Athene, kadiri ya Raffaello Sanzio, 1515.
Mdo 15:36-39 inasimulia ugomvi kati ya Paulo
na Barnaba walipotaka kufunga safari tena (mwaka uleule 49). Mungu hakuzuia
ugomvi huo kusudi hao wawili waeneze zaidi neno lake wakienda sehemu tofauti.
Barnaba na Marko walielekea Kupro, kumbe Paulo alimchukua Sila na kufunga safari iliyodumu miaka mitatu, akielekea kwanza jumuia zile
za bara alizoziunda miaka iliyopita (Mdo 15:40-16:5).
Paulo ni maarufu kwa juhudi zake za kueneza
Ukristo mahali pengi palipokuwa bado, lakini pia tunajua upendo wake kwa watu
aliowatangazia habari njema, na bidii zake kwa makanisa aliyoanzisha: alikuwa
akiwaombea usiku na mchana, akiwaka hamu ya kuwatembelea, akiwaandikia barua za
kusisimua ili kuwatia moyo au kuwakosoa, kutatua matatizo yao na kujibu maswali
mbalimbali. Pengine aliwatumia watu alioongozana nao: kati yao alimpendelea Timotheo akashirikiana naye mpaka kufa.
Kadiri ya Mdo 16:6-15, katika safari hiyohiyo
kwenye mikoa mbalimbali ya Uturuki wa leo, huenda Luka pia akajiunga na msafara
akifuatana na Paulo hadi kufa kwake. Yeye anatia maanani uongozi wa Mungu
ambaye kwanza aliwazuia mara mbili wasielekee walikokusudia, halafu kwa njozi
alionyesha ni mapenzi yake wavukie Ulaya katika Ugiriki wa leo.
Inavyojulikana, Wayunani walikuwa na hamu
kubwa ya kupata maarifa kuliko wengine, halafu kubishana nao kwa ufasaha na
kuwashinda. Katika mazingira hayo, falsafa na dini zilikuwa mada kuu na
kuingiliana na hadithi za ajabuajabu kuhusu miungu, malaika na wengineo. Karibu
barua zote za mitume zilikabili hatari hiyo, ambayo ikazidi kuwa kubwa na
kuleta mafarakano katika Kanisa hasa katika karne II, ilipoitwa “Gnosis” (= ujuzi). Hasa Paulo alijitahidi kuishinda mapema iwezekanavyo.
Huko Ugiriki wakaanzisha Kanisa kwanza Filipi, halafu Thesalonike. Kutokana na dhuluma za Wayahudi, Paulo alilazimika kuondoka akafika Athene, mji mkuu wa falsafa, akajaribu kutangaza Injili kwa ufasaha wa maneno ili kuwavuta hao watu
wa elimu; kumbe akashindwa kabisa (Mdo 17). Ndipo alipoelewa kuwa imani
haitegemei akili na elimu, akaamua kuhubiri kwa unyofu tu mafumbo ya imani (1Kor 1:17-2:5).
Mdo 18:1-11 inasimulia mang’amuzi mengine
aliyoyapata katika jiji la Korintho, lenye bandari mbili katika bahari tofauti zilizoleta urahisi wa kuvusha bidhaa toka moja hadi nyingine badala ya kuzisafirisha kwa meli kandokando ya rasi. Kutokana na umuhimu huo na wa kuwa makao makuu ya mkoa wa Akaya (Ugiriki kusini), pamoja na biashara kubwa, kulikuwa na mchanganyiko wa
watu, wakiwemo watumwa na makahaba wengi. Huko alikaa mwaka mmoja na nusu
kutokana na kufunuliwa na Yesu kwamba ana wateule wengi jijini. Kweli utume wa
Paulo ukazaa sana, ingawa kabla hajafika walikuwepo tayari Wakristo kadhaa kama
Akula na Priska waliofukuzwa na kaisari Klaudio mwaka 49 watoke Roma pamoja na Wayahudi wote hasa kutokana na mabishano
yao kuhusu Kristo.
Barua mbili kwa Wathesalonike
Paulo Akiandika Nyaraka Zake, karne
ya 17.
Mtume
Paulo alikuwa amekimbia Thesalonike baada ya wiki 3 tu za utume, hivyo aliogopa kwamba huenda dhuluma zikawakatisha wanafunzi tamaa. Kumbe, akina Timotheo walipofika
Korintho toka Thesalonike, walimpa Paulo ripoti kuhusu hali ya Kanisa la kule
na kumuondolea wasiwasi: dhuluma zilikuwa zikiendelea lakini Wakristo wachanga
wa huko ni imara katika imani yao mpya, isipokuwa hawaelewi vizuri mambo fulanifulani, hasa kuhusu vikomo
vya binadamu. Hapo Paulo akawaandikia kwa furaha barua tuliyonayo mpaka leo ili kuwahimiza na kuwaelimisha zaidi: ndiyo
andiko la kwanza la Agano Jipya kwa kuwa ni wa mwaka 51 hivi. Barua
hiyo haina mafundisho mazito isipokuwa kuhusu
mambo ya mwisho (hali ya marehemu na ujio
wa pili wa Bwana). Ni tulivu na ya kirafiki, ingawa
inatoa maonyo upande wa maadili (1Thes 1:1-3:13; 4:13-17; 5:1-11; 5:16-28).
