WANAWAKE KUWA WACHUNGAJI

 Mistari muhimu ya kukumbuka:-


1 WAKORINTHO 14:34-36:-

34 Wanawake na wanyamaze katika kanisa, maana hawana ruhusa kunena bali watii, kama vile inenavyo torati nayo.

35 Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa.

36 Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu?


1 TIMOTHEO 2:11-12:-

11 Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.

12 Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.


Katika sehemu ya kwanza ya somo hili lilopita tuliona na kuchambua juu ya hoja potofu zinazotumiwa na watu kuhusu mwanamke kutokuwa Mchungaji au Muhubiri. Tulijiona usahihi wake na kujifunza mengi juu ya suala hilo katika kipengele hicho.
Lakini leo tunamalizia juu ya hoja yao nyingine potofu na kupiga hatua tena kumalizia vile vipengele vilivyosalia.

HOJA YAO YA TATU .

Watasema,

Katika wale mitume 12 wa Yssu . Hatuoni mahali popote ambapo Yesu alichagua mwanamke hata mmoja, bali wote walikuwa ni wanaume !

[ L U K A 6:12-16 ]

Hata kama Yesu hakuchagua mwanamke mtume miongoni mwao Thenasara . Hilo sio zuio la kuwafanya wanawake basi wasiwe mitume leo . Hata wakina Paulo na Epafrodito hawakuchaguliwa wala kujulikana kabisa mwanzoni miongoni mwa wale mitume kumi na mbili . Lakini kipindi kingine cha baadaye sana kilichofuata , ndipo tunaona Yesu tena akiendelea kuwaita watu wengine pia kuwa mitume mfano wao.
[ WAGALATIA 1:1-2; WAFILIPI 2:25].

Kama ilivyokuwa nyakati za kanisa la kwanza na bado hata nyakati za dunia ya leo bado Yesu anaendelea kuwaita watu wengine kuwa mitume, manabii, wainjilisti, waalimu, na wachungaji ili kazi ya ufalme wa Mungu izidi kuimarika na kupanuka katika kuujenga mwili wa Kristo. Mitume na manabii hawakuishia tu wakati wa Biblia bado hata leo Yesu anaendelea kuwainua watu mbalimbali kuwa mitume na manabii n.k. Neno la Mungu linatuambia Yesu ni yule yule, jana, leo na hata milele. Habadiliki. Haleluya!
[WAEFESO 4:11-12; WAEBRANIA 13:8 ] .

Bado hata leo Yesu anaweza kuwaita wanawake wengine kuwa mitume na tena hata wachungaji, waalimu, manabii n.k. Maana hizi zote ni karama za huduma ambazo Roho Mtakatifu huzitoa KWA KILA MTU, kama apendavyo Roho mwenyewe; Na sio kwa wanaume tu pekee yao
[1 WAKORINTHO 12:1-11, 28-31] . Maana hakuna upendeleo wowote wa kijinsia kwa Mungu, wanaume na wanawake wote hukubaliwa kwa msingi huo pia
[ MATENDO 10:34-35].

Kama nilivyotangulia kusema Yesu kutokuchagua mwanamke mtume miongoni mwa wale Thenashara. Hilo halimainishi kwamba Yesu hakutaka wanawake wasiwe mitume au hawezi kuwa mitume. La asha!

Yesu hakuchagua mtume mwanamke miongoni mwao kipindi hicho kwa sababu kuu mbili.

Kwanza ,

Wayahudi katika utamaduni wao walikuwa hawanaga mazoea ya kuchangamana sana na wanawake kwa mfungamano mmoja ulio wa karibu zaidi ; Torati iliwatenga na kuwashusha chini kithamani wanawake mbali na waume katika mambo mbalimbali ya kiibada hata ya kijamii . Wanawake walifanywa duni kuliko wanaume [ WALAWI 15:19-30].

