UKOMBOZI NA UPONYAJI
Ukombozi na Uponyaji.
Paulo na sila walifungiwa mahali kwa sababu mapepo waliamua kumtumia mfalme ili kuliharibu kanisa, waliwafungia mahali wakifikiri kuwa sauti zao hazitasikiwa, lakini ilipofika usiku Paulo na Sila wakaamua kuimba na walipoimba Mbingu ilishangaa na kuja kuwasaidia.
Kuna miujiza itatokea ambayo haujawahi kuiona, inaweza ikawa unataarifa mbaya kutoka kwa madaktari kuwa kutokana na ugonjwa ulionao inapaswa utolewe kizazi na hautaweza kuzaa tena, au umeambiwa ugonjwa ulionao hauna dawa, na wengine wameambiwa kuwa ugonjwa ulio nao utakuwa nao mpaka ufe, sikia nikwambie ni hivi ibilisi ndio atakayekufa na huo ugonjwa lakini si wewe, Yesu alikufa msalabani kwa ajili yako.
Unaweza ukawa katika ukoo wenu hakuna aliyewahi kuendesha gari na wewe na kaka zako na mabinamu zako hakuna anaye endesha gari kwa sababu mmefungiwa mahali, lakini leo utatoka kwa Jina la Yesu.
Yesu hakwenda msalabani kwa ajili yake mwenyewe, bali alikwenda kwa ajili yako, siku ile Yesu alimshinda ibilisi ili wewe uweze kuwa huru.
Leo mapepo yaliyondani yako, nyumbani kwako kwenye makaburi ya babu zako leo yatakujua wewe ni nani kwa maana utukufu utakufunika.
Roho za mizimu zipo katika kila ukoo au familia, wao wapo kama walinzi ili kukuangalia wewe usifanye mambo makuuu katika maisha yako, wako ili kukufanya wewe uteseke, wanakulinda ili usifurahie maisha, hao walinzi leo watakwenda kukuachia kwa jina la Yesu na wewe utakwenda kufanikiwa kwa jina la Yesu.
Mathayo 10:8 “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.” leo ufunguo ambao Yesu alimnyang’anya ibilisi wa kukufanya wewe uwe maskini au mgonjwa Yesu aliuchukua huo ufunguo na kutukabidhi sisi ili tuweze kuwa huru, leo ni siku yako ya kuachiliwa huru.
Yesu alipokufa msalabani hakwenda ili kujaribu kufa bali alikufa, hivyo wewe hauhitaji kufa.
Yesu hakuwa anajitahidi kumwaga damu yake, la! Bali Yeye alimwaga damu yake, hakuna kilicho salia mbinguni duniani wala kuzimu hakuna kilicho salia ili kukusababisha wewe uteseke, kila kitu ambacho kingepaswa kufanywa ili wewe uwe huru, uponywe na kukombolewa kilikwisha kutimia.
Hauhitaji kumuomba Yesu akuhurumie, Yeye alikufa kwa ajili yako mwambie Bwana nataka kile ambacho umekusudia kunipa siku ya leo.
Ombi.
Mwambie ibilisi aachilie maisha yako na chochote alicho haribu arudishe kwako maana Yesu alikufa kwaajili yako ili wewe uwe huru.
Kutoka 15:26 “ akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.” Je! wewe umeisikiliza sauti ya Bwana Mungu wako na kusikia maagizo yake? Kama umefanya hivyo inamaana kuwa hauhitaji kuwa na maradhi kwa sababu umetii sauti yake, hivyo hauhitaji kuwa na magonjwa maana hakuna magonjwa wala laana kwako kama Yesu yupo pamoja nawe, hakuna ushahidi wowote wa kukufanya wewe uwe mgonjwa bali upo ushahidi wote wa wewe kuwa huru.
Yeye Bwana ndiye anaye kuponya na si watumishi wanao kuombea, wao ni kama njia ya kuruhusu yatokee yale ambayo Mungu amekuandalia kwa siku hiyo.
Kutoka 23:22-23 “Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali.” Wale wote walio kuloga ili uteseke Bwana atawageukia na kupigana nao badala yako.
Kutoka 23:25 “Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako.” Yeye ataondoa ugonjwa unao kutesa,
Yesu alipo kufa alikufa kwa ajili yako.
1Yohana 3:8 “atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” Mwana wa Mungu alidhihirishwa hapa duniani kwa kusudi moja tu, kusudi gani hilo? Kuzivunja kazi za ibilisi.
Kazi hizo ni zipi?
1. Dhambi
2. Maradhi
3. Magonjwa
4. Umaskini
5. Kushindwa
Kazi hizi tano zilimfanya ibilisi atawale ulimwengu kwa sababu ya udhaifu na upumbavu wa Adamu alimsababisha ashindwe, hivyo Yesu alikuja ili kuharibu kazi hizi tano.
Tunamamlaka yote ya kuziharibu kazi za ibilisi,
Kwa sababu Yesu alikuja kuharibu dhambi, maradhi, magonjwa, umaskini na kila aina ya kushindwa kwako, hivyo Yesu hakuja kubembeleza dhambi wala mapepo.
kwa jinsi alivyoshughulika na dhambi ndivyo hivyo alishughulikia magonjwa, maradhi na mapepo kuyafukuza kwa watu.
Tunawezaje kupata nguvu ya Mungu ndani yetu? Kwa kunena kwa lugha maana tunapo nena kwa lugha tunamruhusu yule Roho wake kutuhuisha ili ile nguvu yake ipate kuingia ndani yetu.
Maoni