Miezi michache baadaye akarudia kuwaandikia
kutokana na taarifa nyingine zilizomtia tena wasiwasi. Akawafafanulia zaidi
ujio wa Bwana na dalili zake, akiwahimiza hasa kufanya kazi kwa bidii na
kuwajibika wakati wa kungojea ujio wa pili wa Yesu badala ya kuiacha kwa kisingizio cha kwamba, eti Kristo amesharudi
(2Thes 2:1-15; 3:6-15). Mpangilio wa barua hizo ni uleule wa barua
zitakazofuata: baada ya salamu na shukrani kwa Mungu, yanafuata mafundisho ya
imani, halafu maadili, na hatimaye salamu nyingine.
Mwaka 52 Paulo aliondoka kwa hiari Korintho
kuelekea Yerusalemu na Antiokia. Njiani alihubiri kidogo Efeso, makao makuu ya mkoa wa Asia Ndogo (Uturuki Magharibi wa leo), lakini hakukubali kubaki muda mrefu zaidi,
ila aliwaacha huko Priska na mumewe akiahidi kurudi, Mungu akipenda (Mdo
18:18-22). Huo ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya mseja na watu wa ndoa
katika utume.
Mdo 18:24-28 inasimulia kwamba, baada ya
Paulo kuondoka, alifika Myahudi wa Aleksandria, jina lake Apolo. Kama vile wenzake wengi wa Misri alikuwa na elimu ya Kiyunani na ujuzi
wa Biblia.
Tena alikuwa motomoto katika kufundisha
habari za Yesu, ingawa hazijui sawasawa, hasa hana habari ya ubatizo wake mpya
(kasoro hiyo ikaendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa sababu baadhi ya wanafunzi wa
Yohane Mbatizaji hawakumuamini Yesu, hivyo wakaendeleza ujumbe wa mwalimu wao).
Priska na mumewe wakamuelimisha zaidi, halafu
wakampa barua ya kumtambulisha kwa Wakristo wa Korintho alipokwenda kuhubiri.
Wamisionari wa namna hiyo wakazidi kustawisha na kuvuruga makanisa walau mpaka
mwisho wa wakati wa mitume.
Safari ya tatu ya Mtume Paulo (54-58)
Baada ya kukaa Antiokia mwaka mmoja na nusu
Paulo akafunga tena safari akiyapitia makanisa ya Galatia na Frigia ili kuyathibitisha (Mdo 18:23). Hatimaye akafika Efeso ambapo akabaki
tangu mwaka 54 hadi 57, akifundisha kila siku na kueneza sana Injili katika
mkoa mzima (Mdo 19:1-10). Pamoja na hayo aliandika barua kadhaa, ambazo baadhi
zimepotea, nyingine tunazo hadi leo (kwa Wagalatia, kwa Wafilipi, ile ya kwanza
kwa Wakorintho, inawezekana Filemoni pia).
Barua hiyo iliandikwa na Paulo akiwa Efeso. Tofauti na zile kwa Wathesalonike, hii ni kali sana kwa kuwa Paulo
aliiandika (mwaka 54 hivi) mara baada ya kusikia kwa mshangao na huzuni kwamba wanafunzi wake wa mkoa wa Galatia wanataka kupotoshwa na Wakristo wengine wanaosisitiza haja ya kushika Torati ili kupata wokovu. Ili kumpinga Paulo na mafundisho yake kuhusu neema, wazushi hao walikanusha pia mamlaka yake kama mtume, eti, hajawahi kumuona Yesu, na anarahisisha masharti ya dini ili ajipatie wafuasi na heshima.
Basi, ilimbidi ajitetee na kusimulia baadhi
ya matukio ya maisha yake yanayotusaidia kumfahamu zaidi na kutambua kwamba msimamo wake wa awali kama Farisayo haukumuelekeza hata kidogo kupuuzia Torati. Ni tukio la ghafla la
kutokewa na Mfufuka tu lililoweza kupindua mtazamo wake. Baada ya hapo, msimamo
wake mpya ulikubaliwa na viongozi wa Kanisa mama la Yerusalemu waliotambua karama yake ya pekee kwa uongofu wa mataifa. Akitetea uhuru wao kuhusu masharti ya Torati, Paulo hakukosa kueleza kwamba hauruhusu
kufuata udhaifu wa kibinadamu (unaowakilishwa na mwili), bali ni kwa ajili ya kufuata mwongozo wa Roho
Mtakatifu ambao ni wa juu kuliko Torati na hatimaye
unazaa tunda lake bora.
Akiandika kwa hasira takatifu ili kuzuia Injili isibadilishwe wala msalaba usibatilishwe - kwa sababu wokovu ukipatikana kwa kushika Torati, Kristo amekufa bure - mara baada ya salamu akashambulia kwa nguvu wazushi hao
na kuonyesha kwa Biblia kuwa haiwezekani kujipatia uadilifu kwa kujaribu
kufuata sheria za Musa walivyotaka wao. Kinyume chake uadilifu wetu unatokana
na imani kwa Kristo na msalaba wake.
Ilimbidi kwanza ajitetee kuwa mtume halisi anayefundisha
kulingana na mitume wengine, halafu aonyeshe tunavyookolewa kwa imani, si kwa
kufuata sheria, hatimaye atoe mawaidha kuhusu uhuru
wa Kikristo, kwamba unategemea kumfuata Roho Mtakatifu
si tamaa za dunia (Gal 1:1-12; 2:15-3:14; 4:4-20; 5; 6:7-18).