Sasa Yesu alizaliwa chini ya sheria ili awakomboe waliko chini ya sheria (Wayahudi). Na kwa maana hiyo laiti kama Yesu mwanzoni mwa huduma yake, angemchagua mwanamke mtume miongoni mwao na kuambatana naye kila kona. Kutokana na mapokeo ya desturi za wayahudi, ki-ukweli huduma ya Yesu isingeweza kupokelewa kirahisi machoni pao . Isingekuwa rahisi Yesu kuweza kuwahubiria na kuwapata wayahudi. Sasa kwa hekima ya Yesu ilibidi achukuliane na hali yao hiyo ili kuwa rahisi kuwapata, ni mbinu pia aliyoituma Paulo mtume
[ GALATIA 4:4-5; 1KOR 9:19-22 ]

Lakini wakati ulipotumia na majira yalipofika. Baada ya Yesu kuimaliza kazi yake ya ukombozi pale msalabani. Alifutilia mbali kila namna ya desturi na ubaguzi wa Torati uilowabagua wanawake na wanaume, mataifa kwa Waisraeli . Akawafanya wote waliokuwa wawili kuwa mmoja pasina tofauti yoyote [ WAEFESO 2:13-18]

Ndiomaana mwanamke wakati wa Torati alishushwa chini; lakini katika neema ya Kristo mwanamke wakati wa Agano jipya amepandishwa juu zaidi . Hakuna cha mwanaume wala manaumke, wote ni wenye haki sawasawa mbele za Mungu katika utumishi wa wokovu wao . Mwanaume hana la kujivuna zaidi ya mwanamke wala mwanamke zaidi ya mwanaume mbele za Mungu .
[1 PETRO 3:7; WAGALATIA 3:26-28; 1 WAKORINTO 4:6-7] .

Sababu ya pili,

Yesu hakuweza kumchagua mwanamke mtume miongoni mwa wale Thenasara waliombatana naye, alifanya hivyo ili KUEPUSHA DHANA POTOFU TU .

Ni muhimu kufaham Yesu katika huduma yake hapa duniani hakuwahi kuwa na mke yoyote wala hakuwahi kuwa na mpango wowote wa kuoa.

Na kumbuka Yesu karibu muda wote alikuwa akikaa nao , akitembea nao wanafunzi wake huku na kule na hata kulala nao pamoja milimani .

Sasa katika mazingira kama hayo ingetokea Yesu akamchagua mtume mwanamke miongoni mwao wa kuambatana naye kila kona aendako . Unafikiri nini ? Bila shaka watu wangeanza kujaji na kumuisia sana Bwana Yesu vibaya mno na hata kumzushia maneno tofauti. Ndiyomaana katika maneno yote ya uzushi alionenewa Yesu, kamwe hawakuhi kumwita "Yesu ni Malaya au kumtuhumu kwa uzinzi/ uasherati " . Maana wangeipatia wapi hiyo sababu hata kama ni ya kuzusha? Maana hawakuwahi kumwona Yesu akiketi na wanawake popote. Yesu alipokuja akila na kunywa, walimwita eti mlafi na mlevi huyu [ MATHAYO 11:18-19] . Imagine Sasa kama Yesu Ingetokea akachagua mtume mwanamke wa kuambatana naye, enhee si ndio wangepata neno tena la kuzusha, Yesu kahaba huyu !! Na hivyo jambo hilo lingechafua sana huduma yake.

Biblia inasema katika YOHANA 4:25-28: -"Yule mwanamke akamwambia, Najua ya kuwa yuaja Masihi, (aitwaye Kristo); naye atakapokuja, yeye atatufunulia mambo yote. Yesu akamwambia, Mimi ninayesema nawe, ndiye. Mara hiyo wakaja wanafunzi wake, wakastaajabu kwa sababu alikuwa akisema na mwanamke; lakini hakuna aliyesema, Unatafuta nini? Au, Mbona unasema naye? Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu."

