USHUHUDA ULIO HAI NI NGUVU YA MWAMINI
USHUHUDA ULIO HAI NI NGUVU YA MWAMINI
Ushuhuda ni silaha ya nguvu dhidi ya adui zako. Ufunuo 12:11 “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”Mungu alisema yeyote anayetaka uzima lazima atoe uhai wake lakini ukiuzuia uhai wako basi hauna uzima kwa maana ibilisi atakuharibu na kukuangamiza.
Kutoa kuna nguvu sana, unapotoa uhai wako hapo ndipo nguvu ya mwamini ilipo.
1 Yohana 4:4 “Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na Mungu nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika dunia.”
Tunatokana na Mungu kwa jinsi gani? Kwa kupitia kuishi kwako, unapojitoa kwa Mungu inamaana kuwa unakuwa si wewe tena bali unakuwa ni mali ya Mungu. Pale unapokuwa ushuhuda ulio hai ndipo unakuwa na maisha ya utoshelevu, unakuwa mkuu kuliko wa ulimwengu, na kwa sababu hiyo unakuwa na haya:-
• Hakuna anayeweza kukuangamiza kwa sababu wewe ulishakufa,
• Magonjwa na maradhi hayawezi kukuangamiza kwa sababu ulikwisha kufa.
• Wachawi hawawezi kukuchawia kwa nini? Kwa sababu wewe ni mkubwa kuliko wao.
• Ajali haiwezi kukuharibu kwa sababu unakuwa uko juu ya ajali.
Haya yote yanawezeshwa kwako kupitia Pendo la Mungu lililo ndani yako.
Mambo yanayofanya ushuhuda ulio hai katika maisha yako.
1. Pendo la Mungu ndani yako linakufanya uwe ushuhuda ulio hai,
2. Kwa sababu ya muingiliano kati ya mbingu na dunia unakuwa ushuhuda ulio hai.
• Kwa jinsi unavyojipenda mwenyewe kwa Mungu unamfanya Mungu aishi hapa duniani na wewe unaishi mbinguni ilihali upo duniani, yaani kunakuwa na muingiliano.
• Ushuhuda ulio hai maana yake ni maisha yako yameingiliana kati yako na mbinguni, hivyo mtu hawezi kuelewa wewe upo wapi, kwa sababu mawazo yako ni ya kimbingu ilihali upo duniani.
3. Katika maisha ya kufanana na Mungu maisha ya ushuhuda ni maisha ya kufanana na Mungu.
4. Maisha ya ushuhuda ni maisha ya uwakilishi wa mbinguni hapa duniani,
5. Ni maisha ambayo Mungu anatembea, anaishi, anasema, anakula, anavaa na kufanya mambo hapa duniani kupitia wewe, hii ndio tunaona maisha ya ushuhuda, watu hawatamuona Mungu bali wataniona mimi, ukinipuuza mimi Mtumishi wa Mungu unampuuza Mungu na ukinisikiliza mimi unamsikiliza Yeye.
Maisha ya ushuhuda ni haya, kula, kutembea, kuongea kwa ajili yake na lolote ulitendalo kwa ajili yake.
Ukristo sio maisha yaliyo tupu la bali ni maisha ya utele.
6. Maisha ya ushuhuda ulio hai ni maisha ya uhuru, ni maisha nje ya hukumu.
• 1 Yohana 4:15 “Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu.” Siku ulipompokea Yesu awe Bwana na mwokozi wa maisha yako (ulipookoka) Mungu alifanya makao yake ndani yako, kama umeokoka inamaana kuwa wewe ni mwenyeji wa Mungu umembeba Mungu ndani yako.
• Kuna tofauti kati ya watu waliookoka na watu ambao hawajaokoka, kwa waliookoka unaweza kuwaona wanatembea wanakula, wanavaa, wanalala kama watu wengine lakini wao sio wa ulimwengu huu na wapo duniani ili kumuwakilisha Mungu huku duniani.
• 1 Yohana 4:16-17 “Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake, Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, kama yeye alivyo, ndivyo tulivyo na sisi ulimwenguni humu.”
Ndio akili yako inaweza isielewe lakini wewe amini tu kuwa kama Mungu alivyo ndivyo ulivyo na wewe ulimwenguni, unapotembea tambua kuwa wewe ni wa Mungu na muwakilishi wa Mungu huku duniani.
Ni kwa nini vitu havitokei katika maisha yako? Ni kwa sababu wewe haukiri wala hauyasemi yale unayoyaamini, Mungu husema na vitu vikatokea na wewe sema mpaka vitokee.
Tangaza kile unachokiamini kwa maana kwa jinsi unavyotangaza ndivyo mazingira yanavyoumba nalo linatokea, tangaza na kukiri mpaka kitokee. Mungu hatawahi kuja hapa kwasababu wewe tayari upo na ni muwakilishi wake hivyo tangaza ili vitu vitokee.
Amosi 3:7 “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” Kwa nini? Mungu anataka mtu atangaze ili Yeye apate kutimiza, muhusishe Mungu, unamuhusishaje Mungu mambo yako? Kwa kutangaza.
Je! Una neno lolote ambalo unataka litokee katika maisha yako? Tangaza hilo neno sasa, ukiamka asubuhi tangaza hilo neno, ukienda kazini na popote pale utakapokuwa tangaza hilo Neno na litatokea kwako.
Neno lina nguvu jifunze kuweka ukiri katika maisha yako nalo litatokea kwako.
Warumi 11:36 “Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.” Vyote vyatoka kwa Mungu mimi na wewe na kila kitu huku duniani vimetoka kwake na viko kwa uweza wake hivyo usiwaogope wanadamu wao wametoka kwa Mungu, wewe uko kwa ajili ya Mungu na umetoka kwa Mungu hivyo hakuna wa kukudhuru.
Yapasa ujitoe mzima mzima kwa Mungu kwa wewe kufanya hivyo ibilisi anakuwa hana nafasi kwako.
Ukiri:
• Bwana mimi nilitoka kwako kwa maana hiyo najitoa kwako na ninarejea kwako acha ikawe utukufu.
• Bwana mimi ni utukufu wako leo narejea kwako.
Kuanzia leo jifunze kuwa na ukili yale mambo ambayo unataka yatokee katika maisha yako yatangaze na uyatolee sadaka nayo yatatokea kwako.
Maoni