Luka hakusimulia mateso yote ya Paulo, kwa
mfano alivyohukumiwa mwaka 56 hivi hukohuko Efeso (1Kor 15:32; 2Kor 1:8-9).
Akiwa kifungoni alifikiwa na mjumbe toka Filipi aliyemletea msaada wa pesa na
wa huduma kwa niaba ya Wakristo wa mji huo. Paulo kabla hajamrudisha alipenda
kuwaandikia barua nzuri ya shukrani pamoja na kuwaeleza sababu ya kufungwa (Fil
4:10-20). Barua ni nzuri pia kutokana na uhusiano wa upendo kati ya Paulo na
Wakristo hao, ambao kati yao wanawake walishika nafasi ya pekee toka mwanzo.
Tunaona wazi Paulo alivyokuwa na furaha hata kifungoni, kwa kuwa alizoea
kuridhika na kila hali. Kwake muhimu ilikuwa tu kumfikia Kristo.
Kama kawaida mawaidha hayakosekani, lakini si
makali: hasa alihimiza umoja kwa kufuata mfano wa Yesu aliyejishusha kutoka
Umungu wake hadi kifo cha msalabani. Kwa ajili hiyo alitumia maneno ya wimbo
ambao unadhihirisha imani kamili katika umungu wa Kristo, ingawa ni kati ya
zile za kwanzakwanza kutungwa (Fil 1:12-3:1a; 4:4-7).
Lakini kuna sehemu kali kuhusu wazushi ambayo
inaanza ghafla (Fil 3:1b-4:1) na kufanya baadhi ya wataalamu wadhani kuwa barua
jinsi ilivyo tangu karne I ni mshono wa barua mbili au tatu za mtume kwa
Wafilipi.
Paulo akiwa kifungoni (labda Efeso mwaka 56
au 57) alimuandikia Filemoni. Tofauti na barua zote zilizotangulia, hiyo haikuandikwa kwa kanisa
fulani, bali kwa Mkristo binafsi, tajiri, pengine wa Kolosai. Ingawa si muhimu upande wa teolojia, inaonyesha upendo wa mtume kwa wale aliowaongoa, na jinsi udugu wa
Kikristo ulivyoanza kutikisa utumwa.
Barua mbili kwa Wakorintho
Kutoka Korintho habari za kusikitisha
zilimfikia Paulo akiwa Efeso (pengine mwaka 57): katika Kanisa hilo ambalo
alilianzisha na kulipenda sana kulikuwa na shaka kuhusu imani, mafarakano,
upinzani wa Wakristo wa Kiyahudi dhidi yake, na makwazo.
Kilichohatarisha zaidi jumuia hiyo ni karama
mbalimbali ambazo hao Wakristo wachanga walizijali mno na hatimaye wakajivunia
kuwa nazo. Vilevile walivutiwa kumfuata mtu kama Apolo, mwenye ujuzi na ufasaha
mkubwa, mambo yaliyopendwa sana na Wagiriki. Ilimbidi Paulo arekebishe hali
hiyo ili kuokoa hasa umoja wa Kanisa na heshima kwa viongozi wake halali.
Basi mwaka mzima akawa na mahangaiko kwa
Wakorintho akawaandikia walau barua nne au tano, ingawa sisi tunazo mbili tu;
pengine sehemu za baadhi yake zimeshonwa ndani ya 2Kor.
Mpangilio wa barua
ya kwanza una salamu na shukrani, halafu hukumu juu ya
matatizo ya Wakristo hasa kufarakana (1Kor 1:10-16; 2:1-4:16), kuzini na
kushtakiana mahakamani (1Kor 5-6). Baada ya hapo akaanza kujibu maswali yao
mbalimbali: kuhusu ndoa na useja (1Kor 7), nyama zilizotolewa sadaka kwa miungu (1Kor 8:1-11:1),
mwenendo katika ibada na karama (1Kor 11:20-33; 12:4-13:13; 14:18-40), na
hatimaye ufufuko wa wafu (1Kor 15:1-28,33-49).
Mwishoni kuna maagizo, taarifa na salamu
mbalimbali (1Kor 16:1-4). Ndiyo sababu barua ni ndefu na inagusa mambo mengi
ambayo Paulo aliyatazama kwa hekima ya juu inayotokana na msalaba wa Kristo.
Kati ya mambo mengi muhimu zaidi, barua hiyo inatunza simulizi la kwanza la karamu ya mwisho ya Bwana Yesu (11:23-25) na kanuni ya imani ya kwanza inayoorodhesha
pia matokeo ya Kristo Mfufuka (15:3-8).
Mdo 19:21-20:1 inasimulia alivyohama Efeso
kutokana na matatizo kuzidi, akaelekea Makedonia na Ugiriki. Toka huko alipata
nafasi ya kuhubiri huko Iliriko, yaani Albania ya leo kwenda kaskazini (Rom 15:19). Wakati huo alipata habari tofauti
kabisa kuhusu Wakorintho, akawaandikia tena na tena kabla hajawaendea kwa mara
ya tatu. Labda kwa kuwa ni mshono wa barua hizo mbalimbali, mpangilio wa Waraka
wa pili kwa Wakorintho haueleweki, ingawa ina salamu na shukrani
mwanzoni, na salamu nyingine mwishoni kama kawaida. Katikati mada kuu ni tatu:
kujitetea, mchango na mashambulizi dhidi ya wapinzani. Barua hiyo inatusaidia
hasa kumjua Paulo mwenyewe (2Kor 11:1-12:13).
