MBUNIFU WA UMEME NA ZANA ZAKILIMO NJOMBE AFARIKI DUNIA


  • Njombe
    . Mamia ya wananchi wamejitokeza kushiriki maziko ya aliyekuwa mbunifu wa umeme na zana za kilimo mkoani Njombe, John Fute maarufu kama ‘Mzee Pwagu’ aliyefariki dunia Ijumaa, Julai 28, 2023.
  • Mzee Pwagu ambaye  alijipatia umarufu kutokana na kazi zake na kuitwa Ikulu na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati John Pombe Magufuli, ameagwa na kuzikwa leo nyumbani kwake mtaa wa Msete Halmashauri ya Mji wa Njombe.
  • Wakizungumza kwa masikitiko leo Jumapili, Julai 30, 2023 wananchi walioshiriki mazishi ya Mzee Pwagu wamesema msiba huo ni mkubwa kwao kutokana na shughuli alizokuwa anazifanya zilikuwa na manufaa siyo tu kwa upande wake bali kwa jamii iliyomzunguka, mkoa na taifa kwa ujumla.
  • Marehemu Mzee Pwagu wakati wa uhai wake alitengeneza umeme ambao unakadiriwa kuwa na killowatt 28 kwa ajili ya matumizi yake na majirani waliomzunguka.
  • Kupitia utengenezaji wa pampu za umwagiliaji, marehemu atakumbukwa hasa na wakulima wa parachichi kwani aliwasaidia katika kuwezesha kilimo cha umwagiliaji kupitia pampu ambazo ziliweza kuvuta maji kutoka mabondeni mpaka kwenye mashamba yao.
  • Mbali na mafanikio hayo, Mzee Pwagu alitumia ujuzi alionao katika kuwafundisha wengine ili nao waweze kupata ujuzi huo ambao utawasaidia wao na jamii kwa ujumla.
  • Baraka Kungu mkazi wa mtaa wa Msete amesema ubunifu wake umewasaidia kuwawezesha kupata maji kutokana na mtambo ambao aliufunga Mjimwema Kijiweni ulioweza kutoa maji bondeni na kupandisha mlimani.
  • "Kwa pale kijiweni asilimia kubwa wanatumia maji ya Pwagu kwahiyo ni msiba mkubwa kwa kata ya mji Mwema na Njombe nzima na nadhani kwa taifa kwa ujumla," amesema Kungu.
  • Rebeca Hepelwa, Mwenyekiti wa wakulima wa parachichi  amesema marehemu aliwasaidia wananchi wengi hasa wawekezaji wa kilimo cha parachichi na kunufaika kutokana na kipaji chake."Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Pwagu, naamini kabisa amewasaidia wananchi wengi hasa wawekezaji wa Njombe katika kilimo cha parachichi," amesema Rebecca.
  • Msemaji wa familia ya John Fute (mzee Pwagu) Lusungu Lyanzile amesema marehemu Pwagu alizaliwa mwaka 1958 katika hospitali ya Kibena iliyopo Halmashauri ya Mji wa Njombe.
  • Amesema mwaka 1980 marehemu ndipo alianza kujishughulisha na ubunifu wa umeme wa nyumbani, viwandani na ujenzi wa laini za umeme mkubwa.
  • Amesema katika ubunifu wake wa umeme kwa mara ya kwanza alitengezeza  volt 12 hapo ndipo aliendelea kutumia uwezo wake binafsi na kutengeneza umeme wa kilowatt 28 ambazo alitumia kwa matumizi yake binafsi na matumizi mbalimbali.
  • Amesema kutokana na ubunifu wake mwaka 2013 Serikali ilikwenda kuzindua jengo la karakana kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru.
  • Amesema ubunifu wa marehemu ulimfanya kuitwa Ikulu mwaka 2019 na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano hayati John Pombe Magufuli na kuzawadiwa cheti cha ubunifu na tume ya sayansi kutoka Ofisi ya Rais.
  • Amesema Aprili 26, 2023 marehemu alianza kuona hali yake haipo sawa hivyo kwenda Hospitali ya Kibena kwa ajili ya matibabu na baada ya vipimo aligundulika kuwa na matatizo ya saratani.
  • "Baada ya tatizo kujulikana alianza matibabu na hali yake ikarejea na kupata unafuu hivyo alirudi na kuendelea na kazi zake," alisema Lyanzile.
  • Amesema June Mosi, mwaka huu ghafla hali yake ilibadilika tena na kupelekwa hospitali ya Ikonda ambako alitibiwa kwa mwezi mmoja na wiki mbili.
  • Amesema Julai 27 Julai hali yake ilibadilika tena na kupelekwa Hospitali ya Rufaa Njombe na kugundulika kuwa na matatizo ya presha, kisukari pamoja na figo."Hospitali ya rufaa Njombe walitoa rufaa apelekwe Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya kwa matibabu hivyo aliruhusiwa na kurudi nyumbani," ameongeza Lyanzile.
  • Amesema alipofika nyumbani hali ilibadilika tena na kupelekwa Hospitali ya Kibena ambapo julai 28 saa mbili usiku alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu.
  • Nao wabunifu waliokuwa wanashirikiana na marehemu Mzee Pwagu akiwemo Rainel Ngailo ambaye naye aliitwa Ikulu na hayati Magufuli amesema licha ya kuwa na majonzi kutokana na msiba huo lakini kuna ahadi ambayo ilitolewa na Serikali ya kuwasaidia wabunifu lakini mpaka sasa haijatekelezwa.
  • "Hayati Magufuli alitoa wito Serikali kuwa watu hawa wasaidiwe nilikuwepo mimi mwenyewe Rainel Ngailo na John Fute lakini toka amefariki yeye kwakweli hatujasaidiwa," amesema Ngailo.
  • Katibu wa Chama cha Mapinduzi kata ya mji Mwema John Kilasi amesema marehemu alitia nguvu na shirika la umeme (Tanesco) mkoa wa Njombe kuanza kusambaza umeme haraka kwasababu alitengeneza ushindani.
  • "Mahali alipokuwa waliona kuwa wakizubaa tayari atawapiku huyu Tanesco wa Msete kwahiyo walikuwa wanaharakisha huduma mahali alipo," amesema Kilasi.
  • Naye mtoto wa marehemu Lusungu Fute amesema marehemu wakati wa uhai wake alikuwa anawapitisha katika kile alichokuwa anakifanya tangu wakiwa watoto mpaka sasa hivyo kuahidi kuendeleza yale yaliyoachwa na marehemu baba yao.
  • "Kwa kumuenzi kwake sisi ni kuendeleza alichokifanya ni tunu aliyotuachia tutakayoendelea nayo," amesema Fute

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JINSI YA KUMSHINDA SHETANI

NGUVU YA DAMU YA YESU

VIPAJI VYA ROHO MTAKATIFU