INJILI NA MAZINGIRA YA MTU.

 

INJILI NA MAZINGIRA YA MTU.

Wafilipi 3:7-8 “Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo. Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;”

 

Paulo alikuwa mwaminifu katika dini yake ya Kiyahudi aliyokuwa nayo, Bwana akamgeuza na kumuingiza upande wa pili yaani upande wa Yesu ili aweze kufanya vizuri upande huu; tunamuona Paulo hata alipoingia upande wa Yesu alisimama na kuihubiri injili kwa uaminifu, kuna watu ambao wana roho au tabia ya uaminifu ndani yao hata kabla hawajaokoka, Mungu wa Mbinguni anamgeuza huyo mtu ili apate kumwabudu Mungu wa kweli na kutenda vizuri na kwa uaminifu wote.

Unaweza kumkuta mtu anatamani kusonga mbele lakini kuna watu wanamzuia asisonge mbele, unapaswa kuwa mwaminifu ili Mungu asimame na wewe na kukupa wepesi wakusonga mbele.

Kile ulichonacho usikubali kukaa nacho chini wala kuzimia moyo simama kwenye kile ambacho Mungu amekupa nawe utatokeza.

 

Kuna mtu ndani yake ana kitu kizuri inaweza ikawa ni uimbaji lakini akitamani kuimba kuna mtu anakuja na kumwambia hauwezi, kama Mungu alikupa hicho simama katika uaminifu naye Mungu atakufanya utokeze mahali kwa ajili ya utukufu wake.

Daudi aliweza kuwa mfalme wa Israel kwa sababu ya Goliati, kwa nini? Kizingiti kikubwa cha Israel kilikuwa ni Goliati, kwa sababu hiyo ili Mungu ajipatie mtu mwaminifu asiyeogopa ni lazima aweke kizingiti mbele ili huyo mtu apate kukivuka na Mungu apate kujitwalia mtu huyo. Kipawa ulichonacho hakiwezi kutokeza au kuchanua bila kuwekewa kizingiti mbele yako, kile kizingiti kinachowekwa mbele yako siyo kwa ajili ya kukumaliza bali ni ili uvuke upate kusonga mbele.

Kuna mahali uliwekewa kizingiti na ukashindwa kukivuka, ni lazima ufike mahali utambue ninani aliyekupa hicho kipawa ili uvuke kizingiti na kusonga mbele.

Kuna wakati ulipoteza wito wa Mungu ndani yako na ukaanza kuona mambo hayaendi ukaanza kuuliza kwa nini mambo hayaendi ni kwa sababu ulikata tamaa, leo inuka na usonge mbele, vuka vizingiti ili uweze kufikia ukuu ambao Mungu amekukusudia.

Daudi alipojitokeza na kumpiga Goliati Taifa zima la Israeli walishangaa yule mtu aliye watishia amekwisha kufa, baada ya Daudi kumuua Goliati watu wote wa Israeli walijapanga katika sifa na kumsifu Daudi, ukiona umefanya jambo fulani na watu wakaanza kukusifia hakikisha unamrudishia Mungu utukufu wote.

Wewe unakwenda kumuua Goliati wako ambaye anakutesa, inuka sasa jipe ujasiri vaa silaha za Mungu na usimame ili upate kushinda.

Sauli aliposikia wana wa Israel wanamwimbia na kumsifu Daudi akaogopa kwa kuwa alijua ufalme wake unakwenda kwa Daudi na ndipo akataka kumuua Daudi. Unapo fanya jambo ambalo wengine wameshindwa kulifanya hakikisha unakaa vizuri kwa maana wapo ambao watataka kukuangusha ili usije ukafika kule ambapo Mungu amekukusudia.

Vizingiti vinavyowekwa mbele yako siyo kwa ajili ya kukuangamiza, la! Bali vipo kwa ajili ya kukuvusha, Daudi alikutana na vizingiti ili vimvushe kutoka katika kuchunga kondoo wa baba yake ili aweze kusimama kwa ajili ya Taifa zima la Israeli.

Jambo lolote ambalo Mungu ameliweka katika maisha yako na wewe ukalisimamia kwa uaminifu hakuna mtu atakayeweza kukunyang’anya.

Mahali unapopita kwenye misukosuko na hali ngumu hauoni hata muelekeo inaweza kuwa ni ugonjwa uliokuwa nao umefika hali hata unajiona kuwa unakufa, unapaswa kujua kuwa katikati ya hayo masumbufu ndipo Bwana  anajitokeza, weka imani yako kwake naye ataonekana kwako.

Kuna watu baada ya kuokoka wanaogopa kwenda hata nyumbani kwao kwa sababu wanaogopa kuwa wanaweza kulogwa, sikia nikwambie usiogope wala usiangalie mazingira yao simama kinyume nao simama katika mamlaka uliyopewa na ujitokeze mbele yao na Mungu atakuwa pamoja na wewe, acha uoga. Usiwe muoga kwa sababu mchawi hana nguvu kuliko Mungu uliyenaye.

Injili ya Yesu inapofanya kazi yake ikifika katika mazingira ya mtu, inabadilisha mazoea ya huyo mtu na kumleta kule ambapo Mungu anataka, ukiingia katika msingi ule ambao Mungu anataka ndipo sasa hiyo injili inaanza kukurekebisha kutoka katika yale ambayo unafanya na kuona ni faida na kumbe ni hasara.

Kama wewe nyumbani mwako hauwezi kuangalia watoto au mke wako anaishije, basi wokovu wako ni sifuri, Lazima uwajali watu wa nyumbani mwako kwanza. Katika mazingira yoyote unayopitia uwe mwaminifu mbele za Bwana na mwisho wa siku kitatokeza mwisho wa safari yako.