Mitume Petro na Paulo kadiri ya El
Greco.
Ingawa Paulo alikaa Efeso miaka mitatu, moyo
wake wa kimisionari haukutulia kwa sababu alikumbuka alivyotabiriwa atafanya
kazi hata mbali zaidi. Ndiyo maana alitaka kwenda Ulaya magharibi, yaani Roma
na halafu Hispania, nchi iliyohesabika kuwa mwisho wa dunia. Ila kabla ya kwenda huko
alipanga kuleta mchango wa Wakristo wa mataifa kwa wenzao wa Yerusalemu.
Basi, mwishoni mwa miezi mitatu aliyokaa Korintho (Mdo 20:2-3) akijiandaa kupanda meli, yaani mwanzoni mwa mwaka 58, Paulo aliwaandikia Wakristo wa Roma ili kuandaa utume atakaoufanya katika jiji hilo.
Huko Ukristo uliingia toka mwanzo kabisa, ukiletwa na baadhi ya Wayahudi wengi walioishi Roma ambao walibatizwa Yerusalemu kwenye Pentekoste ya mwaka 30.
Wayahudi wote walipofukuzwa na Kaisari Klaudio (49), Wakristo wa mataifa mengine wakabaki ndio wengi, nao wakaachana na
masharti mbalimbali za Kiyahudi, kama yale kuhusu vyakula.
Muda mfupi baada ya Klaudio kufa (54), Wayahudi walianza kurudi, kumbe wakakuta mabadiliko hayo makubwa
ndani ya Kanisa, nao wakajiona wamewekwa pembeni kidogo, kama si kudharauliwa na
Wakristo wa mataifa.
Mtume Paulo akijua umuhimu wa Roma, mji
mkuu wa ulimwengu wa zamani hizo, aliwaandikia Wakristo wa huko barua ndefu tena nzito kuliko zote. Alitaka kuwaeleza kwa maandishi ya mpango
mafundisho yake kuhusu wokovu, kwa sababu walikuwa wamesikia habari tofautitofauti juu yake bila ya
kukutana naye.
Pamoja na kuwaandaa hivyo wampokee vizuri,
alichukua nafasi ya kuimarisha umoja wao ulioingia dosari. Akiandika kwa utulivu mkubwa kuhusu mambo aliyokwishawaongelea kwa hasira Wagalatia, Paulo aliweza kuinua pande zote mbili za Kanisa hilo zielewe zaidi fumbo la mpango wa Mungu kwa ajili ya watu wote, na hivyo ziheshimiane kwa upendo, ulio utimilifu wa Torati.
Hasa aliwaonya Wakristo wa mataifa wasidharau
Wayahudi, kwa sababu hao bado ni wateule wa Mungu.
Mtume Paulo akijua umuhimu wa Roma, mji mkuu
wa ulimwengu wa zamani hizo, aliwaandikia Wakristo wa huko barua ndefu tena
nzito kuliko zote.
Ingawa haina mafundisho yote ya Paulo, barua
hii imechangia teolojia ya Kikristo kwa kiasi kikubwa, hasa upande wa magharibi.
Kwa namna ya pekee inajibu kinaganaga maswali
kuhusu wokovu: unapatikana kwa njia gani? Kwa nini Wayahudi wengi walishindwa
kumuamini Yesu ili kuupata? Kwa nini mataifa yameupokea badala yao? Aliyepata wokovu
anaishi vipi? Je, Wayahudi wametupwa moja kwa moja?
Ndiyo sehemu kuu ya barua (Rom 1:16-32; 2:1-29; 3:9-20; 3:21-31; 4:1-8; 4:23-25; 5:1-21; 6:1-14;
7:7-25; 8:1-39; 9:1-5; 11:1-36), ambayo inafuata salamu (1:1-8) na shukrani.
Paulo alisisitiza kwamba wote ni wakosefu na
wanaweza kuokolewa na Mungu tu: hiyo ni neema tupu, maana hakuna anayeweza kuistahili kwa juhudi zake.
Neema hiyo tunaipata kwa kumuamini Yesu ambaye alikufa akafufuka kwa ajili yetu ili sisi tuishi upya kwa ajili
yake tukiongozwa na Roho Mtakatifu.
Chini yake Mkristo atafanya mema mengi na
makubwa kuliko yale yanayodaiwa na Torati, ambayo ni njema lakini haitutii nguvu ya kuitekeleza.
Upande wa mataifa, toka mwanzo Mungu aliwapa mwongozo mwingine wa maisha, yaani dhamiri.
Hata hivyo pande zote mbili zilishindwa
kufaidika na miongozo hiyo wakahitaji msaada bora zaidi ili kumpendeza Mungu.
Uadilifu sasa unapatikana kwa imani na ubatizo katika kifo na ufufuko
wa Yesu.
Hiyo njia mpya ya Mungu kuwaokoa watu wote
haiendi kinyume cha ahadi zake kwa Israeli ya Kale. Paulo anathibitisha hilo
kwa hatua nne akitumia madondoo mengi ya Agano la Kale. Hamzungumzii Myahudi
mmojammoja, bali wote jumla; wala hazungumzii jukumu lao kuhusu kifo cha Yesu.