Jaribu tu kuwaza kama Yesu walimkuta na mwanamke tu hapo akiongea naye. Wakabaki wamestajabu wakihisi tofauti . Sasa ingekuwaje kama Yesu angechagua mtume mwanamke miongoni mwao. Sio ndio wanadamu wangesema ni mke wa Yesu huyo ?! Buzi wake.

Biblia inatufundisha juu ya hayo ikisema
1 TIMOTHEO 1:19:-

"Uwe mwenye imani na DHAMIRI NJEMA, ambayo wengine wameisukumia mbali, wakaangamia kwa habari ya Imani.

2 WAKORINTO 8:20-21:-

20 Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii tunayoitumikia;

21. tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu.

Hii ndiyo sababu ya msingi pia iliyomfanya Yesu kumtomchagua mtume mwanamke miongoni mwao ili kuiepusha ile dhana potofu , awe na ushuhuda wa dhamiri njema isiyo na hatia machoni pa wanadamu. Hilo tu !

Baada ya kufahamu hayo.

Leo tena katika sehemu ya pili ya somo letu .Tunapiga tena hatua kutokea pale tulipoliishia.

KIPENGELE NO:-2

UHALALI WA MWANAMKE KUHUBIRI/ KUFUNDISHA KANISANI .

Neno " Kuhutubu". Maana yake ni kuhubiri au kufundisha au kutoa hotuba .

Mwanamke Ki-biblia anaruhusiwa kufundisha au kuhubiri Neno la Mungu sawasawa tu na mwanaume. Biblia inasema katika

1 WAKORINTO 11:5

"BALI KILA MWANAMKE ASALIPO, AU ANAPOHUTUBU, bila kufunika kichwa, yuaaibisha kichwa chake; kwa maana ni sawasawa na yule aliyenyolewa."

1 WAKORINTHO 14:3-5, 23-32:-

3 BALI YEYE AHUTUBUYE, asema na watu maneno ya kuwajenga, na kuwafariji, na kuwatia moyo.

4 Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa .

5 Nami nataka NINYI NYOTE mnene kwa lugha, lakini ZAIDI SANA MPATE KUHUTUBU, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa .

23 -32. Haya! Ikiwa kanisa lote limekusanyika pamoja, na wote wanene kwa lugha, kisha ikawa wameingia watu wajinga au wasioamini, je! Hawatasema ya kwamba mna wazimu? LAKINI WOTE WAKIHUTUBU , kisha akaingia mtu asiyeamini, au mjinga, abainishwa na wote, ahukumiwa na wote; siri za moyo wake huwa wazi; na hivyo atamwabudu Mungu, akianguka kifudifudi, na kukiri ya kuwa Mungu yu kati yenu bila shaka. Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga. Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri. Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu. Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue . Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze. Kwa maana NINYI NYOTE MWAWEZA KUHUTUBU MMOJA MMOJA, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe. Na roho za manabii huwatii manabii.

WAKOLOSAI 3:15-16:-

"Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja ; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, MKIFUNDISHANA na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.

TITO 2:3:-

" Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali WAFUNDISHAO MEMA.

1 TIMOTHEO 5:2, 17:-

"Wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu; hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.

ZABURI 68:11

" Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari njema ni jeshi kubwa"

Soma pia WAFILIPI 4:2-3 .

Maandiko hayo ya Neno la Mungu kwa ujumla wake yanatuonesha na kutufundisha waziwazi kwamba mwanamke anayo haki ya kulihubiri na kulifundisha Neno la Mungu ndani ya kanisa na hata nje ya kanisa.

WATUMISHI WA MUNGU WANAWAKE

Nabii ni msemaji wa Mungu tena ni mwonaji wa siri za Mungu. Biblia inasema katika AMOSI 3:7:-"Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote , bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri zake" .

Nabii ni ngazi muhimu mno na ya juu mno katika utendaji wa kazi za Mungu. Lolote Mungu analotaka kulifanya lazima apitie kwa manabii.

Walikuwepo wanawake manabii ambao Mungu aliwainua na kuwatumia kutoa ujumbe wa Neno lake kwa watu wote. Na wanaume waliketi chini yao wanawake hawa, wakiongozwa nao na kuwasikiliza.