 Ombi

Mwambie Bwana kunakipawa ulinipa ili kinipe faida lakini sikioni kwa sababu nimejawa na kiburi kinachosababisha kipawa changu kipotee, ninakuomba Bwana Yesu unibadilishe ili kile kipawa change kipate kuonekana.

WAKATI WA KUGEUKA NA KUDADISI

Maisha ya wokovu tuliyonayo ni mazuri na ni matamu kama utazingatia.

Kutoka 3:1-8 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. Bwana akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi.

Mungu alikuwa anamuandaa Musa kwa ajili ya kazi, Musa aliandaliwa kwa mazingira ya ajabu sana alitakiwa kuuwawa alipokuwa mdogo lakini alipata Neema ya kufichwa kisha akalelewa katika nyumba ya kifalme na akapata mafunzo ya kifalme.

Musa alikimbia akiwa na miaka 40 na akakaa jangwani kwa muda wa miaka 40 na baada ya hapo ndipo akakutana na Mungu na kumpa majukumu ya kufanya. Usiseme kuwa umechelewa katika utumishi wako kwa sababu unamiaka mingi, hapana kwa Mungu hakuna kuchelewa bali kilajambo lina majira yake.

 

Musa alipokuwa kule jangwani akichunga mifugo ya mkwewe ndipo akaona kijiti kikiwaka moto; Baada ya Musa kukiona kile kijiti ndipo akasema “Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa”. Musa kwanza kabisa alisimama, akageuka na kudadisi kile kijiti, Mungu akitaka kumtumia mtu yeyote kwanza atamuwekea ishara fulani ambayo itamfanya avutiwe na akisha vutiwa afanye maamuzi ya kugeuka, ili Mungu aweze kufanya naye kazi. Ili Mungu apate kukutumia lazima uwe mdadisi wa kile ulichokiona mpaka kikakuvutia wewe uokoke.

Waliyokuwa tayari kudadisi ndiyo waliyogundua siri za Mungu, uponyaji na maajabu ya Mungu katika wokovu wao kwa sababu walichukua hatua ya kugeuka na kudadisi.

Watu waliyo na kiu ya kudadisi mambo ya Mungu ndio wale ambao Mungu anaona kuwa wameelewa na anaweza kufanya nao kazi.

 

Mungu aliposema na Musa kwa ishara Musa alielewa na akaamua kugeuka na akamuona Mungu kupitia hiyo ishara aliyoiona, sasa je! wewe Mungu hakukuonesha ishara? Mungu alikuonesha ishara wala haukuiona lakini leo hii unataka Mungu aseme na wewe.

Mungu alipokuonesha ishara kwa kukuponya je! Ulikaa chini na kudadisi kwa nini alikuponya? Mungu alipoamua kuondoa dhiki zako na ukaanza kuziona Baraka zake je! Ulikaa chini ukatafakari au ulichukulia ni kawaida tu? Mungu anakuonesha ishara kuwa Yeye yupo, ndio maana akaondoa vita katika ndoa yako, akakuondoa kunako umaskini, je! Mungu alipokuonesha ishara hizo wewe ulikaa chini na ukatafakari?

 

Ili uweze kujua uweza wa Mungu na utendaji wake ni lazima uamue kugeuka na kudadisi. Musa alikuwa na kiu ya kukutana na Mungu ndiyo maana akaamua kuchukua hatua ya kugeuka.

Je wewe haukuona ishara, au bado unaangalia umaskini unaokutesa au bado unaziendea njia zako za kale? Musa alipoamua kugeuka alikiangalia kile kijiti na akakaza macho yake sawasawa ili ayaone maono ya Bwana. Amua kugeuka na kukaza macho yako sawasawa ili upate kuona kile Bwana alichokuandalia.

 

Wana wa Israel walipokuwa jangwani hawakuweza kuendelea mbele kwa sababu hawakuwa na maono mazuri na ile nchi wanayoiendea bali walikuwa na mawazo juu ya lile jangwa wanalo lipitia. Ukiamua kugeuka ili upate kuyaona maono yako usifanye mchezo na wokovu wako, usiwe mtu wa kurudi nyuma wala usifanye mchezo na Mungu wako, kwa maana kwa wewe kufanya hivyo hautaweza kukipata kile ambacho Mungu amekiandaa kwa ajili yako.

Unahitaji kuamini kile ambacho umekiona na usiondoe macho yako katika hicho ndipo Mungu atakuwa tayari kufanya kazi wewe.

Kutoka 3:4 “Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.” Mungu alipomuona Musa ameamua kugeuka ili atazame ndipo Mungu akamwita Musa kwa jina lake ili ampatie maagizo, je! unataka Mungu akuite kwa jina lako? Amua kugeuka,  Je! unataka mwaka huu wa utambulisho Mungu akakutambulishe? Amua kugeuka na kukaza macho yako katika kumtazama YEYE, acha kuangalia mazingira unayoishi au uliyotokea kwa maana ukiyatazama hayo yatakukatisha tamaa. Yamkini umetokea katika familia ya kimasikini, babu na baba yako ni masikini sasa ukiwatazama hao kamwe hautaweza kufika kule ambapo Mungu amekukusudia, kaza macho yako kwa Bwana YEYE aliye muweza wa yote ili uweze kuyapata yale aliyoyaandaa kwa ajili yako.

Mungu hakumtafuta Musa akiwa kati kati ya watu bali alimtafuta akiwa pekeyake, kama unataka kumuona Bwana kaa peke yako.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JINSI YA KUMSHINDA SHETANI

NGUVU YA DAMU YA YESU

VIPAJI VYA ROHO MTAKATIFU