Maadili mema yatafuata kama matunda, na Paulo, kama kawaida ya Wakristo wa
kwanza, baada ya ujumbe au fundisho la imani, anayaeleza hasa katika sehemu ya pili ambayo ina mawaidha mbalimbali (Rom 12:1-2,9-21; 13:8-14), yakifuatwa na taarifa, salamu na doksolojia.
Kwa kuwa Paulo hakuwafahamu vizuri Wakristo
wa Roma, maneno yake ni ya jumla na si ya mpango. Hasa ni kwamba madai ya Torati hayawezi kuongoza mwenendo wa Mkristo, lakini huyo anatakiwa kuzingatia
anavyodaiwa hasa upendo kwa wote.
Maisha ya Mkristo yawe ibada kwa Mungu katika Roho
Mtakatifu. Umoja
wa Kanisa unamdai ajitahidi kushinda mabaya kwa mema.
Kila kiungo cha mwili huo mmoja anadaiwa juhudi kwa ajili ya ustawi
wa wote ili maisha yawe sadaka kwa Mungu.
Akigusa zaidi maisha ya Kanisa la Roma ya wakati huo, yaliyovurugwa na masuala madogomadogo kuhusu vyakula na sikukuu, Paulo alidai wenye nguvu watekeleze upendo kwa walio dhaifu zaidi,
pamoja na busara, uelewa, mfano wa Yesu na uaminifu kwake.
Maelekezo hayo yanaweza kusaidia daima
kukabili mvutano wowote kati ya wenye mitazamo tofauti (finyu na mpana, au wa
kizamani na wa kisasa zaidi). Lengo ni ule umoja uliofundishwa katika sura nane za kwanza.
Ukristo baada ya Paulo kufika Roma
Kusulubiwa kwa Mt. Petro kadiri ya Caravaggio.
Paulo kupeleka mchango Yerusalemu (Mdo
20:16-21:36) ndio mwisho wa kipindi cha utume wake mkubwa zaidi. Sura tisa za
mwisho za Matendo ya Mitume zinatusimulia kinaganaga habari zake kuanzia 58
hadi 63, ambapo karibu miaka yote alikaa kifungoni akisubiri kesi (Mdo
23:12-24; 24:22-25:22; 28:11-16,23:30). Bila ya shaka ilikuwa ya majaribu
makubwa kwake, lakini ilimpa nafasi ya kutafakari mafumbo ya wokovu kwa undani
zaidi tena, na ya kumshuhudia Kristo mbele ya wafalme (Agripa II na nyumba ya Kaisari) alivyotabiriwa. Kwa Luka ni muhimu sana kwamba
Paulo alifika Roma na kuanza huko kazi yake ya utume, kiasi kwamba hakuendelea
kuandika kilichofuata.
Hasa kwamba mwaka 64
mfalme Nero alianza dhuluma za serikali dhidi ya Wakristo
zilizoendelea mpaka 313, ingawa si mfululizo. Petro na Paulo waliuawa mjini
Roma kati ya mwaka huo na mwaka 68, wakiliachia Kanisa la mji huo usimamizi wa
makanisa yote. Kuhusu kipindi hicho tuna ushahidi wa vitabu mbalimbali vya
Kipagani, vya Kiyahudi na vya Kikristo. Baadhi yake ni vile vya mwisho vya
Agano Jipya ambavyo tunataka kuendelea kuvichambua. Waandishi wake pengine
walitumia majina ya mitume ili kuyapa nguvu maandiko yao: inawezekana walikuwa
warithi wa mamlaka yao na kuendeleza kazi zao. Mkazo wa vitabu hivyo unaelekea
miundo ya Kanisa (uchungaji) kuliko umisionari (uvuvi).
Katika hiyo miaka ya
mwisho ya ufunuo, Wakristo wa mataifa wakazidi kuwapita wale wa Kiyahudi kwa
idadi na kwa umuhimu. Nafasi ya Yerusalemu katika Kanisa ulizidi kupungua
kutokana na hali ya nchi, yaani vurugu kati ya Wayahudi, Wayunani na serikali
ya kikoloni. Mwaka 62 Yakobo, ndugu wa Bwana na kiongozi wa Kanisa la huko,
aliuawa na Wayahudi. Tangu mwaka 66 hadi 73 hao walipigania uhuru wakashindwa;
mwaka 70 Yerusalemu ulitekwa tena na Waroma na kuteketezwa pamoja na hekalu
lake. Kuanzia hapo hadi leo dini ya
Kiyahudi imebaki haina ukuhani
wala sadaka; nguvu yake ni katika masinagogi inapofanyika ibada ya Neno la
Mungu chini ya walimu wa sheria. Maangamizi hayo yalizidi kutenganisha Wakristo na
Wayahudi, hasa kwa sababu Wakristo wa Yerusalemu walikimbilia ng’ambo ya
Yordani badala ya kupigania uhuru, halafu wakarudi mjini mpaka vita vya pili
vya Kiyahudi (132-135) ambapo Waroma wakabomoa tena Yerusalemu na kuwafukuza
Wayahudi wote wasiweze hata kuingia wilayani na kuona kwa mbali mlima wake.