(1) NABII DEBORA

WAAMUZI 4:4-5:-" Basi Debora, nabii mke , mkewe lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule. Naye alikaa chini ya Mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima vya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue" .

(2) NABII HULDA

2 WAFALME 22:12-18.

(3) NABII MIRIAMU

KUTOKA 15:20.

(4) NABII ANNA

LUKA 2:36-38

Si hilo tu. Wanawake nao ni watumishi wa Mungu sawasawa tu na wanaume. Kama vile Roho wa Mungu anavyoweza kumtumia mwanaume kuhubiri au kuwa mchungaji, Nabii, Mtume n. k. Ndivyo hivyo hivyo Roho wa Mungu anavyoweza kuwatumia wanawake pia. Biblia inasema katika

MATENDO 2:17-18:-
"Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia WATUMISHI WANGU WANAUME NA WANAWAKE Roho yangu, nao watatabiri."

KUTOKA 38:8:-"Kisha akafanya hilo birika la shaba, na tako lake la shaba; shaba hiyo ilikuwa ni ya vioo vya wanawake wenye kutumika, waliokuwa wakitumika mlangoni mwa hema ya kukutania "

KIPENGELE NO:-3.

UHALALI WA MWANAMKE KUWA MCHUNGAJI

Kwanza tunaona Yesu alisema katika

MATHAYO 19:28-29:-

"Yesu akawaambia, Amin, nawaambia.......Na KILA MTU aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike , au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu , atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele."

Unaona Bwana Yesu amesema hapo KILA MTU (HAJABAGUA JINSIA) AWE MWANAMKE AU MWANAUME ambaye ameacha vitu vyote na kuamua kuyatoa maisha yake yote kwa ajili ya utumishi wa kazi yake Yesu. Atapokea mara mia na kuurithi uzima wa milele.

Wako wanawake mashujaa miongoni mwetu walioamua kuacha kazi zao nzuri na shughuli zao zote za kiuchumi, Baada ya Mungu kweli kuwaita katika kazi ya uchungaji ; Wameyatoa maisha yao yote kwa ajili ya utumishi huo , kama Mungu alivyowaita na kuwathibitisha.

Hakuna Andiko lolote katika Biblia ambalo linasema au kukataza kwamba wanawake wasiwe wachungaji. HALIPO. Bali kinachobakia zinakuwa ni tafsiri potofu tu za watu katika maandiko wanaosema kwamba wanawake hawawezi kuwa wachungaji. Ila Neno la Mungu halikatazi mwanamke kuwa mchungaji. MSIDANGANIKE wapendwa [ WAKOLOSAI 2:4 ].

NB

Ni muhimu kufaham uchungaji au utume au uinjilisti n. k. Ni wito au karama anayopewa mtu kutoka kwa Mungu. Sasa Biblia inasema, HII KARAMA YA HUDUMA YA UCHUNGAJI, MUNGU AMEITOA KWA WATU WOTE haijalishi ni mwanamke au mwanaume , kama apendavyo Mungu. Biblia inasema katika

1 WAKORINTHO 12:4-6, 11:- " Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU NI YEYE YULE AZITENDAYE KAZI ZOTE KATIKA WOTE . Lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, AKIMGAWIA KILA MTU PEKE YAKE kama apendavyo yeye."