Kanisa la mji huo wa
biashara karibu na Efeso lilianzishwa na mwanafunzi wa Paulo, labda Epafra, halafu likaingiwa na mafundisho ya ajabuajabu
yaliyochanganya mambo ya Kiyahudi na ya Kipagani na yaliyozingatia mno ukuu wa malaika juu ya ulimwengu.
Ndiyo sababu huenda Paulo,
akiwa kifungoni Roma kati ya miaka 61 na 63, akawajibika kuliandikia barua
inayoonyesha kuwa Kristo ni mkuu kuliko wote: vyote kabisa viliumbwa kwa njia
yake na kwa ajili yake, tena katika ubinadamu wake umo utimilifu wote wa Mungu.
Yeye ndiye “fumbo” kwa kuwa Mungu ametimiza mpango wa wokovu kwa njia yake.
Hakuna sababu ya kutafuta kwingine hekima na maarifa, wala ya kujiwekea
masharti ya kibinadamu yasiyosaidia kuokoka (Kol 1:13-29; 2:6-3:4; 3:5-17).
Mpangilio wa barua ni
kama kawaida: utangulizi, mafundisho ya imani, maonyo kuhusu uzushi, mawaidha
na hatima.
Paulo aliweza kuandika
barua hii akiwa kifungoni Roma kati ya miaka 61 na 63 ili isomwe katika
makanisa yote ya mkoa wa Asia Ndogo, wenye makao makuu Efeso. Mafundisho yake
yanalingana na yale ya barua kwa Wakolosai ila yamechimbwa zaidi, kiasi kwamba
barua hii inaonekana kuwa kilele cha teolojia ya Paulo. Pamoja na kuchambua
fumbo la wokovu katika Kristo, inachambua hasa fumbo la Kanisa kama mwili wa Kristo ambamo kichwa kinaeneza wokovu ulimwenguni kote.
Kwa msingi huo inasisitiza na kudai umoja kamili kati ya waamini (Ef 1:1-2;
1:17-23; 2:11-22; 3:1-21; 4:1-16).
Jina hilo linajumlisha
barua moja kwa Tito na mbili kwa Timotheo, ambao walikuwa washiriki
wakuu wa utume wa Paulo, wakawa waandamizi wake. Wataalamu wanabishana sana
kuhusu mtunzi wa barua hizo, wengi wakidhani zimeandikwa na mfuasi wa Paulo
mwaka 95 hivi, huku wengine wakishikilia aliziandika mwenyewe, kwa msaada wa
karani fulani, miaka ya mwisho ya maisha yake (63-67), ambapo baada ya kufunguliwa
aliweza kusafiri tena mashariki (Ugiriki na nchi za kandokando) na pengine hata
magharibi (Hispania). Barua ya pili kwa Timotheo inaonekana kama wasia wake
alioandika kifungoni akisubiri kuuawa.
Barua hizo zinaitwa za
kichungaji kwa kuwa ziliandikwa kwa maaskofu hao ili kuwasaidia kufanya vizuri
kazi zao, hasa kwa kushika imani sahihi, kupinga uzushi, kuchagua vizuri
viongozi ambao wawawekee mikono, kuchunga vema Wakristo wa aina mbalimbali, kuwa
na mwongozo kuhusu ibada, n.k. Ndiyo sababu ni muhimu sana kwa miundo ya Kanisa
iliyokuwa mbioni kupata sura yake ya kudumu. Pamoja na hayo zinahimiza kukubali
mateso kwa ajili ya Injili: ndio msimamo wa Mchungaji mwema (Tito 1:5-9; 2;
1Tim 1:18-2:10; 3:1-4:16; 6:2b-21; 2Tim. 1:3-14; 2:1-18; 3:14-17; 4:1-8).
Mtume Paulo alipokaribia
kumaliza kazi yake, wengine kati ya mitume na wanafunzi wao walianza kuandika
kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu. Mmojawao ni Petro, kwa msaada wa Sila, akiwa Roma
karibu na kuuawa. Baada ya kufanya utume Antiokia, aliweza kwa urahisi
kutembelea mikoa ya Uturuki Kaskazini wa leo. Wakristo wa huko ndio walioandikiwa
barua hii yenye mafundisho na ibada kuhusu ubatizo na Pasaka. Pamoja na hayo
walihimizwa wasiogope maneno ya watu wengine wasiopendezwa na uongofu wao: hali
ngumu ni fursa ya kulingana zaidi na Yesu mpole na mteswa (1Pet 1:1-12;
2:19-25; 3:13-5:14).
Miaka hiyohiyo ya 60
Mkristo mwingine, mwenye asili ya Kiyahudi na elimu ya Kiyunani, aliwaandikia
Wakristo wa Kiyahudi wenzake si barua hasa bali hotuba kamili iliyoambatanishwa
na kipande cha barua. Hali iliyosababisha uandishi ni baadhi yao kuvutiwa tena
na dini yao asili na ibada zake hekaluni: kishawishi kilikuwa kikubwa hasa kwa
sababu Kanisa lilikuwa bado mwanzoni, bila ya mahali maalumu pa kusali wala
ibada za fahari. Mwandishi aliwaonya kuwa wakimuasi Yesu hawamrudii Mungu aliye
hai, aliyejifunua hasa katika Mwanae, bali wanamsulubisha tena kwa makusudi
mazima na kustahili tu moto wa milele.
Sehemu kubwa ya
maandishi hayo inalinganisha Yesu na ukuhani wake katika hekalu la mbinguni
upande mmoja, na ukuhani wa Agano la Kale huko Yerusalemu upande mwingine.
Hivyo mwandishi alielekeza safari ya kiroho katika imani inayofanana na ile ya watakatifu wa
Agano la Kale.
Kwa kuwa lengo halikuwa
la kinadharia, bali kuhimiza uaminifu, kila baada ya kuchambua ukweli fulani
aliongeza mawaidha ya kufaa. Ubora wake ni kulinganisha mambo ya kale na
utimilifu wake katika Agano Jipya, pia kuthibitisha ukuu wa Kristo kama kuhani
wa milele (Eb 1:1-2:4; 4:11-5:10; 7:1-8:13; 10:19-11:40; 13:22-25).
Tulivyoona, kwa muda wa
miaka 30 na zaidi Wakristo walitangaza habari za Yesu hasa kwa midomo, halafu
kwa barua na maandishi mengineyo. Lakini wakati huohuo (miaka ya 50?) baadhi
yao walianza kukusanya kwa maandishi ushuhuda wa mitume na wengineo kuhusu
mafundisho na maisha ya Yesu, kama vile mifano aliyoitoa, mabishano yake na
Mafarisayo, na hasa mateso yake. Kati yao tunaambiwa Mathayo aliandika kwa
Kiaramu, ingawa hatuna hata kipande cha kitabu chake na cha vinginevyo. Ila
Wainjili wetu walivisoma na kuvitumia kwa kutunga vya kwao. Baada ya Injili zao
nne kupatikana, Kanisa likaacha vitabu vya kwanzakwanza hata vikapotea.
Wataalamu wengi
wanakubaliana kusema Marko ndiye aliyetangulia kuandika kitabu kamili juu ya
maisha na mafundisho ya Yesu kuanzia utume wa Yohane Mbatizaji hadi ufufuko
wake. Ndiye aliyekiita kitabu cha namna hiyo Injili, hata neno hilo, lililokuwa
na maana ya ujumbe kuhusu Yesu, likaja kuwa na maana mpya ya kitabu cha habari
za Yesu. Marko aliandika akiwa Roma mwaka 65 hivi, mara baada ya serikali
kuanza kuwatesa Wakristo, na akiwa na nia ya kuwaimarisha katika dhuluma.
Baada ya Marko, watu
wawili tena waliandika vitabu kama cha kwake, wakikitegemea kwa kiasi kikubwa
na kukipanua kwa habari za utoto wa Yesu, mafundisho mengi zaidi n.k. Wataalamu
wanaona Injili hizo za Mathayo na Luka ziliandikwa kati ya miaka 80 na 90, hata
hatujui ipi imetangulia. Mazingira ni yaleyale ya Mashariki ya Kati, labda
Antiokia, ila walengwa ni tofauti. Injili ya Mathayo iliandikwa kwa ajili ya
Wakristo wa Kiyahudi wakati mabishano kati ya Kanisa na Israeli yalipozidi, na
ina lengo la kuwaimarisha katika imani yao kuwa Yesu ndiye Masiya, ndiye Musa
mpya. Kumbe Luka ambaye alikuwa Mpagani kwanza aliwaandikia hasa Wakristo wa
mataifa akisisitiza upendo wa Yesu kwa wote, na kwa namna ya pekee kwa maskini,
wakosefu na wengine waliodharauliwa.
Injili hizo tatu
zinaitwa “ndugu” kwa jinsi zinavyofanana katika mpangilio, katika habari na
pengine katika maneno yenyewe; kwa Kigiriki zinaitwa “sunoptiki”, yaani
zinazotazamika kwa pamoja. Kama tulivyoeleza, Luka aliiongezea Injili yake
kitabu cha pili, yaani Matendo ya Mitume, kama mwendelezo wake, kwa kuwa aliona
kazi ya Kristo inakamilishwa na Roho Mtakatifu katika ile ya Kanisa.
Kitabu kingine ambacho
labda kiliandikwa miaka ya 80 kina jina la Yakobo, lakini wataalamu hawapatani kuhusu huyo ni nani,
aliandika wapi na lini. Kwa hakika walengwa wa kitabu ni Wakristo wa Kiyahudi
wenzake, lakini si barua halisi, bali ni mchanganyiko wa mawaidha yanayofuata
mtindo wa vitabu vya hekima. Lengo lake ni kuhakikisha Ukristo usiishie katika
mawazo mazuri, bali imani ijitokeze katika matendo mema. Lengo lingine ni
kuwakuza mafukara na kuwakemea matajiri, kadiri ya mwelekeo wa Kanisa la
Yerusalemu (Yak 1:1-2:26; 4:1-5:6).
Hatujui vizuri mwandishi
wa barua hii ni nani (ingawa anajiita ndugu wa Yakobo), wala aliandika lini
(wengi wanakisia miaka ya 80), wala aliwaandikia akina nani (barua ni kwa wote,
ingawa baadhi wanahisi walengwa kuwa ni Wakristo wa Kiyahudi walio nje ya
Israeli). Ujumbe ni kujihadhari na wazushi wanaobunibuni mafundisho mapya
badala ya kushika imani ile iliyofunuliwa mara moja na ikatosha; ujumbe huo
ulitolewa kwa kuwatukana na kuwalaani wazushi hao (Yuda 1-4, 17-25).