WAEFESO 4: 8, 11-12:-

" Hivyo husema,Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa. Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu ; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe. "

Karama ya huduma ya uchungaji au uinjilisti , ualimu , utume n.k. Siyo kwa ajili ya wanawaume tu pekee yao hata wanawake pia . Maana Mungu anamgawia kila mtu kama apendavyo yeye mwenyewe .
[ 1 PETRO 4:10-11 ]

Uzee wa kanisa ni suala linalohusiana pia na kazi ya uchungaji ki-biblia, uzee wa kanisa na uchungaji husimama kwenye kazi ile ile moja. Uzee wa kanisa ndio uchungaji wenyewe ki-biblia [ 1 PETRO 5:1-4; MATENDO 20:17, 28] . Na kwa maana hiyo yuko mama mmoja katika Biblia alikuwa ni Mchungaji kwa kazi aliyoifanya. Mchungaji maana yake ni mtu mwenye watoto wa kiroho, ambao anawalisha na kuwachunga. Sasa huyi mwanamke naye alikuwa ni Mchungaji kwa msingi huo. Biblia inasema katika 2 YOHANA 1:1, 4:-" Mzee, kwa mama mteule na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi pekee yangu, bali na wote waijuayo ile kweli . Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba" .

Mwanaume huyu Akila na mwanamke huyu Priska, mke na mume. Kwa pamoja wote wanatajwa kila mmoja wao katika kuhusika kuifanya kazi ya Mungu ya uchungaji waliokuwa nayo juu ya kanisa.
[ WARUMI 16:3-4 ]

Si hilo tu. Neno la Mungu pia linasema "SISI SOTE TUMEFANYIKA KUWA MAKUHANI KWA MUNGU " [1 PETRO 2:5-6, 9-10; UFUNUO 5:9-10]. Kwa hiyo mwanamke naye anaruhusiwa kuwa Mchungaji ki-biblia. Hakuna zuio lolote. Hao wanaopinga hawaijui Biblia.

KIPENGELE NO:-4

UFAFANUZI WA ANDIKO LA 1 WAKORINTO 14:34-35 .

Andiko hili kimsingi halikuwafungia wanawake mlango wa moja kwa moja kutokuhubiri. Hapana. Tumeona katika maandiko mengi na pia Paulo Mtume akiwaruhusu wanawake kuhubiri maadamu tu wazingatie utaratibu unaowapasa , kama kufunikwa vichwa vyao wakati wa kuomba au kuhubiri. Mfano :- 1 WAKORINTO 11:5-6, 13 .

Sasa katika Andiko hilo la 1 WAKORINTO 14:34-36. Paulo mtume aliwakataza wanawake wasinene au wasihubiri katika kanisa . Kimsingi hakumainisha wanawake wote katika wote. Bali wanawake waliozuiliwa " NI WALE WANAWAKE TU WENYE TABIA CHAFU na waliokuwa wakileta fujo (machafuko ) ndani ya kanisa " . Maana anasema wanawake wa namna hii, wakiruhusiwa kuhubiri au kunena ni AIBU katika kanisa
[ 1WAKORINTO 14:32-34, 35].

Faham hili,

SIFA ZA HAO WANAWAKE WA KI-KORINTHO .

Tukisoma katika 1 WAKORINTO 4:16-17:- " Basi, nawasihi mnifuate mimi. Kwa sababu hii nimemtuma Timotheo kwenu, aliye mwanangu mpendwa, mwaminifu katika Bwana, atakayewakumbusha njia zangu zilizo katika Kristo, kama vile nifundishavyo kila mahali katika kila kanisa."

Na kwa maana hiyo. Yale tunayoyasoma katika waraka wa Timotheo. Ni maelekezo yanayohusiana pia na yale yalikuwapo ndani ya kanisa la Corintho . Paulo mtume alitoa maelekezo ya ufafanuzi juu ya hali ya kasoro ilikuwapo.

Sifa za baadhi ya wanawake wa ki-korinto.

(1) Walikuwa na tabia ya kuwatawala na kuwapelekesha wanaume zao

Paulo anatoa ufafanuzi :- 1 WAKORINTO 11:3; 1 TIMOTHEO 2:12-15.

(2) Hao wanawake walikuwa kama waalimu kwa waume zao ndani ya Ndoa. Yaani mwanamke ndio anakuwa msemaji na mwenye kauli ya mwisho juu ya mwanaume .

Paulo anatoa ufafanuzi :- 1 TIMOTHEO 2:12-13.