Siku hizi wataalamu
wanakubaliana kukanusha barua hiyo kuwa imeandikwa kweli na Mtume
Petro, wakisema ni kitabu cha
mwisho kuandikwa katika Biblia (labda Roma mwaka 100 hivi). Kwa hakika
iliandikwa baada ya barua ya Yuda, kwa sababu inatumia maneno yake mengi.
Inawezekana mwandishi alitumia vilevile maneno ya Petro ambayo sasa yamepotea;
kwa vyovyote aliandika kwa mamlaka yake kwa makanisa yote ili kuthibitisha
mapokeo. Pamoja na kupinga uzushi, lengo la barua ni kueleza sababu gani Bwana
anachelewa kurudi. Mafundisho mengine muhimu yaliyomo yanahusu uvuvio wa Roho
Mtakatifu juu ya waandishi wa Biblia (Paulo mmojawao), wito wetu wa kushiriki
umungu, uwepo wa ulimwengu mpya baada ya huu wa sasa kuangamizwa (2Pet
1:3-11,19 21; 3:8-18).
Kundi la mwisho la
vitabu vya Agano Jipya linajulikana kwa jina la Yohane, kwa kuwa Injili ya nne,
barua tatu na kitabu cha Ufunuo viliandikwa na mtume huyo na wanafunzi wake.
Akiwa kijana kuliko mitume wenzake, Yohane alijaliwa kuishi miaka mingi na
kuandika hadi miaka 70 hivi baada ya Yesu kwenda mbinguni. Miaka hiyo yote
alizidi kutafakari na kuhubiri maneno na matendo ya Bwana akitambua mafumbo
mengi yaliyofichika ndani yake. Pengine alirekebisharekebisha maandiko yake
mpaka mwishoni, halafu akawaachia wanafunzi wake kuyakamilisha na kuyaeneza kati
ya Wakristo wa mkoa wa Efeso ambapo Yohane aliongoza Kanisa miaka mingi.
Ufunuo ni kitabu pekee
cha kinabii katika Agano Jipya; kilikamilika mwaka 95 hivi; lengo lake ni
kuwaimarisha katika tumaini Wakristo waliozidi kudhulumiwa na serikali ya Roma.
Kimejaa mafumbo kama kawaida ya mtindo wa kiapokaliptiko. Mtindo huo ni mgumu
kueleweka kwa sababu mwandishi hakuweza kutamka wazi watesi watakaoangamizwa ni
akina nani. Tena alipenda kusisitiza anatoboa siri za Mungu alizojaliwa kuzijua
kwa njia za ajabu (njozi, malaika n.k.). Tunahitaji kutafsiri mifano mingi
(vitu, viungo, rangi n.k.) na tarakimu (saba, kumi na mbili n.k.). Kwa ajili
hiyo ni muhimu kujua maana zake katika Biblia (Ufunuo umejaa madondoo ya Agano
la Kale: mistari 274 kwa 404!).
Mpangilio wake kwanza
una barua saba kwa makanisa ya mkoa wa Efeso, halafu sura 4-22 zina unabii
kuhusu mambo yajayo, yaani vita vikali zaidi na zaidi kati ya Kristo na shetani
ambaye anatumia dini na serikali za Kipagani. Ushindi utakuwa wa Kristo na
Kanisa, ambao hatimaye wanachorwa kama bwanaarusi na bibiarusi katika utukufu
wa Mungu. (Ufu 1;4-5; 12; 21-22).
Injili ya Yohane
Injili hiyo ni tofauti
sana na zile ndugu kwa mtindo na kwa mpangilio, kwa mafundisho na kwa habari
zenyewe. Labda Yohane alisoma walau mojawapo, asipende kurudia habari zilezile,
bali kuzikamilisha na kuzisahihisha akiwa ni shahidi bora kati ya mitume wote.
Hata hivyo hakutaka kuandika kitabu cha historia tu, bali habari njema hasa kwa
kuchimba ishara alizozitenda Yesu zinazotufumbulia fumbo lake mwenyewe na
sakramenti zake. Lengo ni kuwafanya wasomaji wamuamini kuwa ni Mwana wa Mungu
na kwa kumuamini wapate uzima wa milele. Injili hiyo inatudai tukomae katika
maisha ya sala na kutafakari, tukizidi kumuuliza Yesu, “Wewe ni nani?”. Katika
Injili hiyo atatupa jibu moja baada ya lingine. Kitabu kilikaribia kukamilika
mwaka 90 hivi; toleo la mwisho na sura ya 21 ni kazi ya wanafunzi wa Yohane
miaka kama 10 baadaye (Yoh. 20:30-31; 21:24-25).
Barua tatu za Yohane
Ziliandikwa kati ya
mwaka 90 na 100, wakati ambapo jumuia za wafuasi wa Yohane zilianza
kusambaratika. Mafundisho na lugha vinalingana na Injili ya nne. Barua ya tatu na ya pili hazina mafundisho
muhimu, tofauti na ile ya kwanza inayodai imani
sahihi na maisha matakatifu
ili mtu astahili kuitwa Mkristo kweli. Inakaza umwilisho wa Mwana wa
Mungu na haja ya kuishi kwa
uadilifu, na hasa kwa upendo (1Yoh 1:1-4; 2:3-11; 3:11-4:21; 2Yoh 7-13).
Maoni