(3) Walikuwa hawana utii, Adabu wala utulivu kwa waume zao . Yaani walikuwa wanawake mapepe, kicheche (Hawajatulia)

Paulo mtume anatoa ufafanuzi :- 1 TIMOTHEO 2:11.

(4) Walikuwa si wanawake waliostarabika kitabia . Walikuwa ni wambeya (wanoko), wachongezi, wasengenyaji, wavivu n.k.

Paulo mtume anatoa ufafanuzi :- 1 TIMOTHEO 5:2, 11-15.

(5) Walikuwa wenye kujipamba kwa mavazi ya kikahaba na kwa mapambo ya kidunia .

1 TIMOTHEO 2:9-10; 1 PETRO 3:1-6.

(6) Walikuwa ndani yao hawana moyo wa kiasi , uvumilivu, upendo n. k.

1 TIMOTHEO 2:9, 14-25.

(7) Walikuwa ni wanawake ambao hawana tabia ya Utakatifu

Paulo mtume anatoa majibu ya ufafanuzi :- 2 TIMOTHEO 3:6; 2 KORINTHO 7:1

Kwa sababu ya sifa hizo walizokuwanazo hao wanawake hao. Paulo mtume akawakataza wanawake wa jinsi hiyo, wasihubiri ama kunena neno, wanyamanze kimya katika kanisa. Na ni kweli kama mtu hana kielelezo cha usafi na tabia njema (hana ushuhuda). Akisimama na kuhubiri mbele za watu itakuwa ni AIBU badala ya heshima.
[ WARUMI 2:23-24; TITO 2:4-5]

Na pia Biblia inaposema katika Andiko la 1 TIMOTHEO 2:12:" Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanaume ,bali awe katika utulivu"

Kuna maneno mawili tofauti ya kiyunani yanamtaja mwanamke. Ambayo ni " GUNE` " na " THELUS" . Neno Gune` ni mwanamke aliyekwishwa kuoelewa au mke. Na Thelus hutumika kumtaja mwanamke yoyote kwa jinsia yake.

Katika Andiko la 1 TIMOTHEO 2:12-15. Mwanamke aliyetamkwa hapo kwa kiyunani ni GUNE' au mke. Kwa maana hiyo maelekezo ya Andiko linazungumzia yale yaliko katika mahusiano ya ndoa kwa wanandoa tu siyo katika kanisa kama wengi wanavyotafsiri kimakosa. Adamu na Hawa wanaotajwa hapo walikuwa ni mke na mume. Katika Ndoa hairuhusiwi mwanamke kumtawala au kuwa na mamlaka juu ya mume wake. Namna yoyote ya mwanamke kutaka kumwajibisha ki-nidhamu mume wake (kumfundisha) . Hilo ni kosa. Ndani ya ndoa Mwanaume ndiye kichwa cha mwanamke na mwanamke ni mpokea maagizo (mtekelezaji).Huo ndio utaratibu uliowekwa na Mungu.
[ WAEFESO 5:22-24] .

M W I S H O.

Kwa maana hiyo. Hata kanisa la leo. Wakiwapo watu, au wanawake wenye tabia mbaya kwa waume zao na katika jamii, ambao mwenendo wao hauwi kama inaivyopasa Injili ya Kristo [ WAFILIPI 1:27] . Wanawake wa jinsi hiyo wanyamanzishwe katika kanisa wasipewe nafasi ya kunena Neno. Maana itakuwa ni Aibu wanawake hao kunena katika kanisa.

Lakini kama wanawake hao watakuwa na Tabia safi katika Kristo. Biblia imewapasa ruhusa kuhubiri ndani ya kanisa na hata nje.
[ 1 PETRO 3:1-2; ISAYA 58:1; ZABURI 68:11 ]

Mungu awabariki wote kwa kila asomaye ujumbe wa Neno hili. Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja nawe.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JINSI YA KUMSHINDA SHETANI

NGUVU YA DAMU YA YESU

VIPAJI VYA ROHO MTAKATIFU